"NDOA isiyo rasmi kisiasa" baina ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na chama cha upinzani cha Tanzania Labour Party (TLP) mkoani Kilimanjaro imemweka katika mazingira magumu kisiasa James Mbatia wa NCCR-Mageuzi anayegombea Ubunge wa jimbo la Vunjo.
Katika hali isiyotarajiwa kisiasa vyama hivyo viwili vimekuwa katika ushirikiano usio rasmi katika mkoa huo kukabiliana na vyama vinavyounda umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika kampeni za uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Ushirikiano huo ulithibitika wiki iliyopita wakati wa mikutano ya kampeni ya mgombea wa nafasi ya Urais wa CCM Dk. John Pombe Magufuli katika jimbo la Vunjo ambapo Mwenyekiti wa TLP Taifa Agustine Lyatonga Mrema alimnadi mgombea huyo wa CCM wakati chama chake kina mgombea anayewani Urais Maxmillan Lyimo.
Akiwa katika mji mdogo wa Himo wiki iliyopita Mrema alimnadi Dk. Magufuli akimwelezea kama mtu anayefaa kuwa Rais wa Tanzania kutokana sifa zake za uchapakazi, uadilifu na ujasiri wa kusimamia uamuzi.
Taarifa zilizofikia Raia Mwema kutoka ndani ya jimbo la Vunjo zinabainisha kuwa ubia huo wa kisiasa baina ya CCM na TLP unaweza kumwathiri na mgombea wa nafasi ya Ubunge katika jimbo hilo kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi James Mbatia.
Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa aliwahi kuwa Mbunge wa Vunjo kati ya mwaka 1995-2000 kabla ya kuangushwa katika uchaguzi wa mwaka 2000 na Jesse Makundi wa TLP.
Mbatia anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mgombea wa CCM Innocent Shirima pamoja Agustine Mrema (TLP) ambaye ndiye anayetetea kiti cha Ubunge wa jimbo hilo.
Kwa mujibu wa wakazi wa jimbo hilo katika mikutano yake ya kampeni Mrema amekuwa akikaririwa mara nyingi kuwa kama wananchi wa Vunjo hawatakuwa tayari kumchagua yeye basi wampigie kura mgombea wa CCM Innocent Shirima ambaye anamtaja kama "mjukuu" wake.
Kwa mujibu wa moja wa viongozi wa TLP katika jimbo hilo aliyeomba jina lake lihifadhiwe hatua hiyo Mrema imetokana na kuwepo kwa uhasama mkubwa kisiasa kati yake na Mbatia tangu wakiwa pamoja ndani ya NCCR-Mageuzi kati ya mwaka 1995-1999.
"Mrema na Mbatia ni mahasimu wakubwa kisiasa tangu enzi za NCCR-Mageuzi na Mrema amewahi kulalamika mara nyingi hadharani kuwa Mbatia amekuwa akimfanyia "fitina" za kisiasa katika jimbo lake," kilieleza chanzo chetu.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa ushirikiano huo baina ya Mrema na CCM umemweka katika wakati mgumu kisiasa Mbatia na uwezekano wa kushinda nafasi ya Ubunge katika jimbo hilo umeelezwa kuwa ni finyu.
"Wagombea wote wa CCM na TLP wamekuwa wakimshambulia Mbatia katika majukwaa ya kisasa hali ambayo inamweka katika wakati mgumu Mwenyekiti huyo mwenza wa Ukawa," aliongeza mtoa taarifa wetu.
Aidha Mbati pia amejikuta katika wakati mgumu zaidi kufuatia kuibuka kwa mgogoro baina yake na wagombea Udiwani wa Chadema katika kata 16 za jimbo ambao wamegoma wote kumfanyia kampeni katika kata zao kama sehemu ya makubaliano baina ya vyama vinavyounda Ukawa.
Kwa mujibu wa makubaliano ya awali baina ya vyama vinavyounda Ukawa, Mbatia alipewa heshima ya kuwakilisha umoja huo kugombea Ubunge Vunjo na Chadema walipaswa kumwunga mkono.
Kutokana na kuwepo kwa hali hiyo imeelezwa kuwa Mwenyekiti huyo wa NCCR-Mageuzi amekatiza safari yake ya kuambatana na mgombea wa nafasi ya Urais Edward Lowassa katika kampeni zake kitaifa na kurudi Vunjo kujaribu kuzima nguvu ya Mrema na CCM. .
Akizungumza na gazeti hilo moja wa wagombea wa nafasi ya Udiwani kupitia Chadema, alisema wagombea hao wamegoma kumfanyia kampeni Mbatia kutokana na kutofautina kuhusu mgawanyo wa kata kwa nafasi za Udiwani baina ya vyama hivyo.
"NCCR-Mageuzi hapa hawana mtandao wa wanachama katika jimbo hili, tofauti na Chadema ambao tuna viongozi kuanzia ngazi ya matawi na kata hivyo tulipaswa kupewa kipaumbele," alieleza.
Mgombea huyo aliongeza: "Lakini wenzetu wametanguliza tamaa wamesimamisha wagombea wao kata zote 16 kinyume na makubaliano ya vyama vyetu kitaifa," alidai.
Akizungumza mwishoni mwa wiki na Raia Mwema kuhusu ushirikiano huo wa kisiasa Mrema alithibitisha kuwa ni kweli amekuwa akishirikiana na CCM kwa lengo la kumzuia Mbatia asiwe Mbunge wa jimbo hilo.
"Huyu Mbatia hata hivyo hana, mtandao wa wanachama wa NCCR-Mageuzi hapa Vunjo, wanaomfuata ni mamluki na mamluki huwa hawashindi vita"aleleza Mrema.
Katibu wa Chadema Basil Lema alikiri kuwepo kwa mgogoro baina Madiwani wa Chadema na Mbatia na pia CCM kushirikiana na TLP.
"Ni kweli mgogoro kati ya wagombea wa nafasi za Udiwani na mgombea Ubunge (Mbatia), tunajaribu kufanya suluhu kwa kutumia viongozi wa kitaifa kwa kuwa wale wa ngazi ya wilaya wameshindwa kuutatua mgogoro"alisema Lema.
Katibu huyo wa Chadema hata hivyo aliponda ushirikiano wa CCM na TLP na kusema kuwa inadhihirisha "undumilakuwili" wa Mrema katika siasa za upinzani.
"Kuna vibaraka wa CCM ndani ya vyama upinzani na mwenendo wa Mrema unathibitisha hilo, lakini nawashangaa CCM kwa kuendekeza siasa za majitaka kuwarubuni wapinzani kila wanapokabiliwa na upinzani mkali wakati wa uchaguzi," aliongeza.
Kwa upande wake mgombea Ubunge wa CCM katika jimbo hilo Innocent Shirima alijigamba kuwa kutokana na mazingira ya kisiasa yaliyopo ana uhakika wa kushinda nafasi hiyo na kulikomboa jimbo hilo.
"Kwa nyakati tofauti tangu kuanza kwa chaguzi za mfumo wa vyama vingi jimbo la Vunjo limeongozwa na Wabunge wa upinzani wa vyama tofauti, hivyo CCM tutatumia fursa hii kisiasa kushinda na kulikomboa jimbo hili," alisema Shirima.
Juhudi za kumpata Mbatia hazikuweza kufanikiwa mwishoni mwa wiki kutokana na simu yake kutokuwa hewani kwa muda mrefu.
Taarifa zaidi zilizofikia gazeti hili kutoka mkoa huo wa Kilimanjaro zinabainisha kuwa Ukawa hata hivyo wana hali nzuri kisiasa katika majimbo Hai. Rombo, Same Magharibi na Same Mashariki.
Aidha taarifa zinaeleza zaidi CCM imejikita na inaweza kushinda majimbo ya Siha, Mwanga, Moshi Mjini na Moshi Vijijini.
Katika jimbo Hai Mwenyekiti wa Chadema Taifa Freeman Mbowe anakabiliana Danstan Mallya (CCM), wakati jimbo la Siha mgombea wa CCM Agrey Mwanri anakabiliana na Dk. Godwin Mollel (Chadema).
Katika Jimbo la Moshi Mjini, duru za siasa zinaeleza kuwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi, mgombea wa CCM Davis Mosha anaweza kumwangusha Jaffary Michael wa Chadema.
Aidha upinzani mkali kwa wagombea wa CCM uko katika majimbo ya Same Mashariki ambapo Anne Kilango anakabiliana na Dk. Naghenywa Kaboyoka (Chadema) na inatajwa kuwa hali mama Kilango kisiasa si shwari na anaweza kuangushwa katika uchaguzi huo.
Aidha pia katika jimbo la same Magharbii mgombea wa CCM Dk. Mathayo David Mathayo anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mgombea wa Chadema Cris Mbajo ambaye anatajwa pia anaweza kushinda jimbo hilo na kuondoa utawala wa muda mrefu wa CCM
Raia Mwema.
0 Comments