[wanabidii] Mbeya wahoji uadilifu viongozi wa Ukawa

Wednesday, August 19, 2015


Felix Mwakyembe

 

  Chadema sasa wakwepa ajenda ya ufisadi

    Kauli ya kumwachia Babu Seya yashtua polisi


MKUTANO wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Luanda jijini Mbeya wiki iliyopita, umeacha simulizi na mikanganyiko miongoni mwa wakazi wa jijini hapa.

Umati uliohudhuria mkutano huo umeacha simulizi kutokana na wingi wa watu wakiwa kutoka wilaya zote za Mkoa Rukwa, Iringa na Ruvuma.


Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ujio wao ulikuwa mahsusi kwa ajili ya kutafuta wadhamini wa mgombea wao, Edward Lowassa, ambaye naye alihutubia mkutano huo kwa muda usiozidi dakika ishirini.

Hotuba ya mgombea huyo iliacha mkanganyiko pale alipotoa ahadi ya kumwachia mwanamuziki nguli wa dansi nchini, Nguza Vicking anayetumikia kifungo baada ya kukutwa na hatia, ikiwamo ya kuwanajisi watoto.


Baadhi ya watu waliokuwapo mkutanoni hawakusubiri kuitafakari ahadi ile baadaye, bali walianza mjadala muda ule ule, wakihoji mantiki ya ahadi ya mgombea huyo kumwachia huru mtu ambaye hata Mahakama ya Rufaa nchini ilimtia hatiani.


"…kumwachia Babu Seya tena, hii kali ya mwaka, wale majaji wa Mahakama ya Rufaa wako vizuri sana, asingekuwa na hatia wangemwachia,"alisikika askari mmoja wa Jeshi la Polisi aliyekuwapo mkutanoni pale mara baada ya ahadi hiyo kutolewa.


Mbali ya ahadi hiyo yenye shaka kutoka kwa mgombea huyo wa Ukawa, ahadi yake hiyo, iwapo itatekelezwa, inatajwa kuwa ni sawa na uvurugaji wa utawala bora, lakini pia naye Mwenyekiti wa Chadema alifanya tukio lililodhihiri baadaye kuwa ni kituko cha aina yake.


Mbowe, kwa mbwembwe, aliwatangaza wanachama wapya waliojiunga na chama hicho siku hiyo ya mkutano, na miongoni mwao ni wabunge wawili waliomaliza muda wao, Mchungaji Luckson Mwanjale, Jimbo la Mbeya Vijijini na Modestus Kilufi, Jimbo la Mbarali. Wote wakiwa kutoka CCM.

Hata hivyo ni Kilufi pekee aliyejitokeza uwanjani pale na kutambulishwa, wakati Mwanjale aliitwa mara kadhaa na Mbowe pasipo kutokeza. Akiwatambulisha, Mwenyekiti huyo wa Chadema alisema; "walipokuwa katika chama chao cha zamani walitufanyia nanihino, tuwapokee!"


Mwenyekiti huyo aliitikiwa na umati uliokuwepo wakisema wapokee, lakini muda wote huo Mchungaji Mwanjale hakuwepo uwanjani hapo, hatua iliyosababisha Mbowe kutoa kauli nyingine tata akidai inawezekana mbunge huyo amechelewa kutokana na msongamano wa magari lakini angefika uwanjani hapo.


Kutokana na tukio hilo la kutangazwa na kutonekana, waandishi wa habari walianza kumtafuta Mwanjale ili kupata kauli yake na alipopatikana alionyesha kushangazwa na taarifa hizo za yeye kujiunga Chadema, akisema hajawahi kuwaza jambo hilo na kwamba asingeweza kujiunga na chama hicho kabla ya kushauriana na familia yake.


Katika mahojiano yake na Raia Mwema kwa njia ya simu, Mchungaji Mwanjale alisema kuwa wakati msafara wa Lowassa ukiwasili katika Uwanja wa Ndege Songwe, naye alikuwepo akiwa pamoja na jamaa zake na kwa sababu ni mtu wanayefahamiana alisalimiana naye.


Mchungaji Mwanjale anasema inawezekana lile tukio la yeye kusalimiana na Lowassa lilichukuliwa kimakosa na baadhi ya watu wakiwemo viongozi wa Chadema, kwamba kwao alikuwa amejiunga tayari na chama hicho.

"Makamo haya unaenda Chadema ili iwe nini, pamoja na makosa ya chama, wengine kutotendewa haki, sina mawazo ya kuhama chama," alisema Mwanjale.


Wakati mchungaji huyo akikanusha, baadhi ya wadau wa siasa za Mbeya nao wanahoji mantiki ya kiongozi mkuu wa Chadema kutangaza jambo ambalo hana uhakika nalo. Wanabainisha kuwa kama ni kweli hakukuwa na mawasiliano basi viongozi hao wanawakosea wenzao staha.


Wakati Mchungaji Mwanjale akitangazwa kwenye mkutano wa hadhara, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile naye alizushiwa kuhamia Chadema lakini katika kipindi kifupi kiongozi huyo alikanusha, akisema hajawahi kuwazia jambo hilo na kwamba bado yupo CCM na hajabadilika.


"Kwa umri wetu huu, sio kuhama vyama, bali unampigia yule unayemuona anafaa na mwenye uwezo wa kutuongoza," anasema Mzee Mwakipesile katika mahojiano ya simu na mwandishi wetu, na kuongeza; "Lowassa tunafahamiana na alikuwa kiongozi wangu, tumefanya naye kazi akiwa Waziri Mkuu mimi nikiwa Mkuu wa Mkoa, tulikuwa naye bungeni kwa miaka 10, inawezekana watu wanatumia vibaya uhusiano wetu huo."


Taarifa za kuhama kwa wanasiasa hao zilikuwepo kabla ya ujio wa Lowassa Mbeya, na wote, sababu kuu ya kuzushiwa ikiwa ni ukaribu wao na mgombea huyo wa Chadema.

"Tatizo Chadema wanatafuta watu wote waliokuwa jirani na Lowassa akiwa CCM, wanachanganya urafiki na itikadi, huo ni udhaifu mkubwa," anasema Charles Mwakipesile aliyekuwa miongoni mwa watangaza nia wa CCM na kushika nafasi ya tatu katika kuwania ubunge Jimbo la Mbeya Mjini.


Mwakipesile ambaye pia anashikilia nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya CCM anasema kuwa wanachama wenzao wanaokimbilia Chadema baada ya kushindwa kwenye kura za maoni wanadhihirisha umamluki wao walipokuwa ndani ya chama hicho.


"Mtu amekuwa kiongozi wa miaka mitano, leo anaondoka baada ya kuanguka huku akitoa kashfa lukuki kwa chama kile kile alichokitumikia, ni udhaifu mkubwa," anasema Mwakipesile na kuongeza; "….mimi nawaheshimu sana wanaohama bila ya msukumo wa kuanguka kwenye uchaguzi, hao ni wakomavu wa kisiasa."


Chanzo cha ndani, waliokuwapo Uwanja wa Ndege Songwe kumpokea Lowassa vinabainisha kilichojitokeza Mchungaji Mwanjali alipokwenda kumsalimia Lowassa ni utani uliokuwepo akihamasishwa kuhamia Chadema naye akajibu, "tupo pamoja."

Chanzo hicho kinabainisha kuwa yawezekana Chadema walichukulia kauli ile kama jibu la kukubali kwa Mchungaji huyo kuhamia kwao. Katika kuthibitisha hilo, chanzo hicho kinasema ndio maana hata Mbowe alitoa kauli mbili, kwanza akisema yupo hapa, kwa maana ya mkutanoni na ilipobainika hayupo akasema inawezekana amekwama njiani kutokana na msongamano wa magari.


Katika mkutano huo walikuwepo viongozi mbalimbali wa vyama vinavyounda Ukawa akiwamo, Mgombea Mwenza katika urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Juma Duni, Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia na Dk. Emmanuel Makaidi.


Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi alikuwa miongoni mwa wazungumzaji katika mkutano huo, ambapo pamoja na mambo mengine alikituhumu Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuingiza mkoani humo shahada 5,000 za kupigia kura na kutishia akisema; "…wakijaribu kufunga goli la mkono tutatuma beki kuzuia, kule pembezoni akifunga tunakata kiganja kwa nyengo, mteule wa CCM kaingizwa bweni la zeluzelu."


Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia alimshauri Rais Jakaya Kikwete kuwa mtulivu na msikivu pamoja na chama chake katika kipindi hiki. Pamoja na ushari kwa Rais Kikwete, aliwasihi pia wananchi wa Mkoa wa Mbeya kuhubiri amani ili uchaguzi uwe wa amani pasipo kubaguana.


Hata hivyo Mwenyekiti Mwenza kwenye Ukawa, Freeman Mbowe alisema umoja huo hautapiga magoti kuwabembeleza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iwapo wataona wanaonewa bali watajibu kwa vitendo.

"Ukawa hatutopiga magoti tukiona tunaonewa, tutachukua…," akajibiwa na umati uliohudhuria "action!"


Pamoja na ahadi yake ya kumwachia Babu Seya iwapo ataingia madarakani, Lowassa pia aliahidi kulibadili Jiji la Mbeya na kuwa la kimataifa pamoja na Uwanja wa Ndege wa Songwe nao uwe wa kimataifa. Nao baadhi ya wasikilizaji katika mkutano huo wakasemezana wakihoji; "kwani sasa sio wa kimataifa?"


Katika jambo lililowashangaza baadhi ya wafuatiliaji wa siasa mkoani humo, ni hatua ya viongozi wa Ukawa kukwepa ajenda yao ya ufisadi, ajenda iliyowajenga na kuwapambanua kama viongozi makini wanaochukizwa na hali hiyo nchini ambayo imekuwa ikifichuliwa karibu kila mwaka na ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).


Katika mkutano wa Mbeya, sio Mbowe wala Mbatia au Makaidi aliyethubutu kutamka neno, fisadi au ufisadi. Hatua hiyo iliwafadhaisha baadhiya wapenzi wa mageuzi mkoani humo, wakibainisha kuwa wametelekezwa na viongozi wao.


"Watu wamepoteza maisha, Mwalukali alipigwa risasi hapa na leo hii ana ulemavu wa mkono, tuliwaamini kuwa wanapigania haki, tukaingia barabarani, leo hii wamethamni pesa zaidi kuliko sisi, siasa chafu kabisa hizi," alisikika mkazi wa Soweto beya akilalamika


Chanzo Raia Mwema Toleo la 419, 19 Aug 2015

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments