[wanabidii] LOWASSA KAFARA CCM KUJARIBU KUZUIA MABADILIKO

Friday, August 21, 2015
LOWASSA KAFARA CCM KUJARIBU KUZUIA MABADILIKO

Na Ananilea Nkya

Nimeandika hoja hii baada ya kusoma na kusikia hoja zinazotolewa na baadhi ya Watanzania kwamba eti CHADEMA , CUF, NCCR-Mageuzi na NLD -vyama vinavyounda UKAWA kwa kumsimamisha Edward Lowassa kugombea Urais vimepoteza usafi wa kuongoza mapambano dhidi ya ufisadi.

Ukweli ni kwamba viongozi wa CHADEMA na UKAWA kumsimamisha Lowassa kuwa mgombea urais wamecheza kama Pele. Tena wanastahili pongeze kubwa maana walitumia akili kali na saikolojia ya hali ya juu kubaini kuwa CCM ilikuwa ilicheza mchezo mchafu kisiasa kuwatumia wapinzania kumpakazia Lowassa ufisadi na hatimaye CCM kupata nguvu ya kumtoa Lowassa kafara ili eti CCM ionekane inajisafisha ufisadi.

Wanaodhani CHADEMA na UKAWA wamekosea pengine hawajaelewa kuwa tangu upepo wa mabadiliko wa kukataliwa mfumo chama kimoja kuwa madarakani kwa muda mrefu ulipoanza kuvuma duniani kote mwishoni mwa miaka ya 1980, baadhi ya wanaCCM hawajakubali kwa dhati kabisa ukweli huo na kuamini kwamba CCM inaweza kupunzishwa kuongoza nchi angalao kwa miaka mitano.

Hasa baada ya Mwalimu Nyerere CCM kuondoka duniani, CCM imebaki na viongozi ambao hawako tayari kutumia ujasiri kuongoza mabadiliko kwa amani. Baadhi ya vongozi wanaojali zaidi maslahi ya wana CCM wachache wanaotumia kauli kama hirizi kauli aliyowahi kuitoa Mwalimu Nyerere kuwa bila CCM imara—Tanzania itayumba kujidanganya wenyewe na kudanganya wananchi.

Wanasahau kwamba Mwalimu Nyerere kama mwanafalsafa na mwanasiasa makini alikuwa anatoa maamuzi ya kijasiri kwa faida ya taifa na wananchi kulingana na hali halisi ya wakati husika kwa kusoma upepo wa wananchi. Kwa mfano Nyerere aliwahi kusema CCM si mama yake akimaanisha Tanzania na Watanzania ni muhimu zaidi kuliko umuhimu wa CCM kuwa madarakani.

Mfano Mwalimu Nyerere mwaka 1992 alionyesha mfano kwamba maslahi ya nchi na wananchi ndiyo muhimu kuliko maslahi ya CCM alipokubali kwenda kinyume na uamuzi wa wanaCCM wengi waliokuwa wamekataaa—mabadiliko—kuanzishwa vyama vingi nchini ili vyama vibadilishane uongozi wa nchi --kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Lakini baada ya Mwalimu kuondoka dunaini kila mwanaCCM anayechaguliwa kuwa Rais, kwa kuogopa kulaumiwa kwamba eti kama CCM haitachaguliwa kupitia sanduku huru la kura atabeba lawama za kufanya CCM iondoke madarakani, serikali zote za CCM baada ya Mwalimu Nyerere kuondoka duaniani zimekuwa zinajihusisha na ufisadi.

Serikali ya CCM imekuwa ikikwapua kwa wizi wa wazi mabilioni ya fedha za umma na kufanya maovu mengine mengi kuhakikisha CCM haiondoki madarakani. Hivyo chaguzi zinafanyika kama geresha tu—kudanganya wafadhili na mataifa kuwa Tanzania ni nchi ya demokrasia ya vyama vingi.

Mfano uchaguzi wa mwaka 2005 serikali ya CCM chini ya Rais Mkapa ilikwapua fedha za wananchi kutoka Benki Kuu Akaunti ya EPA shilling bilioni 133 ambazo ziliiwezesha CCM kumweka madarakani Rais Kikwete.

Mwaka jana 2014 serikali ya CCM chini ya Kikwete ilikwapua shilingi bilioni 306 kutoka akaunti ya Tegeta escrow Benki Kuu kwa ajili ya kuiwezesha CCM kushinda uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu unaofanyika tarehe 25 Oktoba mwaka huu 2015.

CCM wakishaingia madarakani jambo muhimu kuliko yote Rais na serikali yake analolifanyia ni kubuni ufisadi wa kuipatia CCM fedha na mbinu nyingine za kuiwezesha CCM ibaki madarakani uchaguzi unaofuta. Hakuna kazi muhimu ya kuwaondolea wananchi umaskini inayofanyika kwa kiwango na juhudi kubwa.

Kwa sababu hiyo, kikundi kidogo cha watawala, wengi wakiwa ni kutoka CCM na familia zao wamejikuta wakinufaika kwa kuwa matajiri kufuru kwa muda mfupi ili hali wananchi wengi wakibaki maskini na mafukara wa kutupa.

Mfano wabunge (kikundi cha watu wasiozidi 400) wengi wakiwa ni wanachama wa CCM kila mmoja analipwa si chini ya milioni 10 kila mwezi kama mishahara, wacha marupurupu na posho za vikao vya kamati, posho za safari na mamilioni mafao kila baada ya miaka mitano. Lengo wawe na fedha nyingi za kununua kura za wapiga kura maskini uchaguzi unaofuata CCM ibaki madarakani.

Ndiyo sababu kila mwananchi wakiwepo watu muhimu kama walimu wa vyuo vikukuu na madaktari hivi sasa nao wameamua kuwa wanasiasa.

Zaidi baadhi ya wanaotafuta madaraka ya kisiasa wanatumia mbinu chafu sana ikiwa ni pamoja na ushirikina wa kuuwa watu wenye ulemavu wa ngozi (albinism) waweze kupata nafasi ya kuingia katika kundi la watawala—kupata utajiri wa kutisha katika kipindi cha miaka mitano.

Mfamo Wabunge waliomaliza muda wao mwaka huu 2015 kila mmoja ameondoka na kiinua mgongo zaidi ya shilingi milioni 200. Hii ni kufuru katika nchi inayojinasibu kuwa ni maskini na inapita huko na huko duniani kuomba misaada!

Hata hivyo kwa kadri ufukara unavyoendelea kuwatafuna wananchi wengi, na kwa kadri uelewa wa wananchi wanaoteseka kwa umaskini unavyoongezeka kwamba CCM na utawala wa serikali yake ndicho chanzo cha umaskini wao, CCM imebaini kuwa haiwezi tena kushinda uchaguzi kupitia sanduku huru la kura kwa kutegemea kete moja tu—kununua wananchi mafukara peke yake.

Hivyo katika miaka ya hivi karibuni CCM imeanza kuendesha siasa za maji taka—kuchafuana wao kwa wao na hatimaye wameamua kutoana kafara-lengo kuu likiwa ni kuzuia wananchi wasitumie sandundu la kura kufanya mabadiliko—kuchagua vyama vingine kuongoza nchi.

Hivyo Rais Kikwete, hata kama ndani ya umungu wa moyo wake hakubaliani na CCM inavyotumia ubabe kukataa mabadiliko kinyume na asili ya binadamu, amekuwa akifanya mambo kutimiza matakwa ya baadhi ya wanaCCM —kujaribu kuzuia mabadiliko—ili tu kuepuka lawama- amalize muda wake bila kuonekana ndiye kasababisha wananchi kuipunzisha CCM uongozi kwa kipindi cha miaka mitano.

Kwa kufanya hivyo Rais Kikwete amejikuta akiporwa ujasiri wake aliokuwa nao kama mwanasiasa ambaye Mwalimu Nyerere alimuamini.

Kumbuka Mwalimu Nyerere alinukuliwa na gazeti la Nipashe na Majira 26/5/95 akisema baada ya Rais Mwinyi baadhi ya vijana ambao alikuwa anaona wana nia ya dhati kabisa na uwezo mkubwa wa kuongoza Tanzania ni Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na Edward Lowassa.
Lakini kwa Kikwete kukubali kuyumbishwa na wana CCM wachache wasiokubali mabadiliko anaonekana kufumbia macho utekelezaji wa kile mwanafalsafa Mwalimu nyerere alichokisema---kwamba Watanzania wanataka mabadiliko.

Mfano Rais Kikwete alipata fursa ya kusimamia mabadiliko kwa kuandika Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi. Lakini kikundi kidogo cha wahafidhina ndani ya CCM kilimtisha akajikuta anaweka pembeni ujasiri wake aliokuwa nao wa kusimamia mabadiliko hayo muhimu kwa maendeleo ya taifa hili.

Kama uamini jiulize ni kwa nini Kikwete aliachia Bunge la Katiba lililojaa asilimia 80 ya wanachama likazika Rasimu ya Katiba ya wananchi pale Dodoma mwaka jana 2014 -- Rasimu ambayo ingeleta Katiba yakuweka misingi ya kuleta madadiliko Tanzania—mabadiliko ya kuhakikisha kikundi kidogo cha watawala hakijitajirishi kwa ufisadi na kujigawia mali za umma huku mamilioni ya wananchi wakibaki maskini na mafukara wa kutupa?

Baada ya Kikwete kupoteza fursa ya kuleta mabadiliko kwa kuandika Katiba Mpya, umma uliofukarishwa umeendelea kupata uelewa kuwa CCM na serikali yake ndicho chanzo cha umaskini wao.

Hivyo ili kuendelea kubaki madarakani serikali ya CCM imekuwa ikijihusisha na ufisadi ili ipate fedha za kuwarubuni walala hoi wakati wa kampeni za uchaguzi.

Mfano mwaka 1995 Rais Benjamini Mkapa alijikuta serikali yake ikifanya ufisadi katika akaunti EPA (bilioni 122) zilizotumiwa na CCM kumuweka Kikwete madarakani.

Ukitafakari utaona kwamba katika ufisadi Tegeta escow, serikali ya CCM imekapua billion 306 mara tatu ya ufisadi wa EPA mwaka 1995 ilipokwapua bilioni 122 ili kipate fedha nyingi zaidi la kuwalaghai wapiga kura mafukara ambao wameendelea kupata uelewa kuwa CCM inaiba fedha za umma kununua wapiga kura wakati wa kampeni za uchaguzi.

Hivyo serikali ya CCM inayoongozwa na Kikwete ambayo imeshuhudia nguvu ya wananchi kudai mabadiliko ikiwa kubwa kuliko wakati mwingine wowote, inajaribu kila mbinu chafu na safi ili CCM ibaki madarakani baada ya uchaguzi mwaka huu.

Ndiyo sababu serikali ya CCM kupitia msemaji wa chama hicho Nape Nnauye imeanza kuwaambia Watanzania kuwa CCM lazima ishinde uchaguzi wa mwaka huu hata kama ni kwa kutumia goli la mkono (wizi au lolote lile chafu).

Zaidi Rais Kikwete amefikishwa mahali pabaya kulazimika kubuni mchezo mchafu kujaribu kuwadanganya Watanzania kuwa eti CCM na serikali yake ni safi, haijihusishi na ufisadi unaofukarisha wananchi isipokuwa wanachama wachache wa CCM ndio mafisadi.

Ili kujaribu kutafuta kujenga uhalali wa CCM kubaki madarakani baada ya uchaguzi wa mwaka huu 2015, Kikwete amejikuta akilazimika kumtoa kafara Lowassa kwa kumpakazia ufisadi wa Richmond.

Wananchi wanauliza kama Lowassa alikuwa ndiye mhusika wa Richmond ni kwa nini Spika wa Bunge Anna Makinda (mmoja wa watawala wa CCM), hakuagiza tume ya Bunge iliyoongozwa na Mbunge wa CCM Harrison Mwakyembe kumhoji Waziri Mkuu Edward Lowassa?

Pili wananchi wanahoji kama CCM haijamtoa Lowassa kafara kwa kumbebesha ufisadi wa chama hicho ili kupumbaza hasira ya wananchi dhidi ya ufisadi wa CCM kwenye uchaguzi wa Oktoba mwaka huu 2015 ni kwa nini Rais Kikwete alikubali Waziri wake Mkuu Edward Lowassa ajiuzulu kwa ufisadi wa Richmond 2008 wakati ufisadi wa kutisha ulifanywa na serikali ya CCM kwenye akaunti ya Tegeta escrow 2014 Kikwete aliwatetea mawaziri waliogawiwa fedha hizo na Ikulu ilikuwa ndiyo mtuhumiwa namba moja?

Mimi si mwanasiasa wa chama chochote cha siasa hapa nchini ninachoangalia ni chanzo cha umaskini wa wananchi wengi Tanzania.

Ndiyo sababu Watanzania wengi nikiwepo mimi mwenyewe kwa sababu tulipewa habari nusu nusu zilizotolewa kimkakati na serikali ya CCM kuhusu kashfa ya Richmond kumpakazia Lowassa ufisadi, tulipubwazwa tukaisaidia CCM kumchafua Lowassa kuwa ni fisadi wa Richmond.

Lakini baadhi ya wananchi walianza kujua kuna ukweli uliofishwa kuhusu Richmond pale TV moja ilipokuwa imemwalika Lowassa aotoe yake ya moyoni live siku chache baada ya kujiuzulu, lakini kipindi hicho cha TV kikafutwa ghafla.

Hata hivyo ukweli huo umekuja kujulikana mwezi Julai mwaka huu Lowassa alipotoa hadharani baada ya kuachana na CCM na kujiunga na CHADEMA.

Sasa wananchi wamefahamu kuwa CCM chini ya serikali ya Rais Kikwete iliamua kumtoa Lowassa kafara kwa kumpakazia ufisadi wa Richmond ili kuiokoa CCM isiadhibiwe vikali na wananchi kwenye sanduku huru la kura –kwa ufisadi alinawasababishia umaskini na ufukara.

Ndiyo sababu hivi sasa CCM na baadhi ya wanahabar wanapakazia CHADEMA na UKAWA kuwa eti ni mafisadi baada ya kumpokea Lowassa (kafara wa CCM) na kumpitisha kuwa mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Isitosha hivi sasa kikundi cha watawala wachache wa serikali ya CCM wanahaha na wanamzonga Kikwete azuie mabadiliko kwa mkono kwa kufanya kila uchafu kupumbaza Watanzania kwa kutumia kete ya eti Lowassa ni fisadi wa Richmond hivyo hana sifa ya kugombea Urais wa Tanzania, bali Magufuli ndiye mtu safi.

Wananchi wenye akili zao wanajiuliza hivi mwenye kashfa za kifisadi kati ya Lowassa na Magufuli ni nani? Ni Lowassa aliyepakaziwa Richmond au ni Magufuli aliyeongoza watawala kujiuzia kwa bei chee nyuma za umma zilizogarimu wanannchi mabilioni ya fedha?

Wananchi pia wanajiuliza kama Lowassa ni fisadi wa Richmond ni kwa nini serikali ya CCM haijamshitaki mahakamani miaka minane tangu ufisadi huo ulipotokea?

Hivyo pengine baada ya Lowassa kutafakari nafsi yake na kuona kuwa CCM imemtoa kafara asigombee Urais ili kuzuia mabadiliko, ameamua kufanya maamuzi magumu ya kuhama CCM --kushiriki kuongoza masikini na mafukara wanaotafuta mabadiliko.

Lowassa ameamua kutekeleza alichokitabiri Mwalimu Nyerere kwamba CCM isipokubali kuongoza wananchi wapate mabadiliko wanayoyataka—wananchi watayatafuta mabadiliko hayo nje ya CCM.

Ni dhahiri CCM ilipoteza fursa adimu ya kuongoza wananchi kwenye kuleta mabadiliko kwa kuandika Katiba Mpya-- kuweka misingi ya kukomesha mfumo wa utawala unaowezesha watawala kuwa matajiri wa kupindukia huku mamilioni ya wananchi wakiwa mafukara na nchi ikinuka aibu ya umaskini wa kijitakia ikiwa rasilimali nyingi za asili.

Wanaomchochea Rais Kikwete asikubali mabadiliko yachukue mkondo wake, wameunda timu ya kampeni yanye wajumbe wengi waliohusika kumpakazia Lowassa ufisadi wa Richmond ili eti kwenye kampeni waendelee kumpaka ufisadi Lowassa, CHADEMA na UKAWA wakidhani Watanzania hawana akili ya kutafakari.

Lengo lao ni moja. Wanajua kabisa kuwa kwa kutumia sanduku huru la CCM haiwezi kuchaguliwa. Wanataka kutumia kisingizio kuwa CHADEMA na UKAWA imechafuka eti kwa kumsimamisha Lowassa Urais ambaye CCM imemtoa karafa – kwa kumpakazia ufisadi wa Richmond.
Lakini baada ya kupata salamu za wananchi kupitia mafuriko yao kwenye kumtambulisha Lowassa kwamba wao wanaelewa fisadi kamili ni CCM, sasa CCM imeshtuka imeanza kutumia polisi kuwaadhibu wananchi. Pengine baadaye itatumia jeshi kabisa.

Zaidi imeamua kujaribu kampeni za ardhini -nyumba kwa nyumba, bila shaka kutumia mabilioni ya fedha serikali ya CCM ilizokwapua Tegeta escrow kununua shahada na kura za mafukara.

Kwenye kampeni za nyumba kwa nyumba mtu kwa mtu ndiko ufisadi mbaya wa kisiasa unakofanyika—kununua, kutisha na kuumiza wananchi mafukara.
Swali ni je Watanzania wangapi wapiga kura watakubali CCM inapopita majumbani mwao kuuza shahada zao kwa sukari, kanga au fedha hata kama CCM itaamua kumpa kila mpiga kura shilingi milioni moja?

Ni mpiga kura gani atakayekubali KUDANGANYIKA kwa kununuliwa na CCM kwa vijizawadi vya fedha nguo KUSALITI mamilioni ya watanzania wanaoendelea kuteseka kwa ufukara kila baada ya uchaguzi kwisha na CCM kubaki madarakani?

Wananchi pia wanauliza je mabilioni ya escrow yatawanunua wajumbe wa NEC ili wavuruge daftari la wapiga kura, au wachakachue kama uchaguzi wa 2010 au wataharibu daftari la wapiga kura, mashine na vifaa vya kupigia kura, au kuchelewesha kwa makusudi kufungua vituo vya wapiga kura ili kuvuruga uchaguzi CCM ishinde kwa goli la mkono?

Kadhalika wananchi wanauliza wanaomshinikiza Kikwete asikubali mabadiliko wakiona hilo haliwezekani je watamuua Lowassa waliomtoa kafara au viongozi wa CHADEMA na UKAWA waliompokea Lowassa na kumwezesha kufikia azma yake ya kujitolea kuwatumikia watanzania ili kuvuruga uchaguziwa mwaka huu?

Wananchi wanauliza maswali hayo baada ya kubaini kwamba huenda wasiomtakia mema Kikwete astaafu kwa amani wamejaribu kuwalaghai baadhi ya viongozi wakuu wa UKAWA ili kujaribu kuvuruga UKAWA – lakini UKAWA kwa vile ni sauti ya mafukara-sauti ya umma imeendelea kuwa moto mkali wa nyika dhidi ya CCM.

Hivyo binafsi namshauri Rais Kikwete akubali kuwa baba wa pili wa Taifa hili baada ya Nyerere kuondoka. Akubali kusimamia wananchi watumie sanduku huru la kura kwenye uchaguzi wa mwaka huu 2015 kupata mabadiliko ya uongozi wanayoyataka.

Wananchi wana imani na UKAWA kwamba wakiingia madarakani Katiba mpya inayotokana na maoni ya wananchi itaandikwa.

Huo utakuwa ni mwanzo wa mabadiliko wanayoyataka wananchi—kuhakikisha watawala hawajitajirishi kupindukia kufisadi fedha za wananchi huku wananchi wengi wakibaki mafukara. CHADEMA na UKAWA wasipotimiza hili na kuonyesha kwa vitendo maendeleo watakayokuwa wameyaleta kwa miaka mitano, ni lazima wananchi watatumia sanduku la kura kuwapunzisha.

Ninaamini ni wenye kutetea maslahi binafsi tu ndiye atakayemlaumu Rais Kikwete kwamba eti CCM isipochaguliwa Oktoba 25, Kikwete atakuwa ni chanzo cha wananchi kuamua kuipunzisha CCM kwa miaka mitano.

Nitakuwa wa kwanza kuwapinga watu hao na kumtetea Kikwete hata kama ni kwa kuamua kuingia kwenye siasa kwa kujiunga na CCM .

Hakika Rais Kikwete ukisimamia wananchi wazungumze kuhusu hatma ya uongozi wan chi yao kwa kutumia sanduku huru la kura bila CCM kuingiza mkono mchafu, wewe mwenyewe ukistaafu utaishi kwa amani na furaha huku baadhi yetu tukikuona kama baba wa Pili Taifa taifa hili, baada ya Mwalimu Nyerere.

Mwisho ninaruhusu yeyote anayetaka kuchapisha au kutangaza redioni natelevisheni niyoyoyaandika hapa TV au kuchapisha na kuwasambazia Watanzania wote popote walipo ujumbe huu afanye hivyo. Wanawaza kuwasambazia watu mitaani, kwenyemikutano ya kampeni, mashuleni vyuoni popote pale—lengo likiwa moja—sote Watanzania tuujue ukweli kuhusu ufisadi na mchango wake katika kuwafanya Watanzania waishi katika umaskini. Lakini muhimu kila Mtanzania ajue hakuna mshindi wa kujisifu—mshindi ni nchi yetu Tanzania na Watanzania wote.

MUNGU IBARIKI YANZANIA.



Ananilea Nkya
 E-mail:ananilea_nkya@yahoo.com

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments