[wanabidii] Ni Afadhali Mtu Mmoja Afe

Thursday, April 14, 2016
Magazeti leo yameandika kile alichokisema Mwadhama Polycarpo Kadinali Pengo wakati wa ibada ya kumbukumbu ya Hayati Edward Moringe Sokoine aliyefariki kwenye ajali ya gari 12 Aprili 1984. Kwa wale ambao walikuwa hawajazaliwa, ni kwamba kifo cha Sokoine ni kifo kilicholeta simanzi kubwa kwa karibia Watanzania wote kuanzia tuliokuwa wadogo wakati huo mpaka kwa wakubwa. Na watu wengi mpaka leo hawaelewi ilitokeaje gari ya Waziri Mkuu kugongwa na gari nyingine, mbele kukiwa na magari, nyuma kukiwa na magari, Waziri Mkuu akiwa amekaa kiti cha nyuma, lakini akafariki yeye pekee yake. Lakini kwa sababu ya heshima na imani kubwa ambayo Watanzania tulikuwa nayo kwa kiongozi wetu mkuu, Mwalimu Nyerere ambaye naye msiba huo ulimchanganya sana hadi kulia hadharani, hatukuhoji zaidi maana katika hotuba yake ya simanzi kubwa alituambia, 'Watanzania tukubali kuwa Sokoine amefariki kwa ajali ya gari', wote tuliyachukua maneno hayo kwa imani kubwa mpaka leo. Mungu amjalie raha ya milele marehemu Sokoine kutokana na mapenzi yake na matumizi ya vipawa vyake alivyopewa na mwenyezi Mungu kwaajili ya faida ya watu wanyonge na maskini.

Ni kwenye ibada hiyo ya Kumkumbuka Hayati Sokoine ndipo Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo alipoeleza kuwa Rais Magufuli akiwa Chato alimpigia simu, na kati ya mambo ambayo Rais Magufuli alimwambia yeye Kadinali ni kuwa, 'Kama ningejua Urais ndiyo hivi nisingegombea', naye Kadinali akamwambia Rais, 'Ni afadhali mtu mmoja afe lakini Taifa lisiteketee'.

Wengi tunaendelea kutafakari, ni nini hawa watu wawili waliongea mpaka kufikia huko? Japo ni rahisi kusema kuwa kwa mzalendo wa kweli, huwa yupo tayari kufa kwaajili ya watu wengine lakini kifo ni kigumu na bahati nzuri hutokea bila ya kuwa na taarifa ya kabla. Sisi wengine tutaendelea kuomba kusiwepo na wa kufa na pia Taifa lisiteketee.

Binafsi ningekataa tamaa kama ningesikia kuwa Rais Magufuli alimwambia Kadinali kuwa anamshukuru Mungu amemsaidia kuwa Rais na sasa anafurahia nafasi aliyopewa ya kuwaongoza Watanzania. Tafsiri rahisi ingekuwa hajali shida za wananchi. Nchi hii ina watu asilimia kubwa wanaoishi kwa shida na kwa kubahatisha kuliko idadi ya wenye uhakika wa maisha. Kuna watu wanakufa muda usio wao kwa sababu ya kukosa matibabu, kupata matibabu duni au kutibiwa kwa dawa zilizo chini ya viwango. Kuna watu wanakufa kila siku kwaajili za magari, pikipiki, mitumbwi na basikeli kwa sababu ya udini wa vyombo wanavyosafiria, barabara mbaya, ukosefu wa wataalam na vyombo vya uokoaji, n.k. Lakini pia kuna watu wasiopata chakula cha kutosha au chakula bora, kuna watu wana makazi duni kabisa, kuna watu wanafikiria ni kwa namna gani watanunua hata blanketi au shati. Kuna watoto pia ambao Mungu kawajalia vipaji mbalimbali lakini kutokana na umaskini wa wazazi wao kamwe vipaji vyao havitakuja kuonekana.

Hayo yote yanatokea wakati tukiwa na rasilimali ambazo kila mmoja anazijua. Hayo yote yanatokea Tanzania ikiwa na uongozi wa kwake yenyewe kwa zaidi ya miaka 50. Hayo yote yanatokea tukijidai kuwa tuna uongozi bora, sera na mipango mizuri ya uchumi, tuna sheria na vyombo vya kusimamia utawala wa sheria, vyombo vya kusimamia maadili ya uongozi wa umma, tuna taasisi mbalimbali za kusimamia mipango ya kuondoa umaskini usiondoka. n.k.

Kama miaka yote tumekuwa na hayo yote lakini nchi haikupiga hatua, ina maana vyombo hivyo ama vyote au vilivyo vingi vina matatizo makubwa. Na mahali pa kuanzia siyo kuviboresha bali kuviunda upya vikiwa na maelekezo mapya, sheria mpya za kuviendesha na za kuvisimamia. Ili kuweza kuyafanya haya kuna watu wanatakiwa kuondolewa, na kuna watu wapya wenye fikra mpya wanatakiwa kuingizwa. Na hapa ndipo ugumu wa kazi ya Urais unapokuja.

Maana wanaotakiwa kuondolewa ni watu ambao nyuso zao siyo ngeni kwa Rais Magufuli. Wengine ni makada wa Chama aliowafahamu kwa miaka mingi. Wengine ni marafiki aliowafahamu kwa miaka mingi. Wengine huenda waliwahi kuwa wakubwa zake katika utumishi wa umma, wengine ndugu au marafiki wa viongozi wenzake. Wengine ni watu aliowategemea sana kuwa msaada katika uongozi wake lakini anagundua kuwa siyo msaada bali ni 'majipu'. Kuweza kuwachukulia watu wa karibu yako, ambao sura na sauti zao unazijua, kwa faida ya watu ambao hata majina yao huyajui, inahitaji roho ya pekee, na roho hiyo iwe ya Kimungu.

Mheshimiwa Membe aliwahi kudokeza ilivyo ngumu kumchukulia hatua mtu unayemfahamu na uliyemteua mwenyewe.

Lakini tunachoweza kumwambia Mheshimiwa Rais ni kuwa utendaji bora hupimwa katika ugumu na siyo katika urahisi. Ni aheri amegundua mapema kuwa kazi ya Urais ni ngumu, hasa unapoongoza nchi ambayo mifumo mbalimbali haifanyi kazi, sera zipo kwenye mafaili lakini hazifanyiwi kazi, sheria zipo kwenye makabrasha lakini zinapindishwa kwa namna watu wenye malaka wanavyotaka, n.k.

Jambo la kujiuliza, je watendaje wengine wote nao wanatambua kuwa kazi zao ni ngumu? Mawaziri wote wanatambua kuwa uwaziri ni kazi ngumu? Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wanatambua kuwa kazi yao ni ngumu? Polisi wanatambua kuwa kuwalinda wananchi, tena kwa haki bila upendeleo ni kazi ngumu? Mahakama zinatambua kuwa kutoa hukumu kwa wakati wake na kwa haki ni kazi ngumu? Mifuko ya kijamii wanajua kuwahakikishia maisha mazuri wanachama wao badala ya kuhangaika na majengo ya kifahari yasiyowasaidia moja kwa moja wanachama wao ni kazi ngumu? Madaktari wanatambua kuwa kuwahudumia watanzania kwa upendo na uadilifu ni kazi ngumu? Au hawa wengine wanasali na kumshukuru Mungu kuwaweka mahali walipo?



Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments