Katika biblia hakuna kosa lililo dogo wala kubwa kuliko lingine. Makosa yote ni sawa mbele za Mungu. Jambazi, mchawi, fisadi, kibaka na mzinzi, wote watapata hukumu iliyo sawa sawa. Dhana hii ni tofauti na jinsi tunavyoichukulia hapa duniani ambapo kila mtu huadhibiwa kulingana na uzito wa kosa alilotenda.
Kosa kubwa kuliko yote hapa Tanganyika ni kuendelea kuikumbatia serikali dhaifu na ya kifisadi inayoongozwa na CCM. Serikali hii 'sikivu' imeshindwa kabisa kuboresha maisha ya wafanyakazi katika nchi hii. Kila mwaka tunaambiwa serikali haina fedha huku tukishuhudia ufisadi wa kutisha, matanuzi ya kipuuzi ya viongozi wa serikali, kulipana posho kubwa kubwa, misamaha ya kodi, ufisadi na maovu mengine kama haya yakitendwa na serikali ya CCM kila kukicha. Yote haya yanafanyika kwa gharama za wananchi na mwisho wa siku wananchi wameendelea kuishi maisha ya kusikitisha wakati nchi ikiwa imebarikiwa kuwa na rasimali kedekede kama vile almasi, misitu, tembo, twiga, dhahabu, tanzanite na utajiri mwingine chekwa!
Kitendo cha serikali ya CCM kugoma kuongeza mishahara ya watumishi kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015 ni uhaini, ugaidi na uuaji ambao haukubaliki hata kidogo. Watumishi wa umma wamekuwa wakiishi kama yatima katika nchi hii huku kikundi kidogo cha mafisadi wasiozidi 50 wakiendelea kutumbua rasimali za taifa na kuishi kama vile wako peponi. Ni lini hasa serikali hii ya kijangili itaacha kuwadharau, kuwanyonya na kuwaonea wafanyakazi katika nchi hii kwa kuthamini mchango wao katika maendeleo ya taifa?
Mwaka wa jana tumeshuhudia serikali hii ikigoma kupunguza kodi ya mishahara na badala yake ikapunguza kwa 1% tu, kiwango ambacho ni sawa na bure. Tumeshuhudia wajumbe wa Bunge Maalum la Matusi (BMM) wakilipwa mamilioni ya shilingi kwa ajili ya kutukana tu na kazi hiyo ya kutukana wameifanya kwa muda mrefu hadi imebidi waongezwe muda mwingine wa kuendelea kutukana na kukejeli maoni ya wananchi. Pesa kama hizi zinazopotea bila sababu ya msingi, zingepaswa zitumike kuboresha mishahara ya walimu. Walimu tumekuwa tukiishi kama wakimbizi. Huwezi kuamini kwamba mshahara wa mwalimu mwenye shahada hauzidi Tsh 300,000 kwa mwezi. Kila mtu ni shahidi kwamba wajumbe watukanaji wa bunge la katiba wanalipwa zaidi ya kiasi hicho cha pesa kwa siku wakati mwalimu anayeeelimisha taifa hulipwa chini ya kiwango hicho kwa mwezi na wakati mwingine kukaa zaidi ya miezi 6 bila kulipwa mshahara. Jamani, usawa wa binadamu upo wapi katika nchi hii?
Natoa wito kwa wafanyakazi wote, hasa walimu, kujitahidi kuwahi kufika kazini. Mkifika kazini tieni saini kwenye vitabu vya mahudhurio, kisha endeleeni kupiga soga mpaka muda wa kazi unapoisha mrudi majumbani kwenu. Ndio. Hatuwezi kila siku tuwe tunatumiwa na mafisadi kama ngazi ya kupandia na kuning'inia madarakani huku sisi tukiendelea kuishi maisha ya dhiki. Ifike wakati walimu tujitambue na tukatae kunyonywa na mafisadi ilhali tunao uwezo wa kukataa unyonyaji huu. Mkakati huu wa kutofundisha utasaidia kuzalisha wajinga na wajinga wakishakuwa wengi itakuwa sio rahisi kutawalika. Hapo ndipo sasa wafanyakazi tutakapoanza kuthaminiwa. Malipo yetu yataboreshwa na tutakuwa hatucheleweshewi mishahara. Ule utaratibu wa kufundisha chini ya kiwango umeonekana kwamba haulipi tena. Kufundisha chini ya kiwango huzalisha watu wenye elimu nusu ambao ni rahisi kutawalika. Ni bora sasa tuanze mapango mpya (BRN) wa kutokufundisha kabisa ili tuzalishe vilaza halisi wasiotawalika tupate kuheshimiana.
SOLIDARITY FOR EVER!
0 Comments