[wanabidii] UNAFIKI, UZANDIKI NA UNDUMILAKUWILI WA CCM

Saturday, August 03, 2013

Chama Cha Mapinduzi, CCM bado kinaonekana kuendeleleza sera yake ya kupinga muundo wa serikali tatu ambao hivi sasa unapendekezwa pia katika rasimu ya Katiba Mpya inayoendelea kutolewa maoni na wananchi kupitia mabaraza mbalimbali ya katiba. Itakumbukwa kwamba hapo awali tume mbili zilizowahi kuundwa kukusanya maoni ya wananchi ilipendekeza uwepo mfumo wa serikali tatu katika Muungano kati ya iliyokuwa Tanganyika na Zanzibar lakini mapendekezo yao hayakutekelezwa.

Rasimu ya Katiba Mpya imezingatia maoni yaliyotolewa na wananchi wa Tanzania ambao ndio wenye maamuzi juu ya hatima ya nchi yao. Tukumbuke kwamba wakati Jaji Warioba anawasilisha Rasimu alisema tume yake imezingatia maoni yaliyotolewa na wananchi kwenye tume ya Jaji Kisanga na Jaji Francis Nyalali. Katika tume zote hizi mbili, WANANCHI waliohojiwa walipendekeza pawepo na serikali 3. Tume ya Nyalali na Jaji Kisanga zilipata maoni kutoka kwa wananchi, ambao ndio waliotaka uwepo wa serikali tatu. Sasa inakuwaje CCM wadai kwamba wanaotaka serikali 3 wana maslahi yao binafsi? Tangu lini maslahi ya wananchi yakawa maslahi binafsi? Wasitake kuupotosha umma kwa maslahi yao binafsi na kwa maslahi ya mafisadi na mchwa wachache waliojaa kwenye chama.

Inasikitisha kwamba CCM wanataka kuwaamulia wananchi aina ya serikali wanayaoitaka wao. Huku ni kusigina demokrasia na ni dharau kubwa kwa wananchi. Siku zote CCM inadhani kwamba wananchi ni mazezeta na kwamba hawawezi kujiamulia mambo yao wenyewe. Sasa ikiwa wananchi ndio wanaotaka serikali tatu, iweje kikundi kidogo cha wanachama wa CCM wajifungie chumbani huko Dodoma na kuazimia kuchakachua maoni ya wananchi? Ni nini wanachokitafuta hapa kama sio kulinda maslahi ya mafisadi, mchwa, wauza unga na mabwanyeye wachache?

Nchi hii ina jumla ya watanzania million 45. Wanachama wote wa CCM hawazidi million 1! Iweje kikundi cha watu million 1 watake kuchakachua maoni ya watanzania million 45? Hii ndiyo demokrasia kweli? CCM wanataka kubaka maoni ya wananchi kwa manufaa ya mafisadi na wauza unga wachache kama walivyozoea kuwatumikia mafisadi huku wakiwaacha wananchi kwenye mataa! Hii haikubaliki hata kidogo. Ifike wakati wananchi waone kwamba CCM haiweki maslahi ya wananchi mbele isipokuwa wanalinda maslahi ya wachumia tumbo wachache ndani ya chama na serikali. Hii maana yake ni kwamba serikali ya CCM haina nia njema na ustawi na mustakabali wa wananchi bali inawatumia kama ngazi ya kutimizia haja zao za kiutawala na kinyonyaji!

Maoni yaliyozaa rasimu ya Katiba hii yalitolewa na wananchi wote bila kujali dini, kabila, kanda, vyama, jinsia au hali zao. Kwa hiyo, sio busara hata kidogo kwa CCM kuwaelekeza wanachama wake wakatae muundo wa serikali 3 wakati ni wanachama hao hao ndio waliohojiwa na kukubali kuwa na muundo wa serikali 3! Kufanya hivyo ni sawa na kuwashikia akili watanzania na kuwaona kama hawakuwa na akili nzuri wakati wanatoa maoni ya kuwa na serikali 3. Na nitawashangaa sana wananchi na wanachama wa CCM watakaokubali kushikiwa akili na kubatilisha maoni yao ya awali ya kuwa na serikali 3.

Tujiulize ni kwa nini tume zote tatu (Tume ya Warioba, Jaji Kisanga na Nyalali) waliamua kukusanya maoni ya wananchi badala ya kuwaachia CCM wawaamulie wananchi kama wanavyotaka. Kama hali ni hiyo basi ni bora tume hizi zisingeundwa na kutumia mamilioni ya walipakodi katika kusaka maoni ya wananchi. Basi tungewaachia CCM (wajuzi wa kila jambo) wajifungie ukumbi wa Chimwaga huko Dodoma watuamulie watanzania aina ya katiba tunayopaswa kuwa nayo—jambo ambalo ni kubaka demokrasia waziwazi.

Enyi wanaCCM/wananchi, akili za kuambiwa changanyeni na za kwenu. Saa ya ukombozi ni sasa. Msikubali kamwe kulamba matapishi yenu wenyewe. Acheni msimamo wenu wa kuwa na serikali 3 ubaki vivyo hivyo. Nina imani kwamba wakati mnatoa maoni yenu mlikuwa watu wazima na mlikuwa na akili timamu. Wapuuzeni hao wanasiasa wanaotaka kuchakachua maoni yenu kwa maslahi ya mafisadi na wachumia tumbo wachache. Wekeni maslahi ya nchi mbele ya maslahi ya chama na mafisadi. Mafisadi huzaliwa na kufa lakini Taifa la Tanzania litadumu milele. Tafakari, chukua hatua!

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments