Kuna tatizo kubwa zaidi kuliko uchinjaji wa wanyama. Chanzo cha yote haya ni mapungufu ya utashi katika uongozi wa Taifa letu. Nchi hii haiongozwi na viongozi wa dini bali inaongozwa na serikali, kwa hiyo serikali haiwezi kukwepa lawama ya kutokuwajibika kwa kisingizio cha viongozi wa dini ndiyo wanaosababisha.
Watu kila mara wanaongelea kuwa haya yanayotokea siyo desturi ya Watanzania. Wengi wanadai kuwa kwa miaka mingi watanzania wamekuwa wamoja, hawana udini wala ukabila. Na wengi wanaamini au wanataka kuwaaminisha wengine kuwa hali hiyo ilitokana na mazoea, desturi na utamaduni wa Watanzania. Huo ni UWONGO MKUBWA.
Umoja wa Watanzania, unaopiga vita ubaguzi wa kidini, kikabila, kikanda au namna nyingine yeyote ilikuwa ni matokeo ya uongozi thabiti, uongozi imara uliokuwa hauyumbi na uliokuwa umeamua kuwa hautaki kuiona Tanzania inayosimama katika mgawanyiko wa kidini au kikabila. Huu ulikuwa ni uongozi wa Mwalimu Nyerere na wenzie akina Rashid Kawawa, ambao walikuwa na imani tofauti kabisa za kidini lakini waliokubaliana juu ya umuhimu wa kuwa na jamii yenye umoja na amani. Kwa hiyo umoja wa Watanzania na amani iliyokuwepo kwa miaka mingi ni matokeo ya jitihada za viongozi waliokuwa na upeo mpana na nia njema kwa Taifa, hiki ndiyo tunachokikosa leo, na matokeo yake tumeanza kuyashuhudia.
Kuna habari nyingi, na nyingine hazipo wazi ambapo Mwalimu aliwahi kuwa mkali sana juu ya mashekhe waliokuwa wakitaka kueneza udini. Pia wapo mapadre waliowahi kufukuzwa na Mwalimu kutoka nchini kwa kuonesha kupanda mbegu za ubaguzi wa kidini. Mwalimu aliyafanya hayo kwa dhamira na siyo kwa unafiki, na wapo waliomwita ni dikteta, lakini ni aheri kuwa dikteta wa kutafuta amani na umoja kuliko kuwa mwanademokrasia wa kumpa uhuru kichaa abebe panga huku hamjui anaenda nalo wapi.
Haya yanayotokea sasa yameanzishwa, yamekuzwa, yamepaliliwa na sasa yanaanza kutoa matunda. Huu uovu wakati unapandwa serikali ipo, Rais yupo, na vyombo vyote vilivyopewa haki ya kusimamia utaifa wetu vipo. Serikali haina moral credibility ya kushangaa yanayotokea sasa wakati imekuwa ni shuhuda wa hatua zote kuelekea kwenye matokeo tunayoyaona leo.
Serikali na Rais hawakuchaguliwa kuwa taasisi za ushauri bali kama taasisi zenye mamlaka kamili ya kusimamia utaifa wetu kwa kuongozwa na sheria tulizoziridhia wenyewe kuwa ndiyo zinazoweza kusimamia amani na umoja wetu. Kwa muda sasa, kwenye masuala yanayohusiana na fujo za kidini serikali imeacha jukumu lake kama msimamizi mkuu wa sheria, na kujigeuza kuwa ni chombo cha ushauri, hilo siyo jukumu la serikali.
Kama Taifa ni lazima tuwe na mambo ambayo hayastahili kuguswa wala kuchezewa, ambayo kila mtanzania anajua kuwa ukiyagusa hayo, huna nafasi katika Taifa letu, na mojawapo kubwa ni umoja na amani ya Taifa letu. Jitihada na matendo yoyote yanayopalilia au kuhamasisha chuki au utengano kwa misingi ya kidini au kikabili yanahitaji prompt action, tena yenye adhabu ya juu kabisa maana wanaoplilia hayo wanawapa adhabu ya kifo Watanzania wote. Kwenye hilo awe ni shekhe, padre, mchungaji, mwinjilisti au ustaadhi, hawastahili kuwa salama.
Kwa sasa, ni muhimu serikali ikatuambia kwa nini imetufikisha hapa, na itatutoa namna gani.
Bart
0 Comments