[wanabidii] UCHAGUZI UJAO TUCHAGUE MTU BADALA YA CHAMA, SUMAYE WAMUONAJE?

Friday, January 31, 2014

Naona joto la urais la uchaguzi wa urais 2015, limezidi kupanda kuliko hata nilivyotarajia, huenda hii ni kwasababu ndani ya CCM kutakuwa na zoezi la kumtafuta mrithi wa Kikwete tafauti na ilivyokuwa 2010 ambapo Kikwete alipitishwa tu. Pamoja na hayo, hivi uchaguzi ujao tuchague rais tukiongozwa na hisia cha uchama au za mgombea?

 

Vyama vyetu vyote vya siasa nchini vinafanana kimfumo, ingawa kisera vinatafaautiana. Kutokana na kufanana huko kimfumo, tukija kwenye suala la kuchagua rais wa nchi ni bora tukaangalia mtu badala ya kuangalia chama.

 

Kuchagua chama ni sawa na mtu aliyeambiwa achague kati ya Lila na Fila, au kati ya Coca Cola na Pespsi Cola; vinywaji ambavyo vimetokona malighafi moja. Ila waweza kuamua kumchagua mzalishaji badala ya kuchagua bidhaa husika sanjari na kumtaka atoke tafauti japo kidogo ingawa kimsingi hatoweza kutoka nje ya mfumo kabisa.

 

Kama kuna haja ya kuchagua chama[kwa vyovyote vile ipo], basi chama chenye utafauti wa kimfumo na CCM ndicho ambacho chapaswa kuchaguliwa. Itambulike, tunaweza kusema tumeitoa CCM madarakani si kwa kuingiza chama chenye jina tafauti na CCM bali kwa kuingiza chama chenye mfumo tafauti na CCM, kipo?

 

Huku nikizingatia hoja yangu hii, tuitoe CCM madarakani kwa kuzingatia moja kati ya mambo mawili. Mosi, aidha kitokee chama tafauti na CCM kitakacho weka mgombea bora wa urais kuliko mgombea wa CCM au kitokee chama ambacho kimejitafautisha na CCM kimfumo, tafauti hizo zionekane dhahiri kwenye katiba yake.

 

Kwa kuligundua hilo, ndio maana mimi binafsi nikija katika suala la uchaguzi wa rais wa nchi nimeamua kuwaacha wanachama na mashabiki wenzangu wa vyama vya siasa wachague mavi ya panya kwenye mchele, na mimi nitaendelea kuchochea kuni mbichi ili sima yangu ipate kuiva. Kwani sasa imeshakuwa dhahiri vyama vyetu vyote vimekuwa mithili ya moshi machoni au siki menoni au mlio wa miiba chini ya sufuria.

 

Uchaguzi ujao ni vema tuchague mtu badala ya chama. Kwa maoni yangu, kwa waliotangaza nia wote, na kama Sumaye ni mmoja wao, basi kati ya hao wote Sumaye ni mbora wao. Kama wagombea watabaki hawahawa waliotangaza nia, na kikitokea chama kilicho tafautiana na CCM kimfumo basi ubora wa Sumaye hauta fua dafu kwa chama hicho.

 

Dunia ndio hino hino, ambayo tangu kuumbwa kwake hakuna mja aliyeishi juu yake aliyefanikiwa kujitenga na siasa. Katika maisha ya mwanasiasa kila afanyacho lazima kilenge kuathiri maamuzi ya umma kwa maslahi ya huo umma na si kwa maslahi yake na chama chake.

 

Dhana hii yahitaji akili kubwa kuifahamu na ni njia ambayo yahitaji uthubutu na ujasiri hata uweze kuziruhusu nyayo ziikanyage, kinyume chake utashindwa kujitafautisha na mwomba chumvi. Mwomba chumvi aghalabu huombea chungu chake na si cha jirani yake. Hii ni falsafa kubwa, ipo siku nikipata wasaa nitaifafanua INSHALLAH!

 

TANBIHI:  

Kwa kuchelea kurefusha makala haya na nisitoke nje ya mada, sikusema kwanini Sumaye ni bora kuliko hawa waliojitokeza sasa, ila nataraji katika uchangiaji wa mjadala huu tutaujua ubora na upungufu wa Sumaye. Tujadili sasa. Mungu Ibariki Tanzania.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments