SPIKA wa 60 wa Bunge la Marekani, Nancy Pelosi, akizungumzia uhakika wa chama cha Democratic kupata wabunge wengi mwaka 2014, alisema; "..usiwapuuze wapinzani wako, lakini usiwape uwezo wasiokuwa nao". Hili ni somo ambalo Ukawa walipaswa kujifunza mapema.
Wiki mbili kabla ya muda wa kampeni kumalizika na wananchi kupata fursa ya kupiga kura, Mgombea wa Chadema, Edward Lowassa chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) amefanya mikutano michache zaidi na kuwasiliana na wananchi katika maeneo machache ukilinganisha na mgombea wa CCM, Dk. John Pombe Magufuli.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na maofisa wa Ukawa, mpaka mwishoni mwa wiki jana, mgombea wao alikuwa amefanya kampeni katika mikoa takribani 26, akifanya wastani wa mikutano minne ya kampeni kila mkoa. Kwa idadi hiyo mgombea huyo anakuwa na wastani wa mikutano rasmi 104.
Wakati mgombea wa Ukawa akiwa amefika mikoa yote kasoro minne, anaonekana amekuwa na mikutano michache ukilinganisha na mgombea wa CCM Dk. John Magufuli ambaye mpaka wakati huo, alikuwa amefanya ziara za kampeni kwenye mikoa 20, akiwa amefanya mikutano rasmi 180.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Mikakati ya Ukawa, Profesa Mwesiga Baregu, mgombea wao amezunguka takribani mikoa 26 kwa ajili ya kunadi sera za Chadema zinazoungwa mkono na vyama vitatu vya Ukawa (CUF, NLD na NCCR Mageuzi) pamoja na kuomba kuungwa mkono kwa kupigiwa kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
"Kila siku mgombea wa Chadema alifanya mikutano minne, pamoja na ile ya mgombea mwenza, kwa siku moja Ukawa ilifanya mikutano nane na kila mahali ilidhihirisha mafuriko ya kweli ya watu na ushindi kwa mgombea wetu.
"Mgombea urais pamoja na mgombea mwenza wamekwishakuzunguka, mikoa ya Dar es Salaam, ambako wamefika mara mbili, Iringa, Njombe, Mtwara, Ruvuma, Lindi, Rukwa, Katavi, Pwani, Kigoma Tabora, Tanga, Morogoro, Dodoma na mikoa ya Unguja na Pemba," alisema.
Mikoa mingine ni Singida, Shinyanga, Geita, Simiyu, Kagera, Manyara, Mwanza, Arusha, Kilimanjaro pamoja na mikoa mingine ambayo kwa sasa wanafanya marudio kwa mgombea wao kwenda kunadi sera pamoja na kuomba kuungwa mkono kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Akizungumzia mikutano isiyo rasmi ambayo wagombea wao wameifanya katika kipindi hiki cha kampeni, Baregu alisema ni mingi sana na si rahisi kuitolea tathimini kwa kuwa mingi ya mikutano hiyo ilikuwa ni ya kushtukiza kutokana na baadhi ya watu kuzuia misafara ya wagombea kwa ajili ya kueleza changamoto zao.
Kwa mujibu wa mratibu wa safari za mgombea wa CCM, Daniel Chongolo, Magufuli mpaka mwanzoni mwa wiki hii alikuwa amepiga kampeni katika wilaya 118, vijiji 6,102 na alikuwa amesafiri umbali wa kilomita 19,620.
"Mgombea wetu amefanya kampeni katika mikoa 20 ya Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe, Ruvuma, Mtwara, Morogoro, Tanga, Mara, Simiyu, Tabora, Kigoma, Geita, Kagera, Shnyanga, Iringa, Dodoma, Singida, Manyara, ambako amehutubia mikutano 180 na mikutano isiyo rasmi kwa kusimamishwa na wananchi 486," alisema Chongolo.
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, Abdallah Bulembo aliliambia Raia Mwema kuwa kupitia mikutano hiyo, wamefikia idadi ya Watanzania milioni 16 ambao ni sawa na asilimia 81.98 ya wapiga kura.
"Katika muda huo mgombea wetu ametambulisha na kuombea kura wagombea ubunge 219 na tumefikia idadi hiyo hiyo ya majimbo kati ya majimbo 265 nchini nzima, tumeweza kufikia kata 3,721 na kutambulisha wagombea udiwani wetu, kwa kampeni tulizofanya tuna uhakika na ushindi mnono," alisema Bulembo na kuongeza kuwa muda wa wiki mbili zilizobaki zinatosha kufika maeneno ambayo hawajafikia.
Kuwasiliana na wapiga kura
Mgombea wa CCM, Magufuli amekuwa akitumia dakika 42 hadi saa 1.15 kuhutubia mikutano yake na kufanya wastani wa dakika 60 katika mikutano hiyo. Kwa upande wa mgombea wa Chadema, Lowassa, amekuwa akitumia wastani wa dakika 5 hadi 25 kuhutubia mikutano yake na kuweza kuhutubia mikutano kwa wastani wa dakika 15.
Mtaalamu wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) Mwanza (kwa sharti la kutotajwa gazetini), aliliambia Raia Mwema kuwa uwezo wa mgombea kuwasiliana na wapiga kura ni sehemu muhimu ya kuwashawishi wavutiwe naye zaidi.
"Kampeni ni sehemu muhimu ya kuvutia kura za watu ambao hawajaamua wanampigia nani, ukipata watu wengi, kama wanavyoita mafuriko, ni fursa ya mgombea kuwasiliana moja kwa moja na wapiga kura, ushawishi unaotokea pale una nguvu kubwa kwenye uamuzi wa mpiga kura, ndiyo maana ni muhimu sana ku - connect (kufungamana) na wapiga kura," alisema mtaalamu huyo na kuomba jina lake lihifadhiwe ili asiingie kwenye malumbano ya kisiasa.
Alisema fursa hiyo pia inaweza kuleta matokeo hasi kwa mgombea kama atashindwa kuwasiliana vyema na wapiga kura wake. "Kila chama kinapokwenda kwenye kampeni wanagombania kura za watu ambao hawajaamua wanampigia kura nani, mgombea akishindwa ku - connect na wananchi
Raia Mwema
0 Comments