(16) Uhuru mkubwa ambao viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini waliutumia bila wasiwasi katika kuhakikisha kwamba kampuni waliyoitaka, Richmond Development Company LLC, inapewa zabuni ya umeme wa dharura; maelekezo ya mara kwa mara ya Waziri Mkuu kwa Wizara katika kila hatua ya mchakato huo; upendeleo wa dhahiri ambao Richmond Development Company LLC iliupata kutoka taasisi mbalimbali za Serikali k.m Kituo cha uwekezaji (TIC) ambacho kilifikia hatua ya kufumbia macho baadhi ya taratibu zake za msingi ili kuipa kampuni tanzu ya Richmond Development Company LLC cheti cha uwekezaji haraka iwezekanavyo; kutotimiza masharti ya Bodi za Makandarasi na Wahandisi na Wizara ya Nishati na Madini kuikingia kifua kampuni hiyo isichukuliwe hatua za kisheria; uteuzi wa mwisho wa Richmond Development Company LLC kuwa mkandarasi kufanywa na Waziri Mkuu mwenyewe tarehe 21 Juni 2006;
uamuzi wa kuiteua Richmond Development Company LLC kuwa mkandarasi kusafishwa na TAKURU ( sasa TAKUKURU) kuwa ulikuwa wa wazi na wa haki; uamuzi wa Serikali kuizuia TANESCO isivunje mkataba na kampuni hiyo licha ya sababu zote kisheria kuwepo, ni baadhi tu ya viashiria vya nguvu kubwa iliyo juu ya Wizara ya Nishati na Madini kutumika katika suala hili na Kamati Teule kutokana na ushahidi wa kimaandishi, kimazingira na wa mdomo, inaiona nguvu hiyo kuwa ni Waziri Mkuu.
Ibara ya 52 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 inatamka wazi kuwa Waziri Mkuu ndiye mwenye madaraka ya juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa siku hadi siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano na ndiye Kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni.
Kamati Teule haikufurahishwa hata kidogo na taarifa hizo zinazomgusa moja kwa moja Mhe. Waziri Mkuu katika kuipendelea Richmond Development Company LLC. Hata hivyo Kamati Teule imetimiza wajibu wake kwa uwazi na ukweli kama ilivyoagizwa na Bunge letu Tukufu.
Kwa kuzingatia umuhimu wa nafasi aliyonayo Mhe. Waziri Mkuu katika uendeshaji wa shughuli za Serikali na uongozi wa nchi kwa ujumla, ni wajibu wake yeye mwenyewe kupima uzito wa matokeo ya uchunguzi huu na wajibu wake kikatiba ndani na nje ya Bunge. Vile vile ni wajibu wa Bunge ambalo linathibitisha uteuzi wake kwa mujibu wa Ibara ya 51 inayothibitisha uteuzi wake.
Kuangalia ikiwa matokeo ya uchunguzi huu hayajaathiri hadhi na uzito wake ndani ya Bunge.
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia Kamati Teule ya Bunge ilifadhaishwa sana na tabia ya baadhi ya watendaji wa Serikali ya kukaidi amri ya kuwasilisha nyaraka zinazohitajika na Kamati Teule. Kamati Teule inaliomba Bunge litafakari kitendo cha aina hii na kufikiria hatua za kuchukua dhidi ya watendaji wa namna hiyo.
Mhe. Dk. Harrison G. Mwakyembe
MWENYEKITI
KAMATI TEULE YA BUNGE
06 Februari 2008
0 Comments