[wanabidii] MAJAMBAZI DAGAA NA MAGUFULI

Monday, September 28, 2015
MAGUFULI NA MAJAMBAZI DAGAA
Ananilea Nkya

Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Dr John Magufuli akichaguliwa huenda nchi yetu ikashuhudia mapambano dhidi ya polisi na raia yakiongezeka kwa sababu serikali yake itaruhusu polisi kuuwa wananchi kwa kisingizio cha ujambazi.

Dr Magufuli katika kampeni zake kwenye uwanja wa Mashujaa mkoni Mtwara tarehe 02 Septemba 2015 alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa serikali yake haitamshitaki polisi yoyote atakayemuua jambazi mwenye silaha.

Dr Magufuli alikaririrwa akisema ''serikali yangu askari akipiga jambazi mwenye silaha kwa risasi hashtakiwi. Kila mara (majambazi) wanavamia vituo vya polisi, mbona hawavamii kambi za jeshi, jeshi la kujenga taifa au Ukonga FFU maana polisi wana nidhamu sasa wanawaonea na kuwaua''.

Wapiga kura wanajiuliza, kama kabla hajachaguliwa Dr Magufuli anaanza kuwaweka wananchi maskini roho juu kiasi hiki, je akichaguliwa mapambano kati ya wananchi walalahoi na vyombo vya dola yataongezeka kiasi gani?

Wananchi wanauliza swali hili kwa sababu ingawa hivi sasa hakuna polisi anayeruhusiwa kuhukumu watuhumiwa wa makosa mbali mbali tena kwa kuwatoa roho ikiwa ni pamoja na watuhumiwa wa ujambazi, lakini umma umeshuhudia polisi wakiwauwa watu hovyo hovyo kwa kuwasingizia ujambazi.

Kwa mfano tarehe 14 Januari 2006 watu wanne wafanyabiashara wa Mahenge mkoani Morogoro, Sabinus Chigumbi (Jongo), Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe na dereva wa taksi Juma Ndugu waliuwawa kikatili na polisi katika msitu wa Pande jijini Dar es Salaam kwa kusingiziwa ujambazi.

Ndiyo sababu wananchi wanauliza je Dr Magufuli akichaguliwa na huku akiwa ameshawaruhusu polisi kuwauwa walalahoi watuhumiwa wa ujambazi—ni raia wangapi walalahoi na wananchi videmodomo dhidi ya serikali wasio na hatia watakaosukiwa zengwe la ujambazi na polisi kutumika kimkakati kuuwawa kikatili ?
Hivi Magufuli ambaye amekuwa kiongozi wa serikali kwa zaidi ya mika 20 hajui kwamba polisi siyo mahakama na kwamba polisi haipaswi kutoa hukumu yoyote kwa mtuhumiwa hata kama ni mtuhumiwa ujambazi mwenye silaha kama ambavyo Dr Magufuli anataka polisi wawahukumu kifo papo kwa papo?

Wakati mgombea Dr Magufuli akitoa ahadi kwamba kwenye serikali yake polisi ndio watakaotoa hukumu ya kifo kwa watuhumiwa majambazi wenye silaha; Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelekeza kuwa ni mahakama kuu ndiyo yenye mamlaka ya kutoa hukumu ya kifo baada ya kesi kusikilizwa na mahakama kujiridhisha kwa ushahidi.

Zaidi wananchi wanajiuliza, nchi itakuwa katika hatari kubwa kiasi gani Dr Magufuli akichaguliwa ambapo ataruhusu polisi kujichukulia sheria mkononi kuwauwa wananchi ambao pengine maisha magumu yamewalazimisha kujitumbukiza kwenye wizi wa kutumia silaha?

Wengine wanauliza hivi Dr Magufuli haoni kwamba baadhi ya wananchi walalahoi wameamua kuwa wezi baada ya kushuhudia watawala wa serikali ya CCM wakifanya ujambazi wa kalamu kuiba fedha za wananchi kwa mfano kama ilivyotokea kwenye akaunti za Tegeta escrow bilioni 306 na EPA bilioni 133 na wako huru wakitembea kwenye mazulia mekundu ya heshima ya nchi ?

Lakini pia wananchi wanajiuliza je Dr Magufuli uchambuzi wake wa masuala ya kijamii umempa jibu kwamba polisi wakiwauwa ''majambazi wenye silaha'' ndio utakuwa mwisho wa mapambano kati ya wananchi na polisi?

Pengine Dr Magufuli anapaswa kujielimisha kujua kuwa chanzo cha ujambazi siyo wananchi na wala siyo polisi bali ni watawala. Kadhalika chanzo cha mapambano kati ya polisi na wananchi siyo polisi wala wananchi bali ni watawala.
Dr Magufuli anapaswa kufahamu kuwa mapambano kati ya polisi na wananchi ni kiashiria kimojawapo cha athari ya mfumo wa serikali ya CCM unaobariki watawala kuwa majambazi papa wa kutumia kalamu kuiba fedha za wananchi bila kushtakiwa, kujilipa mishahara na mafao manono, kutumia mali za nchi kutajirisha wawekezaji kutoka nje huku wananchi wengi wakibaki mafukara.

Zaidi anapaswa kufahamu kwamba maovu yanayohusiana na utafutaji wa mali kwa njia haramu hapa nchini ni matokeo ya CCM kulizika Azimiao la Arusha bila kuweka mbadala wake katika zama hizi mpya za utandawazi wizi.

Tena ikiwa ni zama ambazo mfumo wa uchumi unaotamba duniani baada ya ukomunisti kufa ni wa upebari ambao unaruhusu mtu mwenye uwezo wa kupata apate zaidi hata kama kwa wizi na wa kukosa afie mbali.

Matokeo yake sasa nchi yetu Tanzania ina kikundi kidogo cha watawala wa CCM waliotajika kutisha na ukitaka kuwachokoza waambie CCM ni mbaya, ni chanzo cha ufisadi au hakifanyi vema kwa wananchi.

Lakini wananchi maskini wanaojiingiza kwenye ujambazi wa kutumia silaha hadi kuwa tishio kwa polisi tafsiri yake ni kwamba wanaonyesha kuchukizwa na kitendo cha watawala wachache kujilipa fedha za umma na kugawia mali za umma mchana kweupe huku mamilioni ya wananchi wakiachwa na umaskini wao.

Baadhi ya wananchi waliochoka kuwashangaa watawala wakijitajirisha kwa mali za umma (pengine na polisi wakiwepo) wameamua kutafuta silaha hata kama ni kuvamia vituo vya polisi na kuwauwa polisi ili nao wapatesilaha za kujitafutia fedha na kujitajirisha kama watawala wao.

Hali hii ni hatari kwa mustakabali wa amani ya nchi yetu. Lakini cha kushangaza ni kwamba Dr Magufuli hajui kwamba hata pale mamilioni ya wananchi walipotaka kuisaidia nchi kuondoa mfumo huu wa utawala unaozalisha makundi mengi ya kihalifu katika jamii—majambazi, panya road, wezi wa kutumia kalamu na sheria na kadhalika, CCM na serikali yake walikataa.

Wananchi walipendekeza Katiba Mpya CCM na serikali yake ikakataa kata kata na kuyazika maoni hayo pale Dodoma tena kwa mbwembwe na kutukana wananchi mwaka 2014 hili hali fedha bilioni 130 za wananchi zilikuwa zimetumika kwa ajili ya hicho kilichoitwa Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi nyingine wakigawiwa wanaCCM laki tatu kila mmoja kila siku kwa miezi karibu mitatu.

Kiburi na jeuri ya watawala wa serikali ya CCM kukataa ushauri wa wananchi kutengeneza Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi ili kupunguza pengo la utajiri kati ya watawala na wananchi ndiyo sababu ya wananchi kuikataa CCM hata kama CCM itafanya propaganda za kifisadi kuonyesha inapendwa.

Tena wananchi wanajua kuwa Dr Magufuli akichaguliwa kuwa Rais maana yake ni kwamba serikali ya CCM itaendelea kuwa madarakani kwa kiburi kikubwa zaidi na hivyo majambazi papa wataendele kufurahia nchi huku majambazi dagaa wa ukweli na wa kusingiziwa maisha yao yakikatisha kikatili.

Wananchi wanaona ni kilio tuendako kama hivi ndivyo Dr Magufuli ameamua kushughulikia ujambazi---kuwauwa papo hapo majambazi dagaa na majambazi papa wakipewa heshima ya Jamhuri yetu!

Wananchi wanafahamu kuwa Magufuli akiingia madarakani ujambazi hautakwisha kwa kuuwa majambazi wa ngazi za chini wanaotumia silaha ili hali majambazi wakubwa wanaotumia vyeo vyao vya utawala wakiendelea kukwapua fedha za umma bila kuguswa si hata kwa kuuwawa bali hata kufikishwa mahakamani sheria ichukue mkondo wake dhidi yao.

Kwa mkakati huu wa Dr Magufuli wa kushughulikia majambazi dagaa peke yake tena kwa kuwauwa kikatili huku majambazi papa wakipeta, amani ya nchi itawekwa rehani.

Hii ni kwa sababu hasira ya wananchi zitaongezeka siyo tu dhidi ya polisi bali dhidi ya kila chombo ambacho serikali itakitumia kudhibiti umma unaotamani mabadiliko ya mfumo wa uongozi unaowafanya wananchi wengi kuwa maskini hadi kuamua kuwa majambazi wa kutumia silaha kutoa raia wenzao roho ili kupata fedha waishi maisha ya kufanana na watawala wao.

Kwa hiyo ni vema CCM wakati huu wa kampeni isijidanganye, iwe ni kwa kutumia tafiti za kimkakati ama propaganda nyingine zozote kuwa wanakubalika kwa mamilioni ya wananchi wanaoteseka kwa umaskini na hivyo eti watashinda uchaguzi.

Hata mbinu safi na chafu zikitumika na CCM wakishinda, siyo watakuwa wameshinda kwa sababu wanastahili kushinda la hasha, bali watakuwa wameshinda kwa sababu adui mkubwa kuliko maadui wote nchini kwetu—adui ujinga bado yupo na anaendelea kuitesa nchi.

CCM na mgombea wao wa Urais Dr Magufuli wanapaswa kuwa na miwani itakayowaelekeza kuona kuwa kitendo cha raia wenye silaha (majambazi dagaa) kuvamia kituo cha polisi na kuuwa polisi, ni ishara tosha ya amani kutoweka nchini –maana ni mwanzo wa vita vya kudai haki kati ya kati ya wananchi na polisi—kati ya wananchi na serikali yao.

Ni vita kati ya watawala wachache matajiri na wananchi mamilioni malofa mafukara---ni vita ngumu na vita hatari kwa nchi –vita inayohitaji yeyote atakayechaguliwa kuwa Rais katika uchaguzi wa mwaka huu 2015 kuhakikisha kuwa serikali yake inatafakari na kuweka misingi thabiti ya kumaliza vita hii na si kwa kuruhusu polisi kuuwa majambazi dagaa.

Ni mapambano kati ya polisi na raia majambazi ni ishara tosha kwamba wananchi wameichoka serikali ya CCM iwe inaongozwa na Dr Magufuli au mwanamuziki maarufu nchini Diamond au mwana CCM yeyote mwingine atakayedhaniwa ni kivutio kwa wananchi.

Kadhalika CCM wanapaswa kufahamu kuwa kwa wananchi wengi kushabikia upinzani ni ishara nyingine tosha kwamba wananchi wameichoka CCM na serikali yake wanataka mabadiliko ya uongozi wan chi yao.

Wananchi wamechoka ufisadi wa kimfumo unaofanyika chini ya serikali CCM kuruhusu fedha za wanachi kukwapuliwa kijambazi kutoka benki za nchi na wahusika hawachukuliwi hatua za kisheria.

Hivyo suluhisho siyo kuuwa upinzani au kutukana wapinzani wakati huu wa kampeni, au kuharibu uchaguzi ulinaogharimu mabilioni ya fedha, bali jambo jema ni kukubali demokrasia ichukue mkondo wake ili nchi iweze kuweka mfumo mpya wa utawala ambao misingi yake wananchi wamependekeza kwenye Rasimu ya Katiba Mpya.

Kwa hivyo kama kweli CCM na serikali yake wanaitakia mema Tanzania yetu ---hasa amani ya kweli inaotokana na wananchi wengi kuridhika na uongozi wa nchi yao ni vema na ni muhimu sana wakaheshimu maamuzi ya wananchi watakayoyafanya kupitia sanduku huru la kura hapo tarehe 25 Oktoba mwaka huu 2015. Mungu ibariki Tanzania.

Note: Ninaruhusu yeyote mwenye kutaka kuisambaza, kuichapisha Makala hii afanye hivyo. Lengo sote tushiriki kuijenga Tanzania yetu.




Ananilea Nkya
 E-mail:ananilea_nkya@yahoo.com

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments