[wanabidii] USHAHIDI KWAMBA SERIKALI 3 NI RAHISI KULIKO SERIKALI 2

Wednesday, April 23, 2014
Ushahidi mdogo tu unaoonyesha kwamba serikali 3 ni rahisi kuziendesha kuliko serikali 2 unapatikana katika rasimu ya katiba inayojadiliwa sasa hivi Dodoma, ambayo inapigwa vita na kundi la wengi kwa nguvu zao zote (na hata ikibidi wako tayari kuingia msituni kutetea serikali 2). Sura zifuatazo zinadhihirisha gharama hizi:
 
USHAHIDI WA KWANZA
Sura ya saba, ibara ya 98(2). Kifungu hiki kinasomeka ifuatavyo:
 
"Kwa madhumuni ya ibara ndogo ya 98(1), idadi ya mawaziri na manaibu waziri wa serikali ya Jamhuri ya Muungano, haitazidi 15". Mwisho wa kunukuu.
 
Idadi ya mawaziri na manaibu waziri katika serikali ya sasa ni zaidi ya 60! Kila waziri analipwa mshahara (excluding gharama za nyumba, gari, mafuta, safari na anasa zingine) wa Tsh 20,000,000. Jumla ya mshahara kwa mawaziri 60 wa serikali 2 ni Tsh 20,000,000×60= 1,200,000,000. Hizi ni Tsh 1.2 billion (sawa na Tsh 14.4 bilion kwa mwaka).
 
Mshahara wa mawaziri 15 wanaopendekezwa katika serikali 3 ni Tsh 20,000,000×15=300,000,000. Hizi ni Tsh million 300 (sawa na Tsh 3.6 billion).
 
Kwa hivyo mtaona kwamba gharama ya kuendesha mawaziri 15 wa serikali 3 ni rahisi kwa Tsh billion 10.8 sawa na 75%. Haya, sasa wale mnaodai kwamba serikali 3 ni ghali huwa mnatumia kigezo gani? Msidhani kila mtanzania ni zuzu. Mnaposema ughali au urahsi sharti muoneshe mnakokotoaje hizo gharama, sio watu wanakaririshwa majibu kwenye vikao halafu wanakuja kupayuka hadharani bila takwimu. Huo ni ujuha!
 
USHAHIDI WA PILI
Kwa mujibu wa rasimu ya katiba ibara ya 113(1) na (2) idadi ya wabunge inayopendekezwa kwenye rasimu ni wabunge 70 wa kuchaguliwa (50 kutoka Tanganyika na 20 kutoka Zanzibar) na 5 walemavu watakaoteuliwa na rais. Hawa ni sawa na jumla ya wabunge 75. Bunge la sasa lina jumla ya wabunge 389 wa kuchaguliwa na 10 wa kuteuliwa, sawa na wabunge 399. Kila mbunge hulipwa Tsh 11,000,000 (+5,000,000 za jimbo)=16,000,000. Wabunge wote 399 wanalipwa jumla ya Tsh 399×16,000,000=6,384,000,000 (sawa na billion 6.4). Gharama ya wabunge hawa kwa mwaka ni Tsh 76.4 bilion.
 
Gharama kwa wabunge 75 wa serikali 3 ni Tsh 16,000,000×75=1,200,000,000(sawa na Tsh 14.4 bilion kwa mwaka).
Tofauti ya gharama za kuendesha bunge la serikali 2 ukilinganisha na bunge la seriakli 3 ni Tsh 62 bilion. Sasa hawa waongo wanaosema kwamba kuendesha serikali 3 ni ghali wanatumia kigezo kipi hawa vilaza?
 
KUMBUKA:  
Ukokotozi wa gharama uliofanywa hapo juu haujumuishi gharama za mishahara, marupurupu, mafuta, safari, anasa, nk za makatibu wakuu, makamishina, wakurugenzi na wakuu wa idara katika wizara husika. Ukijumlisha na gharama za kuwalipa viongozi hawa pesa zitakuwa nyingi zaidi ya mara mbili ya hizo zilizokotolewa hapo juu. Huu ushahidi unatosha kabisa kuonyesha kwamba serikali 3 ni rahisi kuliko serikali 2. Kwa hiyo, ule uongo mnaoambiwa na wanasiasa kwamba serikali 3 ni ghali kuliko 2 mnapaswa kuupuuzilia mbali. Wanakudanganyeni kwa maslahi yao binafsi ya kisiasa ili waendelee kukukandamizeni, kukumasikinisha na kukuchukulieni kama mazuzu wa kupandia ngazi za madaraka na kujichumia mali kwa ajili ya matumbo yao binafsi.
 
 
TAHADHARI
Kwa upande mwingine, ifungu hivyo nilivyonukuu hapo juu ni mwiba mkali kwa CCM kwani vinawanyima uhuru wa kujitungia wizara na kuwapa uwaziri makada wao kama zawadi kwa kazi nzuri ya kukitumikia chama. Wanapenda tuendelee na mfumo ghali wa serikali 2 ili wananchi waendelee kubebeshwa gharama za kuendesha serikali kwa manufaa yao binafsi. Mwenye macho haambiwa tazama. Kila mtanzania anapaswa kufunguka macho na kuhoji hizo gharama wanazodai wanazikokotoa kwa kutumia kigezo kipi. Sio mtu unakaririshwa kwamba serikali 3 ni ghali kuliko 2 unakubali tu kama zuzu. Unatakiwa kuhoji. Ujinga wa watanzania kutohoji mambo ndio unaosababisha wanasiasa waendelee kutudanganya na kutufanya ngazi za kupandia na kuning'inia madarakani kwa manufaa yao binafsi.
 
 
N.B
Uchambuzi zaidi kuhusu gharama kubwa za kuendesha serikali 2 ukilinganisha na serikali 3 utafuata baadaye. Nataka wale waongo wanaowadanganya raia kwamba serikali 3 ni ghali kuliko 2 waumbuke mchana kweupe.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments