[wanabidii] DR KINGWANGALA ASEMA YUKO TAYARI KUJIUZULU UBUNGE

Sunday, September 02, 2012
CCM NZEGA YATISHIA KUMVUA UANACHAMA,ASEMA YUKO TAYARI KUJIUZULU UBUNGE
Fidelis Butahe Dar na Mustapha Kapalata, Nzega
SAKATA la makada wa CCM, Hussein Bashe na Dk Hamis Kigwangala
kutoleana bastola, limechukua sura mpya baada ya Jeshi la Polisi
kuingilia kati na kumnyang'anya bastola Kigwangala huku likianza
kuwahoji wapambe wa mahasimu hao.

Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Tabora, (RPC) Antony Lutta zilieleza kuwa jeshi hilo linaishikilia
silaha ya Dk Kigwangala hadi hapo uchunguzi utakapokamilika.

Kauli hiyo ya polisi imekuja siku moja baada ya uongozi wa chama
hicho Wilaya ya Nzega, kutaka suala hilo liondolewe polisi ili
walishughulikie kimyakimya ndani ya chama.

Mwananchi Jumapili lilipomtafuta Dk Kigwangala ambaye pia ni Mbunge wa
Nzega na kumuuliza kuhusu suala hilo alisema: "Bastola yangu mbona
ninayo, hilo halina ukweli, bastola ninayo hapa."

Wakati hayo yakiendelea, uongozi wa CCM wilayani humo umempa onyo kali
Dk Kigwangala ukieleza kwamba endapo ataendeleza msimamo wake wa
kukataa kuhojiwa na chama, atachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na
kunyang'anywa kadi ya uanachama.

Kujiuzulu ubunge
Hata hivyo, mbunge huyo alisema kuwa hana imani na uongozi wa CCM
wilayani Nzega na kwamba iwapo CCM mkoa na taifa hautaingilia kati
mgogoro huo, yuko tayari kujiuzulu ubunge.

Bashe na Dk Kigwangala ambao ni mahasimu wa siku nyingi katika medani
za siasa wilayani Nzega walidaiwa kutoleana bastola Alhamisi iliyopita
walipogongana katika ofisi za CCM wilayani humo, wakati wakirejesha
fomu za kuwania Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) kupitia wilaya
hiyo.

Hata hivyo, pamoja na taarifa hizo kuthibitishwa na viongozi wa CCM
wilayani humo na RPC Lutta, kila mmoja alikanusha madai hayo
akimtuhumu mwingine kuwa ndiyo chanzo cha ugomvi huo.

Wakati Bashe alisema Dk Kigwangala ndiye aliyetoa bastola kumtishia
wakiwa ndani ya Ofisi ya CCM Wilaya, Dk Kigwangala alieleza kuwa
walinzi wa Bashe ndio waliomtishia yeye bastola na kwamba tayari
amelifikisha suala hilo polisi na wanalifanyia kazi.

Kauli ya Kamanda Lutta
Jana Lutta alisema ingawa imemnyang'anya bastola Dk Kigwangala, mbunge
huyo anamiliki silaha hiyo kihalali.

"Taarifa zao tutazitoa baadaye kwa sababu hivi sasa tunakusanya
ushahidi na tunawahoji wapambe wao, ambao inasemekana wakati tukio
linatokea walikuwepo eneo hilo," alisema Lutta na kuongeza:

"Silaha yake ipo katika Kituo cha Polisi Nzega, uchunguzi tulioufanya
unaonyesha kuwa ni yake, anaimiliki kihalali. Ni kweli ndugu yangu
silaha yake tunaishikilia."

Alisema kuwa kazi ya polisi ni kuchunguza tukio zima na ikikamilisha
uchunguzi wake, itaupeleka katika mamkala husika.

CCM watoa tamko zito
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nzega, Francis Shija alisema tangu kutokea
kwa tukio hilo, Dk Kigwangala alikataa kutoa maelezo katika kikao cha
dharura cha Kamati ya Siasa Wilaya kilichofanyika juzi na kile cha
Kamati ya Maadili kilichofanyika jana.

Alisema vikao bado vinaendelea ili kubaini ukweli wa tukio hilo na
kuongeza kuwa uongozi wa chama utahakikisha haki inatendeka kwa
watuhumiwa hao, ili kila mmoja apewe adhabu yake pamoja na onyo kali,
kama wanastahili.

"Vikao vitaendelea ili kubaini ukweli na mtu atakayekaidi kutoa
ushirikiano hatua zitachukuliwa dhidi yake ili iwe fundisho kwa
wengine," alisema Shija na kuongeza:

"Kama Kigwangala ataendelea kukaidi kila tutakapomwita ili aeleze
kilichotokea tutamnyang'anya kadi ya uanachama, ila sidhani kama
itafika huko, tutajitahidi tuyamalize kistaarabu."

Alipoulizwa kuwa taarifa zilizopo kuwa uongozi wa CCM wilaya hiyo
unampendelea Bashe alisema: "Siyo kweli, hatuegemei upande wowote
katika suala hili. Kamati ya Maadili haijaegemea kwa Bashe
tutahakikisha haki inatendeka na chama hiki hakina makundi kila mtu
anavuna alichopanda."

Kauli ya Kigwangala
Kwa upande wake Kigwangala alisema kuwa kikao cha Kamati ya Siasa
kilivunjika jana kwa sababu hakuwa na imani na wajumbe waliokuwa
wakiendesha kikao hicho.

Aliwataja wajumbe wa kikao hicho ambao hana imani nao kuwa ni pamoja
na Shija na Katibu wa chama hicho Wilaya ya Nzega, Kajoro Vyohoroka.

Alisema hata kikao cha maadili ambacho kilifanyika baada ya kuvunjika
kwa kikao cha Kamati ya Siasa, nacho kina watu ambao hana imani nao.

''Siwezi kutoa hoja zangu za msingi kwa kamati hii ya maadili, kwani
hakuna kilichobadilika kwa sababu wanaokisimamia ni Shija na Vyohoroka
na wote wapo upande wa Bashe. Siwezi kukubali kuhojiwa hadi jambo hili
litakapopelekwa katika ngazi nyingine ndani ya chama," alisema
Kigwangala.

Alisema siasa za CCM Wilaya ya Nzega ni 'siasa uchwara' kwa kile
alichoeleza kuwa ni kuwapo kwa makundi yasiyo na msingi wala faida kwa
CCM na kusisitiza kuwa kama jambo hilo halitafanyiwa kazi yupo tayari
kujiuzulu ili kumwacha Bashe aendeleze siasa uchwara.

"Endapo tatizo hili halitaingiliwa kati na CCM ngazi ya mkoa na taifa,
nipo tayari kujiuzulu ubunge na kukabidhi," alisema Kigwangala.

"Mimi silaha ninayo siku nyingi tu na hata mara moja sijawahi
kumtishia mtu maisha, kama unataka kuiona ipo siku nitakuonyesha,"
alisema Kigwangala akimwambia mwandishi wa habari hizi.

http://mwananchi.co.tz/component/content/article/37-tanzania-top-news-story/25905-polisi-wamnyanganya-bastola-kigwangala.html

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.

Share this :

Related Posts

0 Comments