UTANGULIZI
Ni jambo la kutia simanzi kubwa kwa kila mtu anayeitakia mema nchi yetu kuona kuwa mchakato wa kupata katiba mpya hauendi kama wananchi walio wengi walivyotarajia. Nina imani kuwa kama Rais Kikwete alikuwa na dhamira hasa ya kusimamia upatikanaji wa katiba ya Watanzania inayotokana na matakwa yao, atakuwa amehuzunika zaidi. Nina imani kuwa kama CCM, CUF, CHADEMA, NCCR, na vyama vingine vyote vya kisiasa, walikuwa na nia iliyo njema ya kuhakikisha tunapata katiba iliyo bora kwa nchi yetu, watakuwa wamesononeka sana. Nina imani kuwa kama viongozi wa dini walikuwa na nia njema na Tanzania, nao watakuwa wamehuzunishwa sana. Makundi mbalimbali ya kijamii na ya wanawaharakati, na Watanzania wote, kama dhamira yetu ilikuwa ni kuona tuna katiba iliyo nzuri inayojibu matatizo yetu mengi, inayoipambanua nchi yetu ni Taifa la namna gani, sote tutakuwa tumekatishwa tamaa.
Nina imani kubwa Rais wetu hajafanya kazi ya kutosha kuhakikisha tunapata katiba ya wote kwa manufaa ya wote. Nina imani viongozi wa CCM, CUF, CHADEMA, NCCR, n.k. hawajafanya jitihada za kutosha kuwezesha upatikanaji wa Katiba mpya ya wote. Na upande wa vyama kuna kila dalili kuwa hata ile nia ya dhati haipo. Sioni nia ya dhati kwa Chama Tawala CCM, sioni utayari wa CHADEMA, CUF na NCCR. Vyama vya upinzani hawaamini kuwa CCM ina dhamira ya kutafuta Katiba Mpya. Kutoaminiani hakuwezi kutuletea katiba bora. CCM ijenge mazingira ya kuaminika na UKAWA wajenge moyo wa imani.
Tuna tatizo katika uongozi wa Bunge lenyewe, Mwenyekiti Samwel Sita ameonekana ama kutokuwa na uwezo au kutokuwa na dhamira ya kuona Bunge la Katiba linaendeshwa kwa hali ya maelewano, heshima, Umoja na Upendo. Ameridhika na mwonekano wa Bunge la Katiba kuwa wa malumbano, matusi, vijembe na kukosekana kwa umoja.
NAFASI YA RAIS KIKWETE
Kwa sababu inayoandaliwa ni Katiba ya Watanzania wote, Rais Kikwete alistahili kuonekana kwa kauli na matendo ni mtu asiyefungamana kwa namna yoyote ile na siasa za chama au kundi lolote lile ili kila Mtanzania amwone kwa uthabiti kuwa ni kiongozi wa Taifa na anayesimamia Utaifa. Kuhusiana na Katiba, tena Rais Kikwete alistahili kutokuhudhuria vikao vya CCM (japo ni Mwenyekiti) vyenye dhamira ya kuweka misimamo ya kichama kuhusu katiba.
Kama angejitenga na siasa za chama, angejipa uhalali wa yeye kuwa sehemu ya kukimbilia kundi lolote linalohisi haki zake hazizingatiwi kwenye katiba ama kutokana udogo au udhaifu wake. Kwenye jambo hili la Katiba, kama Kikwete alitaka awe msimamizi halali, ingawa sheria haijampa mamlaka makubwa, alistahili kuwa kama refa wa mpira. Rais ajiulize, 'Je, kama kuna timu mbili za mpira, wakati wa mapumziko refa huyo akaenda mapumzikoni na timu mojawapo, na kule akawa anawapa mbinu namna ya kushinda mchezo anaousimamia, hata kama wakati wa mchezo akasimamia sheria zote 17 za FIFA, timu ile nyingine itaendelea kuwa na imani na refa huyu?'.
Tunatambua kuwa ofisi ya Raisi ni Taasisi kubwa ambayo inastahili kuheshimika lakini hii ofisi kama ipo kwa manufaa ya umma na inatambua uwepo wake umetokana na matakwa ya umma, haipungukiwi heshima yake kwa kutambua pale ilipopotoka au kuteleza iwe ni kwa bahati mbaya au kwa kudhamiria. Mheshimiwa Rais Kikwete, Ofisi yako na wewe mwenyewe binafsi utakuwa umeitendea haki nchi yako na watu wake, na utakuwa umeitendea haki nafsi yako pia kama utahakikisha unafanya kila liwezekanalo, iwe ni kujadiliana au hata kujishusha kwa watu wako ili mradi mwisho wa siku ipatikane katiba iliyo bora na ambayo tuna uhakika ina ridhaa ya Watanzania walio wengi.
WAJUMBE WA BUNGE LA KATIBA
Kwa upande wa wajumbe wa Bunge la Katiba, huko kuna matatizo makubwa zaidi maana inaonekana wajumbe wengi hawafahamu wamekwenda kufanya nini, wengi wanadhani wamekwenda kutetea vyama vyao. Vyama vya siasa vimewapotosha wajumbe wa Bunge la Katiba ili waamini kuwa wamekwenda kwenye Bunge la Katiba kutetea maslahi ya vyama. Katiba itakayopatikana kwa mashindano ya siasa za vyama haiwezi kuwa katiba nzuri kwa watanzania maana upeo wa walioandaa unaishia kwenye sera na malengo ya vyama vyao, na siyo 'vision' ya Taifa.
UKWELI HAUBADILIKI
Kwa Mwanamapinduzi, kushindwa siyo chaguo, japo unaweza kurudi nyuma na kujipanga upya. Rais Kikwete usikubali kushindwa, ukikubali wewe siyo mwanamapinduzi. CCM, CHADEMA, NCCR, CUF, viongozi wa dini, vyama vya kijamii na Watanzania wote tusikubali kushindwa.
Rais Kikwete usiseme kuwa huna mamlaka au nguvu za kisheria kuhusiana na Bunge la Katiba, hata kama huna nguvu za kisheria, tuna uhakika una nguvu za kiutawala na nguvu za ushawishi. Haiwezekani Rais ukose nguvu ya ushawishi katika mambo unayoyaamini. Lipumba, Mbowe, Mbatia, Kinana, Maaskofu na Mashekhe, viongozi wa jumuia mbalimbali ambao taasisi zenu zina wawakilishi Bungeni na Mheshimiwa Samwel Sita hamuwezi kuudanganya umma kuwa hamna ushawishi katika makundi mnayoyawakilisha ili kufikia maafikiano yatakayowezesha kupatikana katiba mpya. Labda mtuambie kuwa hamtaki Katiba mpya ipatikane.
Mheshimiwa Jakaya Kikwete, tunamheshimu kwa kuwa ni Rais wetu, na matumaini ya wengi yamejengwa juu yake, ndiyo maana hata wale wanaompinga katika mengi, wanapofikia kwenye suala la Katiba, wanasema kuwa, 'Tunamwomba Rais ---------', hiyo ni kutambua kuwa ana mamlaka makubwa katika mchakato huu hata kama mamlaka hayo hayajaainishwa moja kwa moja na sheria ya mchakato wa kupata katiba mpya.
NANI WANA UWEZO WA KUTUKOSESHA KATIBA MPYA
Tukikosa katiba mpya, watakaokuwa wametukosesha ni hawa wafuatao:
1. Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
2. Rais Mstaafu Benjamin Mkapa
3. Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi
4. Katibu Mkuu wa CCM Abrahamani Kinana
5. Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe
6. Mwenyekiti CUF Ibrahim Lipumba
7. Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi James Mbatia
8. Mwenyekiti wa Bunge la Katiba Samwel Sita
9. Viongozi wa dini
Nimewataja na Marasi wastaafu siyo kwa sababu ya mamlaka yao ya kisheria bali kwa sababu wana ushawishi na wanawajibika kwa umma wa watanzania, ndiyo maana hata wakienda mahali popote tunawasikiliza. Pia nimewataja viongozi wa dini kwa sababu viongozi wote wa serikali, vyama, na Bunge, wote ni waumini wao. Rais Kikwete hawezi kukataa kuzungumza na Mufti mkuu au na maaskofu. Pia Marais wastaafu hawawezi kukataa kuongea na viongozi wao wa dini. Rais Kikwete hawezi kukataa kuongea na Marais Wastaafu. Kinana hawezi kukosa ushawishi kwa wabunge wa CCM, kama ilivyo kwa Lipumba, Mbowe na Mbatia kwa wabunge wa CUF, CHADEMA na NCCR.
Uongozi uliotukuka si ule unaotokana na sheria pekee bali pia unaotokana na ushawishi unaokubalika kwa vile unaowaongoza wanakuamini. Marais wastaafu Mwinyi na Mkapa siyo viongozi kisheria lakini kijamii ni viongozi wakubwa ambao hawastahili kukaa kimya wanapoona kuna mambo yanayowagawa watanzania, na huo ndiyo uzalendo. Sheria zipo kwaajili ya kutupa miongozo lakini utashi, hekima na uzalendo ndivyo vinavyohalalisha uongozi.
NINI CHA KUFANYA
1. Hawa niliowataja kama watu wanaoweza kusababisha tupate au tusipate katiba mpya, watumie busara na hekima zao, ushawishi na sheria zilizopo kusimamisha Bunge kwa muda
2. Viongozi wa vyama vya siasa wakakae na wabunge wao na watoe tamko la kufuta miongozo ya vyama juu ya katiba ili wajumbe wajadili katiba kwa kutegemea utashi wao na matakwa ya watu wanaowawakilisha
3. Wabunge waapishwe upya, na watamke kuwa watatoa michango yao kwa kuzingatia mahitaji ya Taifa na siyo makundi wanayoyawakilisha pekee. Na wakati wote wa mijadala wajitambulishe kwa Utaifa wao na siyo vyama vyao vya Siasa
4. Kanuni za Bunge la Katiba zitamke pia kuwa wajumbe wote waliopo Bungeni ni wajumbe wa kitaifa, makundi yaliyowateua ni njia tu ya kuyapitia ili kuhakikisha kuna uwakilishi mzuri, na wala hawawakilishi makundi yaliyowachagua pekee
5. Vipengere vyote vinavyoonesha utofauti mkubwa wa mawazo au visivyokubalika na wajumbe zaidi ya theluthi 2 (Bara na Visiwani), pamoja na vile vinavyotegemea vipengere hivyo, viamuliwe na wananchi wakati wa kura ya maoni
6. Vipengere visivyobishaniwa au majadiliano juu yake yamewezesha kupatikana kwa makubaliano, vipitishwe na vipigiwe kura ya maoni
7. Utengenezaji wa katiba upitie hatua mbili. Hatua ya kwanza iwe na upigaji kura wa maeneo mawili: Wananchi wapige kura ya NDIYO au HAPANA kwenye vipengere visivyobishiniwa au maafikiano yalifikiwa kwenye bunge la katiba. Vipengere ambavyo havikuwa na muafaka vipigiwe kura ya kuchagua jibu. Wananchi waamue kama wanataka SERIKALI MBILI AU TATU, MABUNGE MAWILI AU MATATU.
8. Vipengere visivyobishaniwa vikipitishwa, na wananchi wakawa wameamua juu ya muundo wa serikali na bunge kwa idadi ya kura zinazokubalika kisheria, Bunge la katiba likae kwa mara ya pili kumalizia sehemu ya rasimu inayozungumzia muundo wa serikali na bunge, na vile vipengere vyote vinavyohusiana na maeneo hayo. Baada ya hapo wajumbe wa Bunge la katiba wapige kura kuidhinisha katiba
9. Bunge lifanye marekebisho ya sheria ya Katiba ili kuruhusu mabadiliko fulani kwa manufaa ya Taifa letu.
10. Mazungumzo ya pande zinazokinzana yasimamiwe na watu huru na wenye hekima, na watu hao si lazima wawe ni viongozi wakubwa bali wanaoaminiwa na pande zote. Wateule wa Rais siyo watu sahihi wa kusimamia mazungumzo haya, siyo kwa sababu hawaaminiki bali kwa sababu ya kuondoa taswira kwamba ni mazungumzo yanayosimamiwa na serikali, serikali ambayo inaongozwa na chama. Ifahamike kuwa msimamizi anaweza kuwa dhamira njema lakini asipoaminika hata nia yake njema wapinzani wake hawawezi kuiona.
11. Rais Kikwete asishiriki vikao vya CCM vinavyoongelea masuala ya katiba, na ushauri wake wote ulitazame Taifa kwanza. Kama ana nia ya kuongea na viongozi wa vyama vya siasa, aongee na viongozi wa vyama vyote kama mlezi wa Taifa, na siyo kama Mwenyekiti wa CCM.
MWISHO
Kitakachotupatia katiba bora ni dhamira safi, kuheshimiana, kuthaminiana, kutambua kuwa pamoja na uwezo wetu kutofautiana katika mambo mengi lakini kila mmoja ana haki sawa katika nchi yetu. Leo hii tuna matatizo makubwa katika usimamizi wa sheria zetu ambapo watu wetu wengi wa hali chini wanaona kuwa sheria hufanya kazi kwao tu, wakubwa haiwahusu. Tunapotaka kuibadili hali hiyo, ni lazima tuanzie na uandaaji wa sheria yetu Mama. Kama kuna watu wanajiona wana nguvu zaidi kuliko wengine na kujipa haki zaidi kwenye kuandaa katiba, basi pasi na shaka katiba itakayoandaliwa nayo itaakisi fikra hizo.
Tunataka katiba itakayomfanya kiongozi mkuu na viongozi wetu wote kuwa watumishi wa wananchi, wanaowahudumia wananchi siyo wao kuhudumiwa na wananchi. Hali hiyo ni lazima ijengeke kutoka hatua za awali za kuitengeneza katiba. Bunge la Katiba lijione kuwa ni taasisi ya utumishi, juu yao kuna 'BOSS', ambaye ni Wananchi wa kawaida. Wajumbe wa Bunge la Katiba wakiwa na mawazo hayo, watakuwa waoga kubadili kipengere chochote kilichotokana na maoni ya 'BOSS' wao kama hakuna sababu za msingi za kufanya hivyo. Lakini pia ni muhimu sana kujiridhisha kuwa tunayoogopa kuyagusa yametoka kwa umma. Kama tuna mashaka, kama inavyoonekana sasa kuhusiana na muundo wa serikali, njia sahihi ni kurudi kupata uhakika toka kwao kwa njia ya kura ya maoni.
Bart
0 Comments