Napenda kuchukua nafasi hii adhimu kukipongeza Chama changu Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)—chama makini, chama imara na Chama Tawala 2015—kwa maamuzi sahihi waliyochukua kuwavua nyadhifa baadhi ya wanachama waliothibitika kuwa nyuma ya waraka wa kukichafua na kukivuruga chama. Haya ndiyo maamuzi sahihi (sio magumu kama CCM wanavyoyaita) yanayopaswa kuigwa na vyama vingine vinavyokumbatia wanachama wakorofi wanaovuruga na kuharibu taswira ya vyama vyao.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilisitisha harakati zake za kuvuana magamba kwa sababu ya kuwagwaya na kuwalinda mafisadi ndani ya chama. Matokeo yake chama chao kimepoteza mwelekeo na mvuto kwa umma wa watanzania. Haya ndiyo madhara ya kuwabeba mafisadi na wasaliti ndani ya CCM. Bwana Nape alitembea nchi nzima akiwananga, kuwatukana na kutishia kuwavua uanachama mapacha watatu (Rostam, Chenge na Lowasa) lakini mwisho wa siku alisitisha zoezi zima na kuwaacha hao virusi waendelee kukivuruga chama, ijapokuwa mmoja wao alizidiwa nguvu na kuamua kuachia ngazi. Lakini bado hili limebaki kuwa doa sugu ndani ya CCM—kulindana na kuogopana kwa kisingizio cha kutokimegua chama kwa kujenga makundi kinzani yenye wafuasi walio na nguvu za kifedha na kifisadi.
CHADEMA hatuogopi kuchukua maamuzi sahihi kuwaadhibu wanachama wowote watakaoonekana kwenda kinyume na Katiba ya chama hata kama wangekuwa na vyeo au nguvu kiasi gani ndani ya chama. Chadema ni chama kinachofuata haki katika kufanya maamuzi kwani wanachama hupewa nafasi ya kusikilizwa kabla ya kuadhibiwa zaidi. Ndio maana chama kimetoa siku 14 kwa wahusika kujitetea kwani wasifukuzwe uanachama kwa makosa waliyoyatenda. Hii ni tofauti na CCM waliotembea Tanzania nzima wakiwatukana mapacha watatu lakini mwishowe wakashindwa kuchukua hatua stahiki kuwaadhibu kwa makosa waliyotenda.
Chama makini, CHADEMA, hakichukui hatua kwa kukurupuka (kama wafanyavyo CCM) kabla ya kuchekecha na kupembua kiyakinifu tuhuma za wahusika ili kuepuka kuchukua maamuzi yasiyotenda haki kwa watuhumiwa. Na tofauti na CCM, CHADEMA haitembei nchi nzima ikiwatukana, kuwananga na kuwadhalilisha wanachama wake wenye makosa bali hufuata taratibu na kanuni za chama katika kutoa maamuzi. Pia naomba ieleweke kwamba wanachama waliopatikana na hatia hawachaadhibiwa na Mbowe, Dr Slaa, Lema, Mnyika au mtu yeyote yule ndani ya chama (kama CCM wanavyotaka kuuaminisha umma wa watanzania) isipokuwa wameadhibiwa na Kamati Kuu—chombo huru kisichomuonea mtu wala kuegemea upande wowote—bali kinachoegemea zaidi katika ushahidi wa tuhuma halisi (sio bandia) na zilizothibitishswa kuhusu mwanachama yeyote yule ndani ya chama. Haya ndiyo yanaitwa maamuzi sahihi.
Natoa wito kwa wahusika kujitetea kwa ukamilifu, bila jazba yoyote, juu ya makosa yanayowakabili na ikibidi wakubali na kutubu na kuahidi kutorudia tena kukisaliti chama na bila kupokea ushauri wowote wa giza (hasa utakaotolewa na upande wa pili—CCM). Lengo la maamuzi yaliyochukuliwa si kumkomoa mtu yoyote isipokuwa ni katika kukiweka chama katika mstari ulionyooka na bila kuyumbushwa na nguvu zozote (halisi au za bandia) kutoka ndani au nje ya chama. Ndio maana imetolewa nafasi kwa wahusika kutoa utetezi wao yakinifu juu ya adhabu iliyotolewa kwao na kwanini wasiadhibiwe zaidi. Hivyo basi, tunatarajia kwamba wahusika watajieleza kwa ufasaha na hatimaye kurejea kukitumikia chama kwa moyo mkujufu na bila kinyongo chochote.
Nawasilisha.
0 Comments