KUMPA JAJI WARIOBA DAKIKA 60 ILI AWASILISHE RASIMU YA KATIBA NI JAMBO LISILO HAKI, NI KINYUME KABISA NA KANUNI ZA BUNGE TULIZOPITISHA NA NI KULIBURUZA BUNGE MAALUM LA KATIBA
Kanuni ya 47(a) ya bunge maalum la katiba inaeleza kuwa "Mwenyekiti(wa bunge maalum la katiba) baada ya kushauriana na Mwenyekiti wa Tume(ya mabadiliko ya katiba) watapanga muda unaofaa kwa ajili ya Mwenyekiti wa Tume(ya mabadiliko ya katiba) kuwasilisha Rasimu ya Katiba katika Bunge Maalum"
Jambo la ajabu ni kuwa, jana jumamosi, mhe. Samweli Sitta(namheshimu sana) ametangaza kuwa, siku ya kesho jumatatu jioni Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ATAWASILISHA RASIMU KWA MUDA USIOZIDI DAKIKA 60.
Taarifa za uhakika tulizonazo ni kuwa, mwenyekiti wetu wa Bunge Maalum(Mhe. Samwel Sitta) hajawasiliana na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ili kupanga muda kama kanuni inavyoelekeza.
Ikumbukwe kuwa, tume ya mabadiliko ya katiba imefanya kazi kubwa sana kwa miezi zaidi ya 20. Kazi hiyo inahitimishwa kesho jumatatu tarehe 17 Machi 2014 saa 10.00 jioni ambapo Jaji Joseph Sinde Warioba ataiwasilisha rasimu na kuielezea ndani ya bunge maalum.
Ikiwa Jaji Warioba anapewa dakika 60 tu kuelezea kwa kina rasimu SURA 17, IBARA 271 na KURASA 148. Jambo hili haliwezekani na halikubaliki hata kidogo. Kwa maoni yangu, Kazi iliyofanywa na tume ya mabadiliko ya katiba kwa miezi 20 haiwezi kuwasilishwa bungeni kwa dakika 60 au saa moja.
Bunge maalum la katiba limetumia wiki tatu kutengeneza kanuni, linatumia siku 3 kwa wajumbe kuapa, ETI BUNGE HILO HILO HALINA SAA 5 au DKK 300 kwa ajili ya KUMSIKILIZA JAJI WARIOBA! Binafsi napata wasiwasi mkubwa sana ikiwa tutakwenda mbele namna hii.
Nchi ya Ghana ilipokuwa katika hatua hii, bunge lao la katiba lilitenga siku mbili (2) kwa ajili ya kuisikiliza tume ya katiba ikiwasilisha rasimu ya katiba, sie hatuna hata siku moja kwa ajili hiyo? Mungu wangu, nchi hii tuna matatizo gani?
Mhe. Samwel Sitta ameaminiwa na wajumbe wengi wa Bunge Maalum nikiwemo mimi, na nadhani watanzania wengi wana imani naye katika kusimamia suala hili, ASIANZE KUJISAHAU NA KUFANYA VITENDO AMBAVYO VITAFANYA TUTILIE MASHAKA NIA YAKE.
Kiongozi mzuri ni yule anayetenda kulingana na makubaliano na anayetenda kwa nia safi ambayo inaaminiwa na anawaongoza kuwa nia hiyo kweli ni safi.
Hoja kubwa aliyoitumia katika kufanya uamuzi huo ni kwamba, KWA TARATIBU ZA MABUNGE, HOJA YOYOTE HUWASILISHWA TU BILA UFAFANUZI. Mimi sikubaliani na mtizamo huu. Najua anarejea utamaduni na utaratibu wa mabunge ya kawaida ya kupitisha sera, sheria, bajeti n.k. Na huwa tunaona mawaziri wanavyoweka hoja zao mezani bila ufafanuzi mkubwa kisha hujadiliwa.
Utaratibu wa mabunge ya kawaida ni tofauti kabisa na bunge maalum la kujadili na kurekebisha na kupitisha katiba. Bunge lolote la katiba linahitaji muda wa kutosha kuisikiliza tume iliyoandaa rasimu ya katiba, kwa sababu uwasilishaji wa rasimu ya katiba ni mpana kuliko kuwasilisha hoja ya bunge la kawaida.
Nasema tena, jambo hili halikubaliki na litatufanya tuanze kutoaminiana mapema sana. Nadhani tume ya jaji Warioba inastahili muda wa zaidi ya saa 4 au walau nusu siku, ili kuwasilisha ufafanuzi wa rasimu husika.
Wabunge wengi wa CCM wana hofu kubwa na Jaji Warioba, na kuna baadhi yao hadi wanasema ingewezekana ni bora angeileta tu bungeni na kuikabidhi kisha akaondoka zake(wanasema waziwazi). Hofu hii inatokana na mapendekezo mengi mazuri ambayo wanadhani yataathiri MITIZAMO YA CCM.
Ushauri wangu wa BURE kwa wajumbe kutoka CCM ni kwamba, KATAA NENO USIKATAE WITO. Ni muhimu wakawa wavumilivu na kumsikiliza Jaji Warioba kwa muda wa kutosha na kisha baada ya hapo wajipange kutimiza azma yao ya kupinga mapendekezo ya tume ya jaji huyu. Ni vema Jaji Warioba asikilizwe ana wito gani, kwa ufasaha mkubwa, kisha kama CCM wanaweza wakatae anayosema, hakuna haja ya KUMTENGEA SAA MOJA ILI AKOSE MUDA WA KUTOSHA KUONGEA na wajumbe wa bunge maalum na watanzania wote kwa ujumla.
Mzee wangu Samwel Sitta asijiamini sana katika uamuzi huu, asianze kuburuzwa na Machungu ya CCM dhidi ya WARIOBA na TUME yake, asikubali KUBURUZWA wala KUTUMIKA kwani atawavunja moyo wananchi na wajumbe wengi wenye nia njema.
Ni vema kabisa na kwa nia njema jambo hili likatizamwa upya, binafsi nimelifikisha rasmi kwa uongozi wa bunge.
Na nimeona pia nishirikiane nanyi watanzania wenzangu kulitafakari.
Julius Sunday Mtatiro,
Mjumbe - Bunge Maalum la Katiba.
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments