UAMUZI wa kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kingunge Ngombale Mwiru kujiondoa kwenye chama hicho umekosolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahaman Kinana, pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Kwa mujibu wa Kinana, tatizo kubwa la Kingunge ni mgombea aliyekuwa akimuunga mkono hadharani kushindwa kupitishwa na vikao vya CCM, lakini kwa mujibu wa Jaji Warioba, Kingunge hawezi kujitenga na udhaifu au uimara unaohusishwa na CCM katika masuala ya uongozi.
Kinana akizungumza na Raia Mwema wiki hii kihusu hatua hiyo ya mzee Kingunge alisisitiza kwamba, kanuni na taratibu kuhusu uteuzi wa mgombea urais CCM zilizingatiwa, na Lowassa, anayepigiwa debe na Kingunge, alishiriki kupiga kura kwa mujibu wa Katiba ya CCM, ndani ya Halmashauri Kuu (NEC) kuchagua majina matatu kati ya matano kutoka Kamati Kuu ili kwenda Mkutano Mkuu, lakini vile vile alishiriki kupiga kura ndani ya Mkutano Mkuu, kuchagua jina moja kati ya matatu yaliyoletwa kutoka NEC.
Kinana anasema Lowassa alishiriki kupiga kura kuchagua majina matano ambayo ni January Makamba, Balozi Amina Salumu, Dk. Asha Rose Migiro, Bernard Membe na Dk. John Magufuli.
Kauli ya Kinana
Kwanza nianze kwa kusema kwamba namheshimu sana mzee Ngombale, amekitumikia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa muda mrefu sana na vile vile ameitumikia nchi kwa muda mrefu pia.
Anastahili heshima na kwa kweli mimi namheshimu sana.
Lakini jambo jingine analozungumza ni kuhusu malalamiko dhidi ya CCM kwamba, chama hakikutenda haki katika mchakato wa uteuzi wa mgombea urais.
Napenda kusisitiza kwamba mchakato wa uteuzi ndani ya CCM umezingatia Katiba ya chama chetu na vikao vyote vilivyofanyika vimezingatia matakwa ya Katiba ya chama.
Katiba ya CCM ukurasa wa 168 kifungu B cha ibara 109, kinaeleza kazi za Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu wakati wa uchaguzi, kwamba ni pamoja na "..kufikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa juu ya majina ya wanachama wasiozidi watano wanaoomba kugombea kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika vikao vya uteuzi, kulikuwa na mjadala mrefu na taratibu zote zilizingatiwa. Tatizo lililopo kwa mzee Ngombale ni moja tu, ni kwamba alikuwa na mgombea wake aliyemchagua kabla hata ya vikao vya chama.
Badala ya yeye kusubiri taratibu na vikao vya chama tayari alikuwa ameshiriki kutengeneza na kutangaza mgombea wake, akaamua mgombea wake ndiye awe huyo huyo bila kujali uamuzi wowote wa vikao. Wagombea wote 38 walitendewa haki kwa kuzingatia katiba na taratibu za CCM.
Tangu mchakato wa uteuzi wa mgombea urais uanze, mzee Ngombale alikuwa na mgombea wake ambaye ilikuwa dhahiri kama hakuteuliwa huyo basi Katiba na taratibu zimekiukwa.
Maelekezo ya kikatiba yapo na yamefuatwa, ukisoma ibara ya 107 kifungu 13(B) inaweka bayana kwamba majukumu ya Kamati Kuu ni kutoa majina matano kwenda NEC ambako yanapigiwa kura na kupatikana majina matatu yanayokwenda kwenye Mkutano Mkuu kwa ajili ya kupigiwa kura na kupata jina moja.
Kamati Kuu ilifanya kazi yake, majina yalipelekwa NEC kote mijadala ilifanyika na hatimaye NEC ilipiga kura na kisha Mkutano Mkuu ulipiga kura.
Na kwa taarifa yenu na wengine ni kwamba, Lowassa ambaye ndiye mgombea wa mzee Ngombale alipiga kura ndani ya NEC kwa ajili ya kupata majina matatu lakini vile vile, katika Mkutano Mkuu Lowassa huyo huyo mgombea wa mzee Ngombale alipiga kura.
Kwa hiyo, Lowassa alishiriki kutafuta wagombea watatu kati ya watano kutoka Kamati Kuu na pia alishiriki katika mchakato wa kupata mgombea mmoja kati ya watatu ndani ya Mkutano Mkuu.
Mgombea ambaye mzee Ngombale alimbeba alishiriki kikamilifu vikao vya NEC na Mkutano Mkuu baada ya mchakato wa awali kukamilika kwa mujibu wa Katiba ya Chama na taratibu zake.
Kuhusu uamuzi wake wa kujivua uanachama wa CCM, niseme tu kwamba alijiunga na CCM kwa hiari yake na kwa kweli amejiondoa kwa hiari yake, sisi tunamtakia kila la kheri katika maisha yake ya kustaafu.
Lakini hili la upatikanaji wa mgombea mfumo uliotumika mwaka huu ndiyo ule ule uliotumika mwaka 1995, mwaka 2005 na katika michakato hiyo, mzee Ngombale alishiriki na kukubaliana na uamuzi wote wa vikao husika.
Mwaka 1995 kulikuwa na wagombea 17, mchakato ukafanyika wakapitishwa watano kwenye Kamati Kuu na baadaye watatu kutoka Halmashauri Kuu kwenda Mkutano Mkuu ambao ni mzee Cleopa Msuya, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete na hatimaye mzee Mkapa akashinda.
Mwaka 2005 mfumo huo huo ulitumika, walikuwa jumla ya wagombea 11, katika Kamati Kuu wakapitishwa watano kwenda NEC na kwenye NEC wakapitishwa watatu kwenda Mkutano Mkuu ambao ni Dk. Salim Ahmed Salim, Jakaya Kikwete na Profesa Mark Mwandosya.
Kwa hiyo, Mzee Ngombale hakitendei haki chama chetu kutokana na tuhuma zake hizo. Na tena niwakumbushe tu kwamba, mwaka 1995 Lowassa alikatwa jina na mzee Ngombale alikuwamo kwenye vikao na aliunga mkono, akakubaliana na uamuzi wa vikao.
Sababu zilizotumika kumwondoa Lowassa mwaka 1995 ndizo zile zile, kwa hiyo utaona mzee Ngombale mwenye mitazamo miwili inayotofautiana. Anazo kauli mbili, ile ya mwaka 1995 ya kukubaliana na sababu za kuenguliwa kwa Lowassa na mwaka huu 2015, sababu zile zile ambazo hakubaliani nazo.
Mzee Ngombale alikuwapo kwenye vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu, na tena mwaka 1995 kwenye NEC atakumbuka kwamba baada ya Lowassa kutuhumiwa, kuna mjumbe mmoja wa NEC alipendekeza aitwe kikaoni ili atoe maelezo juu ya tuhuma dhidi yake.
Lowassa alishindwa kutoa sababu zilizojitosheleza katika kujitetea dhidi ya tuhuma zilizoelekezwa kwake na kikao kikaondoa jina lake.
Lakini pia mzee Ngombale anakumbuka namna John Malecela alivyoondolewa na aliridhika na uamuzi wa vikao. Malecela rufaa yake ilikataliwa na wajumbe wa NEC. Hapa ukweli ni kwamba, chama hakiwezi kuwa na misimamo miwili tofauti kwa jambo moja linalofanana.
Kwa hiyo, uamuzi uliofanyika katika mchakato wa uteuzi wa mgombea urais ulikuwa wa haki na nafikiri mgombea wa mzee Ngombale angepita asingeweza kuzungumza maneno haya..
Alipoulizwa kama yuko tayari kuunda timu ya wazee kwa ajili ya kuzungumza na mzee Ngombale ili asitishe uamuzi wake, Kinana alisema; "Angekuwa ametangaza kwamba anatafakari kujiondoa CCM hapo tungeweza kufanya hivyo lakini yeye amekwishakutangaza kujiondoa CCM, tunamtakia kila la kheri."
Vile vile alipoulizwa kwamba haoni mzee Kingunge anaweza kuwa na athari katika kampeni za sasa za CCM kuisaka Ikulu, alisema; "Sidhani kama kutakuwa na athari yoyote. Takriban asilimia 75 ya maisha ya mzee Ngombale yamekuwa ndani ya CCM na serikali yake.
Ameshiriki kikamilifu kuandaa na hata kusimamia sera na programu mbalimbali za CCM katika nyadhifa za juu zaidi kwenye chama na serikali. Kwa hiyo, leo Watanzania hawatamwamini na kwa kweli watamshangaa sana kama yeye ndiye kinara na msemaji wa mabadiliko hayo yanayozungumzwa."
"Ni miujiza kwa Watanzania kumwamini mzee Ngombale kwamba ndiye wakala wa mabadiliko nje ya CCM. Lakini katika tuhuma zake mzee Ngombale na Lowassa wanasema demokrasia na haki haikufuatwa kwenye mchakato wa uteuzi CCM, jambo ambalo si kweli kama nilivyofafanua, lakini na mimi nataka niwaulize huo mchakato wa kumteua Lowassa kuwa mgombea wa Chadema na kisha Ukawa, umefuata utaratibu?
"Je, kilichofanyika Chadema ni haki na demokrasia? Ninavyojua, Chadema wanayo katiba yao na taratibu zao za namna ya kumpata mgombea urais kwa kushindanisha wanachama wao, lakini vile vile, Ukawa walikuwa na kanuni zao walizokubaliana juu ya namna ya kumpata mgombea urais kwa pamoja.
"Haya yote hayakuzingatiwa, Lowassa alitoa masharti kwa Chadema, kwanza, hakutaka apambanishwe na mwanachama mwingine yeyote kwenye chama hicho katika uteuzi wa mgombea urais – awe mgombea pekee, hakutaka kuwapo kwa mchakato wa urais wa wazi.
"Lakini si tu ndani ya Chadema, hata ndani ya Ukawa, aliweka masharti hayo hayo, awe mgombea pekee ambaye hatashindanishwa na wenzake. Yaani siku ya kwanza alijiunga Chadema, siku ya pili, akateuliwa kuwa mgombea urais na siku ya tatu akateuliwa na Ukawa kuwa mgombea wao pekee. Namuuliza Ngombale, kwenye CCM tumeweka bayana haki na demokrasia ilifuatwa; je, huku Chadema na Ukawa haki imetendeka?
Je, wanachama wa Chadema walipata fursa ya kutimiza haki yao ya kuomba kugombea urais? Vipi kuhusu Ukawa, wagombea wengine walishindanishwa na Lowassa kama matakwa ya kanuni zao yalivyoelekeza?
"Watanzania hawawezi kuwaamini watu wa namna hii na kwa kweli, inashangaza kwamba, alama ya mabadiliko yanayozungumzwa taswira yake ni mzee Ngombale na Lowassa. Watu ambao hawana umadhubuti mioyoni wa kuzungumzia demokrasia ambayo imevunjwa huko huko wanakonadi kile wanachoita mabadiliko.
"Mimi nasema kama ni mabadiliko kwa mantiki ya mabadiliko wanayozungumzia kwa nini hawakuyaleta ndani ya CCM na serikalini ambako walikuwa wametumikia kwa miaka mingi? Hawa wanahadaa Watanzania kama vile ambavyo wanahadaa hata nafsi zao.
Hakuna jambo ambalo limeamuliwa na kutekelezwa kwa ushawishi wa CCM bila Kingunge kwa miaka mingi, kwa hiyo kama CCM inahitaji pongezi zinamhusu Kingunge na kama inahusika kulaumiwa basi hizo lawama zinamhusu," alisema Kinana na kusisitiza kuwa Kingunge hawezi kuwa alama ya mabadiliko.
Kuhusu madai ya Kingunge kwamba, katika Awamu ya Nne, Rais Jakaya Kikwete hakuna jambo la maana alilofanya, Kinana alisema; "Rais Kikwete amefanya kazi kubwa sana kwa kipindi chake cha miaka 10 katika nyanja zote, Ngombale anajua na mgombea wake (Lowassa) anajua na mara kadhaa wamemsifu Rais Kikwete hadharani.
Anaweza kuwa na tofauti zake na Rais Kikwete lakini kusema kwamba hakuna jambo la maana alilofanya, si sahihi. Si jambo linalotarajiwa kutoka kwake."
Kauli ya Warioba
Kwa upande wake, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba naye ameelezea kushtushwa na uamuzi wa Kingunge Ngombale Mwiru, akipinga sababu zilizotumiwa na kada huyo mkongwe kujiondoa CCM lakini vile vile, akikumbuka enzi za ujana wao namna walivyokuwa wakiandaa propramu za chama chao kupitia kundi lao maalumu, maarufu kwa jina la TANU Study Group.
"Nimeshtushwa kusikia Ngombale anatoka CCM, amekuwapo TANU na CCM kwa miaka 61. Tulikuwa naye TANU tukifanya kazi ya ubunifu wa maandishi na uchambuzi katika kusaidia chama, tulikuwa naye pamoja na akina Patrick Qoro, Gisler Mapunda na wengine.
Ngombale anahusika na mafanikio karibu yote ya chama. Hana historia nje ya TANU na CCM. Chochote alichofanya na kufanikiwa msingi wake ni chama. Nadhani ingekuwa sahihi kwake kuendelea na kubaki katika historia hiyo, akaendelea kuitetea.
"Angebaki kutetea itikadi anayoitambua, lakini kitendo chake cha kujiondoa ni udhaifu. Na kwa kweli, amethibitisha kwamba yeye na baadhi ya wenzake ndiyo waliokuwa wakikwamisha mabadiliko ndani ya CCM, mabadiliko ya kukataa uongozi kununuliwa, mabadiliko ya kukataa siasa za mitandao.
Haya ndiyo mabadiliko tuliyokuwa tukiyapigania mimi na baadhi ya wenzangu, huko wao wakishiriki kuyapinga.
"Sisi tulikuwa tunataka mabadiliko ndani ya CCM, tulipingwa, tulisema hakuna umoja tunahitaji umoja zaidi, tulisema uadilifu umetetereka mno katika chama kiasi cha fedha kuwa ndiyo kila kitu. Walitupinga na kwa kweli, katika hili, Kingunge na wenzake walikuwa wakipinga mabadiliko na kushabikia siasa za mitandao na makundi.
Sisi tulitaka maamuzi magumu yafanyike CCM ili kukirejesha chama kwenye mstari. Sasa leo hii, dalili za mabadiliko tuliyokuwa tukiyataka zimekuwa dhahiri, tumepata mgombea ambaye hakutumia fedha kushinda uteuzi, tumekuwa na mgombea ambaye hakuwa na makundi, huu ni mwanzo mzuri wa kufanya mabadiliko ya kiuongozi ndani ya chama na serikalini.
"Ni vigumu kukubaliana na sababu anazozitoa Ngombale, yeye badala ya kufanya uamuzi kwa kuzingatia matakwa ya misingi ya chama chetu, anafanya uamuzi kwa kumfuata mtu. Mtu hawezi kuwa ndiye mustakabali wa chama hata kidogo. Mimi nitaendelea kumheshimu lakini kwa hili (la kumfuata Lowassa badala ya kusimamia misingi ya kiitikadi) sikubaliani naye," alisema Jaji Warioba
Jaji Warioba aliongeza kusema: "Mwaka 2005 tulizungumza masuala haya ya kupinga makundi na mitandao, alivumilia na kutetea hali hiyo. Mimi nadhani kinachomsumbua yeye na watu wengine ni kuangalia matokeo ya mchakato na si taratibu za mchakato. Awali, mimi niliposikia kwamba kuna vijana wa CCM wanakusudia kushinikiza
Ngombale afukuzwe, nilisema wakifanya hivyo watakuwa wamefanya makosa makubwa, lakini sasa amejiondoa mwenyewe kwa sababu ambazo hazina uzito. Kama ni suala la udhaifu wa CCM basi Ngombale hawezi kukwepa udhaifu huo, yeye ni sehemu ya udhaifu
huo. Amefanya makosa kujiondoa CCM."
Kingunge: Kwa nini nimeondoka
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Kijitonyama, jijini Dar es Salaam Jumapili iliyopita, Kingunge alisema anaondoka CCM kwa kuwa hakuridhishwa na mchakato wa uteuzi wa mgombea urais wa CCM, akisema wagombea wote, takriban 38 hawakutendewa haki na Kamati Kuu, na wengi wao majina yao yalichujwa na Kamati ya Maadili ya chama hicho, akisema kamati hiyo haikuwa na uhalali wa kufanya hivyo.
Vile vile Kingunge alidai kwamba Rais Jakaya Kikwete hakufanya jambo la maana katika kuendesha nchi katika kipindi chake cha uongozi wa miaka 10, lakini vile vile, CCM kimepoteza uhalali wa kuongoza nchi, akidai kimeishiwa kile alichokiita pumzi
Chanzo Raia Mwema
0 Comments