[wanabidii] Bunge labana matumizi, laokoa bilioni 6/-

Tuesday, April 12, 2016
BUNGE limeokoa jumla ya Sh bilioni sita kwa kubana matumizi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo posho, safari za nje na viburudisho na limezikabidhi kwa Rais John Magufuli kwa ajili ya matumizi mengine. Fedha hizo ambazo zilikabidhiwa jana kwa Rais John Magufuli na kisha kuamriwa zitumike kununua madawati kwa kila jimbo, zimepatikana ndani ya kipindi cha miezi minne kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana.

Akiwasilisha taarifa ya namna ofisi hiyo ilifanikiwa kubana matumizi, Katibu Mkuu wa Bunge Dk Thomas Kashilillah, alitaja maeneo mengine yaliyohusishwa katika kubana matumizi ni gharama za mafunzo ya nje, machapisho na ununuzi wa majarida. Matumizi yamebanwa pia kwenye gharama za matibabu ya wabunge na familia zao, gharama za mtandao, chakula, malazi kwenye hoteli, machapisho ya hansard, ratiba za kila siku na vitabu vya taarifa mbalimbali.

Alitaja maeneo mengine yaliyopunguziwa matumizi ni gharama za umeme, maji na simu na mafuta ya uendeshaji wa mitambo. Dk Kashilillah alisema katika mwaka wa fedha wa 2015/2016 Mfuko wa Bunge ulitengewa Sh bil ioni 127.3. Kiasi hicho hakikujumuisha Sh bilioni 7.2 kwa ajili ya gharama ya ongezeko la wabunge wapya 36 na madeni yaliyotokana na shughuli za kiofisi ya mwaka wa fedha wa 2013/14 na 2014/15 ambayo ni Sh bilioni 5.6.

"Kwa sababu hizo, Ofisi ya Bunge ilichukua jitihada za makusudi kutafuta fedha ili kulipia mahitaji hayo kwa kutumia bajeti iliyoidhinishwa. Ofisi iliomba Wizara ya Fedha kwamba baada ya uhakiki, madeni yote yalipwe kwa kutumia fedha za ndani ya Mfuko wa Bunge kwa utaratibu wa uhamisho," alisisitiza. Alisema ofisi hiyo ya Bunge, ilianza kujitathmini kuhusu utekelezaji wa bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2015/16 kuanzia Julai mwaka jana baada ya kubaini uwepo wa mahitaji mbalimbali yaliyoidhinishwa ambayo hayakukasimiwa katika mwaka huo wa fedha.

Alitaja mahitaji hayo pamoja na madeni na wabunge wapya ni posho ya jimbo Sh bilioni 3.5, posho ya mafuta Sh bilioni milioni 950.5, posho ya vikao Sh bilioni 1.7 na posho ya kujikimu Sh milioni 959. Alisema pamoja na mahitaji hayo ya matumizi ya kawaida, pia kulikuwa na ongezeko la mishahara kwa wabunge hao 36 linalofikia Sh bilioni 5.1 kiasi ambacho kilirekebishwa na Utumishi na hakukuhitajika kufanyika uhamisho wa ndani.

Alifafanua kuwa matokeo ya ubanaji wa matumizi hayo, ulioanza Julai mwaka huu. Alisema yalihitimisha tathmini ya nusu mwaka wa fedha na hivyo kuwezesha ofisi hiyo kupata kiasi cha fedha cha kulipia madeni, gharama za ongezeko la wabunge wapya na kuwa na salio la Sh bilioni sita.

"Baada ya kufanyika kwa mapitio ya bajeti kwa kipindi cha nusu mwaka, tathmini hiyo iliwasilishwa kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye alielekeza kiasi hicho cha fedha kilichosalia kitumike kwa ajili ya kupunguza tatizo la uhaba wa madawati kwa wanafunzi nchini. Kwa upande wake, Rais Magufuli mara baada ya kupokea hundi kifani kutoka kwa Naibu Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson, alipongeza ofisi hiyo kwa kuokoa kiasi hicho cha fedha jambo alilosema si la kawaida.

Alisema watendaji wa ofisi hiyo, walikuwa na uwezo wa kuokoa fedha hizo na kukaa kimya bila viongozi wao kufahamu, lakini kutokana na moyo wa uzalendo walionao, waliamua kutoa fedha hizo kwa ajili ya kusaidia kutatua tatizo la madawati. "Kiasi hiki cha fedha mlichokiokoa kwa muda mfupi imejidhihirisha kuwa kila jambo linawezekana endapo kuna nia thabiti.

Narudia kuwapongeza watendaji ki ukweli tangu niwe Waziri kwa kipindi cha miaka 20 sijawahi kuona mtendaji akibana matumizi na kuokoa fedha; huu ni uzalendo wa pekee," alisema. Madawati kila jimbo Alisema endapo fedha hizo (Sh bilioni sita) zitatengeneza madawati , kila moja likiwa kwa gharama ya juu ya Sh 50,000, zitafanikisha madawati 120,000 kutengenezwa.

Alisema endapo wapo wabunge wa majimbo 200, kila jimbo litagawiwa madawati 600. "Kwa miezi minne imepatikana Sh bilioni sita, Bunge likibana tena matumizi kwa miezi mingine minne zitapatikana 12 (bilioni) kwa mtindo huu na taasisi na wizara zingine zikiiga, tatizo la madawati na matatizo mengine ya kijamii yatakwisha kabisa," alisisitiza.

Aliongeza kuwa "Dk Kashilillah umenigusa kabisa moyo wangu, nina watendaji wengi tu lakini hakuna hata mmoja aliyeokoa hata shilingi moja. Utendaji wa aina hii ndio tunaotaka, hii ndiyo Tanzania tunayoitaka, kila mmoja wetu akijifunza kubana matumizi tutapiga hatua." Alisema anatambua kuwa kazi ya kutengeneza madawati hayo, wamepatiwa Jeshi la Magereza.

Pamoja na kuwataka kutengeneza madawati hayo kwa ubora na kuwa mfano, aliwapa mwezi mmoja yawe yamekamilika na kukabidhiwa kwa wabunge kwa ajili ya kugawanywa kwenye majimbo yao.

Chanzo Habari Leo

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments