[wanabidii] Ujasiriamali ni ajira kamili

Tuesday, September 24, 2013
Imeandikwa na Albert Sanga, Iringa.

Nikiwa muhula wa mwisho kumalizia masomo ya shahada yangu ya kwanza, siku moja niliingia katika mjadala mzito sana na mama yangu mzazi. Mama yangu alikuwa akishusha pumzi kuona kuwa mwanae sasa ninaelekea kukamilisha ngwe ya elimu ya juu. Mawazo na kiu yake kubwa ilikuwa ni kuona natafuta ajira mapema kitu ambacho mimi nilitofautiana nae na hivyo kuzusha malumbano ya kihoja na kimtazamo.

Wakati mama yangu akiamini mafanikio kupitia kuajiriwa, mimi niliamini (na ndivyo ninavyoamini na kuiishi imani hiyo) kuwa ukombozi wa kweli wa kiuchumi na kifedha (real financial freedom) utakuja kwa kuanza kujiajiri na hatimaye kuwa mwajiri wa wengine katika biashara ama shughuli zangu mwenyewe.

Haikuwa kazi rahisi kuubadilisha mtazamo wa mama yangu. Hivyo nililazimika kutumia ushawishi wa hali ya juu sana na mifano hai. Kwa bahati nzuri nilikuwa nikibishana nae nikiwa tayari nimeshapata kufanya ujasiriamali na yeye alikua shuhuda wa namna nilivyofanikiwa
na baadae kufilisika kabla ya kuanza upya tena.

Hili tukio la kufilisika ndilo lililokuwa linampa 'presha' mama yangu, kwa sababu alinihoji, maswali mengi  "Mwanangu,
 biashara ni kama kubahatisha, hivi kweli na elimu yako hii unataka kuendelea kujiajiri? Je, itakuwaje ukifilisika tena? Huoni kama utakuwa mtu wa kubahatisha licha ya kuwa ni msomi? Kwa nini usitafute ajira ili uwe na uhakika na mshahara wako kila mwezi?"

Bahati mbaya mimi nina ndugu na jamaa wengi ambao wanaamini mno katika mfumo wa kuajiriwa (huenda watanzania wote wako hivyo!). Nikiwa nimepangua (kwa ushindi) mjadala huo na mama nikakutana na ndugu yangu mwingine ambaye alinishangaa kuona nimebadili kutoka masomo ya sayansi kwenda kusoma masomo ya biashara. Kidato cha tano na sita nilisoma masomo ya sayansi (Kemia, Baiolojia na Fizikia) lakini ngazi ya chuo kikuu, niliukana udaktari na kugeukia masomo ya biashara.

Yeye (ndugu yangu) alinipa kauli ifuatayo ambayo hadi leo huwa ninaihesabu kuwa ni ya kitumwa, "Umeacha fani ya sayansi umekimbilia fani ya biashara, utapata shida sana. Fani za biashara siku hizi hazina ajira, wanaozisomea ni wengi mno. Ungebaki sayansi ungekuwa na uhakika wa ajira yako bila shida".

Niliamua 'kumpotezea' kwa sababu mawazo yake na yangu niliona ni kama mbingu zilivyo mbali na nchi. Anawaza niajiriwe wakati mimi ninaumiza kichwa jinsi ya kuwapata wafanyakazi bora niwaajiri!

Fikra hizi za kusomesha watoto ama kusoma ili kuajiriwa ndizo zilizojaa katika fahamu za watanzania wengi. Kwa bahati mbaya sana, kutokana na mabadiliko ya mifumo ya kisiasa na mabadiliko ya uchumi wa dunia; matumaini ya kila anayehitimu masomo yake kuajiriwa yanazidi kuyeyuka siku hadi siku. Hapa nchini Tanzania hadi sasa, kuna nafasi chache sana za ajira ikilinganishwa na idadi ya wasomi inayotapishwa na rundo la vyuo vikuu na vile vya kati.

Ukiacha hilo la ajira kuwa chache, bado kuna changamoto kwa wale wanaobahatika kuajiriwa. Changamoto hiini kutotosheleza kwa mishahara (na marupurupu?) inayotolewa ikilinganishwa na hali ya maisha pamoja na malengo anayokuwa nayo mwajiriwa.

Tena lipo jambo linalozidisha mbinyona misongo miongoni mwa wasomi wetu kutokana na imani ambazo huwa nazo kuhusu maisha. Wengi wawapo masomoni huwa na ndoto za mchana za kuajiriwa leo na kutajirika kesho! Wanapoingia makazini na kukutana na uhalisia kuwa mambo sio rahisi kama wanavyodhani, hapo ndipo huwa kinaanza kizaa, zaa! Udokozi, wizi
na ufisadi huanzia hapa. (Japo kuna kazi hazina cha kuiba!)

Kwa hiyo wanaoajiriwa na wale wanaokosa ajira, wasomi na wasio soma; wote wanajikuta katika changamoto moja kubwa, 'msongo wa maisha'. Kwa maana hii mtu apende ama sipende analazimika kufikiria kiutofauti ilikujiokoa. Suluhisho kubwa kwa changamoto hizi ni ujasiriamali.

Na hii ni dhahiri kwa sababu, mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa yanasababisha matatizo na matatizo siku zote ni fursa. Uhai waujasiriamali unategemea uwepo wa fursa. Ni bahati ilioje kuwa dunia ya leo (ikiwemo Tanzania) imekuwa na fursa nyingi sana za kiuchumi na kibiashara kuliko wakati mwingine wowote tangu kuasisiwa kwa taifa hili. Ni suala la kujizoeza kufikiri na kuona tofauti na wengine.

Hivyo basi utagundua kuwa suala la kusoma ama kusomesha  huku kukiwa na mawazo kuajiriwa ni sawa na kujiandalia utumwa. Hali iliyopo sasa haimtambui mtu aliyeshikilia vyeti vyenye maksi nyingi, ila mazingira yatambeba yule tu mwenye uwezo wa kupambana na kutatua changamoto za maisha zinazomzunguka (bila kujali elimu yake). 

Tanzania ya leo ni lazima tuanze kujiokoa na kuokoa kizazi kijacho, tujenge mazoea ya kutengeneza ajira badala ya kulalamika kila kukicha kuhusu ukosefu wa ajira. Kama nilivyosema awali, ujasiriamali ndio eneo pekee linaloweza kutoa mamilioni ya ajira pamoja na kuwapa watu wengi uhuru wa kweli wa kiuchumi na kifedha. Kwa nini kuwepo na fikra hasi kuona kuwa ujasiriamali sio ajira kamili wakati ujasiriamali unaweza kuwapa watu uhuru wa kweli wa kiuchumi na kimaisha?

Dhana ya ujasiriamali kuchukuliwa, 'poa' kumechangiwa na mwenendo na utamaduni wa makundi kadhaa katika jamii nyingi. Kundi mojawapo nihili la baadhi ya wafanyakazi wa kuajiriwa ambao wamekuwa na vimiradi vidogo vidogo vya ujasiriamali. Lengo lao kubwa huwa ni kupata faida fulani ambayo itasaidia kukabiliana na kutotosheleza kwa mishahara
yao. Kwao hawa ujasiriamali sio kazi ambayo inaweza kusimama peke yake na kumpa mtu uhuru wa kiuchumi na kimaisha.

Kundi hilo lina madhara makubwa kwa taifa kwa sasa na wakati ujao. Hebu chukulia watoto wa mfanyakazi ambaye anaendesha vijimradi vya kijasiriamali eidha kwa kuajiri watu ama baada ya kutoka kazini kwake ili kukabiliana na mshahara usiotosheleza. Picha inayojengeka katika fikra za watoto wake ni kuona kuwa ujasiriamali ni harakati za 'kuganga njaa'.  Watoto hawa wanapokua moja kwa moja hawatakuwa na imani na ujasiriamali hata kidogo.

Lakini ninaomba kuwatambua wafanyakazi ambao hufanya ujasiriamali wakiwa 'serious'. Kikawaida hawa huwa na malengo ya kufikisha mtaji ama hatua fulani kabla ya kuachana na ajira na baadae kuwa mabosi katika shughuli zao wenyewe. Hata inapotokea wameendelea kufanya kazi (walikoajiriwa) ni kwa sababu wanapenda na kufurahia kufanya kazi hizo
na sio kwa ajili ya uhitaji wa fedha (they are doing for funny).

Wengine wanaopanda mbegu hasi za ujasiriamali kutoaminika niwajasiriamali ambao licha ya kwamba wanafanya biashara na ujasiriamali kwa mafanikio makubwa lakini wanashawishi familia, watoto na jamii zao kuamini kuwa ujasiriamali na biashara sio kazi za kufanya. Hawa utawasikia wakiwaambia watoto wao kauli kama hizi; "Usiangalie mali za mimi baba yako, urithi pekee ninaokupa wewe ni kukusomesha ili uje uwe na kazi yako". Kauli hii kwa haraka haraka inaonekana ni yenye busara kubwa lakini kutokana na mabadiliko yanayotokea sasa duniani, hii  ni imani ya kufisha. Siku huyu motto akikosa ajira, utamkuta ameshika bango na anaandamana barabarani kudai ajira (sijui nani atakuwa akidaiwa hiyo ajira)!

Kwa upande mwingine wajasiriamali wenyewe kuna kauli ambazo huwa tunazitumia ambazo zinatuondolea heshima mbele ya fikra za jamii nakutujazia hisia hasi. Hebu fuatilia tofauti ya mfanyakazi wa kuajiriwa na mjasiriamali kauli wanazotoa kabla ya kuondoka asubuhi kuelekea katika mishughuliko.

Mfanyakazi ambaye huenda analipwa mshahara wa chini ya laki tano kwa mwezi anaaga kwa kusema, "Ninaenda kazini, tutaonana jioni". Lakini mjasiriamali ambaye anauhakika wa kuzalisha wastani wa faida ya shilingi milioni mbili kwa mwezi anaaga kwa kusema hivi; "Ninaelekea kuhangaika, ninaenda kuchakarika, tutaoanana jioni!"

Kabla hujaingia katika kufanya biashara zako tayari umeutangazia ubongo wako kuwa kuna mahangaiko siku hiyo! Ndio maana si ajabu kuona kuwa wafanyabiashara wengi licha ya kuwa wanatengeneza mamilioni ya faida kwa mwezi zaidi ya wafanyakazi wa kuajiriwa; lakini bado hawajiamini ukilinganisha na wafanyakazi wa kuajiriwa.

Binafsi katika ujasiriamali nimeizoeza akili yangu kujitambua kuwa mimi ndiye bosi hata kama niwe katika biashara yenye mtaji mdogo kiasi gani. "I'm my own boss". Shida ya wajasiriamali wengi huwa hawathamini hata maeneo wanayofanyia kazi. Kama ni dukani, ni vema ukaweka hata meza fulani ya kisasa na kiti cha 'kujiachia' ili akili yako inavyoingia kazini iwe inapata uhuru wa kifikra na kufurahia mazingira ya biashara.

Unapojitambulisha kwa watu usijitambulishe kinyonge, ongea kwa kujiamini, 'Mimi ni Mkurugenzi wa Massawe Kiosk' ama 'Mimi ndiye mmiliki wa magari yaendayo sehemu fulani' au 'Naitwa Albert Sanga, mmiliki na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Anesa Company Limited,' badala ya kujiweka mnyonge na kusema, 'Naitwa Albert Sanga, nahangaika hangaika na biashara hizi na zile'. Kwa hivi utakuwa na fikra zinazojiamini.

Wajasiriamali tunawajibika kujitoa asilimia zote kufanya biashara pasipo mang'ununiko. Haina tija kuwa katika  ujasiriamali huku tukitamani tena kuajiriwa. Unapochukua hatua ya kuufurahia ujasiriamali uufanyao ndipo utakapogundua kuwa ujasiriamali ni ajira kamili na kazi pekee inayoweza kukupa fedha za kutosha na muda wa kutosha kufurahia maisha.

0719 127 901, stepwiseexpert@gmail.com

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Related Posts

0 Comments