Ni jambo la ajabu kusikia kwamba wajumbe wa bunge la katiba wanalalamika kuhusu kiwango cha Tsh 300,000 watakazolipwa kama posho ya kujikimu kwa siku huku wakijua kwamba kuna watanzania wenzao ambao hulipwa Tsh 150,000 kwa mwezi na hawajawahi kulalamika, kunung'unika wala kuandamana! Kuna mtu ana familia ya watoto kadhaa, anasomesha na kuwasaidia ndugu zake kwa kila hali lakini analipwa mshahara mdogo kama huu KWA MWEZI lakini leo hii mjumbe mmoja wa bunge la katiba eti analalamika kwamba hicho kiasi hakimtoshi kujikimu KWA SIKU!
Huu ni ubinafsi uliopindukia na haukubaliki hata kidogo. Kisingizio kwamba gharama za maisha zimepanda hakina mantiki yoyote kwani maisha hayo hayajapanda kwa baadhi ya watu tu bali yamepanda kwa kila mtanzania. Sote tunabanana hapa hapa na tunapata mahitaji yanayofanana. Sasa itakuwaje huo ughali wa maisha uonekane kwa wateule wachache tu lakini ushindwe kuonekana kwa raia wengine? Au ndio tuseme kwamba wajumbe wa bunge la katiba wao ni broiler (wanaohitaji matunzo bora) na kwamba raia wa kawaida akina sisi 'pangu-pakavu' ni kuku wa kienyeji (hatustahili matunzo bora)? Hili halikubaliki hata kidogo.
Kama kuna mjumbe wa bunge la katiba anayedhani kwamba ameenda Dododma kuchuma pesa, ni afadhali afungashe virago vyake arudi alikotoka na nafasi yake ichukuliwe na sisi kina 'baba kabwela' kuliko kuendelea kutiana hasara isiyokuwa na mpango. Ndiyo. Tunatiana hasara, ebo! Kwani hizo pesa ambazo hao walafi wanataka waongezwe si ni kodi zetu wananchi? Wanataka kututia hasara ati! Kama vipi ipitishwe kura kuwatafuta wale wasioweza kuishi Dodoma kwa kiasi hicho cha fedha ili wajiengue mapema twende tukachukue nafasi zao sawia.
Hili ni tusi kubwa sana kwa wafanyakazi wa umma wanaolipwa Tsh 150,000 kwa mwezi na hawajawahi kulalamika mahali popote. Ikiwa serikali itasukumwa na ushabiki wa kisiasa na kuamua kuwaongeza posho hao walafi itakuwa sio ishara nzuri kwa wafanyakazi wa umma wanaolipwa mishahara midogo. Na ni bahati mbaya kwamba wajumbe wanaoshobokea sana nyongeza ya posho ni wale wa CCM! Kwani hawa wao wana matumbo mapana kiasi gani hadi watake kulipwa mamilioni ya posho au kwa vile wao walishazoea kula pesa ndefu za ufisadi hadi hizo posho za Tsh 300,000 wanaziona kama ni 'vijisenti'?
Kitendo cha wajumbe wa CCM kuendelea kudai nyongeza ya posho kinadhihirisha kwamba ni kweli watu hawa ni mafisadi wa kutupwa kwani walishazoea kujichotea mapesa ya umma huku wakiwaacha wananchi wakifa kwa njaa na kuambulia huduma duni za afya, elimu, maji, umeme na kadhalika. Ndiyo. Huu ni ushahidi wa kutosha kutuonyesha ni jinsi gani matumbo ya hawa jamaa yalivyotanuka hadi yasijazwe na posho ya Tsh 300,000 kwa siku!
Nawaomba wananchi wenzangu tunaoteseka na ugumu wa maisha tuingie barabarani endapo CCM na serikali yake wataamua kujiongezea posho za kujikimu bila kujali hali ngumu ya maisha na kiuchumi tuliyokuwa nayo. Kila siku tunadanganya kwamba serikali haina fedha kumbe kuna fedha lukuki zimefichwa kusikojulikana zikisubiri kugawanwa kiulafi miongoni mwa wajumbe wa bunge la katiba? Shime wananchi tusiukubali unyonyaji huu unaopigiwa upatu na chama cha kifisadi kwa gharama ya maisha duni kwa kila mtanzania! Saaa ya ukombozi ni sasa. Tukae mkao wa kuingia barabarani pindi serikali ya CCM itakapoidhinisha haya malipo ya kishetani.
0 Comments