[Mabadiliko] JK, kiepuke kikombe hiki (Changia)

Sunday, August 24, 2014
JK, kiepuke kikombe hicho!
Na Mashaka Mgeta
 
24th August 2014
Moja ya sifa kuu za kuanguka, kuadhibiwa ama kuangamia kwa tawala za kidunia, ni kiburi. Kiburi kinaweza kujitokeza kwa namna tofauti kulingana na eneo la jiografia ama tamaduni za watu wake.

Kiburi kinapokuwa sehemu ya utawala wa nchi, inaweza kutafsiriwa kuwa ni moja ya ishara kwa hayo niliyoyataja hapo awali, yakiwa ni miongoni mwa mengi yanayoweza kutokea katika tawala za kidunia zikiwamo serikali za mataifa.

Mara nyingi, kiburi cha watawala kinapatikana kupitia Mamlaka ya Dola ama wingi wa idadi yao ikilinganishwa na wachache walio na haki sawa katika ubindamu wao, kama walivyo watawala.

Walio wachache wanakuwa wakidai haki na usawa dhidi ya watawala, lakini watawala, kwa kutaka kujenga mazingira ya kuendelea kuwapo madarakani, wamekuwa wakiwakandamizia, wakiwabeza na wakati mwingine kuwafunga jela walio miongoni mwa wachache.

Hali hiyo inaweza kwenda mbele zaidi pale watawala wanapofanya hila na hujuma kuzima sauti na mahitaji ya walio wengi, ingawa kwa uwakilishi wanakuwa na wawakilishi wachache.

Wanapotokea walio wachache wanapaza sauti, watawala wanawakejeli kwa propaganda zikiwamo zisizokuwa na mashiko, ili mradi kutaka (wachache) wazidi kukandamizwa.

Utawala wa Farao nchini Misri ulipotakiwa kuwaachia wana wa Israel warejee kwao kwa amani, ulikataa. Mungu aliifanya mioyo ya watawala hao kuwa migumu.

Mioyo kuwa migumu ni ishara za kiburi na jeuri. Matukio kadhaa yalielekezwa kwa utawala huo ili 'kuwaamsha' watambue na kuyakubali mabadiliko yaliyopaswa kufanyika, lakini walijawa na kiburi.

Matokeo yake, hata wana wa Israel walipofanikiwa kuondoka Misri, utawala wa Farao ulituma wanajeshi wake kuwafuata hadi walipowakuta wakivuka katika bahari ya Shamu iliyogawanyika 'vipande' viwili.

Kwa kiburi na jeuri yao, majeshi ya Fara yaliingia katikati ya bahari ili kuwakamata wana wa Israel na kuwarejesha utumwani, lakini wakiwa katikati ya bahari, Musa aliyewaongoza Waisrael, alipiga fimbo juu ya maji (kwa agizo la Mungu), maji yakarejea.

 Wanajeshi wa Farao waliokuwa wanatumia farasi waliangamia, hivyo ikawa moja ya adhabu iliyotokana na kiburi cha watawala.

Mfano huo unaweza kuwa wa miaka mingi huku ukighubikwa na 'matunda' ya imani. Lakini hata mwaka 2002, mchakato wa Uchaguzi Mkuu nchini Kenya ulihusisha chama tawala cha KANU, kumsimamisha mgombea Urais wake.

Mtawala wa wakati huo, Rais mstaafu Daniel Toroitich arap Moi, aliwaambia Wakenya kwamba, miongoni mwa raia wa taifa hilo lililo ukanda wa Afrika Mashariki, hakuna aliyefaa kuwa 'mrithi' wake isipokuwa Uhuru Kenyatta.

Kwa wakati huo, Wakenya hawakuwa tayari kuongozwa na Uhuru. Walimuona kuwa ni kiongozi asiyekuwa na uwezo wa kuliongoza taifa hilo.

Kwa jeuri na kiburi, Moi aliamuru na kupitia hila tofauti, Uhuru aliteuliwa kuwania Urais kupitia chama tawala cha KANU.
 
Waliokuwa washirika wa karibu katika chama hicho, ingawa kwa uchache wao, akiwamo Raila Odinga,  walikihama, wakaungana na Wakenya wengine kupingana na wazo la Moi.

Hatimaye KANU iliadhibiwa kwa kupoteza utawala, akachaguliwa Rais Mwai Kibaki kupitia Muungano wa Upinde wa Mvua (NARC).

Hata hivi sasa ninavyoandika, KANU si tu kwamba kimebaki kuwa chama cha upinzani, hata ukubwa wake kwa siasa za Kenya ni kama Asasi ya Kijamii (NGO). Nguvu zake ni kama zimekwisha na kubaki katika kumbukumbu za historia ya nchi hiyo.

Ipo mifano mingi ambayo kama nilivyoieleza awali, inakuwa ishara ya kiburi kinachochochea kuanguka ama kuadhibiwa kwa tawala za kidunia.

Hapa nchini, mjadala unaendelea hivi ni kuhusu kuandikwa kwa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mchakato huo umefikia hatua ya rasimu ya Katiba Mpya kujadiliwa katika Bunge Maalum la Katiba linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma.

Wakati mchakato huo ukiendelea, kundi la wachache wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), limetoka nje, halishiriki vikao hivyo kwa sababu watawala wameingiza masuala yasiyotokana na rasimu hali ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Inawezekana mazingira yaliyopo nchini hivi sasa yanatofautiana kabisa na wakati wa utawala wa Farao huko Misri, utawala wa Moi nchini Kenya ama tawala nyingine zilizojawa kiburi, zikatumia nguvu za Dola kufanya kile wanachokiona kina maslahi kwao.

Lakini si jambo la kuibua malumbano pale inapotamkwa kwamba, mchakato wa Katiba Mpya hasa kupitia Bunge Maalum la Katiba, umeingia dosari.

Wapo wanapiga propaganda kwamba Ukawa inayoundwa zaidi na vyama vya upinzani vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, wana nia ovu kwa mustakabali wa Taifa. Propaganda hiyo inajengwa zaidi na watawala, pengine ni kutokana na kiburi kile kile, kama cha Farao na Moi, japo kutaja kwa uchache.

Lakini uhalisia uliopo ni kwamba, wanaoukosoa mchakato uliofikia hatua ya Bunge Maalum la Katiba, si wapinzani tu, bali hata asasi za kijamii na walio katika chama tawala-Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Sehemu kubwa ya wajumbe ya wajumbe waliounda Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ikiongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba, wanatokana ama kufungamana na CCM.

 Mungu ibariki Tanzania na watu wake nikiwamo mimi.
 
Mashaka Mgeta ni Mhariri wa Dawati la Uchunguzi na mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii. Anapatikana kupitia simu namba +255754691540, 0716635612 ama barua pepe: mgeta2000@yahoo.com au mashaka.mgeta@guardian.co.tz
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI (Home)
 

Share this :

Related Posts

0 Comments