Gazeti la Mizani Toleo Na. 156
31/07/2015
Ujumbe wa ijumaa
Tujiandae kisaikolojia kupokea matokeo ya kushinda
au kushindwa katika uchaguzi wa Oktoba
Assalam Aleykum, ndugu zangu Waislamu na wasomaji wote wa ukurasa huu wa ujumbe wa Ijumaa. Ujumbe unaowajia kila siku ya ijumaa kupitia gazeti hili ukijaribu kueleza, kufafanua na kujibu baadhi ya changamoto za kijamii zinazoikabili jamii yetu, kuanzia ile ya Kiislamu na ile ya Kitanzania kwa ujumla wake.
Leo katika ujumbe wa Ijumaa tutajikita zaidi katika masuala ya siasa za nchi yetu na mustakabali wa amani yetu, wakati huu tunapoelekea katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, hapo mwezi Octoba mwaka huu.
Awali ya yote tumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi kwa kutuwezesha tena kukutana katika ijumaa hii tukiwa wenye afya njema hata kuweza tena kudurusu ukurasa wetu adhimu wa ujumbe wa Ijumaa.
Ama baada ya shukrani hizo tumuombe pia ainusuru nchi yetu pamoja na sisi wenyewe kutokana na majanga na shari zote ambazo zinaweza kusababishwa na harakati za kisiasa zinazoendelea sasa katika nchi yetu tunapoelekea katika uchaguzi huo mkuu.
Ndugu zangu Waislamu na wasomaji wengine, imenilazimu leo kuangalia masuala haya ya kisiasa kutokana na ukweli kwamba hali ya kisiasa iliyopo sasa katika nchi yetu ni tofauti kabisa na ile tuliyoizoea huko nyuma.
Hali hii ni lazima kuchukuliwa tahadhari za dhati katika Saikolojia za wananchi tukiwa njiani kuelekea katika uchaguzi mkuu, wakati wa uchaguzi wenyewe na kubwa zaidi wakati wa kuyapokea matokeo ya uchaguzi huo.
Kwa miaka yote tangu tuingie katika mfumo wa vyama vingi, ilikuwa ni kawaida kwa fikra za wananchi kuamini kwamba pamoja na ushiriki wa vyama vingi katika chaguzi mbalimbali za kisiasa, lakini matumaini makubwa ya ushindi yalikuwa yakielekezwa moja kwa moja kwa chama cha Mapinduzi. Chama kikongwe kuliko vyote katika siasa za nchi yetu, na ambacho kimetawala nchi kwa kipindi chote toka uhuru.
Bila shaka safari hii mambo yamegeuka, ambapo ni wazi kwamba ushindani unaelekea kuwa wa nusu kwa nusu au hata katika baadhi ya maeneo CCM kuonekana kuzidiwa katika mvuto wa kisiasa.
Hata maeneo ambayo yalikuwa ngome kubwa za CCM sasa mabadiliko yanaonekana wazi. Watu wanaeleza waziwazi misimamo yao ya kisiasa hata kama ni ya kuipinga CCM, lakini kubwa zaidi ni kwamba, utendaji wa chama hicho umekuwa ukikosolewa waziwazi hata ndani ya chama chenyewe ikiwa ni pamoja na wakubwa wa vikao nyeti kutoka nje ya vikao na kutoa nje siri za vikao hivyo jambo ambalo halikuwahi kuonekana hata mara moja huko tulikotoka. Hii ni ishara mbaya mno kwa mustakbali wa CCM.
Kwa vyovyote jambo hili litakuwa na athari fulani hata kama kwa sasa bado hazijaanza kuonekana kwa kiwango kikubwa zaidi. Ndio maana nimeona leo nijaribu angalau kidogo kuliongelea jambo hili na kutoa nasaha zangu sio tu kwa vyama vya siasa na wanasiasa watakaoshiriki moja kwa moja vinyang'anyiro vya uchaguzi, lakini pia hata kwa wananchi ambao ndio hasa wapiga kura na washabiki wakubwa wa vyama hivyo pamoja na wanasiasa.
Hadi hapa tulipofikia sasa yako mambo kadhaa ambayo ndiyo yameonekana kupandisha joto la kisiasa katika nchi yetu. Mambo ambayo ni lazima kuwekewa tahadhari za kutosha kwa vile yana nafasi kubwa ya kutuachia athari chanya au hasi katika mustakabali wa amani na usalama wa nchi yetu baada ya uchaguzi kama hayataangaliwa kwa umakini.
Miongoni mwa mambo hayo ni chuki tu ya baadhi ya wananchi kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayosababishwa na malalamiko ya muda mrefu ya vitendo vya rushwa na ufisadi ambavyo chama hicho kimeonekana kushindwa kabisa kuvishughulikia kwa maana ya kuvidhibiti vitendo hivyo.
Kwa miaka yote CCM imeonekana zaidi kuendeleza siasa za kulindana na kuwafanya baadhi ya watu kuwa kama Miungu watu na wenye hati miliki ya uchumi na rasilimali za nchi, huku hatua dhidi ya wahalifu zikiwaelemea baadhi ya watu tu jambo ambalo limeleta taswira mbaya.
Haya yakichanganywa na kashfa za kila siku za vitendo vya Ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za nchi huku wananchi wakizidi kutapatapa katika lindi la umasikini, yamezidi kuvipa turufu vyama na wanasiasa wa Upinzani ambao siku zote mtaji wao wa kisiasa umekuwa ni maslahi ya wananchi.
Hakuna ubishi wowote kwamba sasa hivi siasa za nchi yetu zimebadilika sana na hamasa ya wananchi kushiriki masuala hayo zimekuwa kubwa kuliko wakati wowote katika historia ya nchi yetu.
Tangu tupate uhuru na hususani tangu turejee katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, hakuna wakati wowote ambapo hamasa na joto la kisiasa liliwahi kupanda kwa namna inayoonekana sasa, hususan katika zoei linaloendelea hivi la uandikishaji wananchi katika daftari la kudumu la wapiga kura ambapo vijana wengi wamejitokeza na wanaeleza wazi dhamira yao ya kujiandikisha kwa wingi kiasi hiki.
Aidha makundi hayo ya vijana ambayo zamani yalijiweka mbali kabisa na masuala ya siasa, sasa yamekuwa mbele kutambua na kutekeleza haki na wajibu wao katika masuala ya siasa za nchi, lakini kwa namn ya pekee umekuwawepo msukumo ambao unaonekana ni kukerwa na na wenye kukusudia kubadili mfumo uliopo kwenda kwenye mfumo mwingine japokuwa sina hakika kama wana uelewa wa kutosha juu ya changamoto watakazokutana nazo katika kutimilika kwa dhana inayowasukuma.
Kwa vyovyote hamasa hii haikuja hivihivi isipokuwa zimekuwepo sababu zilizopelekea makundi haya kukumbuka haki na wajibu wao wa kiraia. Na bila shaka sababu hizo zitakuwa ni kujisahau kwa chama kinachotawala kuisimamia serikali yake kiasi cha kuwafanya baadhi ya watu kuiona nchi kuwa kama mali ya kundi la watu fulani ambalo limejenga mfumo unaoonekana katika picha ya tabaka la watawala na watawaliwa.
Ndugu zangu, kwa hali ilivyo sasa ni wazi kwamba wananchi katika makundi mbalimbali wanaonyesha wazi hamu kubwa ya kutaka mabadiliko ya kisiasa, kuanzia ya watu mpaka ya mifumo. Mabadiliko ambayo awali yangeweza kufanywa ndani ya CCM yenyewe na kuwaridhisha wananchi sasa yanaonekana kutafutwa zaidi nje ya CCM hasa baada ya chama hicho kuonekana wazi kutokuwa na uwezo au utashi wa kuyafanya.
Yenyewe imeendelea kubuni misemo na misamiati yenye kuhubiri mabadiliko, kama vile kuvua gamba, kutofautisha siasa na biashara, vita dhidi ya ufisadi na kadhalika, lakini kamwe haikuweza kusimamia na kutekeleza dhamira hizo kwa kiwango kinchoridhisha. Matokeo yake wananchi wamechoshwa na nyimbo hizo na sasa wanatafuta ufumbuzi nje ya CCM.
Hata hivyo, ndugu zangu, hamu hii kubwa ya mabadiliko inahitaji kuwa na udhibiti fulani. tena udhibiti wa watu wanaofahamu vyema maana na athari za mabadiliko ya mifumo ya kisiasa huku wakitanguliwa na dhamira njema ya maslahi ya nchi na wananchi.
Sasa hivi dhamana hiyo ya mabadiliko ya kisiasa baada ya kushindwa kutekelezwa na CCM, inaonekana wazi kuwekwa katika mikono ya Wapinzani. Wapinzani ambao siku zote wamejipambanua kuwa manabii waliobeba maono na wahyi wa kuwakomboa wananchi kutoka katika madhila yanayowakabili kwa kusababishwa na utawala mbovu wa CCM kwa mujibu wa madai yao wenyewe.
Kimsingi si jambo baya lakini ni lazima watu wawe na uhakika na usafi wa mikono hiyo. Hii ni kwa ajili ya kuepuka aina ya mabadiliko yanayoweza kuitoa nchi katika hali mbaya kuipeleka katika hali mbaya zaidi. Uhubiri wa siasa zinazoambatana na ahadi za miujiza ni lazima ufikiriwe kuanzia mara moja hadi mara elfu moja kabla ya kuuamini na kuushabikia.
Ndugu zangu suala lingine kubwa lililotufikisha katika hali ya kisiasa tuliyopo sasa ni maamuzi yasiyo makini ya uongozi wa CCM yenyewe katika kipindi cha utawala wa awamu ya nne. Katika kipindi hicho tumeona serikali ya CCM ikifanya maamuzi mengi ya pupa ambayo bila shaka ndiyo yaliyowasaidia wapinzani wake kupanda chati ya kisiasa na kuwa tishio la kweli kwa mustakabali wa CCM katika uchaguzi wa Oktoba.
Maamuzi kama ya kuanzisha mchakato wa katiba mpya ambao haukuwa na ulazima wowote kimazingira wala mahitajio ya wananchi, umekuwa mtaji mkubwa wa kisiasa kwa vyama vya upinzani hasa pale mchakato wake ulipoonekana kuishinda serikali na kuiacha hatma yake katika sintofahamu kubwa. Kila mmoja wetu anakumbuka vema kuwa ni suala la katibu mpya lililowanufaisha wapinzani na kupelekea kuunda kile kinachoitwa UKAWA ambao leo imekuwa ni nguvu inayowapa nguvu waliokuwa hawana nguvu.
Kama nilivyotangulia kusema kuwa, mchakato huo wa katiba ambao ulianza wakati vyama vyote vikubwa vya upinzani vikiwa katika hali mbaya ya migogoro ya ndani, ndiyo uliopelekea kuanzishwa kwa umoja wa UKAWA ambao sasa ni tishio la kweli kwa mustakabali wa CCM.
Msisimko uliosababishwa na ushirika wa vyama vya siasa vya upinzani vyenye nguvu. ushirika huu ambao ulianzia ndani ya bunge maalumu la katiba na kujipatia jina lake la Umoja wa Katiba ya wananchi, UKAWA, umefanikiwa kujijengea mtaji mkubwa wa wafuasi hasa kutokana na athari za serikali kwenda kinyume na mapendekezo ya tume ya katiba ya Warioba.
Ni jambo lililo wazi kuwa umoja huu haupo kisheria na hivyo hata makubaliano yao hayapo kisheria japokuwa mpaka sasa umeonekana kuwa na mshikamano mkubwa na kuaminiana. Katika fikra za kawaida bila shaka tayari umoja huo umeshafanikiwa kuwa tishio la kweli kwa Chama cha mapinduzi kinyume na ilivyokuwa matarajio ya wengi pale ulipokuwa ukianza.
Hata hivyo upande mwingine umoja huo unaweza kutizamwa kama bomu la kisiasa linaloweza kulipuka wakati wowote mara watakapofanikiwa kuiangusha CCM na kuchukua madaraka kwa vile makubaliano yao yote hayako kisheria na hivyo atakayefanikiwa kuwa rais anaweza kuwageuka wengine kwa kadiri atakavyopenda. Jambo hilo likitokea lazima litasababisha msukosuko mkubwa kisiasa na hata kiusalama.
Sintofahamu nyingine ambazo zimeendelea kuukabili UKAWA na hata viongozi wa vyama vinavyouunda kukiri, ni ile ya migawanyo ya ruzuku na maslahi mengine. Haya yote ni mambo ambayo yanaweza kusababisha mkorogano mkubwa ndani ya serikali itakayoundwa na umoja huo endapo utafanikiwa kuchukua madaraka.
Wakati utata huu ukiendelea ndani ya makubaliano ya UKAWA, jambo lingine limetokea ambalo sio tu limezidi kuuongezea nguvu na ushawishi umoja huo lakini zaidi lina hatari kubwa ya kuleta mpasuko na mtikisiko ndani ya CCM.
Tukio hili ni lile la kuhama kwa kada maarufu na mashuhuri wa CCM kwenda chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, ambacho ndio nguzo kuu ya UKAWA. Mbaya zaidi akiaminika kwamba ameenda huko kwa dhamira ya kugombea Urais kupitia umoja huo huku akitarajiwa kufuatwa na kundi kubwa la wafuasi wake kutoka ndani ya CCM.
Ndugu wasomaji, mara nyingi tumekuwa tukirejea kauli ya Mwalimu Nyerere kwamba pamoja na uwepo wa vyama vingi katika Tanzania tangu mwaka 1992, lakini upinzani wa kweli utatokea ndani ya CCM yenyewe.
Miaka kadhaa baada ya kauli hiyo sote tumeshuhudia ndugu Edward Lowassa, akitoka CCM kwa kishindo kikubwa tena katika wakati ambapo CCM inahitaji mno mshikamano na umoja wa wanachama na washabiki wake ili kukabiliana na vuguvugu kubwa la mabadiliko la UKAWA. Tuliyaona Dodoma ni ishara tosha na kubwa inayoashiria anguko la CCM kutokana na ukweli kuwa mgawanyiko au mpasuko ndani ya CCM halikuwa jambo linaloweza kujificha tena.
Kwa vyovyote hii si jambo dogo kwa CCM na zaidi kwa siasa za nchi hata kama wenyewe wameendelea kujifariji kwamba kitendoo cha Lowassa hakina tofauti na kile cha Lyatonga Mrema ambaye baadaye alikuja kubaini kwamba kuhama kwake hakukuwa na athari zozote kwa chama hicho.
Hata hivyo hii inaweza kuwa ni namna tu ya kujifariji kwa chama hicho kwa vile hali ya kisiasa iliyopo sasa katika nchi ni tofauti kabisa na ile iliyokuwepo wakati wa kuhama kwa Mrema. tukiacha ukweli kwamba Mrema hakuwa na washabiki kama alivyo Lowassa, lakini ni kweli pia kwamba chama chenyewe kilikuwa na watu wenye nguvu kubwa ya kudhibiti mihemuko ya kisiasa ya wanachama na wananchi kuliko ilivyo sasa ambapo hata kuheshimiana kumepotea kabisa ndani ya chama chenyewe.
Bila shaka hii inaweza kuwa hatua mpya na muhimu kuelekea mabadiliko makubwa ya kisiasa ambayo yanaweza kuiweka CCM nje ya madaraka kwa mara ya kwanza. Suala hapa ni, je CCM wataipokeaje hali hiyo? Na je viongozi wake watakuwa tayari kupokea matokeo ya maamuzi ya hukumu ya wananchi kupitia sanduku la kura?
Kwa upande wa pili ni lazima tuangazie matumaini yaliyovuka mpaka ya wapinzani kuamini kuwa huu ndio wakati wao kuiweka Dola na vyombo vyake mikononi mwao. Hii ni dhana nzuri na ni mbaya pia. Ni nzuri iwapo itaambatana na ukweli kwamba siasa matokeo ya ushindani daima ni mawili. Nayo ni kushinda na kushindwa.
Wakati CCM ambayo ni chama kikongwe kinachohusika na mapambazuko ya uhuru na kuipeleka nchi hadi kuifikisha mahala ilipo sasa ikiwa na mtaji wa hakika wa kuwapelekea wananchi maendeleo yanayoonekana kila mahala walipo, wapinzani watakuwa na mtaji duni ambao ni kueleza mahala CCM ilipokosea au kuzembea huku na kutoa ahadi ambazo ni za kinadharia bila mfano. Katika hali kama hiyo si jmbo la busara kujenga matumaini yalivuka mpaka.
Kwa mtazamo huo wacha niitumie kalamu yangu leo kuwaomba wanasiasa wote, wagombea na wapenzi wa vyama vya siasa hapa nchini, tuanze zoezi la kujijenga kisaikolojia kwamba katika mashindano yoyote kuna mshindi na mshindwa.
Tujiweke tayari kupokea na kukubali matokeo ya ushindani. Kukataa kushindwa ni jambo la hatari ambalo kwa hakika utakuwa mwanzo wa kulipeleka taifa katika vurugu na ukosefu wa amani na usalama, na hali itakapofikia hapo hakuna atakayekuwa mshindi wala mshindwa, na hapatakuwa yeyote miongoni mwetu atakayefaidika na uwepo wa ushindani wa vyama vingi vya siasa.
Wabilllahi Taufiiq
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments