[wanabidii] Mbunge wangu Mnyika hata wewe leo umesahau haya ya Lowasa?

Tuesday, July 28, 2015
Wednesday, September 3, 2008
SERIKALI IACHE KUMLINDA LOWASSA
 
Ni mmoja wa mizizi ya ufisadi wa Richmond
    Akamatwe, ahojiwiwe na achukuliwe hatua za kisheria.

Siku chache zilizopita. Nilitoa taarifa hii kwa vyombo vya habari. Hata hivyo, kwa sababu ambazo sizifahamu, habari hii haikutoka katika magazeti mengi ya kila siku. Pengine inaweza ikawa ni njia iliyotumika kufikisha ujumbe(barua pepe) lakini kuna uwezekano mkubwa sababu ikawa ni kuwa Lowassa hakutajwa kuchukuliwa hatua kama hizi ambazo nimezieleza hapa katika yale Maazimio 23 ya Bunge.

Yeye aliambiwa tu atakafakari na kuchukua maamuzi ambayo ataona yanafaa. Yeye akaamua kujiuzulu. Lakini bado siridhiki sana na sababu hii kwa kuwa maazimio hayo 23 hayajasema Karamagi na Msabaha wachunguzwe kuhusu Rushwa kama serikali ilivyoamua. Kama imeamualiwa na Serikali hawa wachunguzwe, kwanini serikali haikumjumuisha na Lowassa? Hii inafanya niamini kwamba bado msimamo huu hapa chini ni mwafaka:

Bwana Lowassa alikiri kwamba alikuwa anafahamu kwamba Richmond ni kampuni ya kitapeli, lakini katika kipindi chote cha uongozi wake aliinyamazia hali hii na kwa kiasi kikubwa aliitetea kampuni hiyo mbele ya macho ya umma. Wakati wa Viongozi mbalimbali wa upinzani walipoweka bayana kwamba Richmond ni kampuni isiyo na uwezo, serikali ilitetea kampuni hiyo.

Vyombo mbalimbali vya habari vilimtuhumu Bwana Lowassa mwaka 2006 na 2007 kama kiongozi wa Shughuli za serikali bungeni, kwamba alishiriki 'kuwaziba midomo' wabunge wa CCM wasijadili suala hili. Pia, ni Bwana Lowassa huyo huyo, alinukuliwa akiwa Arusha akiwataka watanzania wasiijadili kampuni ya Richmond baada ya mvua kuanza kunyesha.

Kama Bwana Lowassa wakati wote huo alijua kama ni kampuni ya kitapeli kama anavyojaribu alivyojaribu kujitetea, uamuzi wake wa kuwaasa watanzania wasiijadili ulikuwa ni wa kulinda ufisadi ambao aliufahamu. Inashangaza pia ni Lowassa huyo huyo alisema alijua kuwa Richmond ni kampuni ya kitapeli; ni Lowassa huyo huyo alisema kwamba alishauriwa vibaya na watumishi wa umma aliowataja kuhusu uwezo wa Richmond; Ni Lowassa huyo huyo aliyesema kwamba alijua kuwa TANESCO chini ya Menejimenti ya Net Group Solution walitaka kuhujumu mchakato wa tenda na hivyo 'kuwanyang'anya'. Lakini ni Lowassa huyo huyo aliyekuwa Waziri Mkuu ambaye angeweza kuviagiza vyombo vya dola kumwezesha kuthibitisha 'utapeli wa Richmond'; hivyo, maelezo ya sasa yanayotolewa kuhusu ushiriki wake yanaonyesha kuwa sasa kuna mwelekeo wa kumlinda.
 
Tunaendelea kushangazwa na Serikali na Bwana Lowassa kutumia utetezi wake kueleza tu nia yake ya kutaka mkataba wa Richmond usitishwe; nia ambayo kama ni kweli alikuwa na uwezo wa kuitekeleza na hakuitekeleza. Tunaitaka Serikali na Bwana Lowassa kuweka bayana ni kwa vipi Richmond ilipewa tenda hiyo na kwa shinikizo la nani.

Bwana Lowassa anakwepa kuyazungumzia haya kwa kuwa anajua kabisa kwamba ni yeye aliyetumia madaraka yake vibaya alipokuwa Waziri Mkuu kwa kukiuka Sheria na Taratibu za Ununuzi kwa 'kupora' mchakato uliokuwa ukiendeshwa na TANESCO, 'kuunda kamati yake' na kuzisukuma mamlaka za ununuzi hali iliyopelekea Richmond kupewa tenda ili hali haikuwa na uwezo uliotakiwa. Ni uzembe huu ambao umelisababishia hasara taifa kwa kulipa shilingi milioni 152 kila siku kwa kampuni ya Dowans iliyohamishiwa mkataba wa kitapeli wa Richmond; na takribani bilioni 172 kwa ujumla ambazo taifa linawajibika kuzilipa kutokana na kukodisha mitambo hiyo. Hvyo tunarudia tena rai yetu ya kutaka fedha zilizozilipwa kizembe mpaka sasa kurejesghwa serikalini.

Kwa vyovyote vile, jitihada za Bwana Lowassa za kuhamasisha ujenzi wa Sekondari Kata, na utumishi wake kama Waziri Mkuu katika kipindi cha miaka miwili, haviwezi kuzidi hasara aliyosababisha katika uchumi wetu kipindi chote tulichokosa umeme wa dharura na wala hailingani na hasara ambayo tunaendelea kuilipa kila siku iendayo kwa Mungu. Maamuzi haya ya Bwana Lowassa yanaendelea kuwaumiza wananchi wote ikiwemo wa Jimbo lake la Monduli ambao wanataabika kwa mzigo wa gharama za umeme.
 
Vijana wa CHADEMA tulitarajia kuwa, baada ya Bwana Lowassa kukiri mwenyewe hadharani kuhusu uzembe wake na matumizi mabaya ya madaraka Rais Kikwete angelekeza hatua za kuchukuliwa dhidi yake badala ya kuendelea kumpamba kama "shujaa wa uwajibikaji', kinyume na hayo tutaamini kwamba serikali yake inaendeshwa kwa 'ubia wa kulindana'.

Aidha tunarudia kutoa rai kwamba Rais Kikwete kuwafukuza kazi watumishi wote wa umma waandamizi ambao wametajwa na Bwana Lowassa kushiriki uzembe na matumizi mabaya ya madaraka; watumishi ambao walitajwa pia na Kamati Teule ya Bunge lakini mpaka sasa wanaendelea kutumikia nafasi zao mbalimbali. Kwa kuwa Waziri Mkuu Pinda ameshatangaza kwamba kwa wale wateule wa Rais, Kamati yake imeshapeleka suala zima kwake, tunategemea Rais atachukua hatua za haraka ili kuonyesha mfano kwa viongozi wengine wa chini yake wanaotarajiwa kuchukua hatua kwa watumishi wa chini.

 Bwana Lowassa alithibitisha kwamba maneno yake kwamba wapo viongozi waandamizi wa Serikali ambao amewataja kwa majina wamefanya maamuzi ya kifisadi, kitendo chake cha kunyamazia ufisadi huo- kinafanya iwe vigumu kwa yeye kutenganishwa na tuhuma za ufisadi zilizomo katika mchakato mzima wa kupewa tenda kwa kampuni ya Richmond na mambo yote yaliyotokea baada ya Mkataba huo kuhamishiwa kwa kampuni ya Dowans.

Aidha tumefadhaishwa na Taarifa ya Waziri Mkuu Pindi kwamba kujiuzulu kwa Waziri Mkuu na Baadhi ya Mawaziri ilikuwa ni ishara ya hatua ambazo serikali imechukua kutekeleza maazimio ya Bunge kuhusu suala husika. Tunarudia kukumbusha kwamba toka sakata la Richmond lilipoanza zaidi ya mwaka mmoja uliopita tulimtaka Bwana Lowassa kujiuzulu kulinda heshima yake lakini alikaidi na kuitetea kampuni ya Richmond. Uamuzi wa yeye kujiuzulu baada ya kashfa yote kuwa hadharani, umesaidia tu kuilinda serikali ya CCM lakini katu hauwezi kumpatia heshima ya uwajibikaji na wala hakuwezi kuwa ishara ya kwamba Maazimio ya Bunge yameshatekelezwa.

Kwa niaba ya Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA), kwa taarifa hii tunarudia kukemea jitihada zozote za kumlinda na kumtangaza Lowassa kuwa shujaa katika taifa letu kwani hali hii ikiachwa kuendelea inatoa mfano mbaya kwa vijana wa Tanzania. Tusingependa kwa namna yoyote katika taifa letu, mtuhumiwa wa ufisadi aliyetajwa pia katika orodha ya mafisadi(list of shame) kulindwa na kuenziwa kama shujaa wa Taifa letu kwani ni kuharibu maana nzima ya ushujaa katika uwajibikaji.

"Inasikitisha kwamba vijana wezi wadogo wadogo wakijazana magerezani. Vijana wamachinga kuendelea kukosa mitaji na maeneo ya kufanyia biashara; wanafunzi wa elimu ya juu wakipandishiwa ada na wengine kukosa mikopo- huku fedha za walipa kodi zikiendelea kuteketea kwa ufisadi na watuhumiwa wa ufisadi wakiendelea kutamba hadharani. Hali hii ikiachwa, itaharibu utawala wa sheria na kuleta matabaka katika taifa letu. Vijana tusingependa kuona nchi yetu inatumbukia kwenye migawanyiko kwa sababu ya kuwalinda watu wachache kwa kisingizio cha haki za binadamu"
 
Imetolewa tarehe 31 Agosti 2008 safirini Kenya na:
John Mnyika
Mkurugenzi wa Vijana
0754694553

Share this :

Related Posts

0 Comments