[wanabidii] TAARIFA YA WIZARA KUHUSU MAFANIKIO YA MUUNGANO

Tuesday, March 04, 2014
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA MAKAMU WA RAIS

TAARIFA YA MAFANIKIO YA MUUNGANO

ITAKAYOTOLEWA NA MHE. WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA RAIS – MUUNGANO TAREHE 4 MACHI 2014, UKUMBI WA HABARI MAELEZO

1.0 UTANGULIZI
Ndugu Waandishi wa Habari, kama mjuavyo kuwa, ifikapo tarehe 26 Aprili, 2014 Watanzania tutashuhudia Muungano wetu ukitimiza nusu karne. Miaka hii 50 ya Muungano imekuwa ni yenye mafanikio makubwa ambayo yamenufaisha wananchi katika nyanja mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kisiasa. Muungano umewapa fursa wananchi wa pande zote mbili kuishi kwa amani na kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo popote walipo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jambo hili linadhihirisha kuwa Muungano wetu umeendelea kuwa nyenzo na utambulisho muhimu wa umoja wetu. Hivyo, katika kuuenzi Muungano wetu ni vyema kwa pamoja tukaendelea kuudumisha, kuutetea na kuuimarisha ili uweze kufikisha karne na miongo mingi zaidi kwa manufaa yetu na vizazi vijavyo.

2.0 URATIBU WA MASUALA YA MUUNGANO
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Sura ya 11 Ibara ya 47(1) (a) jukumu la kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kufuatilia utekelezaji wa siku hadi siku wa mambo yanayohusu Muungano limekabidhiwa kwa Makamu wa Rais. Aidha, kwa mujibu wa Tangazo la Serikali la Majukumu ya Wizara (Assignment of Ministerial Responsibilities Notice), la mwezi Januari, Mwaka 2011, majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwenye shughuli za Muungano ni Kuratibu Mambo ya Muungano; na Kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mambo yasiyo ya Muungano.

3.0 MAFANIKIO YALIYOPATIKANA KATIKA UTEKELEZAJI WA MASUALA YA MUUNGANO 
Katika kipindi cha Awamu ya nne ya Serikali, Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuratibu masuala ya Muungano na kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na na hivyo kuendelea kuimarisha mshikamano na udugu kwa pande zote za Muungano. Mafanikio hayo ni pamoja na:-

a) Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria za Muungano
Mojawapo ya mafanikio makubwa ya Muungano wetu ni kuwepo kwa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baada ya kuasisiwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964, Katiba ya muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipitishwa mnamo mwana 1965 na Baadaye Mwaka 1977 ilitungwa Katiba ya kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, Kuanzia mwaka 2011 nchi yetu imekuwa kwenye mchakato wa mabadiliko ya Katiba baada kuonekana kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano (1977) iliyopo, ina mapungufu mengi na ili yaweze kuondoshwa hapana budi kuwa na katiba mpya, mchakato ambao unaendelea hadi sasa.

Kuwepo kwa katiba kumeboresha upatikanaji wa huduma bora za kisheria katika eneo la Haki za Binadamu, Mikataba, Uandishi wa Sheria na kuhakikisha uendeshaji wa mashauri ya Jinai, Madai na kikatiba yanamalizika kwa wakati. Pia katiba imeweza kuleta mabadiliko mbalimbali katika Nyanja za kisiasa.

Sheria mbalimbali za Muungano zimetungwa na baadhi kurekebishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili zikidhi mahitaji ya utoaji haki ikiwa ni pamoja na mahitaji ya mabadiliko yanayoendelea kwa haraka katika nyanja za kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiteknolojia na pia kurahisisha utekelezaji wa masuala ya Muungano na kuleta ufanisi zaidi.

b) Kuimarika kwa Ulinzi na Usalama wa Nchi
Wananchi wa pande zote za Muungano wanaendelea kuishi kwa amani na utulivu. Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Polisi na Uhamiaji kwa umoja wao kama taasisi za Muungano kwa kushirikiana na wananchi wameendelea kudhibiti matishio ya kiusalama yanayojitokeza na kuimarisha amani iliyopo. Mfano, udhibiti wa uharamia baharini, madawa ya kulevya, usafirishaji wa binadamu, uhamiaji haramu, mashambulizi ya kutumia tindikali na ugaidi. 

Kuwepo kwa ulinzi na usalama wa kutosha kumewezesha kwa kiasi kikubwa wananchi kutekeleza majukumu yao katika hali ya amani na utulivu. Tumeshuhudia kukua na kuongezeka kwa biashara na uwekezaji, utalii na miradi mbalimbali ya kimaendeleo kutokana na hali ya amani na utulivu uliopo.

c) Wananchi kutumia fursa za Muungano za Kijamii 
Wananchi wetu wanashiriki kikamilifu katika kujipatia fursa za makazi, biashara, haki za uraia, elimu na ajira kwa ajili ya kujitafutia maendeleo. Kupitia taasisi za Muungano kama vile Bodi ya Mikopo ya elimu ya juu wanafunzi wenye sifa Tanzania bara na Zanzibar wanapatiwa mikopo ili kukidhi gharama za masomo, hali hii imeimarisha kwa kiasi kikubwa ubora wa elimu ya juu kwani kumekuwa na ongezeko la Vyuo vya Elimu ya Juu kutoka 25 vilivyokuwepo mwaka 2005 hadi 63 vilivyopo sasa pia idadi ya idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa katika vyuo imeongezeka kwa kuwa upo uhakika wa kupata mkopo wa gharama za masomo. 

Aidha, kwa kufurahia matunda ya uraia wa nchi moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wananchi wamekuwa na uwezo wa kwenda au kuishi sehemu yeyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kutumia hati za kusafiria. Kumekuwa na muingiliano wa tamaduni kama aina za vyakula, mavazi, mitazamo, itikadi, maarifa, maadili na kuoleana baina ya wananchi wa pande zote mbili za Muungano hali iliyosababisha Muungano kuwa imara kwa kuwa umekuwa wa kindugu zaidi kuliko wa kiujirani au wa kijiografia kama ilivyokuwa awali.

Kupitia utekelezaji wa Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kufanyiwa marekebisho na Tume hiyo kufanya kazi pande zote mbili za Muungano suala hili limekuza, kulinda na kuhifadhi haki za binadamu katika jamii, limeboresha utendaji kazi na uwajibikaji kwa watumishi na vilevile kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.

d) Mafanikio Katika Nyanja za Kiuchumi
Kuwepo kwa Sera na sheria ya moja ya Benki kuu ya mwaka 1995 kumekuwa ni kichocheo kikubwa cha kukua kwa uchumi kwa pande zote mbili za Muungano. Hali hii imewezesha kushuka kwa mfumuko wa bei kutoka asilimia 30 katika miaka ya 1990 hadi chini ya asilimia 10 kwa miaka ya hivi karibuni; Uchumi umekuwa ukiongezeka kila mwaka sambamba na ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi; Benki na taasisi mpya za fedha zimeweza kuanzishwa nchini kwa pande zote za Muungano. 
Aidha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinashirikiana katika kubuni na kuibua miradi ya kimaendeleo inayofadhiliwa na Serikali kwa kushirikiana na Wahisani wa Maendeleo. Mfano wa miradi hiyo ni pamoja na Mradi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF III, MACEMP, ASDPL na ASDP. Miradi hii kwa ujumla wake imeweza kuwa chachu kubwa ya maendeleo ya Wananchi katika pande zote za Muungano.

e) Kuimarika kwa Masuala ya Usafiri na Usafirishaji
Uboreshaji wa Miundombinu katika sekta ya usafirishaji umeendelea kufanyika hususan ujenzi wa barabara, miundombinu ya umeme na maji. Ongezeko la huduma za usafiri wa anga na majini kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar zimefanya wananchi kusafiri kwa haraka na urahisi kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine ya Muungano bila usumbufu. Jambo hili limeimarisha umoja na mshikamano wetu na hivyo kukuza uchumi na kudumisha uhusiano wa karibu kwa wananchi wetu. 

f) Umoja katika kukabiliana na majanga na Dharura
Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi kwa kushirikiana na mamlaka za kiraia, taasisi za Muungano na watu binafsi wameweza kuonesha umoja na mshikamano mkubwa katika vipindi vya majanga yalizozikumba nchi zetu kwa nyakati mbalimbali mfano katika ajali ya kuzama meli ya MV Spice Islanders iliyotokea tarehe 10 Septemba, 2011 katika Mkondo wa Nungwi, ajali ya kuzama boti ya MV Skargit iliyotokea nje kidogo ya bandari ya Zanzibar tarehe 18 Julai, 2012, wahanga wa jengo la ghorofa 16 lililoporomoka Dar es Salaam tarehe 29 Machi, 2013, kufukua miili ya Watanzania waliokuwa wamefukiwa katika maporomoko ya machimbo ya moramu yaliyotokea huko Arusha tarehe 01 Aprili, 2013 na Januari – Februari , 2014. Hali hii imeimarisha upendo, mshikamano na kuaminiana kwa pande zote mbili na kuufanya Muungano kuwa imara zaidi.

g) Mafanikio katika nyanja ya Kisiasa
Mojawapo ya mafanikio makubwa ya kisiasa yaliyopatikana kutokana na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni kuungana kwa vyama vya siasa vilivyokuwepo kwa wakati huo TANU na ASP na kuunda chama cha Mapinduzi (CCM) mnamo tarehe 5 Februari 1977. Ndani ya Chama kimoja Serikali zetu zimeweza kufanikisha malengo mbalimbali ya kisiasa kiuchumi na kijamii mpaka pale mfumo wa vyama vingi uliporejea tena 1992. Mfumo wa siasa wa vyama vingi, umeleta kupanuka kwa demokrasia, uhuru wa kutoa maoni na uwazi katika uendeshaji wa shughuli za umma ikiwa ni pamoja na masuala ya Muungano.

Hata hivyo, Sheria yetu ya vyama vya siasa inatoa masharti kwamba ili chama kisajiliwe lazima kiwe na wanachama kutoka pande zote mbili za Muungano, ongezeko kubwa la vyama vya siasa ni ushuhuda kwamba wananchi wanapata uhuru wa kutosha katika kuendesha mambo yao ya kisiasa hali inayodhihirisha kukua na kuimarika kwa utawala bora. Katika miaka 50 ya Muungano tumeshuhudia kuendelea kuenziwa kwa Mapinduzi matukufu ya Zanzibar pamoja na Muungano wenyewe. 

Aidha, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeendelea kuendesha chaguzi kwa njia ya utulivu amani na kidemokrasia katika pande zote za Muungano na hivyo kutoa uwiano wa ushindani sawa wa kisiasa kwa vyama na makundi mbalimbali ya kisiasa.

4.0 CHANGAMOTO
Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 50, Muungano bado unapitia changamoto mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kijamii zilizotokea ndani na nje ya nchi na ambazo kwa njia moja au nyingine zinaathiri utekelezaji wa masuala ya Muungano. Changamoto hizo ni:-

a) Uelewa wa Wananchi katika Masuala ya Muungano bado ni changamoto, wananchi wanaendelea kutegemea zaidi habari kutoka kwa wanasiasa kupitia majukwaa mbalimbali, magazeti, na vyombo vingine vya habari ambavyo baadhi huwa vinapotosha jamii kwa kutokuueleza ukweli ama kwa kutokujua au kwa maslahi binafsi. 

b) Mfumo muafaka wa utekelezaji au utendaji wa mambo ya Muungano kwa kuzingatia mahitaji mapya ya kiuchumi, kijamii na kisiasa; na 

c) Masuala ya sheria zinazokinzana baina ya pande mbili za Muungano na hivyo kukwamisha utekelezaji wa baadhi ya masuala ya Muungano.

4.0 HITIMISHO
Dhamira ya Ofisi ya Makamu wa Rais ni kuhakikisha kuwa Serikali zetu mbili ni zinashirikiana katika kuondoa mambo yote yanayoleta vikwazo kwa kuhakikisha yanatatuliwa ipasavyo ili Muungano uendelee kuwa imara na uwe na faida kwa wananchi wa pande zote mbili. Pia, Serikali zitaendelea kuhakikisha kwamba Nchi inaendelea kuwa yenye Umoja, Amani, Utulivu na Usalama ili Muungano wetu uendelee kudumu na kuimarika kwa faida yetu na vizazi vijavyo. 

Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments