[wanabidii] WARAKA WA ALPHONCE LUSAKO alias EMEKHA IKHE KWAKO PROF. RWEKAZA MKANDALA

Wednesday, February 27, 2013
WARAKA WA ALPHONCE LUSAKO alias EMEKHA IKHE KWAKO PROF. RWEKAZA
MKANDALA MAKAMU MKUU WA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM.

NI VEMA UNGENIPIGA RISASI NIKAFA NIKAPOTEA DUNIANI KWA UDHALIMU
ULIOSHINIKIZWA KUFANYA JUU YANGU NA WANAFUNZI WENZANGU NDANI YA TAIFA
LANGU.KULIKO KUKUPIGIA MAGOTI NA KUDHARAU UTU WANGU KWA KUKUOMBA
MSAMAHA USIOTOKANA NA DHAMIRA YA MOYO WANGU. HOW LONG FOR THESE
INJUSTICES IN MY COUNTRY….? NOT LONG MR. PROFESSOR.

Pilato anamuhukumu yesu ingawa haoni kosa lake, anawaogopa wayaudi,
anabembeleza urafiki wa kaysari. Ee Yesu usiye na kosa, hata mimi
ningeweza kutenda mema mengi lakini naogopa macho ya wenzangu na
maneno yao. Ee bwana uniimarishe utashi wangu nijitegemee katika
kushika madaraka yangu.

"Nafahamu mnapigania haki zenu za msingi lakini mjini wananisumbua,
hiki chuo si chuo changu, chuo hiki kina wenyewe na wenyewe wako
mjini, wananiambia kuwa nimeshindwa kuongoza chuo kikuu cha Dar es
Salaam na mimi siwezi kukubali kuwa chuo kimenishinda". Ni maneno yako
Prof. Rwekaza Mkandala uliyoyatoa tarehe 14/12/2012, katika ofisi yako
tukiwa na kikao baina ya sisi wanafunzi nane {8}tuliokwisha fukuzwa
UDSM kwa maandamano niliyoyaongoza tarehe 11/11/2011, ya kudai haki za
watoto wa wavuja jasho walionyimwa mikopo ndani ya vyuo vikuu vya umma
nchini, akiwepo Prof. Makenya Maboko na Prof. Yunus
Mgaya.".nilisikitishwa sana na kauli yako ambayo mpaka leo naikumbuka
"chuo hiki kinawenyewe na wenyewe wako mjini".

Mimi binafsi nafahamu kwa dhati ya moyo wangu kuwa chuo hiki ni cha
watanzania na si cha mtu binafsi au genge la wahuni Fulani ambao wako
mjini kama ulivyosema ambao wanaamua kufanya lolote baya wanalolitaka
kulifanya sababu ya madaraka waliyonayo. Tumewapeni madaraka na
mamlaka ya kutuongoza kwa mujibu wa katiba ya nchi yangu na hatujawapa
madaraka hayo kama nyundo ya kuwapigia wavujajasho ndani ya taifa
langu.

Mh. Profesa, nimeona nikusalimu kwa kumbukumbu iliyopo hapo juu na
niendelee na maada iliyonisibu, lakini pia usisahau kuwahabarisha
usalama wa taifa unaofanya nao kazi, maprofesa wengine hata wanaotoka
vyuo vingine ambao walishiriki kufanya maamuzi ya kidikteta ya
kuwafukuza wazalendo wa taifa hili ambao naamini ni maraisi wajao,
mawaziri wajao, wabunge wajao, wakuu wa mikoa na wilaya.nk.. ndani ya
vyuo vyao kwa kushinikizwa na wanasiasa walioko mjini kama ulivyokuwa
ukijitetea machoni petu kinyume na kweli uliyokuwa unaifahamu. Lakini
pia ni vyema ukawataarifu hao binadamu wa mjini waliokuwa
wanakushinikiza kufanya maamuzi ambayo moyo wako haukuridhia,
wataarifu kuwa kijana Yule Yule niliyemtimua UDSM amesema kuwa
"madaraka mliyo nayo sio ndoa ya milele hivyo waitendee haki nchi
yangu, Nguvu ya pesa walizonazo hazina nafasi milele ya kupoteza haki
ya binadamu yoyote Yule kwa sababu Mungu ni taa ya kila mwanadamu. Kwa
kitendo ulichonifanyia na ulichowafanyia wanafunzi wenzangu ambao
mpaka sasa wamepoteza ndoto zao kielimu ndani ya Taifa lao hakita
potea hivi hivi kama unavyofikiri, kwa sababu ni kinyume na katiba ya
nchi yetu ibara ya 11[2,3] inayotoa fursa kwa kila mtanzania kupata
haki yake ya msingi kielimu ndani yataifa lake.

Mh. Profesa, nakumbuka taarifa za upotoshwaji ulizozitoa mbele ya
vyombo vya habari juu yangu na juu ya wanafunzi wenzangu zenye lengo
la makusudi la kuchafua taswira zetu kwa jamii. Ni ukweli kwamba
unamamlaka, unanguvu ya Pesa na unashirikiana na mfumo wa usalama wa
taifa na uongozi uliopo madarakani kuyafanya uliyoyafanya na
unayoendelea kuyafanya. ndio maana uliweza kutumia vyombo vya habari
vibaya lakini utambue kuwa haki ya mtu inacheleweshwa tu haipotei,
hata ningepigwa risasi kwa wakati huo naamini wapo wazalendo
wangesimama kutetea haki yangu nikiwa kaburini. Ni ukweli kwamba
Umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kututenganisha na familia zetu, ndugu na
jamaa, umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuudanganya umma, umefanikiwa pia
kwa kiasi kikubwa, kutoa taarifa za uongo ndani ya mfumo na nje ya
mfumo. lakini hujafanikiwa kitu kimoja cha msingi kunitenga mimi au
sisi na Mwenyezi Mungu.

Mh.profesa, nimeona umekuwa ni profesa mmoja hatari sana ndani ya nchi
yangu uliyekubali kudharau utu na taaluma ya uprofesa ulionao,
uliyekubali kuminya uwezo wako halisi wa kifikra kwa sababu ya
shinikizo la wanasiasa unaodai wako mjini ambao kiuhalisia hawana hata
uprofesa ulionao. Umekubali kuwaabudu mashetani wanaokushinikiza
kufanya zambi za makusudi katika kupoteza ndoto za vijana watokao
katika familia za wavujajasho. umekuwa ni pilato wa enzi za YESU.
Utambue kuwa Vilio vya vijana tuliofukuzwa vyuoni, vilio na
manunguniko ya ndugu, jamaa na wazazi wetu, dua tulizoomba kwa
Mwenyezi Mungu, hakika zimemfikia Mwenyezi Mungu na usubiri majibu
yake wakati wowote tangia sasa. Ni heri vita inayotafuta haki kuliko
kuendelea kuabudu shetani mwenye majina matatu "HOFU, WOGA NA SHAKA".
Ni heri nipigwe risasi katika mapambano haya nikaweka historia ndani
ya taifa langu kuliko nikaacha dhamira yako ya dhati ikanimaliza ndani
ya taifa langu kimya kimya. Lakini pia NI BORA NIKAWA FORM SIX LEAVER
MILELE, MWENYE FIKRA HURU KWA MASLAHI YA WATANZANIA KULIKO NIKAKUBALI
KUUZA NA KUUDHARAU UTU WANGU KWA KUMUOMBA MSAMAHA PROFESA YOYOTE YULE
ANAYEKANDAMIZA HAKI ZA WANYONGE NDANI YA NCHI YANGU.

Mh. Profesa, unalizika Taifa langu kwa kuzika chuo kikuu cha Dar es
Salaam. Mwenendo hasi wa chuo kikuu chochote kile duniani ni muenendo
hasi wa taifa husika. Umekuwa ni profesa kiongozi wa kulizika taifa
langu na hii nikutokana na upeo wa mtazamo wangu. Umehusika kikamilifu
katika harakati za kuzima fikra huru za wanafunzi ndani ya chuo kikuu
cha Dar es salaam, unatumia madaraka yako vibaya kwa kuwafukuza
wanafunzi waliojitambua, wenye uwezo wa kuhoji mambo, kukosoa mambo,
na kushauri mambo kwa mustakabali mwema wa taifa lao. Unamikakati ya
makusudi ya kukiweka chuo kikuu cha Dar es Salaam kiwe genge la
wahuni, genge la walanguzi na kisiwe kisima cha fikra huru "think tank
of our nation" kama mwanzo kilivyokuwa, unamalengo ya dhati ya
kutengeneza Taifa la Mambumbumbu ili watoto zenu na watoto wa viongozi
wenzako walioko madarakani waendelee kulitawala taifa langu milele,
unawafundisha wasomi nidhamu ya uoga, unashirikiana na usalama wa
taifa kuwatisha wasomi wawe ni wasomi wa madesa na si kulisaidia taifa
lao kwa kujadili mustakabali wa taifa lao. Unaendelea kuwa chanzo cha
kuzalisha viongozi mbumbumbu wataoligharimu taifa langu kama wengine
walivyoligharimu taifa hili. Nikueleze ukweli kuwa Ukimya wa chuo
kikuu cha Dar es Salaam na vyuo vingine nchini Unabomu zito
litalolipuka mda wowote tangia sasa. Umewakandamiza kwa mda mrefu,
wasomi wanamatatizo mengi ambayo yanahitaji kutatuliwa kidiplomasia,
kwa sababu unatumia nguvu kubwa kuwanyamazisha hakika watatatua
matatizo yao kwa nguvu. Huu ni unabii wangu ambao hakika siku za usoni
utatimia. Umefika wakati wako wa kusoma alama za nyakati. Wasomi
wamechoshwa kukandamizwa, wasomi wanataka walisaidie taifa lao ambalo
kwa mda mrefu limekuwa shamba la bibi. Wasomi wanataka kuwa na uhuru
wa mawazo, uhuru wa kukusanyika na kujadili mabadiliko wayatakayo
ndani ya taifa lao. Tusipopata mabadiliko kwa njia ya kidiplomasia
tutayapata kwa njia ya nguvu.

Mh. Profesa, Napenda ufahamu kuwa duniani hakuna jipya, mtesa na
mteswa wote hatima yao kifo yaani binadamu huishi mara moja tu na
hufa. Hakuna mtu kutokana na madaraka yake, vyeo vyake, umaarufu wake,
hadhi yake ya elimu atakufa atazikwa hewani. Sisi sote tutarudi
vumbini. Jaribu kuitendea haki taaluma ya uprofesa kwa kulisaidia
Taifa hili, kinyume na hilo utabakia na uprofesa wa jina usio na faida
ndani ya taifa langu.Nimefikia sehemu ninahoji uhalali wa uprofesa
wako kwa sababu, mambo unayoyafanya ndani ya Taifa langu yananipa
wasiwasi kwani hayaendani na taaluma uliyonayo. Mh.Profesa naomba
litendee haki taifa langu, wewe ni mzee kwa umri sasa tuachie vijana
tutaoishi na taifa hili kwa mda mrefu. Kiache chuo kikuu cha Dar es
salaam kiwe huru. Usiendeleza udhalimu uliokwisha tufanyia sisi,
kinyume na hayo dhambi hii itakutafuna leo na mpaka kaburini kwako.

Namalizia kwa kumnukuu Hayati Mwalim. J.K. Nyerere aliyesema kuwa kazi
kubwa ya vyuo vikuu ni kutafuta ukweli, kusema ukweli na kuuishi
ukweli huo kwa gharama yoyote ile bila kujali madhara yatakayokutokea
kutokana na kweli uliyoisimamia. Nitasema ukweli daima fitina kwangu
mwiko. Kwa wale wote walioandika barua za msamaha kwenu hawakujua
walitendalo,walivamiwa na shetani mwenye majina matatu "HOFU, SHAKA NA
WOGA". Kwa sasa wanajuta, wamekubali kushusha utu wao kwa sababu ya
ukatili wenu. Niliwahi jiuliza swali moja kwa nini waasi wanatokea
katika mataifa mengine, nimepata jibu kutokana na mazingira niliyopo
tusifikie huko lakini najua unakifahamu ulichokifanya, najua unafahamu
upotoshwaji ulioufanya ndani ya mfumo wa uongozi wa nchi hii na nje ya
mfumo, najua unafahamu umepoteza nafsi ngapi za vijana kwa kupoteza
ndoto zao kielimu. Yote haya uyapime katika mizani ya haki na ujiulize
kutokana na uliyo yafanya unastahili nini hapa duniani.
Mh. Profesa. Nakutakia tafakari njema. Muombe Mungu Hekima na Busara
zenye utashi wa kujitegemea katika madaraka yako. Kinyume na hapo
unarithi ya pilato, sauti za walala hoi, wavujajasho wa taifa hili
zitakulilia hata kaburini kwako.

ALPHONCE LUSAKO alias EMEKHA IKHE. w.together@yahoo.com.
TRUTH IS POWER, CHANGES IS MY MISSION AND GOD IS MY LEADER.

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Related Posts

1 Comments
avatar

Ngoja tufanye utafiti yakinifu ili kupata ukweli maana kuna ukweli kulingana mtu na mazingira yake (truth) na kuna ukweli unaotokana na uhalisia (holy truth.

REPLY
:)
:(
=(
^_^
:D
=D
=)D
|o|
@@,
;)
:-bd
:-d
:p
:ng
:lv