[wanabidii] Jumuiya ya Kikristo Tanzania: Tamko la Mapatano ya Mkutano wa Halmashauri Kuu ya 48

Wednesday, July 16, 2014
JUMUIYA YA KIKRISTO TANZANIA

TAMKO LA MAPATANO YA MKUTANO WA HALMASHAURI KUU YA 48 YA JUMUIYA YA KIKRISTO TANZANIA WA JULY 2-3, 2014

UTANGULIZI:

Sisi, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania, tuliokutana tarehe 2 hadi 3 Julai 2014, katika Kituo cha Mikutano na Mafunzo cha Askofu Stefano R. Moshi mjini Dodoma, tumepata fursa ya kutafakari majukumu yetu ya Kitume na Kinabii. Baada ya mjadala wa kina tunatoa tamko letu kama ifuatavyo:

KUIBUKA KWA IMANI NA ITIKADI KALI ZA KIDINI
Tangu mwaka 1994 tulianza kushuhudia vurugu na uvunjifu wa amani kutokana imani na itakadi kali za kidini katika Jiji la Dar es Salaam. Chimbuko la mambo haya lilikuwa kukosekana uvumilivu wa waumini wa dini mbalimbali ambao 
ulichochewa na vikundi vyenye imani kali ya kidini. Ikumbukwe kuwa kabla ya hapo Tanzania haijawahi kushuhudia fujo za kidini za namna hiyo. Kama wengi wetu tunavyoshuhudia leo, imani kali hizi zimeendelea kuongezeka na kuenea katika maeneo mengi hapa nchini hadi baadhi yetu tunaanza kufikiri kuwa serikali imeshindwa kukabiliana na imani hizi ambazo zinaendelea kuleta mauaji, uvunjifu wa amani na kuvuruga umoja wa kitaifa. Kisha, tunaiomba Serikali yetu isipuuze wala kuchelewa kuchukua hatua pale wanapopata habari kupitia vyombo vyake vya usalama na taarifa wanazozipata kutoka kwa raia wema. Endapo serikali itakuwa inapuuza na kuchelewa kuchukua hatua, basi tusishangae nchi yetu ikiingia katika vita kama vile vinavyotokea huko Kaskazini mwa Nigeria.

MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA
Baada ya kujadili kwa kina juu ya hali ya kukosekana kwa maadili ya Viongozi wa Umma na mmomonyoko wa maadili miongoni mwa jamii, Mkutano wetu umegundua kuwa asili ya hali hii ni usimamizi hafifu wa mifumo ya uwajibikaji, udhaifu wa usimamizi wa sheria, udhaifu katika baadhi ya Ibara za Katiba iliyopo na uzalendo kupungua. Matokeo ya haya yote ni uvivu katika maeneo ya kazi, wizi wa mali ya umma kwa njia mbalimbali, kujilimbikizia mali ambazo hazikupatikana kwa njia halali, rushwa za aina mbalimbali, ufisadi, nk. Ili kuondokana na mapungufu hayo ya maadili, wajumbe wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCT inawataka Viongozi wa umma wasio waadilifu waache tabia hizo mbaya zisizokubalika kwa Mwenyezi Mungu na kwa Jamii na wafanye kazi kwa uaminifu na kula kile kilicho halali yao. Pia tunawaomba Viongozi wa Dini mbalimbali kutekeleza wajibu wao wa kulea familia zenye maadili mema kuanzia watoto wanapokuwa wadogo na kuhimiza wazazi kuishi kuwa mifano ya maadili mazuri kwa watoto. Vivyo hivyo, tunawaomba Viongozi wa dini wakemee bila woga maovu yote yanayokiuka maadili ya viongozi wa umma na hata yale yanayotendwa na raia wa kawaida. Aidha, tunawaomba wale viongozi wa umma watakaokuwa wakikemewa wachukulie jambo hilo kama msaada katika utendaji wao na wasichukie na kuwatishia au kuwazushia wale waliowakemea au kuibua maadili yao mabaya.

KUKOSEKANA KWA UVUMILIVU WA KISIASA
Mara tu baada ya Tanzania kuingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, dalili za kukosekana kwa uvumilivu kati ya vyama mbalimbali zilianza kujitokeza. Matokeo ya kwanza yaliyodhihirisha jambo hili ni pale ambapo kulitokea uvunjifu wa amani na mauaji ya raia wachache kati ya vyama viwili vya siasa huko Tanzania visiwani na wengine wachache wakakimbilia nchi jirani. Aidha, hali hii ya kukosekana kwa uvumulivu wa kisiasa umeendelea kuleta fujo mara kwa mara na wakati mwingine hata majeruhi au mauaji yametokea. Pia kumekuwepo na tabia ya wanasiasa kudharauliana, kutukanana, nk. na hali hii inakuwa mbaya zaidi ikionekana hata ndani ya ukumbi wa Bunge na hasa mambo ya jinsi hii yanapofanywa na viongozi waandamizi wa serikali. Jambo hili linalitia Bunge letu na serikali aibu kubwa na Wabunge wanaofanya hivi wajue kuwa tabia hiyo mbaya inayowachukiza wananchi! CCT inawataka Waumini wake na wa dini na madhehebu mengine ambao ni wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa na Wabunge wenye tabia ya kutukanana na kudharauliana waache tabia hiyo mbaya na wajenge utamaduni wa kuvumiliana na kujadiliana kwa hoja kwa kuweka maslahi ya nchi mbele na si ya chama cha siasa. Pia tunaiomba serikali yetu itumie vyombo vyake vya usalama wa raia bila upendeleo wa itikadi za vyama.

VITISHO, MATESO, MAUAJI YA RAIA NA WALINZI WA USALAMA
Ukichunguza kwa kina, katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, kumekuwa na matukio kadhaa ya raia kuteswa vibaya, kujeruhiwa na hata wengine kuuawa bila watuhumiwa kugundulika au wanaogundulika hawachukuliwi hatua zozote za kisheria. Hali hii inawafanya baadhi ya waandishi wa habari na baadhi ya wananchi kuishi kwa hofu na kushindwa kukemea au kutoa habari za maovu ya viongozi wachache wa serikali wanaotekeleza maovu mbalimbali. CCT inawaomba Viongozi wake wote na hata wale wa dini na madhehebu mengine, waandishi wa habari na wananchi wote wanaoitakia nchi yetu mema, kuendelea kutoa sauti ya unabii bila kuogopa vitisho na mateso hayo. Wote tujue kuwa kimya chetu kitaifanya nchi yetu iendelee kutawaliwa kwa ukandamizaji na raia wema wengi ndio watakaoumia.

CHAGUZI ZA KISIASA
Nchi yetu imeshuhudia fujo na uvunjifu wa amani kila wakati wa chaguzi mbalimbali za kisiasa. Hakuna uchaguzi ambao umepita bila wapambe wa vyama vinavyohusika kutukanana, kuzushiana, kudharauliana na hata kupigana. Jambo hili linavua uungwana, kugawanya wananchi na kuchochea fujo na kusababisha uvunjifu wa amani. Kisha, mbaya zaidi, ni pale vyama vinavyohusika vinapotuhumiana kutoa rushwa za namna mbalimbali, ahadi nyingi za kisiasa zisizotekelezeka katika ilani za vyama hivyo au katika mikutano ya hadhara, tuhuma za matumizi mabaya ya vyombo vya dola, tuhuma za kuiba kura kwa njia mbalimbali, tuhuma za kuwepo upendeleo katika Tume ya Uchaguzi, nk mambo ambayo yamewafanya Watanzania wengi wasione umuhimu wa kupiga kura. Tunaiomba serikali isimamie amani ya nchi wakati wa chaguzi mbalimbali na kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa kila mmoja na kwa kila chama cha siasa. Fursa itolewe wazi kwa elimu ya uraia katika maeneo yote ili wananchi wajue nafasi yao katika suala zima la uchaguzi. Pia tunaitaka serikali isimamie Idara yake husika kuhakikisha kuwa Daftari la Wapiga kura linaandikwa/linarekebishwa mapema iwezekanavyo na tena kwa usahihi ili kuwawezesha Watanzania wanaostahili kushiriki kupiga kura bila usumbufu.

KUONGEZEKA KWA PENGO KATI YA WALIONACHO NA WASIONACHO
Japo uchumi wa nchi yetu unakua kwa kasi nzuri, tunashuhudia jinsi pengo la walio nacho na wasionacho linavyoongezeka kwa kasi hasa kwa wananchi wa vijijini. CCT inawaomba Viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali kuwahimiza waumini wao kujiunga katika vikundi na kuanzisha juhudi za kujikwamua na umaskini kupitia Benki za Vijijini (VICOBA) nk. Pia vijana wengi wanaomaliza vyuo mbalimbali hawana kazi za kuaminika na hivyo kuunda kundi lingine la wananchi walio na elimu lakini wasio na kazi maalum hasa kutokana na aina ya elimu inayotolewa hapa nchini. CCT inaitaka serikali kuangalia upya sera ya elimu na kuhakikisha kuwa somo la ujasiriamali linawekewa umuhimu katika kila fani. Pengo hili la walionacho na wasionacho na kundi hili la vijana limeonekana kutumiwa vibaya na wanasiasa wakati wa chaguzi mbalimbali kwani wanajikuta wakishawishiwa kwa urahisi na ahadi zinazotolewa au hata kudanganywa kwa kupewa rushwa ndogondogo na kuwafanya wasifanye maamuzi sahihi ya nani wamchague.

KODI MBALIMBALI:
Kwanza tunaishukuru serikali kwa kuendelea kutambua mchango wa mashirika ya dini katika kutoa huduma za jamii hasa katika afya na elimu na hivyo kutoa misamaha ya kodi kwa mashirika hayo. Pia tunaishukuru serikali jinsi inavyofuatilia matumizi ya bidhaa na mambo mengine yaliyosamehewa kodi. Pamoja na shukrani hizo CCT, inaiomba serikali isilinganishe na kuifanya misamaha inayotolewa kwa mashirika ya dini kuwa sawa na mashirika mengine ya kiraia. Tunaomba mashirikia ya dini yawekewe utaratibu tofauti wa kukaguliwa kuliko na ilivyopendekezwa kuwa kila baada ya miezi sita misamaha hii itachunguzwa na kurekebishwa. Hapa serikali ikumbuke kwamba huduma za jamii zinaendelea na ukaguzi wa jinsi hiyo unaweza ukadhoofisha utoaji wa huduma hizo. Kuhusiana na jambo hili la kodi, tunaiomba serikali yetu ipunguze wingi wa kodi kwa wananchi wa kawaida hasa wanaponunua bidhaa mbalimbali. Jambo hili litasaidia juhudi za kupunguza umaskini. CCT inaitaka serikali kuondoa misamaha ya kodi zote ambazo haziwasaidii wananchi walio wengi moja kwa moja na kwa njia hii kuongeza pato la ndani.

KUHUSU KUANDIKWA KWA KATIBA MPYA
Tangu Mhe. Rais alipoleta wazo la kuandikwa kwa Katiba Mpya CCT imekuwa ikifuatia kwa karibu kila hatua ya mchakato huu na tunatoa mtazamo wetu kama ifuatavyo:

Ø  Tunampongeza Mhe. Rais kwa kusikia kilio cha wananchi wengi kuhusu uhitaji wa kuandikwa kwa Katiba Mpya. Hitaji hili lilijitokeza muda mrefu uliopita na hivyo sasa limepewa uzito mkubwa sana na wananchi na kulichezea au kurudi katika Katiba iliyopo kunaweza kuliletea taifa letu mtafaruku ambao itakuwa vigumu kuutawala.
Ø  Tunampongeza Mhe. Rais kwa utaratibu alioutumia katika kuteua wajumbe wa Tume ya kukusanya maoni ya wananchi.
Ø  Tunaamini kuwa Mhe. Rais anawafahamu vizuri wajumbe wote wa Tume hii na aliwaamini kabla ya kuwaapisha.
Ø  Tunaamini kuwa kila mjumbe wa Kamati ya kukusanya maoni ya wananchi aliheshimu kiapo chake na hivyo kufanya kazi waliyokabidhiwa kwa uaminifu na uadilifu na ya kwamba hawakushawishiwa au kupokea rushwa kutoka kwa kundi, dini au chama chochote cha siasa wakati wa zoezi hili.
Ø  Tunaamini kuwa Tume hiyo ilikuwa aminifu kwa aliyeiapisha, yaani Mhe. Rais na hivyo kumshirikisha kila wakati katika kila hatua na katika kila jambo ambalo walihitaji ushauri wake na ya kwamba walifanya kwa pamoja kama walivyokubaliana.
Ø  Tunaamini kuwa kile kilichoandikwa katika Rasimu ya Pili kilikubaliwa na mwenye kutoa hoja yaani Mhe. Rais na hivyo akaagiza Rasimu hiyo itolewe kama ilivyo kwani aliamini kuwa hayo ndiyo maamuzi ya Wananchi wengi kuhusu Katiba wanayoitarajia. Pia tunaamini kuwa mwenye kutoa hoja alikuwa na uwezo wa kuzuia au Rasimu hiyo isitolewe endapo kuna Ibara ambayo ina mwelekeo ambao ungekuwa hatari kwa mustakabali wa taifa letu.

MAONI YETU KUHUSU AINA YA SERIKALI ZA MUUNGANO: Kwa pamoja Jukwaa la Wakristo Tanzania (CCT, TEC na PCT) lilikubaliana kuwa serikali itakayokuwa na umoja na muungano wa kweli wa nchi mbili ambayo pia itakuwa nafuu sana kuiendesha ni SERIKALI MOJA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA.Tumeshangazwa sana na majadiliano yanayoendelea ndani ya Bunge Maalum la Katiba juu ya serikali mbili au tatu na kuondoa kabisa mjadala wa serikali moja. Aidha, CCT pamoja na wanachama wengine wa Jukwaa la Wakristo Tanzania tutaendelea kusimamia kuwepo kwa SERIKALI MOJA YA MUUNGANO WA TANZANIAkwani tunaamini kabisa kuwa serikali moja ndiyo pekee itakuwa nafuu kuliko mbili au tatu na ndiyo itakayoondoa kero za serikali mbili au zile zinazotarajiwa za serikali tatu. Kisha, Jukwaa hilohilo lilitoa maoni kuwa ENDAPO SERIKALI MOJA ITASHINDIKANA KABISA, BASI MUUNDO WA MUUNGANO WETU UWE WA SERIKALI TATU.Hata hivyo, katika muungano wa namna hii, itapashwa iwekwe Ibara ya fungamano la umoja ambalo litawahakikishia wananchi umoja wao wa Kitaifa utakaodumisha muungano ambao wamekuwa wakiufurahia kwa miaka hamsini sasa.

Baada ya maelezo hayo hapo juu kuhusiana na mchakato wa kuandikwa Katiba Mpya na hasa tukiifuatilia yaliyojitokeza tangu Bunge Maalum la Katiba lianze vikao vyake tunatamka na kushangazwa kama ifuatavyo:

Ø  Hotuba ya kufungua Bunge hilo iliyotolewa na Mhe. Rais ilionyesha hali ya kutokuafiki baadhi ya Ibara au vifungu vilivyowasilishwa na Tume kutokana na maoni ya Watanzania kama yalivyoandikwa katika Rasimu ya Pili. Pia hotuba hiyo ilishusha hadhi ya kazi nzuri iliyofanywa na wajumbe wa Tume ya kukusanya maoni ya wananchi ambaye yeye mwenyewe aliwateua na kuwaapisha. Jambo hili linaweza kufananishwa na mama anayeamua kubeba mimba, kuilea mimba hiyo kwa gharama na kujifungua kwa uchungu halafu mtoto akishazaliwa badala ya kufurahi na kushangilia anaamua mwenyewe kum'beza na kumtelekeza mtoto huyo.
Ø  CCT inawapa pole na kuwapongeza wajumbe wa Tume ya kukusanya maoni ya wananchi na inatambua kwamba walikuwa waaminifu kwa aliyewateua na kwa wananchi wa Tanzania bila kujali itikadi zao za kisiasa au kiimani. Tunawaomba wajumbe wote wa Tume hii wasijisikie vibaya kwa kile kilichotokea kwani kazi yao imeweka historia hata kama itapata upinzani wa namna gani.
Ø  CCT imeshangazwa na lugha za kudhalilisha zisizo za kiungwana zilizotolewa na baadhi ya wabunge wa Bunge Maalum la Katiba kwa wajumbe wa Tume ya Kukusanya maoni. Kwa maneno yao wenyewe, Wabunge hawa wameonyesha kutokumheshimu aliyeiteua Tume hiyo kana kwamba hakufanya vizuri katika uteuzi wake.
Ø  CCT ilishangazwa sana jinsi ambavyo chama kimoja kimekuwa kikiwalazimisha hata Wabunge wanachama wake kukubaliana na kile baadhi yao wanaona inafaa. Tunawaomba viongozi wa vyama vya siasa na Wabunge waheshimu uhuru wa mawazo ya wanachama wao hata kama watatofautiana katika hoja moja au nyingine na wasitumie nafasi zao kulazimisha wanachama wote kukubaliana na mawazo yao. Jambo hili linafanya wanachama wengine wasiwe huru na kuwafanya wakubaliane na kile ambacho hawakipendi mioyoni mwao. Hii ni ishara ya kuwepo Udikteta kwa wananchama wa chama husika. Katika jambo hili CCT inahimiza Wabunge wote waangalie maslahi ya kitaifa kwa upana zaidi na siyo ya vyama vyao.
Ø  CCT inawaomba wajumbe wa Tume ya Kukusanya Maoni ya Wananchi kuwasamehe wale wabunge wote waliowadharau, kuwakejeli na hata kuwatukana.
Ili kujenga hoja yenye nguvu, CCT imefanya utafiti na kuchunguza kile walichosema waumini wa dini na madhehebu mbalimbali wa Bara na Visiwani na kugundua kama ifuatavyo:

Ø  Waumini wengi wa Bara na Visiwani (ikumbukwe kwamba Serikali haina dini bali wananchi wake ni waumini wa dini mbalimbali) walitoa maoni yao kwamba wanataka serikali moja au tatu. Maoni haya yasipochomwa moto kwa sababu ya kupoteza ushahidi yatakuwa katika historia ya Tanzania.
Ø  Katika kuchambua maoni hayo, Tume ilijidhihirishia kwamba Wananchi wengi wanapenda muundo wa Muungano wa Serikali tatu jambo ambalo Tume imeliwakilisha kama lilivyo katika Rasimu ya Pili inayojadiliwa.
Ø  CCT inaendelea kusimamia kuwa muundo wa muungano uwe wa serikali moja lakini pia inaheshimu na kukubaliana na wananchi wengi kuwa muundo wa muungano uwe wa serikali tatu kama inavyoonekana katika Rasimu ya Pili ya Katiba.

Kwa mantiki hiyo, CCT INATAMKA KUWA RASIMU YA PILI YA KATIBA NDIYO MAWAZO YA WATANZANIA NA TUNAHIMIZA KUWA WAJUMBE WOTE WA BUNGE LA KATIBA WAACHE KUJADILI MAONI YA VYAMA VYAO NA WAJADILI NA KUHESHIMU MAONI YA WATANZANIA WALIO WENGI NA WAACHE KABISA KUJADILI MAWAZO YA VYAMA VYAO.

Imetolewa leo Julai 03, 2014
Na MKUTANO WA HALMASHAURI KUU YA JUMUIYA YA KIKRISTO TANZANIA

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments