[wanabidii] Kampuni za simu zinasitiri taarifa za watumiaji wake?

Wednesday, November 12, 2014
Na Yona Maro

Ukikutana na Watanzania 10 angalau nusu yao watakuwa na kifaa au vifaa vya mawasiliano kama  simu na kompyuta.

Vifaa hivi vimesajiliwa kwa majina yao na taarifa zao nyingine ambazo zinaweza kuwa ni taarifa sahihi au la.

Kwa kawaida wakati wa usajili wa laini za simu au vifaa vingine vya mawasiliano, kuna jambo ambalo mara nyingi linasahaulika kati ya mteja wa huduma za mawasiliano na mtoa huduma yaani kampuni husika.

Wateja wengi wa kampuni za mawasiliano hawajui  taarifa zao zinatumikaje na hata pale wanapohitaji baadhi ya taarifa,  ni vigumu kupata labda kutokee tatizo na kuhusishwa vyombo vya dola kama jeshi la Polisi.

Mimi binafsi niliwahi kuuliza maswali kadhaa kwa watoa huduma wa mawasiliano yangu. Niliwauliza: Taarifa zangu zinahifadhiwa wapi na kwa njia gani na nani mwenye uwezo wa kuangalia taarifa zangu?

 Maswali mengine ni;  kwanini sina haki ya moja kwa moja kujua taarifa hizo mpaka polisi ihusishwe na kwanini nikitaka kujiondoa kwenye huduma, kampuni zina uwezo wa moja kwa moja kuniruhusu?

Ukweli ni kuwa mawasiliano ya watu wengi  yanaangaliwa na wanapewa watu wengine bila ya sisi kujua au kujulishwa. Tena utashangaa  muda mwingine mtu unakamatwa kumbe aliyetoa taarifa ni mtoa huduma wako.

Kuna watu wanatumiwa ujumbe mfupi wa maneno na kampuni mbalimbali kupitia mtoa huduma wako, bila mwenye namba ya simu kujulishwa. Na ikitokea anataka kujiondoa basi atakatwa fedha kidogo, hajitoi bure .

Wengine husafiri kwa kipindi kirefu, wanaporudi wanashangaa namba zao za simu zinatumiwa na watu wengine. Hili linafanyika ikiwa tayari walishazisajili namba zao. 

Natambua nchi yetu iko kwenye mchakato wa kuandaa sheria ya mawasiliano. Sheria hii itakuwa  kioo cha masuala yote ya mawasiliano nchini, hivyo ni muda mwafaka wa kuangalia suala hili kwa maslahi ya wateja wa huduma za mawasiliano .

Kwa nchi nyingine zilizoendelea masuala haya walishayafanyia kazi, kwa sababu kuna wateja waliwahi kuzipeleka mahakamani baadhi ya kampuni za mawasiliano na  kushinda mashauri yao.

Nchi kama Marekani kampuni ya mawasiliano inatakiwa kutoa taarifa kwa mteja wake endapo inataka taarifa yoyote inayohusu kifaa chake cha mawasiliano.


Aidha, mteja  anapohitaji kujiondoa kwenye huduma fulani, anapewa utaratibu wa kufuata na mara nyingi ni kwa njia ya mtandao. Kampuni kama Yahoo kwa kawaida inakupa siku 90 ili wakamilishe ombi lako la kujiondoa.

Siku 90 hizi  ni kuangalia kama kila kitu ni salama kuhusu akaunti ya mteja. Ikiwa watajiridhisha kuwa kila kitu kitakuwa shwari, utaondolewa katika huduma zao.

Kwa kuwa huduma za mawasiliano ni haki ya raia wote, suala la taarifa zake anazotoa kwa kampuni za mawasiliano bila shuruti nazo ziwe haki yake.

Kimsingi nihitimishe kwa kusema mteja lazima awe na uwezo wa kuhoji na kupata ufafanuzi wa taarifa zake. Lakini muhimu zaidi awe na uwezo wa kujiondoa kwenye huduma au kampuni fulani bila usumbufu.

http://www.mwananchi.co.tz/Makala/Kampuni-za-simu-zinasitiri-taarifa-za-watumiaji-wake-/-/1597592/2368138/-/item/1/-/kirycxz/-/index.html


--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments