MGOGORO WA BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI, NI KWA FAIDA YA NANI?
Na. J. Mtatiro - Gazeti la Fahamu. J'nne, 27 Novemba 2014.
Bunge la Afrika Mashariki, maarufu kama (EALA) limeingia katika mgogoro mkubwa hivi karibuni. Bunge hilo lilikutana jijini Dar Es Salaam na halikufanya kazi yoyote ya maana. Ilithibitika kwamba, hata baadhi ya wabunge muhimu wa Tanzania hawakudhuria vikao vya bunge hilo vilivyofanyikia Dar Es Salaam bila sababu maalum huku wakichukua posho. Baadaye kikao cha bunge hilo kilivunjika baada ya mgogoro ulioanzishwa na baadhi ya wabunge hasa wa Rwanda, wabunge hao waliondoka bungeni na kufanya akidi ya kuendelea na vikao kukosekana na hivyo bunge hilo likaahirishwa.
Baadaye baadhi ya wabunge ambao ni viongozi wa bunge hilo walikuwa safarini nje ya Afrika na mbunge mmoja wa Tanzania Bi. Shyrose Bhanji alipewa tuhuma nzito za kufanya vurugu katika ndege na hata kuwatukana marais wa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki. Kwa tunaomfahamu Shyrose tulistushwa sana na habari hizo lakini baadaye Shyrose mwenyewe alieleza ni namna gani anavyopigwa vita na kuzushiwa tuhuma mbalimbali kwa sababu yeye ni kinara wa kupinga mapinduzi ya kumuondoa spika wa bunge hilo kutoka Uganda, Bi. Magreth Ziwa.
Nimejaribu kufuatilia sakata hili la EALA kupitia vyanzo mbalimbali na nimegundua kuna mambo mengi yaliyomo ndani ya mgogoro unaoendelea na uchunguzi tu wa awali unaanza kuonesha kuwa inawezekana Shyrose Bhanji anashughulikiwa ili kutimiza kiu ya Uganda na Rwanda ya kumiliki ukuu na kupenyeza ajenda ambazo Tanzania haiwezi kuziunga mkono katika hali ya sasa ya jumuiya hiyo. Baada ya tuhuma za Shyrose kuwekwa bayana, vikao vya EALA vilihamia Kigali, Rwanda, huko ndiko mambo yaliharibika tena, wabunge(hasa wa Rwanda na Uganda) wakagoma kuendelea na vikao hadi Shyrose achukuliwe hatua. Kilichonistua zaidi ni kuwa, katika mkakati wa kumshughulikia Shyrose Bhanji, wamo pia wabunge wa EALA kutoka Tanzania ambao wameungana na Rwanda na Uganda kuhakikisha mbunge mwenzao kutoka Tanzania anashughulikiwa.
Baada ya vikao vya EALA kukwama Rwanda, vilihamia Nairobi - Kenya, wiki iliyopita, ambako nako zilizuka shutuma kwamba Shyrose Bhanji amempiga mwalimu wangu mhe. Nderakindo Kessy. Baadaye siku iliyofuata Bungeni Dodoma, Waziri anayehusika na masuala ya jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Tanzania mhe. Samwel Sitta alieleza kuwa hakukuwa na ugomvi baina ya wabunge hao na kwamba waligongana kwa bahati mbaya. Japokuwa mhe. Mwalimu wangu mama Nderakindo alipotafutwa na baadhi ya vyombo vya habari aliendelea kuthibitisha kuwa amepigwa na Shyrose Bhanji. Nilipitia pia kwenye ukurasa wa "Facebook" wa mhe. Shyrose Bhanji na kuona msimamo wake juu ya jambo hili, ameendelea kusisitiza kuwa tuhuma anazopewa za kumpiga Bi. Nderakindo ni mwendelezo wa chuki anazofanyiwa tangu kusingiziwa amefanya vurugu kwenye ndege n.k. Bi. Shyrose amesisitiza kuwa anaandamwa na mambo ya kutunga kwa sababu haungi mkono ajenda ya wabunge wa Uganda, Rwanda na Kenya ya kumuondoa Spika wa bunge hilo kwa manufaa ya nchi hizo ambayo hayaihusu Tanzania.
Mimi binafsi nawaheshimu sana wabunge wetu hawa wawili. Bi. Nderakindo amenifundisha, Bi. Shyrose nimekuwa naye kwenye harakati kama mwanamke ambaye anaweza kuthubutu na kusimamia jambo fulani. Wote ni watanzania muhimu sana, lakini mgogoro huu wa EALA kuhamishiwa kwao na ukaachwa na eti ukafanywa kuwa jambo lisilotatulika ni kuwadanganya watanzania. Nachoona hapa, hakuna mgogoro kati ya Nderakindo na Bhanji bali misimamo ya pande hizi mbili ya kumuondoa Spika au abakie ndicho kiini cha magomvi haya na uzushi ambao kila mara unatolewa dhidi ya huyu ama yule.
Ni jukumu la serikali yetu kuwaelekeza wabunge wetu kwamba wakasimamie maslahi na matakwa ya watanzania katika bunge hilo. Na kwa vyovyote vile, inapotokea tofauti kati ya wabunge wa Tanzania si jambo la busara ati tofauti hizo zitatuliwe na Wanyarwanda au Waganda au Wakenya. Taifa letu lina historia ya kutatua migogoro ya watu wengine na kuwasaidia, watanzania mara nyingi kila mahali wanapokuwa nje ya Tanzania wamekuwa ni watatuzi wa migogoro yao wenyewe au ya watu wengine kirahisi. Iweje leo tununue ugomvi wa waganda na Wanyarwanda halafu tutengeneze maigizo na mwisho wa siku tuwapelekee wao watutatulie? Mgogoro wa Rwanda baina ya wahutu na watusi kwa kiasi kikubwa umetatuliwa na Tanzania na hata wakimbizi wa Rwanda na Burundi mara zote walikimbilia Tanzania. Walioikomboa Uganda kutoka katika udikteta wa Iddi Amini Dada ni watanzania na majeshi yao. Na hata mwaka 2007 wakenya walipoingia katika machafuko makubwa ambaye aliingia katikati na kuwaokoa katika mgogoro huo hadi wakafikia muafaka wa kugawana madaraka, ni Tanzania na viongozi wa Tanzania. Sasa iweje leo ati Rwanda na Uganda wawe na busara nzito kutushinda ati ndiyo wanakwenda kutatua mgogoro wa wabunge wa Tanzania ambao kwa hakika umetengenezwa na nchi hizo?
Na kinachoshangaza zaidi, hivi wabunge wetu wa EALA wanakwenda pale kumwakilisha nani? Wanakwenda kuiwakilisha Tanzania au wanakwendakuziwakilisha Rwanda na Uganda? Iweje mbunge au wabunge wa Tanzania aungane/waungane na wabunge wa Rwanda au Uganda na kuwashughulikia wabunge au mbunge wa Tanzania? Je, ni kwa maslahi ya Tanzania na watanzania? Kwa mfano, katika mgogoro huu wa sasa wa kumuondoa spika wa EALA, wabunge wote wa Tanzania isipokuwa wawili tu ndiyo wanapenda spika huyo aongoze na amalize muda wake kwani wanaona hana kosa alilofanya. Inasemekana hata tuhuma ambazo spika huyo anapewa hazithibitiki na ni kwa sababu tu yeye ni Mganda ambaye ameshindwa kuchukua kila atakalopewa na waganda, sasa anachukiwa mno kiasi cha kutaka aangushwe. Je, akishaangushwa, Tanzania itapata faida gani? Na EALA itapata faida gani?
Katikati ya mgogoro huu ni mahali sahihi serikali yetu iingilie kati, iwaite wabunge wetu wa EALA na kuwaonya kwamba wanapaswa kusimamia jambo moja. Tunapokuwa ndani ya Tanzania na tukiongelea masuala ya ndani ya Tanzania lazima tuwe na mgawanyiko wa mawazo n.k. Lakini tunapokwenda nje ya Tanzania katika masuala yote ya kuiwakilisha Tanzania ni lazima sisi tuwe watanzania, tuwe kitu kimoja na tusonge mbele kama Tanzania moja inayopigania jambo inalolijua. Inapotokea kwamba kuna wabunge EALA au kwingineko wanakwenda kuungana na wabunge wa Rwanda au Uganda ili kuwapinga wabunge wenzao wa Tanzania, lazima tutambue kuwa kuna tatizo hapo mahali. "Common sense" peke yake hairuhusu mtu kuikana familia yake na kuungana na jirani yake kumpinga mwanafamilia mwenzake katika suala ambalo familia haina maslahi ya maana.
Tutakubaliana kuwa, mwendelezo wa mgogoro huu wa kumwondoa spika Ziwa hauna maslahi kwa nchi yetu maana hata akiondolewa spika atakayechaguliwa hawezi kutoka Tanzania na kwa namna Kenya, Uganda na Rwanda zilivyoshikana haziwezi kuchagua spika kutoka Tanzania. Jambo hili ni pana na linaweza kabisa kuhusiana pia na mgogoro wa kimya kimya kati ya Rais Kagame na Rais wetu, na pia hatuwezi kudharau hatua ya hivi karibuni ya nchi za Rwanda, Uganda na Kenya kukutana katika vikao vya faragha na kupanga mipango ya maendeleo na miradi mbalimbali ya ushirikiano bila kuihusisha wala kuialika Tanzania. Hii ina maana kuwa wabunge wetu wa EALA wanapaswa kuwa kitu kimoja, waweke tofauti kando na kutetea maslahi ya Tanzania. Kutofanya hivyo kuna maana kuwa tutaungana na waganda na wanyarwanda katika kutekeleza mambo wanayoyajua wao na ambayo nchi yetu haitaweza kunufaika nayo na ambayo kwa hakika yatakuwa yanawahujumu watanzania.
Na pia, mgogoro wa EALA una maana kuwa, fedha za walipa kodi zinaendelea kutapanywa, kutumika vibaya na kufujwa kulipa watu wazima ambao hawajadili masuala tuliyowatuma. Na hili ndilo jambo ambalo kila siku linatuumiza. Kwamba tunatumia mabilioni ya fedha kuendesha bunge la jumuiya ambalo halina tija, ambalo haliendi kupanga mipango ya kuipeleka jumuiya mbele zaidi ya kukutana na kutafuta namna ya kupinduana ili kulinda maslahi ya Kenya, Uganda na Rwanda. Katika mgogoro huu wa EALA, ni jukumu la kila mtanzania kuunga mkono upande wa wabunge wa Tanzania ambao wanatetea maslahi ya Tanzania na tuwakemee kwa sauti kubwa wabunge wote wa Tanzania walioungana na wanyarwanda na Waganda ili kuwashughulikia wabunge wenzao wa Tanzania.
(0787536759.)
Phone; +255717536759,
Email; juliusmtatiro@yahoo.com
Twitter; https://twitter.com/Julius_Mtatiro
0 Comments