[wanabidii] MSINGI WA MAHUSIANO BAINA YA WAISLAMU NA WASIO WAISLAMU

Tuesday, February 19, 2013

"Hakika si vingine nimetumwa kuja kutimiza TABIA NJEMA" Hadith Tukufu

  1. Msingi wa mahusiano na mafungamano baina ya waislamu na wasio waislamu:

Ø      Tangazo la Madinah:

         Tangazo la Madinah ndilo lililo kuwa muongozo wa kwanza kutolewa na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwa watu wa Madinah. Aliainisha humo misingi ya udugu ambayo inasimama baina yao ndani ya jamii yao mpya na kwamba wao wote ni umma mmoja. Akawakiria humo Mayahudi dini yao na mali zao na akawaahidi ulinzi na nusra muda wa kuwa kwao wakweli na watiifu kwa dola mpya. Mtume wa Allah aliandika azimio baina ya Muhajirina na Answaari, akafanya maagano humo na Mayahudi, akawakiria dini yao na mali zao, akawashurutizia nao wakamshurutizia. Daktari Mustafa Subaaiy, anasema: "Tangazo hili lilibainisha misingi ya jamii mpya na Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akawakiria humo Mayahudi dini yao na mali zao. Na akawaahidi ulinzi na nusra, tangazo hilo lilibeba misingi ifuatayo:

ü      Umoja wa umma bila ya kubagua baina ya wana wa umma.

ü      Usawa wa wana wa umma wote katika haki na heshima/hadhi.

ü      Kusaidiana umma mzima si katika dhulma, madhambi, uadui na ufisadi, vyo vyote atakavyo kuwa huyo dhaalimu au fisadi.

ü      Kushirikiana umma katika kujenga mahusiano mazuri na adui zake.

ü      Kuijenga jamii juu ya nidhamu na utaratibu mzuri ulio kwima.

ü      Kupambana na wanao jitoa chini ya mamlaka ya dola na uwajibu wa kutowanusuru pindi wakishambuliwa.

ü      Kumlinda atakaye taka kuishi pamoja na waislamu kwa amani na kusaidiana nao na kutowadhulumu.

ü      Wasio waislamu wana haki ya kuendelea na dini yao na kumiliki mali zao. Wasilazimishwe kuwa waislamu wala zisitwaliwe mali zao.

ü      Wasio waislamu wanapaswa kuchangia gharama za kuendesha dola kama iwapasavyo waislamu.

ü      Wasio waislamu waishio ndani ya dola ya Kiislamu, wamewajibikiwa kusaidiana na waislamu kuilinda dola dhidi ya uadui wo wote. Na ni juu yao kuchangia gharama za vita.

ü      Ni wajibu wa dola kumnusuru adhulumiwaye miongoni mwa wasio waislamu, kama inavyo mnusuru muislamu afanyiwaye uadui.

ü      Iwapo maslahi ya umma yako katika suluhu, wana wa umma wote; waislamu na wasio waislamu wamepaswa kuikubali suluhu.

ü      Mtu asiadhibiwe kwa dhambi ya mtu mwingine na wala mfanya jinai hatendi ila kwa jukumu la nafsi yake.

ü      Uhuru wa kuhama kutoka sehemu moja ya dola kwenda nyingine au nje yake unalindwa na himaya ya dola. Na wala hana himaya mtenda dhambi wala dhaalimu.

ü      Jamii inaundwa juu ya msingi wa kusaidiana katika wema na ucha-Mngu na si juu ya madhambi na uadui.

 

Ø      Waraka wa Mtume kwa watu wa Najiraan:

         Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alifanya suluhu na watu wa Najiraan, kwa sharti alizo washurutizia, nao wakazikubali. Kwa makubaliano hayo akawaandikia waraka/mkataba huu:

KWA JINA LA ALLAH MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

         Haya ndiyo aliyo yaandika Muhammad; Mtume wa Allah kuwaandikia watu wa Najiraan iwapo ana utawala juu yao: Hakika katika kila cheusi na cheupe, chekundu na manjano, matunda na mtumwa ni vyao wao amewaachia.....Na kumewapasa watu wa Najiraan kuwafanyia dhifa wajumbe wangu kwa muda wa siku ishirini. Na utakapo tokea uasi/usaliti kwa watu wa Yemen na waislamu wakahitaji kuazima kutoka kwao zana za vita. Basi ni juu yao kuwaazima farasi thelathini, ngamia thelathini na deraya (nguo za vita) thelathini. Na kitakacho hiliki miongoni mwa vilivyo azimwa na wajumbe wangu, basi hicho ni dhamana juu ya wajumbe wangu mpaka wakilipe.


Na watu wa Najiraan na wafuasi wao, wana dhima ya Allah na dhima ya Mtume wake juu ya damu zao, mali zao, mila yao, masinagogi (nyumba zao za ibada) yao, utawa wao, maaskofu wao, waliopo na wasio kuwepo katika wao. Na kila kilicho chini yao; kidogo au kikubwa.......Na wala wasifukuzwe kutoka katika ardhi zao, wala wasitozwe ushuru, wala jeshi lisikanyage ardhi yao......".


Ameushuhudia waraka huu Uthmaan Ibn Affaan na waandishi. Hebu ewe ndugu mwema-Allah auzidishe wema wako-uangalie ukweli huu unao onekana ndani ya waraka wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwa watu wasio waislamu. Ukweli ulio jaa uadilifu na rehema (huruma) na wala hapana ndani yake matumizi ya nguvu kwa watu walio ikhitari ibada ya msalaba juu ya ibada ya Allah.

 

Ø      Waraka wa Abu Bakri kwa watu wa Najiraan:

         Hakika makhalifa  waongofu na watawala waislamu waliuiga mwenendo wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika kuamiliana na wasio waislamu. Baada ya kufariki kwa Bwana Mtume, ujumbe wa watu wa Najiraan ulimjia khalifa wa kwanza wa waislamu; Sayyidna Abu Bakri-Allah amuwiye radhi. Akawaandikia waraka ufuatao:


KWA JINA LA ALLAH MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.


         Haya ndiyo aliyo yaandika mja wa Allah; Abu Bakri – khalifa wa Mtume Muhammad-Rehema na Amani zimshukie-kwa watu wa Najiraan. Amewahami kwa himaya ya Allah na dhima ya Muhammad; Mtume, juu ya nafsi zao, ardhi yao, mila yao, mali zao, wafuasi wao na ibada zao na masinagogi yao. Na kila kilicho chini ya umiliki wao; kidogo au kichache, wasile khasara na wala wasitiwe uzito.........Kwa kuwatekelezea yote aliyo waandikia Muhammad; Mtume-Rehema na Amani zimshukie-na yaliyomo ndani ya waraka huu.......".

 

Ø      Waraka wa Umar Ibn Khatwaab kwa wasio waislamu katika Beitul Maqdis (Jerusalem):

         Ilikuwa ni sehemu ya tabia ya khalifa wa pili wa Mtume; Sayyidna Umar-Allah amuwiye radhi-kwa watu walio suluhiana na kuahidiana nae. Ni kuzitekeleza ahadi zao na kuwa mkweli katika utekelezaji wake. Hili linaonekana wazi katika mikataba ya amani aliyo wapa wasio waislamu katika Beitul-Maqdis. Aliwaandikia Manaswara wa Beitul-Maqdis amani juu ya nafsi, watoto, wake, mali na makanisa yao yote yasivunjwe na wala yasikaliwe. Na ulipo ingia wakati wa swala nae akiwa amekaa kwenye baraza ya juu ya kanisa, alitoka akaswali peke yake nje ya kanisa kwenye ngazi iliyo mlangoni mwake. Na akamwambia Paroko: Lau ningeswali ndani ya kanisa, waislamu baada yangu wangelitwaa hilo na wangesema: Hapa aliswali Umar. Kisha akaandika waraka kuwausia waislamu kutokuswali ye yote miongoni mwao kwenye ngazi hiyo ila mmoja mmoja bila ya kujumuika kwa ajili ya kuswali hapo wala kuadhini juu yake.


Ama ahadi zake kwao, zilikuwa ni mfano katika wepesi na murua, aliwaandikia ahadi ambayo alisema ndani yake: "Haya ndiyo aliyo toa mja wa Allah; Umar Amiri wa waumini kuwapa watu wa Iliyaa katika amani. Amewapa amani kwa nafsi zao, mali zao, makanisa yao na misalaba yao na baki ya mila zao nyingine. Hakika hayatakaliwa wala kuvunjwa makanisa yao wala kuvunjiwa heshima yake........Wala wasiudhiwe kwa sababu ya dini yao na wala asidhuriwe ye yote miongoni mwao. Wala ye yote miongoni mwa Mayahudi hataishi pamoja nao Iliyaa. Na ni juu ya watu wa Iliyaa kulipa kodi kama wanavyo toa watu wa Madaain na kumewalazimu kuwafukuza wezi. Atakaye toka miongoni mwao, basi huyo ana amani juu ya nafsi yake na mali yake mpaka afikilie mahala pake pa amani. Na atakaye bakia miongoni mwao, naye ana amani na kumemlazimu kutoa kodi kama ilivyo kwa watu wa Iliyaa......".


Kwa misingi hii mitukufu ya kiutu, na kwa maadili haya ya Kiislamu yenye usawa, Uislamu uliasisi dola na kuunda umma usio jua mafundo, chuki, ukatili wala dhulma – pamoja na tofauti za utaifa na dini zilizo kuwepo. Wala dola hii haikusimamishwa wala kuendeshwa ila na wema, huruma na moyo wa kiutu. Huo ulikuwa ni utekelezaji wa kivitendo wa kauli ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ambamo anaonyesha mafungamano baina ya imani ya kweli na mahusiano ya kibinadamu:"Hamtaamini (hamtakuwa waumini kweli) mpaka muwe na huruma. (Maswahaba) wakasema: Sisi sote ni wenye huruma. Mtume akasema: Hakika hiyo (niisemayo) siyo huruma ya mmoja wenu kumuhurumia (muislamu) mwenzake, lakini hiyo ni huruma enevu (kwa watu wote)". Twabaraaniy-Allah amrehemu.


-- http://www.uislamu.org/akhlaaq/akhlaaq138.htm

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

Share this :

Related Posts

0 Comments