[wanabidii] ‘Wagombea’ wa Lowassa taabani

Wednesday, October 21, 2015
 
ZIKIWA zimesalia siku tatu kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu Oktoba 25 mwaka huu, wagombea watatu wa nafasi za Ubunge 'waliochomekwa' kwa ushawishi mgombea Urais wa Muungano wa vyama vinavyoundwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) Edward Lowassa, katika majimbo ya matatu ya mkoa wa Arusha wako taabani kisiasa.

Baada ya kuhamia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuteuliwa kuwa mgombea wa Ukawa Lowassa anadaiwa kuwashinikiza kwa masharti makali viongozi wa juu wa chama hicho kuwateua kugombea Ubunge wanaotajwa kuwa 'marafiki' zake wa karibu waliomfuata upinzani.

Aidha wakati Lowassa akitoa masharti hayo kwa viongozi hao tayari Chadema katika majimbo hayo walishafanya uteuzi wa wagombea wa nafasi za Ubunge na Udiwani.

Marafiki na wafuasi wa kisiasa ambao Lowassa anadaiwa kushinikiza wapewe nafasi ya kugombea Ubunge ni pamoja aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha Onesmo Nangole anayegombea Jimbo la Longido.

Wengine ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Ngorongoro Elias Ngorissa ambaye ameteuliwa kugombea katika jimbo hilo na Julius Kalanga anayegombea jimbo la Monduli.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya Ukawa ofisi ya kanda ya kaskazini zinadai kuwa Lowassa pia alifanya jitihada za kutaka wagombea wa majimbo ya Arusha Mjini (Godbless Lema) na Arumeru Magharibi (Gibson Meseyeki) waondolewe ili kupisha wagombea ambao ni chaguo lake.

Hata hivyo juhudi zake hizo zilikwama kutokana na baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema kumgomea na kumweleza kuwa hatua ya kuwaondoa wagombea hao ingesababisha mpasuko mkubwa ndani ya chama chao.

Taarifa zinadai kuwa katika jimbo la Arumeru Magharibi Lowassa alipendekeza mgombea awe 'mfuasi' wake wa muda mrefu kisiasa Goodluck ole Medeye ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Taarifa zaidi zilizofikia Raia Mwema mwishoni mwa zinaeleza kuwa pamoja na Lowassa na Ukawa kuwa na nguvu kubwa ya kisiasa katika mkoa wa Arusha uwezekano wa wagombea wake hao wa nafasi ya Ubunge kushinda katika majimbo hayo ni "finyu" sana.

Sababu inayotajwa kwamba wagombea hao wako taabani kisiasa ni kutokana na kukosa ushawishi wa kisiasa katika majimbo yao, mgawanyiko miongoni mwa wanachama na wafuasi wa Ukawa na wagombea kushindwa kufanya kampeni kwa ufanisi.

Aidha sababu nyingine inatajwa kuwa ni ukata unaotokana na wagombea hao kutegemea kupata fedha za kuendeshea kampeni zao kutoka kwa Lowassa na uongozi wa Chadema ahadi ambayo haikutekelezwa hadi sasa.

Moja wa viongozi wa Ukawa mkoa wa Arusha aliyeomba jina lake lihifadhiwe aliimbia Raia Mwema kuwa hawana matumaini makubwa ya kushinda katika majimbo hayo matatu kutokana mgawanyiko huo.

"Kwa kweli haya majimbo hatuwezi kushinda Ubunge kutokana na sababu kadhaa kama mgawanyiko miongoni mwa wanachama na viongozi wa Ukawa katika ngazi ya wilaya na mkoa na pia "udhaifu" wa wagombea wenyewe" alieleza kiongozi huyo.

Kiongozi huyo aliongeza: "Majimbo haya yote yanakaliwa na watu wa jamii ya wafugaji wa Kimaasai kwa asilimia 90 na jiografia yake ni ngumu kidogo hivyo inahitajika rasilimali watu na fedha ili kuwezesha wagombea kufika vijiji vyote kufanya kampeni lakini imekuwa ngumu kutokana na ukata unaowakabili"

Alisema mgawanyiko uliopo unatokana na wanachama na wafuasi wa Ukawa kukatishwa tamaa na hatua ya uongozi wa juu wa kuwaondoa wagombea walioshinda kura za maoni na wale waliwekeza kwa muda mrefu kukijenga Chadema katika majimbo hayo.

Akitoa mfano kiongozi huyo alisema katika jimbo la Longido mwanachama aliyeshinda kura za maoni Francis Ikayo aliondolewa na kuwekwa 'mgombea wa Lowassa' Onesmo Nangole ambaye hana ushawishi mkubwa kisiasa.

Juhudi za kumpata Nangole anayekabiliana na Dk. Steven Kiruswa wa CCM hazikuweza kufanikiwa mwishoni mwa wiki na wadadisi wa siasa za jimbo hilo wanabashiri kuwa mgombea wa CCM sasa anapewa nafasi kubwa ya kuibuka mshindi katika jimbo hilo.

"Pamoja na kushindwa kunyakua kiti cha ubunge hali hii itapelekea tupate kura cache sana za urais katika majimbo haya matatu ambayo kwa muda mrefu yamekuwa ngome ya CCM," aliongeza kiongozi huyo.

Aidha hali kama hiyo ipo katika majimbo ya Monduli na Ngorongoro ambapo wagombea wa Ukawa Julius Kalanga na Elias Ngorissa wanatajwa kuwa hoi kisiasa.

Kalanga ambaye kisiasa anatajwa kuwa mtu wa karibu sana na Lowassa anakabiliana na Namelok Sokoine, binti wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, hayati Edward Moringe Sokoine, anayegombea kwa tiketi ya CCM.

Akizungumza na Raia Mwema Kalanga alikanusha vikali madai hayo na kuongeza kuwa anao uhakika wa kushinda uchaguzi huo kwa asilimia zaidi ya 70.

"Tunaungwa mkono na asilimia 80 ya vijana ambao ndiyo wapiga kura wengi, tunaungwa mkono na asilimia 60 ya wazee na tunaungwa mkono na asilimia 50 ya wanawake, tumefanya kampeni katika za kuwafikia wapiga kura katika vijiji vyote vya jimbo la Monduli na wengi wametukubali," alisema.

Kalanga alidai kuwa CCM na mgombea wao (Namelok) wamekuwa wakitumia mbinu chafu katika kampeni zao kwa kuwalaghai wapiga kura kwa ushawishi wa fedha na ahadi zingine na wanakiuka sheria za uchaguzi.

"CCM wamebaini kuwa hawawezi kushinda hapa Monduli, ndiyo maana wanatumia mbinu hizo chafu, wanachofanya ni kutaka kupunguza kura za urais pamoja na ubunge ili ionekane kuwa mgombea urais wa Ukawa (Lowassa) hakubaliki kwao," alisema.

Aidha katika jimbo la Ngorongoro mgombea wa Ukawa Elias Ngorissa pia anaelezwa kuwa ana hali mbaya kisiasa kwa kuzidiwa na mgombea wa CCM William ole Nasha.

Taarifa zinadai kuwa mgombea huyo amshindwa kufanya kampeni zake kwa ufanisi hatua ambayo inampa mgombea wa CCM nafasi na urahisi wa kushinda jimbo hilo.
Hata hivyo Ngorissa aliimbia Raia Mwema katika mazungumzo yake wiki iliyopita kuwa katika siasa za sasa changamoto zinazotajwa ni za kawaida.

Katibu wa Chadema. Kalisti Lazaro "Bush", alipinga madai hayo na kuongeza kuwa wamefanya tathmini ya kutosha kabla ya kuwateua wagombea hao na hakuna shinikizo lolote kutoka kwa Lowassa na watu wake.

"Wakati mwingi CCM imejikita katika kutengeneza propaganda za aina hiyo ili kuwavunja moyo wapinzani, ila sisi tumejipanga sana tuna uhakika wa kushinda si chini ya majimbo matano ya mkoa wa Arusha na ikiwezekana hata yote," alisema katibu huyo.

Aidha ukiondoa majimbo haya matatu tathmini ya kisiasa inaonyesha kuwa Chadema/Ukawa bado wana nguvu ya kisiasa kushinda katika majimbo ya Arusha Mjini ambapo uchaguzi wake umeahirishwa baada ya kifo cha mgombea wa
ACT-wazalendo Estomih Mallah.

Majimbo mengine ambayo chama hicho cha upinzani kinapewa nafasi kubwa ni pamoja na Karatu ambapo mgombea wake Willy Qambalo ana uwezekano mkubwa wa kushinda dhidi ya mgombea wa CCM Dk. Willbroad Lorri kwa mujibu duru za kisiasa kutoka jimboni humo.

Katika jimbo la Arumeru Magharibi, Chadema/Ukawa wanapewa nfasi kubwa ya kushinda kutokana na kile kinachoelezwa kuwa mgombea wake Gibson Meseyeki anakubalika kuliko mgombea wa CCM Thomas ole Sabaya.

Uchaguzi wa mwaka huu unatabiriwa kuwa mgumu kwa vyama vyote vikubwa nchini kutokana na kuongezeka kwa hamasa miongoni mwa wananchi kuliko wakati mwingine wowote sababu kubwa ikitajwa kuwa kuongezeka kwa kiwango cha elimu na uraia na pia wananchi kuhitaji mabadiliko ya kiuongozi.

Raia Mwema

Share this :

Related Posts

0 Comments