[wanabidii] NAIBU MWANASHERIA MKUU AMEWASILISHA PINGAMIZI LA AWALI DHIDI YA KESI YA KUHOJI MAMLAKA YA BUNGE LA KATIBA

Thursday, September 04, 2014
Na Mwene Said wa Blog ya Jamii

NAIBU Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, leo amewasilisha pingamizi la awali dhidi ya kesi ya kuhoji mamlaka ya  Bunge la Katiba linaloendelea mjini Dodoma iliyofunguliwa na  Mwandishi wa Habari Said Kubenea dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwamba maombi hayo ni batili kisheria na hayawezi kuthibitishwa mahakamani, hivyo yatupiliwe mbali.

Masaju amewasilisha pingamizi hilo akitoa sababu nne, akiitaka mahakama kutupilia mbali maombi yaliyopo mbele ya jopo la majaji watatu, wakiongozwa na Mwenyekiti Jaji Augustino Mwarija, Dr. Fauz Twaib na Aloyisius Mujuluzi katika Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.

Katika pingamizi hilo lililoambatana na hati ya kiapo, AG kupitia naibu wake, amedai kuwa maombi hayo ya mlalamikaji yana dosari ambayo haiwezi kurekebishika kwa kuwa zinahitaji kifungu maalum cha sheria kinachoipa nguvu mahakama ya kuridhia maombi hayo.

Sababu nyingine, AG anadai kuwa maombi hayo yaliyopo mahakamani hayawezi kuthibitishwa na kwamba hayana mashiko ya kisheria.

Pia, Masaju amedai kuwa maombi yaliyopo mahakamani ni batili kisheria hivyo mahakama iyatupilie mbali.

Jaji Mwarija alisema kesi hiyo itasikilizwa kesho mahakamani hapo.

Katika kesi ya msingi, kesi  hiyo namba 28 ya mwaka 2014, Kubenea anaiomba mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya Mamlaka ya Bunge la Katiba chini ya  vifungu vya 25 (1) na 25 (2) vya Sheria ya Marekebisho ya Katiba namba Namba 83 ya mwaka  2011 imepangwa kusikilizwa mbele ya Jaji Augustino Mwarija, Dr. Fauz Twaib na Aloyisius Mujuluzi.

Pamoja na mambo mengine katika kesi hiyo ya kuomba tafsiri ya mamlaka ya Bunge  hilo, pia Kubenea amewasilisha maombi mahakamani hapo akiiomba mahakama itoe zuio la muda la kusimamisha Bunge hilo ili kusubiri uamuzi wa maombi ya tafsiri hiyo.

Maombi hayo ya kusimamisha Bunge hilo kwa muda yaliyopewa usajili wa namba 29 ya mwaka 2014, pamoja na maombi ya msingi ya tafsiri ya mamlaka ya Bunge yote yalifunguliwa mahakamani hapo leo chini ya Hati ya Dharura.

Katika kesi hiyo ya msingi anaiomba Mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya masharti ya vifungu hivyo vya sheria hiyo na pia itamke kama Bunge hilo lina mamlaka ya kubadilisha maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwa kiwango gani.

Kwa mujibu wa hati ya madai, Kubenea anadai kuwa msingi wa kesi hiyo unatokana na uamuzi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Desemba Mosi, 2011, lililopitisha  Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Anasema sheria hiyo ilikuwa na lengo la kuratibu mchakato wa kutungwa kwa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments