[wanabidii] Wanaotoka CHADEMA wanakijua wanachokifuata ACT?

Wednesday, July 23, 2014
Mnaotoka Chadema, mnakijua mnachofuata ACT?
Na Mashaka Mgeta
 
KUHAMA kutoka chama kimoja cha siasa kwenda chama kingine si kosa kwa mujibu wa sheria za nchi.
Bali ni moja ya uhuru ulio ndani ya haki za binadamu, kwamba kutokana hiari, ushawishi ama vyote viwili vinapotii hitaji la moyo na fikra, basi inakuwa hivyo.
 
Ndivyo ilivyo hata kwa asasi nyingine za kiraia kama madhehebu ya dini. Wapo wanaodumu kwenye dhehebu moja, na wanapojiridhisha kwa nafsi zao, kwamba hawapati kile walichokitarajia, wanahama.
 
Hivi karibuni na hata sasa, taarifa za wimbi la baadhi ya wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kujiunga Alliance for Change and Transparency (ACT) zinazidi kuandikwa na kutangazwa kupitia vyombo vya habari.
 
Ingawa kasi hiyo inaonekana zaidi mikoa ya kanda ya Magharibi hususani Kigoma, lakini inaweza kuenea kwenye maeneo mengine ya nchi. Wakatoka Chadema na kujiunga ACT.
 
Kama nilivyoeleza awali, hilo si jambo baya, si kosa, si uhuni, si uhaini na si uovu wa namna yoyote ile, ili mradi linafanyika kwa nia njema inayolenga kustawisha demokrasia nchini.
 
Inawezekana wanaojiunga ACT wasiwe wanaotoka Chadema tu, wanaweza wakatoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Labour Party (TLP), United Democratic Party (UDP), Chama cha Wananchi (CUF) na vinginevyo.
 
Lakini kwa vile taarifa nyingi zinaelekezwa kwa wanachama wanaotokana na Chadema, na kwa vile waasisi wa ACT walifukuzwa uanachama kutoka Chadema, mjadala utaanzia na kujikita hapo.
 
Binafsi, hatua hiyo ninaona kwa mtazamo usiokuwa mwema sana kwa ACT badala ya Chadema. Ingawa ni hivyo, wapo wanaoamini kwamba ACT inapokuwa kimbilio la wanaotoka Chadema, basi chama hicho (Chadema) ndicho kinachoathirika.
 
Wakati nikiandika makala hii, ikumbukwe kwamba Jumatano ya Machi 5, mwaka huu, niliandika makala yenye kichwa kilichosomeka, Chadema isiwe `itikadi' ya ACT.
 
Maudhui ya makala hiyo inayopatikana hata sasa kupitia http://www.ippmedia.com/frontend/index.php/oi.poc/javascript/page_home.js?l=65464, yanaweza kufanana kwa kiasi Fulani na haya ya leo.
 
Maana yake ni kwamba, ACT, pamoja na 'kuwakomba' wanachama kutoka Chadema, haipaswi kujiegesha kwa chama hicho kinachounda kambi rasmi ya upinzani bungeni, kuwa ni mtaji wa shughuli zake za kisiasa.
 
ACT haitakiwi hata kwa dakika moja, `kujiegesha' kwa Chadema ili kionekane kwamba, kupitia viongozi wake na ushawishi wa namna yoyote kutoka kwao, kina nguvu.
 
'Kuwakomba' wanachama kutoka Chadema kutakuwa na maana kwa ACT ikiwa kutatokana na hiari inayotokana na kupata taarifa sahihi kuhusu itikadi, dira, malengo na mwelekeo wa chama hicho, nao wakakiunga mkono.
Lakini ushawishi wenye nia ovu utakaofanywa, hata kama si kupitia viongozi wa ACT ama waasisi wake, hata wakiwa wanachama wenye hulka ya 'bendera fuata upepo', hautaifanya ACT kuwa imara.
 
Ushawishi wenye nia ovu, ama ule unaotokana na watu kutokuwa na taarifa sahihi zinazoweza kuwafanya wafikie uamuzi sahihi,  mara zote wanapotoka na wanafanya uamuzi usiokuwa sahihi.
 
Ndivyo inavyowezakuwa kwa ACT, kwamba ikiwa wanachama wakiwamo wanaotoka Chadema, watapotoshwa kiasi cha kuchukua uamuzi ambao baadaye utabainika kuwa ni potofu, chama hicho hakitabaki salama.
 
Lazima waliopotoshwa watawahoji waliowapotosha, kwamba kile kilichoelezwa wakati wa ushawishi wenu, kwamba tutakipata huku, mbona hakionekani?
 
Ama ile misingi mliyoihubiri hata kutufanya tutoke kule kuja huku, mbona haipo na badala yake tunaiona `jana ya Chadema' ni bora 'leo ya ACT'? Yanaweza yakaulizwa maswali mengi.
 
Njia pekee itakayokiepusha ACT katika kadhia hiyo, ni kuhakikisha kwamba uimara wake hautokani na 'kuibomoa' Chadema ama kuvivuruga vyama vingine vya upinzani.
 
Tena isieleweke kwamba ninaionyooshea kidole ACT katika hilo, hapana. Ninachoandika ni kuwatahadharisha viongozi na waasisi wake, ili yaliyotokea, kwa mfano,  NCCR-Mageuzi ya enzi za Augustino Mrema, kisha mwanasiasa huyo akatikiswa akiwa TLP, yasije yakatokea ACT.
 
Kwa maana wakati wa mgogoro ulioisambaratisha NCCR-Mageuzi, wapo waliotambua kusudio la kujiunga kwao katika chama hicho. Hawakuyumba, hata hivi sasa bado wamo ama wanashiriki siasa kwa namna nyingine inayofaa.
 
Lakini wapo waliotikisika, wakafuata upepo wa Mrema alipohamia TLP. Miongoni mwao ni aliyewahi kuwa Mbunge wa Moshi Vijijini, Thomas Ngawaiya. Lakini walipofika kule walipobaini kwamba walichokitarajia hakikuwa kilichokuwa kinatokea, Ngaiwaiya `alijisalimisha' CCM.
 
Uongozi wa TLP ukafananishwa na utawala wa kidikteta na kila aliyehoji kwa uwazi ili apate taarifa sahihi, alitimuliwa. Timua timua ikawakumba waliokimbilia TLP kutokana na ushawishi uliowafanya wakose taarifa sahihi kuhusu itikadi, dira, malengo na mwelekeo wa chama hicho.
 
Wanachama waliokuwa na Mrema kule NCCR-Mageuzi, kisha wakamuunga mkono alipojiunga TLP, wakafukuzwa. Wengine wakajiunga Chadema akiwamo Msafiri Mtemelwa na Mbunge (Viti Maalum), Suzan Kiwanga, miongoni mwa wengi.
 
Leo hii, NCCR-Mageuzi imeendelea kubaki kuwa imara, hata kama si kwa wingi wa wabunge kama waliopatikana katika Uchaguzi Mkuu wa 1995.
 
Hata CUF iliwahi kutikiswa kwa nyakati tofauti. Kwa waliojiunga kwa kuzitambua itikadi, dira, malengo na mwelekeo wake, wapo ama wanashiriki siasa kwa namna nyingine inayofaa.
Ipo mifano mingi ambayo nina hakika, viongozi na waasisi wa ACT wanaijua hata kuliko iliyotajwa hapa. Hapo sijagusia uwezekano wa kuingia mamluki watakaojitangaza kutokea Chadema. Bado kwa ujumla wake, mazingira kwa chama hicho hayatakuwa salama.
 
Lakini kama ACT ikifanikiwa kujipenyeza kwa umma, na ninaiombea iwe hivyo, ijipambanue kwa itikadi, dira, malengo na mwelekeo, vyote vikiugusa umma na kuufanya umma ukimiliki chama hicho, basi kitasafiri 'njia njema' na kufika salama. Hilo ndilo liwe kusudio lililo kuu.
 
Mashaka Mgeta ni Mhariri wa Habari za Uchunguzi ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii. Anapatikana kupitia simu namba +255 754691540, 0716635612 ama barua pepe:mgeta2000@yahoo.com au mashaka.mgeta@guardian.co.tz.
 
SOURCE: Nipashe, 23 Julai, 2014

Share this :

Related Posts

0 Comments