[wanabidii] Rais Magufuli Wabadilishe Watanzania - Umaskini ni Hulka

Tuesday, April 12, 2016
Kuna wakati niliwahi kusoma taarifa moja ya hulka ya mtu mweusi. Hulka yake kubwa ni kupenda kutumia kuliko kuzalisha. Kule Marekani kulifanyika utafiti juu ya mtu mweusi. Wamarekani weusi wanachangia 6% ya GDP ya Marekani lakini wanachangia 10% katiika matumizi. Matajiri wakubwa weusi Marekani ni wasanii, pesa yao nyingi wanayopata wanaenda kutumia kwa kununua magari ya kifahari, nguo za kifahari na majumba ya kifahari kwenye makampuni ya Wamarekani weupe.

Wazungu tunaowalaumu kuwa wanatunyonya ni makini sana katika matumizi, na wapo sensitive sana kwa kila linalotokea. Mzungu anaweza kuwa na akiba ya U$500,000 bank lakini leo akisikia kuwa mataifa yanayozalisha mafuta kwa wingi Duniani yanakutana kupanga mbinu za kupandisha bei ya mafuta, kesho yake anaanza kubana matumizi kwenye maeneo mbalimbali, Mzungu akisikia kuwa kuna uwezekano wa kutokea upungufu wa chakula, kama kila siku jioni alikuwa anakula hotelini, anaanza kula sandwichi (mkate uliowekwa mboga za majani, nyanya na mayai). Kama alikuwa amepanga kufunga arusi, anaweza kuahirisha au kupunguza waalikwa mpaka kufikia watu wanne tu.

Lakini Mtanzania anasikia kuwa mwaka huu kuna ukame, atasikia kuwa mafuta yamepanda bei, atasikia MCC wamesimamisha msaada, Magufuli ameongeza kodi kwenye kila aina ya mapato, n.k., maisha yake yapo pale pale. Mtanzania ataendelea kunwa bia 10 kila siku kama alivyozoea, ataendelea kufanya kitchen party, ataendelea kufanya send off na arusi ya kifahari yenye waalikwa wasiopungua 200, arusi ambayo maandalizi yake yataanza mwezi April wakati arusi ni mwezi Agosti. Mtanzania anakuja kushtuka wakati anapoona anataka kwenda hospitali lakini hana hela, anatakiwa kulipa ada ya mwanae lakini hela hakuna, anatakiwa kulipa pango lakini hana hela, hapo ndiyo anaanza kusema kuwa tubane matumizi, unabana matumizi gani wakati huna hela? Maana hata usipotaka kubana matumizi, ukweli ni kwamba huna hela ya kutumia.

Kinachomfanya mtu kuwa tajiri siyo kile apatacho bali ni kile anachokitunza. Huu ni wakati wa makasisi na washekhe kuwaambia waumini umuhimu wa kuwa watunzaji wa mapato yao kwaajili ya manufaa ya familia zao. Wawashawishi waumini wao kuachana na sherehe kama za kitchen party na send off maana siyo hitaji la kiimani/kiibada. Wahamasishwe kutotaka sherehe za kifahari za arusi ambazo kimsingi haziongezi chochote. Ubarikio, ubatizo, kipaimara ni ibada zisizolazimisha sherehe. Wale wanaotaka kuyafanya hayo nao waambiwe wasiwachangishe watu wengine maana kuna watu hawana hela lakini hawana ujasiri wa kusema hawana uwezo wa kuchanga. Viongozi wa siasa nao wawahamasishe watu kuachana na sherehe zisizo na umuhimu.

Rais Magufuli ameonesha njia kwa kutosherehekea sikukuu za kiserikali, nadhani anaogopa kufuta hizi za kijamii na kidini kwa hofu tu ya kuambiwa anaingilia mambo ya kiimani au kijamii. Kama hawezi kuzifuta basi aseme tu kuwa anashauri sikukuu hizi zisherehekewe kwa kusali na uzalishaji mali tu.

Wito wangu ni kwamba tutumie muda mwingi kuzalisha kuliko kutumia.

Tunamwomba Rais Magufuli serikali yake itumie muda mwingi kuwasaidia Watanzania kuwa wazalishaji kuliko kutumia muda mwingi kukusanya kodi. Iwasaidie Watanzania wawe wazalishaji na baadaye ipate kodi ya kutosha. Ni wakati wa wataalam wa biashara, wataalam wa uwekezaji, wataalam wa kilimo, wataalam wa madini, wataalam wa uvuvi, n.k.  kufanya kazi kufa na kupona kuwafanya Watanzania watengeneze faida katika shughuli zao za kiuchumi ili serikali iwe na uhalali wa kukusanya kodi. Shida kubwa tuliyo nayo tuna maafisa biashara wasiojua biashara, tuna maafisa kilimo wasiojua kilimo, tuna wataalam wa madini wasioyajua madini, tuna maafisa uwekezaji wasioujua uwekezaji, tuna maafisa uvuvi wasioujua uvuvi, n,k.

Tuna maafisa mifugo ambao akiachishwa kazi wanashindwa kufuga hata kuku 500. Tuna wahindisi ambao wakiachishwa kazi wanashindwa kutengeneza hata daraja la upana wa mita 3. Tuna wakuu wa mikoa wakiachishwa kazi wanashindwa kuwa na miradi ya kuwawezesha kupata japo shilingi 500,000 kwa mwezi ingawa walipokuwa wakuu wa mikoa walihimiza vijana wanaomaliza vyuo vikuu wajiajiri.

Sasa ni wakati wa serikali ya Magufuli kuwapima wataalam kwa yale wanayoyafanya na siyo kwa uwingi wa vyeti au miaka ya kukaa ofisini. Rais awaulize wataalam hawa ni kwa namna gani wamewasaidia wazalishaji wa sekta mbalimbali kuwa wazalishaji wenye tija. Kama serikali haina msaada kwa wazalishaji, inakosa uhalali wa kukusanya kodi. Ifike mahali serikali iwe na ujasiri wa kusema, 'wewe mkulima tulikutoa kutoka uzalishaji wa magunia 10 ya maharage mpaka magunia 100, kwa nini hutaki kulipa kodi? Wewe mfanyabishara tulikutoa kutoka kuwa muagizaji wa midoli kutoka China mpaka kuwa mmiliki wa kiwanda cha mashati, kwa nini hutaki kulipa kodi?, n.k.

Uhalali wa serikali kudai kodi utokane na uwezeshaji kwa wananchi wake.

Nchi hii inatakiwa kuanza upya maana hata mitazamo, fikra na vitendo vya viongozi na umma kwa ujumla, siyo vinavyotuelekeza kwenye maendeleo. Wakati Rais unapotumbua majipu, kazania pia elimu ya kubadilisha hulka ya watu kutoka kwenye jamii ya watumiaji na kuwa jamii ya wazalishaji. Hakuna moral right ya kutumia bila uzalishaji. Na serikali pia iwe na fikra hiyo. Serikali inapoenda kuwabana walipa kodi ijiulize pia imewasaidia kwa namna gani katika biashara zao. Halmashauri zinapoweka vizuizi barabarani vya ushuru wa mazao, zijiulize zimesaidia nini katika uzalishaji wao.

HUU NI WAKATI WA KUVUNA ULICHOPANDA.

Mkinga Msambichaka

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments