[wanabidii] UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA; HOJA YANGU.

Friday, December 05, 2014

HOJA YANGU JUU YA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA.

Jana nilikuwa mgeni mwalikwa kwenye kipindi cha HOT MIX cha EATV kutoa maoni yangu juu ya uchaguzi wa serikali za mitaa. Nilijaribu kuweka mambo kadhaa, lakini mwongozaji wa kipindi alikuwa akiuliza maswali ambayo kwa kweli hayakuruhusu mtiririko wa moja kwa moja wa mambo yote niliyotaka kuongea.
   Tunajua kuwa kanuni za uchaguzi huu zilichelewa (weshwa) na waziri mwenye dhamana. Bila shaka hii ni kwa kusudi maalumu.
  Mwezi wa saba, waziri aliwaita Morogoro wenyeviti wa vyama vya siasa kujadili pamoja na mambo mengine mapendekezo ya wadau kwenye uchaguzi huu. Kitendo cha kuwaita wenyeviti bila makatibu ambao ndiyo watendaji chenyewe nacho ilikuwa dosari kubwa kwa maoni yangu.
  Hata hivyi mapendekezo yalitolewa na waziri akaahidi kwenda kuyafanyia kazi. Baadhi ya mapendekezo ambayo kwa kweli ni ya muda mrefu ni pamoja na
  1.Uchaguzi huu usimamiwe na tume ya uchaguzi. Hii ni kutaka kuondoa uchaguzi huu chini ya waziri ambaye kimsingi anakuwa mwenyewe na maslahi kwenye uchaguzi.
   2.Uchaguzi wa madiwani ambao ni viongozi wa serikali za mitaa uondolewe kwa ule wa rais na mbunge urudishwe huku.
  3.Umri wa kugombea ushushwe toka miaka 21 hadi 18
  4.Uandikishaji ufanyike kwa muda na elimu ya uraia itolewe na wadau wote badala ya serikali pekee.
  5.Uchaguzi wenyewe usogezwe Feb.2015 kwa sababu kanuni zilichelewa na kuna mambo mengi hapa katikati.

Baada ya kukaa kwa muda mrefu, ghafla kanuni zikatolewa bila kuwaita tena wadau, na mambo mengi waliyopendekezwa hayakufuatwa. Kwa kanuni zilizopo, bado TAMISEMI ndiyo wanasimamia uchaguzi huu, na mambo mengi yamebaki kama zamani.
  Muda wa kujiandikisha umekuwa mfupi sana na utaratibu haukuwa mzuri. Nimeona mahali mwandikishaji amepaki pikipiki na anatumia kiti cha pikipiki kama meza!
  Mipaka ya mitaa haifahamiki sawasawa. Hii imefanya vijana wengi kukosa kujiandikisha kwani umekuwa ni usumbufu mkubwa sana.
  Kanuni iliwataka wagombea "kuchora" nembo ya chama chao na nembo ya halmashauri wanayogombea kwenye fomu ya kuomba kuchaguliwa. Hii ni kuwapa wagombea majukumu ambayo siyo yao. Japo baadaye ilisemwa hilo lilikuwa kosa la uchapaji, lakini wengi walishaathiriwa ikiwa ni pamoja na kuwekewa pingamizi na kuenguliwa.
  Kanuni zinasema anayeweza kuweka pingamizi ni mgombea mwenyewe. Lakini imeonekana double standard kwenye hili maana yupo mgombea wa NCCR akiwekewa pingamizi na kuenguliwa na katibu wa chama CCM wa eneo lile ambaye hakika hakuwa mgombea.
   Chama ndicho mdhamini wa wagombea maana hatuna bado mgombea binafsi (huru)?. Lakini kanuni inataka afisa (katibu) wa chama wa ngazi ya chini kabisa ndiye aweke sahihi kumdhamini mgombea.
   Kama tujuavyo, vyama vingi havina uongozi unaoeleweka huko chini kabisa na chama kidogo kama ACT-TANZANIA chenye miezi saba ni sawa na kukinyima nafasi ya ushiriki maana kwa kweli hakiwezi kuwa na viongozi huko chini. Hii nayo imeleta madhara makubwa kwa vyama pinzani. Labda inaeleza sababu za CCM kupita bila kupingwa. Ningependekeza angalau kwa chama wagombea waidhinishwe na ngazi ya wilaya.
  Watu wachache sana wamejitokeza kujiandikidha na kwa kweli niwapongeze CCM kwa kuhamasisha eanachama wao kujiandikisha. Niliona namna ambavyo makada wa chama walivyokuwa bussy kuhamasisha wanachama wao. Hili kwa sehemu kubwa halikuonekana kwa wapinzani. Sasa kama hatuna uwezo wa kuwafanya wana chama wetu wakajiandikishe tunategemea nani atatupigia kura? Ama je vyama vya upinzani havithamini uchaguzi huu? Mbona sijaona Helkopita (chopa) ikipita vijijini kufanya kampeni?
  Vyama vya upinzani kudharau zoezi hili vitakuja kujuta. Pamoja na kasoro zilizopo, vyama vimefanya nini kuelimisha wananchi? Muda huu kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, wao nguvu zote wameweka kwenye katiba mpya na Escrow account. Sifahamu vema kama hiyo ndiyo elimu ya uraia ama ushawishi ili wananchi wawachague. Ama Operesheni "Delete CCM"!. Sasa hii operesheni ina maana gani? Kwamba sasa hatutaki vyama vingi? Yaani tukii delete CCM tunabaki na chama kimoja?
  Ama kwamba sasa tunaanza kuwa na kiu ya kufuta vyama? Kama tunaanza sasa hivi kuwaza kufuta vyama, tukipata madaraka si tutafunga kabisa uhuru wa watu kutupinga? Kwa maoni yangu jina la operesheni futa CCM ni potofu na linaonyesha hulka za kidikteta.
  UKAWA na wazo la kuachiana nafasi za ugombea nalo limeleta mkanganyiko na yawezekana likaathiri matokeo ya uchaguzi huu. Tumesikia maeneo kadhaa ambapo vimegongana. Hii inaamsha maswali juu ya ushirikishwaji wa wana chama wa vyama hivi katika kuelewa malengo ya UKAWA. lakini ilivyo sasa imeleta mkanganyiko.
  Watu hawana hamasa yoyote na uchaguzi huu. Ukiacha kuonekana hapa na pale kwa pilika lakini hauoni hamasa zozote kubwa.
Je hii maana yake watu wanazidi kupoteza imani katika chaguzi? Ni jambo ka kusubiri.
  Mwisho niseme kuwa uchaguzi huu ni kiashiria kikubwa cha uchaguzi mkuu ujao. Kwa kweli katika tofauti ya miezi michache tu, atakayeshinda serikali za mitaa ndiye hushinda uchaguzi unaofuatia karibuni. Sina sababu ya kudhani kutakuwa na muujiza hapa kwetu. Kwa mambo yalivyo naweza kusema kwa hakika CCM watashinda uchaguzi huu wa serikali za mitaa kwa asilimia kubwa tu. Na kwa hiyo ni CCM ndiyo itakayoshinda uchaguzi mkuu wa mwakani. Hili liko hivi hata kama tunatapika kila tukilisoma.
Mwl.Ludovick.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments