[wanabidii] Magazeti ya “Mwananchi”, “Nipashe” yajishusha hadhi, yadhalilisha Watanzania

Sunday, September 15, 2013
BARAZA LA WALALAHOI

Magazeti ya "Mwananchi" na "Nipashe" yamejishusha hadhi, yametudhalilisha Watanzania

  • Yatuombe radhi mara moja, tena ukurasa wa kwanza
  • La sivyo tuna haki ya kwenda Mahakamani kudai fidia

Na Paul Francis Mongi | Mwenyekiti wa Baraza la Walalahoi

ILANI YA MWANDISHI: Makala haya, kabla ya kufika hapa, yalipelekwa kwenye gazeti moja la kila siku – ikiwa ni mpango yachapishwe kwenye toleo la Jumapili ya 22 Agosti 2013. Mwandishi alimtuma swahiba yake, ambaye ni mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ichapishayo gazeti hilo, kumpelekea Mhariri Mkuu, kutokana na "uzito" wa makala haya. Mhariri huyo alimjibu swahiba huyo wa mwandishi kwamba "Kaka ni maoni mazito ambayo tukiyatoa yanaweza kuvunja uhusiano wetu". Mhariri huyo alitoa msimamo huo kutokana na tamko la pamoja la Jukwaa la Wahariri Tanzania (Tanzania Editor's Forum – TEF), kwamba, iwapo kutatokea upotofu/uvunjifu wa maadili na 
weledi katika tasnia ya Uandishi wa Habari, kwa mfano, gazeti kuandika habari zinazopotosha jamii kwa kutokuwa na weledi wala kuzingatia miiko ya tasnia, basi, mhariri yeyote yule ahakikishe kwamba upotofu/uvunjifu huo wa maadili, kwa kushirikiana na wahariri wenzake, unapata suluhu kwa "ndani" bila ya kuandika habari au kuchapisha makala ambayo itaonekana kulikosoa na/au kuliumbua gazeti linaloshtakiwa kwa upotofu/uvunjifu huo wa maadili, iwapo, (a) kuna makala ambayo itakuwa imeandikwa na mtu yeyote – aliye au asiye mwandishi – na (b) iwapo kutakuwa na malalamiko rasmi kutoka kwa mtu ambaye atakuwa, kwa namna moja au nyingine, mhariri anaweza kuandika taarifa ya kuomba radhi na kuichapisha kwenye ukurasa ambao habari hiyo ilitola, kwa kiwango kile kile cha uzito uliotumika, au (c) kumtaka mlalamikaji kupeleka malalamiko yake kwenye Baraza la Vyombo vya Habari (Tanzania Media Council – MCT), kupata usuluhisho rasmi, kazi ambayo, kisheria, Baraza hilo limepewa. Kitakachoamuliwa MCT ndicho kitakachokuwa msingi wa mlalamikaji kukubali kauli ya MCT au kuuchukua uamuzi huo na kwenda Mahakamani, ambapo sheria itachukua mkondo wake. Utaratibu huu wa TEF uliasisiwa kwa lengo la kupunguza kesi nyingi ambazo ziliviandama vyombo vya habari, ambapo, kwa kuwa hakukuwa na utaratibu huu, aidha, hakukuwapo na Baraza la Vyombo vya Habari, vyombo vingi vya habari vilishtakiwa Mahakamani na kuamriwa kulipa fidia lukuki. Mwandishi wa makala haya, ambayo yalikuwa yaanzishe safu mpya iitwayo "Baraza la Walalahoi", ameamua kuyachapisha makala yake haya kwenye Blog hii, na kuanzisha safu hii mpya, kwenye Blog hii, ili ukweli usiopingika upate kufahamika, kwani, siku hizi, Watanzania wengi walio ndani na nje ya nchi, hutumia muda wao wa kutosha kusoma wavuti mbali mbali, kwa lugha mbali mbali, ikiwa ni mojawapo ya mbinu za kujiendeleza kielimu pamoja na kupata taarifa zinazohabarisha, zinazoelimisha na zinazoburudisha – misingi hii mitatu, kutoa habari, kutoa elimu na kutoa burudani ikiwa ni nguzo muhimu za tasnia ya Uandishi wa Habari. Baada ya Ilani hii ndefu, sasa Mwandishi anakukaribisha ujongee kwenye Baraza la Walalahoi na kupata uhondo huu, ambao, kwa mara ya kwanza kabisa, unatolewa kwenye toleo la Jumapili, Septemba 15, 2013! Karibu ndugu msomaji.

TASNIA ya uandishi wa habari – kwa Kiingereza "journalism" – ni mojawapo ya tasnia tata na tete kuliko nyingi zilizoko kwenye nyanja ya "sanaa". Ni tata na tete kwa kuwa, kosa moja dogo tu, laweza kukisababishia chombo cha habari kesi kubwa ambayo, iwapo mwandishi au mtayarishaji wa makala au kipindi cha redio/runinga angekuwa makini zaidi katika kufanya utafiti, hata ule wa kawaida tu. Tofauti na ilivyokuwa miaka ya 1990, hivi sasa, waandishi wa habari nchini Tanzania wamekosa ari, azma na ashki ya kujituma; kumezuka wimbi la waandishi, pengine hata wahariri – na hili ndugu zangu Charles Misango na Manyerere Jackton wataliunga mkono, kwani wao ni waandishi wakongwe kama mimi – kwamba, kutokana na uvivu wao huo wa kupindukia, msomaji, mara nyingi, hujikuta hatendewi haki kwa kuwa habari zinazochapishwa kwenye magazeti huwa hazina "kina" wala "uwiano" unaotakiwa kimaadili na kiweledi! Hili ni tatizo, tena tatizo kubwa!

Ndugu Walalahoi wenzangu, nikiwakaribisha kwenye makala haya (si makala hii... Kiswahili kigumu!) ya kwanza kabisa, nimeona nisipoteze muda mwingi wa kumung'unya maneno, bali, niende moja kwa moja kwenye ukweli wa mambo jinsi ulivyo. Sitakuwa nimewatendea haki, ninyi "walalahoi" wenzangu – japokuwa mimi ni msomi, lakini bado "mlalahoi" – kwa kuanza kumezameza maneno, huku nikiyamung'unya na kuyatema, pasi na kuhakikisha kwamba yamemeng'enywa ipasavyo kwenye kinywa na ubongo wangu. Lazima ukweli usemwe: "Mwananchi" na "Nipashe", wote kwa pamoja, wamejishushia hadhi na wametudhalilisha sisi Watanzania, kwa hiyo watuombe radhi, tena haraka MNO! Napenda kuwaambia kwamba maoni yangu haya, hayafungamani na maoni ya Mhariri wa gazeti hili, wala uongozi wa kampuni inayomiliki na kulichapisha. Ni maoni yangu binafsi, ambayo kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nina haki ya kuyatoa, pia kuwa na haki ya kukingwa kuzuiwa kuyatoa! Ukiisoma na kuilewa Katiba, japokuwa ina viraka vingi, utaishi kwa amani na utulivu wa kiasi, na hutababaishwa na "makanjanja" au "vihiyo" na watendaji "feki" kwenye taasisi mbali mbali, binafsi na za umma.

Wengi wenu mtaniuliza, kunani tena naanza makala haya ya kwanza kwa kuwashtaki "Mwananchi" na "Nipashe", vyombo vya habari vinavyosadikiwa kuwa vyenye weledi mkubwa katika tasnia hii ya habari? Kaeni kitako, naanza kuwadadavulia.

Mosi, kwa mujibu wa wasomi na wanafalsafa waliobobea kwenye tasnia ya habari, ipo dhana isemayo "Asiyefanya utafiti hana haki ya kusema/kuandika!" ikimaanisha, iwapo mwandishi wa habari hatafanya utafiti wa kina katika jambo analotaka kuliandika, hatakuwa na haki ya kuliandikia, na kwa mujibu huo huo, Mhariri wake naye atawajibika kwa athari zozote zile zitakazotokea, ziwe chanya au hasi.

Kwenye habari iliyochapishwa kwenye gazeti la "Mwananchi" la Jumatatu, Septemba 9, 2013, yenye kichwa cha habari "Meli ya Tanzania yanaswa na tani 30 za bangi Italia", iliyoandikwa na mwandishi wa gazeti hilo, Mwinyi Sadallah, gazeti hilo lilichapisha habari hiyo, ambayo ilidadavuliwa na kutafsiriwa – tena bila kuhakikiwa – kutoka gazeti la "Daily Mail" la Uingereza, kutoka kwenye wavuti wake -www.dailymail.co.uk/news/article-2415052/Drug-smugglers-set-50million-hash-jump-overboard-Mediterranean.html - ambapo, "Daily Mail" likiwa linatumia wavuti wake wa "Mail Online", liliandika habari hiyo Jumamosi, Septemba 7, 2013, mwandishi akiwa Nick Pisa, ikiwa ni siku mbili KABLA ya "Mwananchi" kurudia habari hiyo hiyo, tena bila hata ya kusema imetoka wapi; hapa tunaona makosa mawili, tayari: Kutoandika chanzo cha habari, na kuirudia habari ikiwa imeandikwa kijuu-juu na makosa lukuki.

Kosa la msingi ni kwamba, "Mwananchi" walishindwa kabisa kutafsiri kichwa cha habari cha habari iliyotoka "Mail Online", ambapo kilisema "Bungling drug smugglers set £50million of hash on fire and jumped overboard after being caught by coastguard in the Mediterranean", tafsiri yake ikiwa "Wafanya magendo wa madawa ya kulevya wafanya madudu kwa kuchoma bangi za Paundi Milioni 50 baada ya kukamatwa na askari wa doria wa baharini kwenye bahari ya Mediterraneo". Tafsiri nyepesi sana, lakini kwa ushabiki wao, na ukanjanja uliokubuhu, wakaamua kuandika "Meli ya Tanzania..."

"Mail Online" liliweka vichwa vidogo cha habari kwamba (1) meli ilinaswa na helikopta ya Walinzi wa Baharini wa Italia; (2) meli ilisajiliwa nchini Tanzania, wakati watu tisa walijirusha baharini wakikimbia kukamatwa; na (3) tani 30 za bangi zilipakiwa nchini Uturuki.

Msingi wa habari hii ni kwamba, meli ilinaswa ikiwa njiani kwenye sehemu ya bahari ya nchi ya Malta, ikiwa kwenye eneo la kimataifa la bahari ya Italia, kwa hiyo, baada ya kupata taarifa za kiintelijensia, Walinzi wa Bahari wa Italia (Le Guardia di Finanza), waliifuatilia na kuinasa wakitumia helikopta zao. Kwa kuhofia kukamatwa na Walinzi hao, watu tisa waliokuwa ndani ya meli hiyo walijirusha baharini wakiwakwepa walinzi hao, hata hivyo, ikawa kazi bure kwani walihitaji msaada wa kuokolewa kwa kuwa walikuwa kwenye eneo la bahari lenye kina kirefu! Ili kuficha ushahidi, wafanyabiashara hao wa magendo, wauzaji wa madawa ya kulevya, wakadhani kwamba wangefanikiwa kuzichoma tani zote 30 za bangi, lakini moto huo ulizimwa na meli ya kuzimia moto ya Walinz wa Habari wa Italia, hivyo kuokoa kiasi kikubwa cha bangi hiyo ambayo ingeteketea. Picha za tukio hilo la kusisimua, bado mpaka sasa zinasambaa kama wadudu (virusi) duniani kote kwenye mtandao wa Intaneti.

Cha msingi zaidi, "Mail Online" waliandika ukweli, kwamba meli hiyo – MV Gold Star – ilisajiliwa nchini Tanzania kupitia Zanzibar, ambapo ilipewa bendera ya Tanzania, mnamo mwaka 2011. "Mail Online" hawakuandika kwamba MV Gold Star ni meli ya Tanzania; kuna tofauti kubwa ya kisheria, kati ya usajili na umiliki. Kwa mujibu wa sheria za kimataifa za usajili wa vyombo vinavyotumika kwenye maji, chombo (Marine Vessel – MV) kinaweza kusajiliwa nchi yoyote ile atakayo mmiliki wake, iwapo kitakidhi matakwa ya kisheria ya nchi hiyo, na kupewa bendera ya nchi hiyo, lakini haimaanishi kwamba chombo hicho kinamilikiwa na nchi hiyo. Tafsiri halali ya kisheria, ambayo wahariri wa "Mwananchi" na "Nipashe" wanaweza kushtakiwa kwayo, ni utata unaojitokeza kwa kuandika "Meli ya Tanzania..." ambapo inaashiria kwamba meli hiyo inamilikiwa na Serikali/Nchi ya Tanzania. Tafsiri halali ya "Meli ya Tanzania..." kwa lugha ya Kiingereza ni "Tanzania's ship...". Hata kama wahariri hao wangetumia maneno "Meli ya Kitanzania..." yaani "Tanzanian ship...", bado kungekuwa na utata, kwani, hata kama meli hiyo inamilikiwa na raia wa Tanzania, bado, umiliki huo hauwezi kuifanya meli hiyo kuwa "ya Kitanzania". Kimsingi ni kwamba, "kusajiliwa" kwa meli hiyo huko Zanzibar – ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – ambako ni Tanzania, hakuwezi kukwepa ukweli kwamba, meli hiyo "ilisajiliwa" Tanzania, na kwamba, si mali ya Tanzania.

Huu ndio msingi wa kesi inayosadikiwa kupelekwa kwenye Mahakama Kuu ya Kimataifa ya Kibiashara (Kitengo cha Masuala ya Vyombo vya Maji), kuwashtaki wamiliki wa MV Gold Star kwa kukiuka sheria za kimataifa zinazozuia usafirishaji wa madawa ya kulevya kwenye meli zinazosajiliwa Tanzania.

Ndio, "Mwananchi" walifanya utafiti wao – japokuwa kidogo – kwa kuwapigia simu baadhi ya watendaji nchini Tanzania, kama vile mkurugenzi mkuu wa SUMATRA na msajili wa meli wa Zanzibar, n.k., ili kupata maoni yao kuhusu tukio hili. Hawakufanikiwa kwa kiwango kikubwa kwa kuwa tukio lilikuwa limetokea siku za mwisho wa wiki, ambapo watu wengi wanakuwa hawapo kazini. Badala ya kusubiri hadi habari hiyo "iive" zaidi, "Mwananchi" wakakurupuka kuichapisha wasije kuwa "out-scooped" na magazeti mengine. Inaonekana walipata tetesi kwamba "Nipashe" nao walikuwa na habari hiyo, na, ili wasipitwe na habari hiyo na kuwa wa kwanza kuipeleka sokoni, "Mwananchi" wakakimbia kuchapisha habari ambayo ilikuwa na makosa ya msingi.

Kinachonikwaza – kwa kuwa mimi ni Mwenyekiti wa Baraza la Walalahoi, mwenye haki na wajibu wa kutetea maslahi ya Walahoi wenzangu – na ambacho kinapasa kuwakwaza Walalahoi wenzangu ni kwamba, jina la Tanzania limetumika vibaya, pasi na kuwa na sababu ya msingi, kutokana na "mazoea" ya kuandika habari kishabiki, ili waweze kuuza nakala nyingi. Nilipoitazama habari hiyo kwa mara ya kwanza – kama kawaida yangu, siku yangu huanzia (baada ya sala ya asubuhi) kwa kusoma magazeti yenye wavuti – nililazimika kufanya utafiti kwa kuipata habari hiyo kwenye wavuti wa "Mail Online", kutokana na waraka huo huo uliochapishwa kwenye wavuti wa kijamii wa "Jamii Forums", ambao uliweka kiunganishi cha wavuti huo. Niliisoma kwanza habari ya "Mail Online" na kisha kuisoma kwenye "Mwananchi", na kugundua makosa mengi. "Mwananchi" walidadavua kwa ku-"copy-and-paste" kilichoandikwa "Mail Online" bila hata kuandika chanzo cha habari hiyo, japokuwa waliandika kwamba picha zilitoka kwenye shirika la habari la Reuters. Mwe!

Zanzibar wana kila haki ya kulalamika kwamba meli hiyo SI ya Zanzibar wala Tanzania. Sisi Watanzania, vivyo hivyo, tunayo haki hiyo! Jina la nchi limetumika vibaya: Sasa tunatambuliwa – pengine – kuwa wamiliki wa meli zinazofanya biashara haramu za mihadarati!!!!! Mungu aepushie mbali! Hata meli??? Labda, safari nyingine, baada ya hili kupita, "Mwananchi" na "Nipashe" wataandika "Ndege ya Tanzania..." katika mtazamo ule ule wa kuchakachua lugha maridhawa ya Taifa, Kiswahili??!! 

"Nipashe" waliandika kwa kichwa cha habari hicho hicho, na kuirudia habari hiyo hiyo - japokuwa sikuisoma – kana kwamba wao ni kasuku wa kurudia kila kinachoandikwa kwenye wavuti za nchi za nje!!! Waliona kwamba kwa kuandika "Meli ya Tanzania..." wangeuza nakala nyingi sana; hawakufikiria athari hasi ambazo zingetokea. Je, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiamua kuvichukulia hatua za kisheria vyombo hivyo kwa kuandika habari za kichochezi zilizojaa uongo, wataweka wapi nyuso zao zilizokosa hata chembe ya soni?

Kabla hatujaenda Mahakamani kudai fidia, kwa kutudhalilisha, "Mwananchi" na "Nipashe" tuombeni radhi Watanzania wote, kwa kutumia vibaya jina la nchi yetu hii! Au ninyi "Mwananchi" kwa kuwa ni chombo kinachomilikiwa na kampuni ya Nation Media ya Kenya, basi, mnaona ni sawa kwa kuwa "itasaidia" kuendelea kuharibu sifa nzuri za nchi yetu? Loooo! Ujirani gani huo??? Serikali ya Tanzania, kupitia Ofisi ya Msajili wa Magazeti, inapaswa, sio tu kutoa onyo kali kwa wahariri wa "Mwananchi" na "Nipashe" kwa utovu wao huo wa maadili na weledi, bali pia inapaswa kuwataka wajitetee kwa maandishi na kutoa sababu za kutoadhibiwa kwa mujibu wa sheria, ikiwa ni, kutozwa faini au kufungiwa kuchapisha kwa muda fulani, pamoja na kutoa tamko la ukurasa wa kwanza kuiomba radhi Tanzania na kuwaomba radhi Watanzania. Jambo la kuhusishwa moja kwa moja, kwamba, Tanzania inafanya biashara ya mihadarati kupitia meli zake si jambo la kupuuzia; ni jambo la kufedhehesha, kusikitisha na kudhalilisha. Hivi sasa tunazitambua athari zinazowapata Watanzania wenzetu wawapo safarini kupitia mipaka ya kimataifa – ama kwenye nchi kavu au kwenye viwanja vya ndege – ambapo hupekuliwa hata sehemu ambazo hazifai kupekuliwa, hivyo kudhalilishwa, kutokana na nchi yetu hii kuwa na sifa mbaya juu ya mihadarati. Swali la msingi la kujiuliza hapa ni kwamba: "Je, Wahariri wa "Mwananchi" na "Nipashe" wanataka dunia nzima ielewe kwamba hata Serikali ya Tanzania inafanya biashara hiyo ya mihadarati??!"

Binafsi, kwa upande wangu, kuanzia leo naanza kuhamasisha hapa nyumbani, wasinunue tena magazeti haya mawili – "Mwananchi" na "Nipashe" – na wakinunua NAYACHOMA MOTO! Potelea mbali! Na kampeni hii itakuwa sehemu ya #NyundoCampaignTZ! Mnatuchosha na ukanjanja wenu! Nitasema tu! Nawashauri Watanzania wenzangu kuyasusia magazeti haya ambayo yamekosa weledi na yamevunja maadili ya tasnia ya habari. Huu si uandishi! Huu ni UKANJANJA! UKOMESHWE!

Nitatumia wavuti na mitandao ya kijamii kuwahamasisha Watanzania kuyasusia magazeti haya mawili, na mengine yatakayoonesha upotovu huu wa nidhamu, ili kieleweke kwamba, sisi ndio wanunuzi na wasomaji wa magazeti haya, na sisi ndio wenye haki ya kudai kupata habari sahihi, zisizo na hata chembe ya uongo, zilizokidhi kanuni na sheria zote za tasnia hii ya habari, kwani, kinyume na hapo, waandishi hawa – kama walivyofanya wenzao kule Burundi na Rwanda – wanaweza hata kuchochea vita ya wenyewe kwa wenyewe hapa nchini. Tuliwaona wenzetu wakinyolewa; hatukutayarisha maji kichwani. Lakini sasa, hata huko kunyolewa tusikurubie, kwani wote tunajua madhara ya vita – vita si Mungu! Haina huruma!

--------

P.S.: Baada ya Mwandishi kukataliwa kuchapishwa makala yake haya, amepata habari kwamba meli ya MV Gold Star ni mali ya mfanyabiashara mmoja maarufu sana hapa nchini, ambaye, kwa mujibu wa maadili ya tasnia, jina lake haliwezi kuandikwa kwenye chombo chochote kile cha habari, kutokana na kukosekana nyaraka zinazothibitisha umiliki wake huo wa meli hiyo tata. Kwa mujibu wa kanuni na sheria za uandishi wa habari, Mwandishi au Mhariri hatakuwa na haki ya kuandika habari zenye tuhuma nzito kumhusu mtu yeyote, pasi na kuwa na ushahidi usiopingika mahakamani, ikiwa ni pamoja na nyaraka au matamko yaliyorekodiwa kwenye, ama, hadhira mbali mbali au kutoka kwa mtu mwenye kutoa tuhuma hizo, akiwa amerekodiwa sauti yake au picha jongefu, akitoa matamko yanayothibitisha tuhuma hizo. Hivyo, Mwandishi, kwa masikitiko makubwa, hawezi kuwaambia wasomaji, jina la mmiliki wa meli hiyo ya MV Gold Star, kwa kuwa hana nyaraka yoyote au matamshi yoyote yale yanayothibitisha umiliki wa meli hiyo kwa mfanyabiashara huyo wa Tanzania, ambaye anadaiwa kuwa na asili ya Mashariki ya Kati. Ni hayo tu.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Related Posts

0 Comments