[wanabidii] WAISLAMU KUONEWA - ALICHOSEMA MHE IDD SIMBA

Friday, May 09, 2014

UNAYAKUMBUKA HAYA?

TUJIKUMBUSHE YA ZAMANI
Aliyoyasema Mhe. Idd Simba katika mkutano
"Assalaam alaykum Warh. Wab.
NDUGU Waislamu mimi nimeomba tukutane leo katika nafasi yangu ya Ubunge wa Jimbo la Ilala. Nimekuja kama Mbunge wa Ilala, lakini pia nimekuja kama Muislamu.
Wanaonijua hawatakuwa na mashaka juu ya imani yangu katika dini ya Uislamu. Wanaonijua hawatakuwa na mashaka juu ya moyo na uwezo wa kulilia haki za Waislamu.
Kilichonileta ni nini. Nilikuwa safarini niliposikia kwamba katika maeneo ya jimbo ambalo mimi naliwakilisha kumetokea maandamano ambayo yalisababishwa bila shaka na kero ambazo ziliwakabili Waislamu. Katika maandamano hayo palitokea ghasia, watu walikamatwa.
Ni wajibu wangu kama muwakilishi wa watu ambao wana kero, wanahisi yapo mambo mabaya kwao, labda yalikuwa bado hayajashughulikiwa kikamilifu.
Sasa mimi niliporejea katika hiyo safari yangu na kusoma kwenye magazeti na kusikia kwa jamaa kwamba yalitokea mambo hayo niliona ni vizuri tukutane na Waislamu. Nijue kilichowakera ni kitu gani na niliwakosea nini mimi; mpaka sikuambiwa hayo yanayowakera.
Nataka kujua; mosi; ni mambo gani yaliyowakera Waislamu mpaka tukafikia hatua kuchukua hatua kama ile (ya kuandamana). Namimi nasema niliwakosea nini mpaka tukashindwa kutumia mazingira ambayo tumeyozoea ya mimi kuitwa na kuelezwa zile kero.
Nilivyojua mimi ni kama wasichana wanaotaka kuvaa hijab huwa wanavaa hijab. Pia mimi sijasikia kama kuna mwanafunzi amenyimwa nafasi ya kwenda kuswali wakati wa swala ya Ijumaa.
Sasa mimi nasema hivi, yaliyonileta ni hayo nataka nisikie kutoka kwenu ni nini kilichowasibu.
Waliyoongea Waislamu katika kikao hicho
MAHMOUD MOHAMED MADENGE:
Mhe. Simba ni Muislamu Mtanzania, kiongozi ambaye serikali yake inazungumza kwamba inataka kuzungumza kwa ukweli na uwazi. Sasa na sisi kama Waislamu tunataka kukuambia ukweli na uwazi.
Mwenyezi Mungu anakataa unafiki na ametoa sura nzima ndefu inayozungumzia habari ya unafiki. Bwana Simba unawahadaa Waislamu kwamba wewe hujui wamepigwa nini (kwanini waliandamana).
Waislamu wametangaza wiki nzima tutaandamana, hijaab, Hijaab, suala la hijaab tutaandamana jamani. Na wewe Mhe. Waziri Mbunge wao upo, unajua habari hiyo. Kwanini usijibu kwamba jamani e msije mkaandamana sheria iko (inayoruhusu hijaab). Leo unakuja hapa unatuhadaa kwamba eti hujui kwanini tuliandamana. Hivyo sio vizuri haifai.
Serikali mpaka sasa; ndugu yangu Simba upo kwenye serikali kama ningekuwa mimi ningejiuzulu. Kwa sababu moja. Serikali zote duniani hata za makafiri , binadamu akifa wanafungua "inquest" ya kujua amekufaje.
Lakini toka Waislamu wauliwe Mwembechai mpaka leo bado. Serikali mnatupeleka wapi Waislamu?
Nyinyi ndio maadui wa Uislamu kama hamtafanya kutafuta njia, mkae chini muwaambie Waislamu mmeacha uadui nao kwa vitendo, hawatawasikia.
Hatutaki upendeleo tunataka haki yetu. Haki, haki, haki ni kwa mtu yeyote. Ukiikosa unainyang'anya kwa nguvu kwa sababu ni haki yako.
*******************
HAJI:
MIMI nina maswali lakini kabla sijatoa maswali yangu nataka nitoe maelezo mafupi. La kwanza nilivyoelewa mkutano huu umeitwa na mwanasiasa halafu amewaita Waislamu. Aidha viongozi wa chama chake wameshatamka, wametamka na wataendelea kutamka kwamba wananchi wasichanyange dini na siasa. Hilo la kwanza, la pili, ninalotaka kuweka wazi kwa sababu yeye ni mwanasiasa na ni mtu wa CCM. Leo hii Mheshimiwa Mbunge umetokana na Waislamu. Lakini chama chake hakiwataki na kinafukuza Waislamu. 1957 wazee wetu Halmashauri Kuu ya TANU wote walikuwa Waislamu isipokuwa mzee Rupia na Mwalimu Nyerere, lakini mpaka kufikia leo kwa sababu moja au nyingine mmetufukuza katika chama. Wewe msimamizi mmojawapo wa SUKITA wanafuga nguruwe. Tuna mifano ya dhahiri shahiri ya watu waliacha kazi kwa sababu ya nguruwe. Aidha, chama kinachotawala, tunakuwa tunaona Masheikh wanaonewa, wanadhalilishwa, wako hoi taabani. Na wanasiasa wote wanajua, na Chama Cha Mapinduzi kinajua. Sasa mimi nataka kuuliza swali la kwanza la msingi, faraja uliyokuwanayo Mheshimiwa Mbunge wewe ni Muislamu. Kwanza 1995 ulichukua juhudi gani angalau kutuita Waislamu katika ushauri tunapopata matatizo. Kwa sababu mojawapo ya viongozi ni kuwafuata watu bila ya kujali dini wala kabila zao. Sasa isiwe sasa hivi unakuja kutuhoji kwamba kitu hiki tunajua na si kukuomba utusaidie kwa sababu huu ni wakati wa vyama vingi. CCM washasema mengi kwamba wenye ndevu wapigwe na mawe. Mzee Kileo hebu simama kidogo, huyu ana kesi ya mabomu miaka saba. Maisha yake yako hatarini hajui mwisho wake utakuwa nini, kila siku anaripoti. Huu ndio uhuru tulioutafuta?
Kwa kumalizia tu juzi katika session ya Bunge Mheshimiwa Waziri wa Elimu alisimamisha hoja katika Bajeti yake lakini kwa bahati mbaya Wabunge wote au naweza kusema Wabunge wote 190 wakamzomea.
Sasa Wabunge walipomzomea, Waziri Mkuu akaminya kuna Mwanasheria Mkuu, Chenge naye akaminya. Mpaka Waislamu wakasema tutaandamana, tutaandamana, tutaandamana, hukuzungumza lolote wala kuingia katika harakati kuhakikisha kwamba maandamano hayafanyiki. Mpaka watu wakaingia katika maandamano, hayo yanayosemwa maandamano. Waislamu kwa mara nyingine tena wakapigwa, Msikitini wakavamiwa wakaingiliwa sehemu takatifu za Misikiti yetu na viatu. Na kuwatumia baadhi ya wanaodai kuwa wao ni Waislamu. Waislamu kwa mara nyingine tena wakanyanyaswa hadharani.
Kinamama wakasachiwa hata vituo vya polisi hawajafika kwamba wao wana mabomu. Hakuna mwanasiasa yeyote aliyezungumza hata kusema mimi nina uchungu na Msikiti wangu. Wewe usingezungumza kama Muislamu lakini ungesema hapa sheria ya nchi imevunjwa. Tungekuelewa sisi lakini leo wewe kuja kutuhoji juu ya maandamano tunaona kama vile unatunyanyapaa.
*******************
RICCO:
Kwanza tunamshukuru Mwenyezi Mungu (s.w.) kufikia hapa. Waziri katoa nafasi yaulizwe maswali, mimi ninavyoelewa kazungumza mambo mawili. Amezungumza kwamba ni mambo gani yaliyowakera. La pili kasema, tulimkosea nini mpaka tusimwite tukafanya maandamano moja kwa moja. Sasa pale mimi naona kwanza hakuna swali, awali ya yote matatizo ya Waislamu yamewakera kwa sababu gani nazungumza hivyo kwa sababu serikali hii ya Tanzania imezoea mambo ya uongo uongo. Juzi Rais alitamka kwamba anashughulikia mambo ya Mwembechai. Lakini si kweli kwa sababu gani, mauaji yametokea Mwembechai, anatafutwa Ponda! Kosa kubwa la mauaji sababu yake, anatafutwa Ponda. Sasa Waziri kaja hapa mimi nilivyomuelewa tumueleze matatizo yetu apeleke mbele lakini mimi nasema hawezi kushughulikia maswali ya Waislamu. Hawezi! Labda Waziri aseme amekuja hapa tumfanyie kampeni mwaka 2000 lakini sio matatizo ya Waislamu. Sasa mimi natoa mapendekezo yangu binafsi kama kiongozi wa Al-Mallid. Namwambia Waziri mambo yanayotukerea sisi pamoja na kwa Rais katamka kwamba watu waswali siku ya Ijumaa, wanafunzi wavae hijab, hili ni suala dogo. Suala kubwa ambalo sisi tutalifanyia maandamano makubwa sana ni watu wapumzike siku ya Ijumaa wasiende kazini. Kwa sababu Wakristo Jumapili wanapumzika, Wasabato Jumamosi inakuwaje sisi Waislamu Ijumaa tusipumzike. Kwa hiyo hili tunalidai la kwanza kama utalifikisha.
Halafu jambo lingine ambalo tumeshatamka na nafikiri hutalifikisha lakini kwa kuwa wewe ni Mbunge tunataka suala la mauaji ya Mwembechai lishughulikiwe haraka tusidanganywe danganywe. Na jambo la tatu ambalo ni la mwisho, polisi wanawanyanyasa Waislamu hasa sisi tunaofanya mihadhara. Unapoomba kibali si sheria katika katiba kuomba kibali lakini wanatunyanyasa hasa huyu Bwana jana (Magezi) kaomba kibali wamemnyima. Anafanya mhadhara kwa nguvu na tufafanya hivyo kwa nguvu.
*******************
SHEIKH OMAR BASHIR:
NASHANGAA kabla sijasema lolote. Nafahamu kuwa aliyekuwa mpishi jikoni ndiye anayejua ladha ya chakula. Sasa ikiwa wewe mpishi unatoka barazani kisha unauliza kwani nyinyi mnakula nini wakati wewe ndiwe uliyepika!
Maswala ya kuandamana yalitokea Bungeni na yeye ni Mbunge alikuwa kule. Ilikuwa hakuna haja tena ya yeye kuuliza kwani tatizo lenu nyinyi nini. Hivi kweli anatueleza... hivi Idd Simba hajui kwanini watu wameandamana! Si kweli.
La pili, mimi nina wasiwasi mkubwa sana kwamba hii tunafanyiwa mchezo. Kwa sababu kama Rais aliyakubali masuala ya Mwembechai na mpaka sasa hajasema chochote, na sasa anakuja Waziri tunamueleza sijui aende wapi na huku yaliyoko kichwani hayajatekelezwa. Miguu iende wapi kichwani kule kumeharibika. Hakuna majibu mpaka sasa suala la Mwembechai.
Swali si nini Waislamu wanataka, swala Waislamu ni raia ni Watanzania kama raia wa Tanzania (basi wanastahiki) haki zote si masuala ya hijabu tu.
Mungu alimwambia Daud. Daud tumekufanya kiongozi uwahukumu watu, watendee watu wote haki.
Waislamu ni watu wa amani lakini wanajua uonevu na wanajua haki na hali hiyo haitokwisha ila itazidi siku hata siku. Ili serikali ipate salama na nchi ipate amani waonekane Waislamu kuwa ni raia kama raia wengine.
Ikiwa Rais alitambua walichoandamana Waislamu, vipi Mbunge asijue. Hamuoni pana kichekesho hapa. Ikiwa Rais alisema suala la hijaab ruhsa tena limo ndani ya Katiba vipi leo Waziri aje atuulize "kitu gani mnachoandamana". Tusikae tukapotezeaa muda tuna kazi muhimu.
Ajue Idd Simba kama Muislamu arejee kwa Mwenyezi Mungu atawajibika juu ya mambo ajitahidi kwa uwezo wake juu ya kuunusuru Uislamu. Atumie mali zake na atumie nafsi yake na ajue hapa ataondoka na atakwenda Akhera. Amechukua dhamana kuwa ni kiongozi wa kufikisha. Afikishe bila ya kumkhofu mtu, amkhofu Mwenyezi Mungu.
Rudi kama Waziri mwambie kiongozi (Rais) kwamba tatizoj la WaislamuHawakubali kuonewa.
Si njia salama kutumia mabomu wala bunduki kuna watu watakuwa vichaa kila utakapowapiga mabomu, na wao itafika siku nao watajua wapige mabomu. Waislamu watu wa amani na Qur'an imefundisha amani lakini haifundishi ujinga na kukubali kuonewa. Swali lingine yafaa niulize Ponda anatafutiwa nini


--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments