[wanabidii] Kwa nini Rose Kamili si kamili

Wednesday, September 09, 2015
Kwa nini Rose Kamili si kamili
 
MALUMBANO ya kisiasa nchini yanazidi kupamba moto baada ya mke wake wa zamani wa Katibu Mkuu wa zamani wa Chadema Dk Willibrod Slaa, Rose Kamili kuibuka na kusema amesikitishwa na kauli alizozitoa mume wake huyo alipozungumza na waandishi wa habari Septemba Mosi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kamili alisema wakati Dk. Slaa anatangaza kung'atuka kwenye siasa alisema amekuwa akila mihogo na familia yake, jambo ambalo si la kweli. Alisisitiza kuwa japokuwa mihogo siyo chakula kibaya, lakini watoto wake, Elimiana na Linus Slaa hawakuwahi kuishi kwa kutegemea chakula hicho ingawa walitelekezwa na baba yao tangu mwaka 2010.

Kamili ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu wa Chadema, alisema Dk Slaa aliwadanganya wananchi aliposema kuwa haongei na mgombea wa urais wa Chadema anayeungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa na Waziri Mkuu wa zamani Frederick Sumaye kuwa siyo kweli kwa kuwa amekuwa akiwasiliana na viongozi hao.

Alisimulia kuwa mwaka 1995 wakati Dk Slaa alipoenguliwa na CCM kugombea ubunge Jimbo la Karatu, alikwenda nyumbani kwa Lowassa kuomba ushauri. Lowassa alimshauri ajiunge na chama chochote na kuongeza kwamba marafiki zake Dk Slaa nao walimshauri aingie chama chochote.

Alisema anamshangaa anavyosema haongei na Lowassa na kuhoji hizo chuki anazosema yeye kama padri mstaafu zinatoka wapi? Kwa hakika, Mama Kamili ameshindwa kuonyesha uongo wa Dk Slaa zaidi ya kuidhalilisha familia yake.

Nasema hivyo kwa sababu kauli ya Dk Slaa kuwa alikuwa akishindia mihogo na familia yake ili aisadie Chadema ni lugha ya picha ambayo haikuwa na maana kuwa kweli walikuwa wakila mihogo.

Alichokuwa akimaanisha Dk Slaa ni jinsi alivyojitolewa kuisaidia Chadema kwa hali na mali ikiwamo kutokuwa karibu na familia yake na hata wakati mwingine kulazimika kutoa fedha zake yake ya mfukoni ili chama hicho kiimarike, lakini hakumanisha familia ilikuwa ikilala njaa.

Sidhani kama Mbunge huyo hajui lugha za alama kiasi kwamba alazimishe kupindisha maneno ya mzazi mwezake kwa ajili ya kunufaisha Ukawa.
 
Kama Mama Kamili anadiriki kumsema Dk Slaa kuwa anatumiwa kisiasa na CCM kwa kuwa alisema aliyoyasema, anataka kutuambia hata yeye basi anatumiwa na Ukawa kumdhalilisha mzazi mwenzake hadharani?
Ni jambo la hatari sana mama huyu kukubali kuisambaratisha familia yake kwa kukubali kutumika kisiasa kisiasi hicho.

Tuhuma kwamba Dk Slaa ni dhaifu kwa wanawake tena likitolewa mbele ya watoto wake, linaonyesha kuwa Rose Kamili hajakamilika.

Nasema hajakamilika kwa sababu kwa mwanamke ambaye amekamilika huwezi kuwabeba watoto wako wakubwa wenye watoto wao kwenda kumdhalilisha mzazi mwezako katika televisheni. Hii kwanza inawajengea watoto chuki dhidi ya baba yao na kingine kuwadhalilisha mbele ya jamii.
Kama Rose Kamaili anadai kuwa ametelekezwa na Dk. Slaa tangu mwaka 2010, alipeleka wapi mashtaka ya kutelekezwa ? Je, anataka kuuaminisha umma kwamba Dk Slaa hajali familia yake?

Naamini Rose Kamili ni Mbunge ambaye anajua haki zake kwa vyovyote vile hangeweza kwa muda wote ule kukaa kimya wakati anaonewa, hadi leo ndipo aibuke. Rose Kamili anacheza siasa, tena siasa zenyenye ni nyepesi ambazo hazina mashiko.

Tuhuma nyingine kwamba Dk Slaa kaahidiwa ubunge na uwaziri kama CCM itashinda. Nayo ni hoja nyepesi kwa sababu hivi kiongozi akikosoa Chadema lazima awe anatumika ?

Ina maana Chadema inaongozwa na malaika ambayo haina matatizo kiasi kwamba ionekane kwamba mtu akiinyoshea kidole kuikosoa tayari huyo anatumika na CCM ?

Nadhani Rose Kamili na watu wengine wenye mwelekeo kama huo wanapaswa kufahamu kwamba kila mahali kuna mazuri na mabaya.
Alichokifanya Padri Dk Slaa kuonyesha hisia zake za kutofautiana na mawazo ya wenzake kuhusu ujio wa mgombea wa urais kupitia Katibu ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.

Ndiyo maana baada ya kuona kuwa mawazo yake yamezidiwa na wengine wakati akiona kuwa kushiriki katika jambo hilo ni kuumiza nafasi yake aliamua kuandika barua ya kujiuzulu wadhifa wa katibu mkuu wa Chadema.
Hiyo ndiyo demokrasia ya kweli kwenye jambo ambalo unaona hukubaliani nalo. Uamuzi wa Dk Slaa sio wa kwanza kufanyika unafanyika katika vyama vingine.

Uamuzi alioufikia aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba wa kujiuzulu wadhifa wake kupinga kukaribishwa kwa Lowassa ndani ya Ukawa, unafanana sana na ule wa Dk Slaa.

Huwezi kusema kuwa viongozi hao wote kwa umoja wao wamehongwa na CCM ili kuihujumu Ukawa. Mbona hivi sasa tunashuhudia makada wengi wa CCM wanahamia Ukawa, ina maana nao wamehongwa ?

Mhemuko wa kisiasa uliopo sasa nchini usiwe kikwazo, watu waachwe atoe uamuzi wao wa kuhamia chama kipi ili mradi hawavunji sheria za nchi.
 
Raia Tanzania

Share this :

Related Posts

0 Comments