Kitila Mkumbo
ACT-Wazalendo wamejipambanua
VYAMA vya siasa vinavyoshiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu vimekamilisha awamu ya kwanza ya kampeni ya siku 30, tangu zilipoanza rasmi Agosti 22, 2015. Kutokana na nguvu ya kampeni na idadi ya wagombea waliowekwa katika uchaguzi huu, ni vyama vitatu tu ndivyo vinavyoonekana kuwa 'serious' katika kusaka ushindi. Vyama hivi ni vile vinavyounda Ukawa, CCM na Chama cha ACT-Wazalendo. Kwa sababu hii, katika makala haya ninafanya tathimini ya siku 30 za mzunguko wa kwanza wa kampeni kwa kuvilenga vyama hivi kama mfano wa rejea ya hoja zangu.
Kampeni zilianza kwa hamasa kubwa kwa vyama vyote hivi kufanya mikutano mikubwa ya uzinduzi. CCM ndiyo walianza kwa kuzindua kampeni zao katika mkutano mkubwa uliofanyika Agosti 22, 2015 katika Viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam. Mkutano huo uliongozwa na Rais Kikwete na kuhudhuriwa na viongozi wote waandamizi wa chama hicho, wakiwamo marais wastaafu Mkapa na Mwinyi.
Wiki moja baadaye, yaani Agosti 29, 2015, mgombea wa Ukawa, Edward Lowassa, naye alifanya mkutano mkubwa wa uzinduzi wa kampeni zake katika Viwanja vya Jangwani. Mkutano huo ulihudhuriwa na maelfu ya watu walioanza kumiminika tangu asubuhi na wengine kudaiwa kulala hapo hapo uwanjani. Kesho yake, yaani Agosti 30, 2015, Chama cha ACT-Wazalendo nacho kilizindua kampeni za urais kwa stahili yake katika mkutano mkubwa uliofanyika katika Viwanja vya Mbagala Zakheim na kuhudhuriwa na mamia ya wakazi wa Dar es Salaam.
Mgombea wa Ukawa, Edward Lowassa, ndiye aliyeleta hamasa kubwa katika uchaguzi huu na kubadilisha kabisa taswira ya siasa zetu. Kama nilivyopata kusema huko nyuma, Lowassa ni moja ya miamba ya kisiasa Tanzania ambaye umaarufu wake umedumu kwa zaidi ya miongo miwili. Tuhuma nyingi za ufisadi ambazo amekuwa akipewa tangu alipokuwa CCM na sasa akiwa upinzani hazielekei kufifisha nyota yake kisiasa. Kwa haiba yake, taswira yake kisiasa na nafasi zake alizokuwa nazo ndani ya CCM na serikali yake hakuna ambaye angeota kirahisi kwamba kuna siku Lowassa angevaa ujasiri wa kuhama chama chake cha zamani kilichomlea kwa zaidi miongo mitatu. Ndiyo maana mimi binafsi sipati kigugumuzi hata kidogo kumsifu kwa ujasiri alionao na bidii yake ya kupigania kile anachokiamini.
Lowassa alianza harakati zake za kusaka urais kwa hamasa kubwa tangu alipokuwa ndani ya CCM. Ndiye mgombea katika chama hiki aliyezunguka zaidi katika kusaka wadhamini na kupata wadhamini wengi zaidi. Ndiye mgombea aliyeonekana kuungwa mkono zaidi kihamasa na kitafiti katika wagombea 42 waliojitokeza. Haishangazi basi kwamba 'kukatwa' kwake na vikao vya CCM lilikuwa ni jambo lililokitikisa chama hiki na nchi kwa ujumla.
Hapa hatuna budi pia kuwasifu CCM kwa ujasiri wa kumuengua mtu aliyeonekana kuwa na nguvu kubwa za kisiasa. CCM walichukua hatari kubwa ya kisiasa kwa kumuengua Lowassa kama hatari ambayo Chadema waliichukua kwa kumkaribisha katika chama chao na hatimaye kumpa nafasi ya kugombea.
Lowassa alianza harakati zake za kugombea ndani ya upinzani kwa hamasa na mbwembwe kubwa katika taswira ambayo ilionyesha kana kwamba kila kiumbe hapa Dar es Salaam kilikuwa kinamuunga mkono yeye. Ule umati uliojitokeza kumsindikiza kwenda kuchukua fomu ya kugombea urais Agosti 10, 2015 ulikuwa sio wa kawaida na unaweza kulinganishwa na ule uliojitokeza siku ya kupokea mwili wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ulipokuwa unarudishwa Dar es Salaam kutoka London alikofariki mwezi Oktoba mwaka 1999. Aidha, mikutano yake ya utambulisho aliyoifanya hata kabla ya kampeni kuanza katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Mwanza na Arusha ilikuwa siyo ya kawaida. Hakuna shaka pia kwamba mkutano wa uzinduzi wa kampeni zake na ile iliyofuatia baada ya hapo imekuwa na mafanikio zaidi kiidadi na kihamasa kuliko ya vyama vingine.
Hata hivyo, katika mzunguko wa kwanza wa siku 30, kampeni za Edward Lowassa zimekumbwa na majereha makubwa ambayo yasipotibiwa vizuri yataathiri sana uwezekano wake wa kushinda katika uchaguzi huu. Jereha la kwanza limesababishwa na chama alichojiunga nacho. Kwa takribani mwongo mmoja tangu mwaka 2007, viongozi wa Chadema walifanya kazi kubwa ya kujipambanua kama chama kinachosimamia uadilifu na kupiga vita ufisadi. Neno lenyewe ufisadi liliingizwa rasmi katika lugha ya siasa na viongozi wa Chadema. Viongozi hawa walifanikiwa kumuweka Lowassa mbele kama taswira ya ufisadi wa CCM. Sasa inapotokea kwamba chama hiki kinamfanya mtu kiliyemuita ni kamanda wa ufisadi kuwa ndiye tena kamanda wa mapambano dhidi ya ufisadi, hawawezi kueleweka angalau kwa watu wenye akili zao.
Jeraha hili lilitiwa pilipili na uamuzi wa Profesa Ibrahim Lipumba na Dk. Wilbrod Slaa wa kujiengua ikiwa ni kupinga ujio wa Lowassa ndani ya Ukawa kwa kukataa siasa za ulaghai, uwongo na ukigeugeu, ambazo zinazidi kujikita hapa nchini. Bila kwenda ndani ya hoja walizotoa akina Slaa na Lipumba katika kujiuzulu kwao, nafasi walizokuwa nazo ndani ya Ukawa, ni wazi kuwa uamuzi wao ulikuwa pigo kwa harakati za Lowassa na Ukawa katika kampeni zao za kusaka dola.
Jeraha la pili ni aina ya kampeni ambazo Lowassa amekuwa akizifanya, na hasa hotuba anazotoa. Lowassa amekuwa akitoa hotuba fupi na zisizoeleweka. Kwa mfano, siku ya uzinduzi wa kampeni zake katika Viwanja vya Jangwani, wakati mamia ya wahudhuriaji na watazamaji wa televisheni wakimsubiri amwage sera zake, yeye aliishia kuzungumza
kwa dakika chache na bila kugusia mambo ya msingi katika ilani ya chama chake. Badala yake Lowassa akawaambia wananchi waliokuwa wanamsubiri kwa hamu aeleze sera zake waende kusoma hotuba yake na ilani katika tovuti ya Chadema.
Aidha, katika kampeni zake Lowassa amekuwa akitoa kauli tata na ambazo zinatia shaka kuhusu umakini wake kwa kuwa na makosa mengi ya kizembe katika mazungumzo yake. Kwa mfano, akiwa kanisani Tabora mapema mwezi huu aliwaambia waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kwamba nchi hii tangu ipate uhuru haijawahi kuwa na Rais mlutheri. Pamoja na kwamba hakuwaomba moja kwa moja Walutheri wamchague yeye kwa kuwa ni mlutheri mwenzao, ni wazi kwamba alikuwa anajaribu kujenga mazingira ya kisaikolojia ya kuwashinikiza Walutheri wenzake wamachague yeye ili nao waingie katika historia ya kutoa Rais wa Tanzania. Mifano mingine ni ile inayohusu maoni yake ya namna ya kushughulikia kesi za viongozi wa taasisi za kidini waliopo rumande kwa tuhuma za kufanya vitendo vya ugaidi, ambazo zilitia shaka juu ya dhamira yake kuzingatia utawala wa sheria.
Jeraha la tatu ni mgawanyiko unaoendelea ndani ya Ukawa. Mapema wiki iliyopita Makamu Mwenyekiti na Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, ambao ni washirika wakubwa wa Ukawa, walijitokeza hadharani kulalamikia kile walichokiita kuonewa na Chadema katika mambo mawili. Mosi, NCCR-Mageuzi wamepewa majimbo 12 tu. Pili, katika majimbo 12 waliyopewa, Chadema wamevamia na kuweka wagombea katika majimbo saba. Ndiyo kusema NCCR-Mageuzi wana majimbo matano tu ambayo hayana wagombea wa Chadema! Kwa wanaofahamu mfumo wetu wa siasa wanajua kwamba kwa mgawanyo huu NCCR-Mageuzi ndiyo imejifuta katika ramani ya siasa za Tanzania. Kwa hiyo malalamiko ya viongozi wa NCCR-Mageuzi ni ya msingi sana lakini yamekuja kwa kuchelewa mno. Tayari
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe, amewajibu viongozi hao kwa kejeli na, kama kawaida ya viongozi wa Chadema, kudai kuwa wanatumiwa na CCM. Hakuna shaka kwamba mazingira haya ya mgawanyiko, mtifuano na mgawanyiko ndani ya Ukawa ni jeraha lingine na yataathiri sana kampeni za Lowassa. Bahati mbaya kwa Lowassa ni kwamba sio rahisi kutibu majereha haya kwa sababu viongozi wake ndani ya Ukawa wanaamini kila changamoto wanayokumbana nayo inasababishwa na CCM na sio upungufu ndani yao!
Dk John Pombe Magufuli ni mwanasiasa aliyepatikana katika mazingira yaliyowaibua marais Mwinyi na Mkapa. Kama ilivyokuwa kwa Mwinyi na Mkapa, Dk Magufuli hakupewa nafasi ya maana ya kuteuliwa kugombea nafasi ya urais kupitia CCM. Hivyo uteuzi wake ulipokelewa kwa mshangao wa furaha kwa kuwa hakutarajiwa. Hata hivyo, watu wengi walimuona kama mtu aliyestahiki kuteuliwa kutokana na historia yake ya utendaji wa miaka 20 serikalini.
Dk Magufuli alitamba kisiasa nchini sehemu kubwa ya mwezi Julai kwa kiwango ambacho aliuzubaisha upinzani hadi Julai 27, 2015 pale ilipojulikana rasmi kwamba Lowassa alikuwa anajiunga na Ukawa. Baada ya Lowassa kujiunga na Ukawa Magufuli alipotea ghafla katika ulingo wa kisiasa na habari zikawa zimetawaliwa na Lowassa na Ukawa hadi kampeni zilipoanza.
Dk. Magufuli aliibuka tena katika hali ya kujitutumua siku ya uzinduzi. Maandalizi mazuri ya mkutano wa uzinduzi na hotuba kalikali za viongozi wa CCM yalimpa Dk. Magufuli nguvu mpya na kuondoa uzubaifu wa kisiasa uliomkumba kwa takribani mwezi mmoja tangu alipoteuliwa. Tangu kuzinduliwa rasimi kwa kampeni Dk. Magufuli amefanya mikutano mingi kuliko wagombea wengine sambamba na mgombea wake mwenza Samia Suluhu.
Kampeni za Magufuli zinaonekana kubebwa na mambo makubwa mawili. Mosi, Dk. Magufuli anaonekana kuwa na nguvu kubwa za kufanya kampeni bila kuchoka. Amekuwa akihutubia mikutano mingi kwa siku na yote anaonekana kuwa na ukakamavu wa kimwili, kisaikolojia na kisiasa. Pili, Dk. Magufuli ameuvaa upinzani ndani ya CCM kwa kukemea madhila yaliyosababishwa na serikali ya chama chake kwa kiwango ambacho angekuja mgeni asingeamini kama huyu ni mgombea wa chama tawala. Kikubwa zaidi, Dk. Magufuli 'ameiba' ajenda ya ufisadi na sasa anaongea kwa ukali na kujiamini zaidi kuliko waasisi wa ajenda hii, yaani Chadema. Hii ni mbinu muhimu kisiasa kwa Magufuli katika kipindi ambacho CCM inaonekana kuchokwa kuliko kipindi kingine chochote katika historia ya uhai wake.
Hata hivyo, Dk. Magufuli haonekani kama ni mtu makini sana kutokana na kauli zake tata. Kwa mfano, mara kadhaa amejaribu kuwatisha wapiga kura kwa kulinganisha mabadiliko ambayo wapinzani wanayahubiri na mabadiliko yaliyotokea Libya, bila kuzingatia ukweli kwamba mabadiliko ya Libya hayakufanywa kidemokrasia. Aidha, Dk Magufuli amekuwa akikilinganisha Chama Cha Mapinduzi na Chama cha Kikomunisti cha China kilichosimamia mabadiliko makubwa ya kiuchumi nchini humo, bila kujali kwamba chama hicho na siasa za China kwa ujumla ni za kidikteta. Kwa harakaharaka unaweza kumuona Dk Magufuli kama mtu anayetamani kutawala kidikteta.
Aidha, baadhi ya sera ambazo Dk Magufuli anahubiri hazina ukweli. Kwa mfano, suala la kutoa elimu bure hadi kidato cha nne tayari ni sehemu ya sera mpya ya elimu nchini iliyozinduliwa na Rais Kikwete mwezi Februari mwaka huu. Pili, Dk Magufuli anasema ataunda mahakama maalumu ya kushughulikia ufisadi wakati ukweli ni kwamba katika Ilani ya CCM hakuna hata neno ufisadi! Mambo haya yanamfanya Dk Magufuli aonekane ni mwana CCM mwingine tu na hivyo kufifisha jitihada zake za kujitofautisha, ambalo ndilo linaonekana kuwa lengo kuu la kampeni zake.
Katikati ya CCM ya Magufuli na Ukawa ya Lowassa, tunacho chama kipya cha ACT-Wazalendo. Chama hiki kimeanzishwa mwaka mmoja uliopita na kilizinduliwa rasmi miezi sita iliyopita, yaani Machi 2015. Tangu kuanzishwa kwake, chama hiki kimejipambanua kwa mambo mawili makubwa. Mosi, kimeibuka na mfumo mpya kabisa wa uongozi ambao haupo katika vyama vingine vya siasa nchini Tanzania.
Huu ni mfumo ambao una mwenyekiti wa chama na kiongozi wa chama. Pili, ni chama pekee nchini ambacho kinajitambulisha waziwazi na itikadi ya kijamaa na kuamua kutembea katika misingi ambayo Mwalimu Nyerere aliasisi. Sera zake na Ilani yake ya uchaguzi huu zimejengwa katika itikadi hii, falsafa ya Unyerere na misingi kumi.
Chama cha ACT-Wazalendo ndicho kilikuwa chama cha kwanza kutoa ilani yake hadharani tangu mwezi Machi 2015, kikiainisha misingi ya chama na vipaumbele vinne vya kisera katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Kwa maoni ya Johnson Mbwambo, mwandishi nguli wa makala kupitia Gazeti la Raia Mwema aliyoyatoa katika Gazeti hili toleo Na. 422, kama hakitatetereka, hiki ndicho chama kinachoelekea kuwa chama mbadala Tanzania kwa sasa na muda mrefu ujao.
Chama hiki kilijipambanua zaidi kupitia hotuba za viongozi wake walizozitoa siku ya uzinduzi wa kampeni zake Agosti 30, 2015, tukio ambalo lilirushwa moja kwa moja na vituo kadhaa vya televisheni. Kilichowavutia zaidi watazamaji na waliohudhuria uzinduzi huo ni hotuba ya mgombea urais wa chama hicho, Anna Elisha Mghwira, ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho.
Kwa uhodari wa uwasilishaji na uzito wa maudhui ya hotuba ambazo amekuwa akizotoa katika mikutano yake zinazoainisha kwa umakini na urahisi sera za chama chake, mwanamama huyu amejipambanua bayana katika wagombea urais wa mwaka huu. Baadhi ya wafuatiliaji wa siasa za Tanzania na kampeni za uchaguzi wa mwaka huu wanaeleza wazi kwamba kama wapiga kura wataamua kuchagua kwa kuzingatia misingi, sera na umakini wa mgombea bila shaka mama huyu ndiye anayestahili kuwa rais wa awamu ijayo ya utawala wa nchi yetu.
Bila kujali matokeo kitakachopata katika uchaguzi huu, Chama cha ACT-Wazalendo kimejipambanua zaidi kiitikadi, kimsingi na kisera na umakini wa uongozi, na pengine ndicho chama chenye 'future' zaidi katika siasa za Tanzania kuliko chama kingine.
Raia Mwema
0 Comments