[wanabidii] UTAJIRI WA LOWASSA UNAVYOYATESA MAKANISA

Sunday, July 06, 2014
Na Prudence Karugendo
KATIKA mafundisho ya Injili, ambayo ni maelezo kuhusu Yesu Kristo, inaelezwa kwamba mama
mmoja alikamatwa na kupelekwa mbele ya Kristo akituhumiwa
kufanya ukahaba huku wadau waliomkamata wakimtaka Kristo
kutoa hukumu ili mama huyo aadhibiwe kulingana na maelekezo ya torati.
Kristo alitumia hekima yake na kusema sawa, anayejielewa ni
msafi hajapata kutenda kosa la jinsi hiyo na awe wa kwanza kutoa adhabu husika. Kauli hiyo
iliwafanya watu wote kutawanyika huku Kristo akimwambia mama
yule aende zake na asirudie
makosa yale.
Tunaona kwamba Kristo
hakutumia njia yoyote
kujinufaisha na udhaifu wa
mwanamke huyo zaidi ya kutoa fundisho kwamba tunapohukumu
ni lazima kwanza tujitazame sisi
tuna usafi gani unaotuhalalisha
kuwahukumu wengine.
Hapa nchini kwetu kuna aina ya kashfa ambayo imetokea kufanana
na makosa yanayotajwa kwenye torati kama makosa ya mauti,
ufisadi. Kama ilivyosemwa kwenye torati kwamba mzinzi anapaswa
apigwe mawe mpaka afe, hata ufisadi unaonekana kuchukiwa
kiasi cha kufananishwa na uzinzi kwenye torati, fisadi anatazamwa kwa jicho baya sana na Watanzania kwa sasa.
Wapo watu wanafanya ufisadi na kujinufaisha nao lakini huku wakiunyanyapaa, hawataki kujiita wala kujulikana kwamba ni mafisadi.
La kushangaza ni kwamba ufisadi unaonekana ni mbaya, mchafu,
watu hawautaki wala kuhusishwa nao, lakini hawakomi kuufanya!
Kwa kuufanya ufisadi ni mtamu ila anayeufanya anaona aibu kuitwa
fisadi!
Mtu anayeitwa fisadi, hata kama anajielewa kuwa anaufanya
ufisadi, tena kwa makusudi, na akielewa kwamba ananufaika nao,
atapiga kelele kwamba
anatukanwa, anaonewa wivu na mambo mengine ya kuipinga sifa hiyo ambayo kila mmoja wetu
anaiona ni mbaya isiyofaa kwa mtu kutambulishwa nayo katika
jamii.
Mbunge wa Monduli, Edward
Lowassa (CCM) jamii imemuweka wazi kuwa ni fisadi. Sitaki kumhukumu kwa vile sina ushahidi wa kutosha wa kunifanya
nimuone hivyo. Ila nitasema kile
ambacho jamii inakichukulia kama
ukweli kumhusu.
Lowassa ni mtumishi wa muda mrefu katika serikali na baadaye akawa Waziri Mkuu kabla ya
kujiuzulu kwa kashfa ya kuipa zabuni ya ushindi kampuni ya kuzalisha umeme wa dhararua ya
Richmond.
Wapo wanaomuandama Lowassa wakitaka asulubiwe kwa kashfa
hiyo ya ufisadi sawa na
mwanamke aliyepelekwa kwa Kristo akituhumiwa kwa ukahaba. Lakini
hata hivyo wanaobeba tuhuma hizo dhidi ya Lowassa hakuna
hata mmoja anayeweza
kututhibitishia kwamba ni msafi asiyepata kutenda kosa kama lile
analotuhumiwa nalo Lowassa.
Kwa hapo fundisho la Kristo ndipo
linapochukua nafasi yake kwamba asiyepata kufanya au kuhusishwa
na ufisadi na awe wa kwanza kumsulubu Lowassa.
Ninalotaka kuliangalia katika makala haya ni namna Lowassa
alivyoingia katika mbeleko ya kanisa na kanisa kumuwekea kinga, lakini kinga iliyo tofauti na
ya Kristo kwa mwanamke
aliyedaiwa ni kahaba.
Kristo aliposema kwamba
anayejijua ni msafi na awe wa kwanza kurusha jiwe kutekeleza sheria ya torati ya kumpiga mawe
mzinzi mpaka afe, alijikuta
amebaki na yule mwanamke peke
yake baada ya watu wote
kutawanyika kwa aibu.
Kumbe watu wote walikuwa
wakilitenda kosa lile. Baada ya hapo ndipo Kristo akamuasa mwanamke yule kutorudia makosa
yake. Yule mwanamke akawa ameshinda kesi kwa njia ya aina yake.
Lakini linapokuja suala la kanisa na Lowassa tunaona kitu kilicho tofauti kabisa. Kanisa linapinga
ufisadi, ila linajaribu kutumia mbinu kama aliyoitumia Kristo
kumnusuru mama mzinzi. Pamoja na ukweli huo kanisa linashindwa
kumwambia Lowassa nenda
usirudie kutenda makosa haya.
Baada ya kutaka kumnusuru
Lowassa kwa njia ya Kristo kwa mwanamke mzinzi Kanisa linang'ang'ani kubaki na Lowassa kwa manufaa yanayoonekana ni ya
Kikanisa. Kanisa linaonekana kumweka Lowassa kwenye mbeleko
yake na kuzunguka naye kila
pahala, kitu kinachoonekana kama
vile kanisa lina namna
linavyojinufaisha na tuhuma
zinazomkabili mtu huyo.
Katika nyakati tofauti
tumeshuhudia kanisa likimualika Lowassa katika shughuli zake
mbalimbali kana kwamba bila yeye kufika shughuli hizo haziwezi kupata baraka za Mungu!
Ndiyo, tumeishapata somo
kwamba kutuhumiana si kuzuri.
Kristo alisema kwamba anayejua
kwamba hajatenda kosa kama lile
na awe wa kwanza kutoa adhabu
husika. Lakini hata hivyo Kristo
hakufundisha kwamba tunaweza
kujinufaisha na tuhuma
zinazomkabili mtu.
Kwahiyo kama kanisa linamuona
Lowassa hana hatia basi
lingemwambia nenda zako
usirudie kufanya au kujihusisha
na kashfa za aina hiyo na kisha
kuachana naye.
Lakini kitendo cha kanisa
kuandamana na Lowassa karibu
kila pahala likijinufaisha na
michango na misaada anayolitolea
kinatoa picha kwamba Lowassa
anatiwa nguvu na kanisa ili
aendelee kupata kwa njia
anayotuhumiwa nayo huku akiwa
amelindwa na kanisa. Kwa maana
nyingine kanisa linamtia Lowassa
ujasiri mpya ili kama ni ufisadi
aendelee kuufanya kwa nguvu na
kasi mpya!
Hakuna namna ambayo kanisa
linaweza kusema kwamba
linaupinga ufisadi ilhali
likimtegemea mtuhumiwa wa
ufisadi aliwezeshe kwa namna
mbalimbali kwa kukitumia kile
anachotuhumiwa nacho.
Utasikia Lowassa kaalikwa katika
kutunisha mfuko wa kanisa fulani,
mara kaalikwa kwenye uzinduzi wa
ujenzi wa kanisa, mara ujenzi wa
kigango, kutiwa wakfu, uzinduzi
wa kwaya nakadhalika. Na kote
huko mwalikwa huyo anamwaga
mapesa au ahadi.
Kwa nini kanisa halijiulizi mtu
ambaye kwa muda wote wa
maisha yake amekuwa mtumishi
wa serikali fedha zote hizo
anazipata wapi? Kwa nini hiyo
isiwe njia ya kulifunua kanisa
macho na kuanza kukiona kile
ambacho mtu huyo anatuhumiwa
nacho?
Kwa njia hiyo tunawezaje kukosa
kuamini kwamba katika fungamano
la makanisa na Lowassa kuna kitu
ambacho kimejificha ndani yake,
kitu ambacho kinawezekana kuwa
ni mpango wa nilinde nikulinde?
Kwa nini mtu ambaye
anaandamwa na tuhuma za utajiri
mchafu aonekane msafi kwa kanisa
na kubebwa kila mahali akiwa
amepewa kipaumbele?
Kama nilivyoonyesha mwanzo
kuhukumiana kwa tuhuma tu
ambazo hazikuthibitishwa si
jambo jema, hata Kristo
alionyesha kutokubaliana nalo.
Lakini vilevile kujinufaisha kwa
kumkingia kifua mtuhumiwa nalo
si jambo jema, sababu tunaona
kwamba hata Kristo hakufanya
hivyo.
Kwahiyo ingefaa kanisa litoe
maelezo ya kwa nini lisihusishwe
na ufisadi baada ya kuonekana
linambeba mtu anayetuhumiwa
kwa ufisadi na kumkingia kifua
huku likiwa linajinufaisha naye
kwa njia mbalimbali.
Pamoja na hilo mtindo wa kanisa
kutaka waamini wake watoe
asilimia kubwa ya vipato vyao kwa
kanisa bila kujali vyanzo vya
vipato hivyo ni dosari kubwa kwa
kanisa. Kuna uwezekano mkubwa
kanisa likajikuta linauchochea
ufisadi, hata ujambazi, kwa
kuvibariki vitu vilivyopatikana kwa
njia hizo haramu baada ya vitu
hivyo kutolewa kanisani kama
sadaka takatifu.
Mtazamo wangu ni kwamba kanisa
lingetakiwa kujitenga na tamaa
inayoweza kulifanya lionekane
linashadidia uasi kwa
kuwakumbatia tu watu wenye mali
kana kwamba inatangazwa kwenye
Injili kwamba wenye nacho ndio
watakaoupata ufalme wa
mbinguni.
Injili inatueleza wazi kuwa tajiri
kufika mbinguni ni vigumu kuliko
ngamia kupita kwenye tundu la
sindano. Kwa kulizingatia hilo
inabidi tujiulize kanisa linapata
wapi ujasiri wa kuwakumbatia
matajiri, ambao tayari
wanaonyeshwa kwamba kuupata
ufalme wa mbinguni ni kitu
kigumu kwao, badala ya
kuwashauri wakagawe mali zao
zote kwa masikini na kumfuata
Kristo kama Kristo mwenyewe
alivyomshauri Zakayo? Ikumbukwe
Kristo hakumwambia Zakayo
kwamba utajiri wako wote leta
kwamgu. Alimshauri akaugawe kwa
masikini.
Kwa mtazamo huo ningeweza
kulielewa kanisa kama lingempa
Lowassa ushauri wa kuachana na
utajiri wake kwa kuwanufaisha
maskini ili yeye apate kuokoka
kuliko kanisa lenyewe kujinufaisha
na utajiri huo wa Lowassa ambao
ni kama unalinajisi hekalu hilo la
Mungu.
prudencekarugendo@yahoo.com
0784 989 512
Julai 7, 2013

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments