Kuna ule msemo maarufu unaosema kwamba 'Ukistaajabu ya Musa utaona ya Firauni'. Msemo huu bado ungali unasadifu hali halisi iliyopo hapa nchini. Juzi nimesikia baadhi ya makada wa CCM wakitiana moyo kwamba mchakato wa katiba mpya utafanikiwa hata kama UKAWA wasiporejea bungeni. Ili kutimiza adhima yao hiyo ovu, wameanza mkakati wa kuchakachua kanuni za Bunge Maalum la Matusi (BMM) ili njia yao hiyo ya kishetani ipate kunyooka. Wameenda mbali zaidi na kujifariji kwamba wanaweza kubadilisha mfumo wa upitishaji wa maamuzi unaotaka kwamba vifungu vya katiba vipitishwe kwa 2/3 ya wajumbe kutoka Tanganyika na Zanzibar ili sasa viweze kupita kwa 2/3 ya wajumbe waliomo bungeni bila kuzingatia utanganyika wala uzanzibar!
Mimi nasema hivi: hizi ni dua za kuku na hawa watu hawajui wanalolifanyalo. Nawafananisha na wale wajinga katika biblia waliotaka kujenga mnara wa Babeli. Watu hawa walitaka kujenga mnara mrefu hadi mbinguni kwa Mungu. Mungu akawaona hawana akili, akawachanganya lugha hata wasipate kuelewana. Matumani yao yakaishia patupu. Hiki ndicho wajumbe wa CCM waliobaki ndani ya bunge la BMM wanachotaka kufanya. Ni kama vila Mungu ameishawavuruga akili—hawajui wanachokifanya. Wamebaki tu wakiendelea kutumbua posho za wananchi kwa kujipa matumani hewa ya kubadilisha kanuni za utunzi wa katiba.
Inashangaza sana kwamba ndani ya hawa wabunge kuna maprofesa wa sheria walioenda shule lakini wanashindwa kuchanganua suala dogo kama hili. Kimsingi kubadilisha kanuni za bunge inawezekana lakini suala la kubadilisha sheria ya 2/3 ni suala gumu ambalo haliwezekani hata kidogo. Labda kama wanataka kuuvunja muungano na wanataka kusiwepo na serikali ya Shirikisho wala ya Mkataba.
Njia pekee iliyobaki ya kunusuru mchakato huu ni kama UKAWA watalegeza msimamo wao na kurejea bungeni. Na hili litawezekana kwa maridhiano tu. Lakini kwa kuwa CCM hawana mpango wa maridhiano wala nia njema ya mchakato wa katiba, sioni uwezekano wa UKAWA kurejea bungeni. Kwa lugha rahisi ni kwamba mchakato huu wa katiba ni kama vile umeishafika tamati.
Kinachoniuma zaidi ni kuona mamilioni ya pesa za wananchi yanateketea bure. Ni afadhali pesa hizi zingetumiwa kuongeza mishahra ya wafanyakazi au kuboresha huduma za jamii kuliko ambavyo zimetumiwa ovyo na hawa wachumia tumbo wachache wa CCM.
0 Comments