[wanabidii] RASIMU HII YA KATIBA ITATETERESHA NA HATIMAYE KUVUNJA MUUNGANO

Thursday, March 06, 2014

RASIMU HII YA KATIBA ITATETERESHA NA HATIMAYE KUVUNJA MUUNGANO


Utabiri wa Mtoto wa Mkulima


Mjadala wa Rasimu ya katiba ya kwanza na ya pili umejikita zaidi katika mapendekezo ya Tume ya Jaji Warioba kuwepo kwa Muungano wa Serikali Tatu. Msukumo wa kuitaka hoja hii ikubalike umetuondolea umakini wa kutathmini hata huo muundo wa Serikali tatu unaopendekezwa. Cha kushangaza zaidi ni pale wajumbe wa Tume wakiongozwa na Jaji Warioba mwenyewe, wanapotutaka tuukubali mfumo wa Serikalu tatu bila tafakuri. Rai yangu kwa Watanzania ni kuwa ‘tusifunge milango ya kujifunza kuhusu katiba tunayoitaka eti kwa kuwa tu Tume,chama cha siasa, ‘Jukwaa la katiba’, au nguli mwingine yeyoteametushawishi tuikubali’. Nadhani tuwapongeze Tume ya Katiba kwa kazi nzuri kwa sababu kuna baadhi ya mambo kwenye hiyo Rasimu ni muhimu sana. Lakini Tume haina budi ituachie uhuru wetu wa kuijadili Rasimu hii na kuitolea maoni na maamuzi kwa nafasi zetu. Mimi ningependa kuchukua nafasi yangu kama mtabiri tu. Natumia uhuru wangu wa kujieleza kutokana na Kifungu cha 18 cha katiba na wajibu wangu kwa taifa kama mwanazuoni. Mwaka 2012 mchambuzi na mtabiri wa masuala ya kisiasa Mutahi Ngunyi (Kenya) alitabiri kabla ya uchaguzi kuwa Ushirika wa JUBILEE(Uhuru Kenyatta na William Ruto)nchini Kenya ulishashinda uchaguzi huo tangu tarehe 18 Disemba 2012 pale tu daftari ya kuandikisha wapiga kura lilivyofungwa rasmi. Kwa maono yake,ingawa hakupenda litokee hilo, walakini JUBILEE ilikuwa na mtaji mkubwa zidi ya CORD (Raila Odinga)katika kile alichokiita ‘the tyranny of numbers’. Watu wengi waliunanga utabiri huo, lakini mwisho wa siku sote tunafahamu yaliyotokea.


Nadharia ya miungano ya Profesa Mwesiga Baregu, inatuambia kuwa kuna misukumo ya aina nne inayozifanya nchi ziungane. Wa kwanza ni upendo/udugu na historia ya ushirikiano ambayo nchi hizo imekuwa nazo. Ya pili ni nchi kutarajia kuwa itanufaikakiuchumi/maendeleo ndani ya  muungano. Tatu, ni tishio la kushambuliwa kivita huzifanya nchi kuungana ili ziwe salama zaidi. Nne, nchi moja yenye nguvu kulazimisha nchi ingine/zingine kuwa katika muungano kwa kuwa ina uwezo wa kulipa gharama za kuendesha muungano. Kwa ujumla, misukumo hiyo hutegemeana na mazingira halisia ya nchi hizo au ukanda huo. Kwa Tanzania, ingawa, udugu na historiaya pamoja ndo tunavyovisisitiza katika utangulizi wa Rasimu, walakini wachambuzi wengi wamewahi kuandika tangu miaka ya 1960 kuwa ni tishio la ndani juu ya ulinzi na usalama wa nchi na lililotokana na ‘vita baridi’ kuwa ndiomambo yaliyotusukuma kuungana mwaka 1964. Ningependa kuafikiana na hoja hii, lakini swali la msingi katika mjadala wetu ni mambo gani yanatusukuma kuendelea kuwepo kwenye muungano baada ya miaka 50 sasa?


Kiuhalisia, udugu na historia ya pamoja ni misukumo dhaifu sana. Historia inatuonyesha kuwa misikumo hii imeshindwa kuulinda Muungano wa Somalia na Somaliland, kama vile ilivyoshindwa kuzuia Eritrea isijitenge kutoa Ethiopia. Kwa Tanzania bado msukumo huu ni dhaifu pia. Msukumowa tishio, ingawa umekuwa na nguvu siku za nyuma, hauna mashiko tena. Watu watazungumzia siasa za ndani na mashindano ya kushika Dola kwa upande wa Zanzibar, lakini tumechagua mifumo ya kidemokrasia na nchi hizi mbili, Zanzibar na Tanganyika zinaweza kujiendesha bila wasiwasi. Msukumo wa nguvu unakosa uhalisia kwa Tanzania kutokana na hali yetu ya kiuchumi. Sio Tanganyika wala Zanzibar mwenye uwezo wa kulazimisha muungano na kubeba gharama zitokanazo na muungano huo. Lakini msukumo ya kunufaika kimaendeleo ya kiuchumi ndio msukumo ambao unaleta maana zaidi kwa kuwa ndio ambao unazifanya jumuiya nyingi Afrika na kwingineko ziendelee kuundwa na kudumu.   Kwa tathmini yangu Rasimu hii yakatiba itateteresha Muungano na baadae kuuvunja kabisa kwa sababu zifuatazo:


Kwanza, inatengeneza Serikali ambayo itakosa Uhalali kwa Raia. Uhalali ninaouzungumzia hapa sio ule tu wa kupiga kura ya maoni na kupitisha katiba, bali wananchi kuendelea kuiona Serikali yao inafaa muda hadi muda. Kwa mujibu wa mambo ya Muungano, Serikali hii itatoa huduma za aina mbili tu kwa wananchi. Itatoa hati za kusafiria na kushughulikia mambo ya uhamiaji, na pili itatoa ‘ulinzi na kuhaikisha usalama wa raia na mali zao’. Ingawa hizi huduma ni za muhimu, lakini ni vigumu kuamini kuwa hivi ndio vipaumbele vya Watanzania. Yawezekana utendaji wa hao walinzi wa amani na usalama utaboreshwa, lakini ilivyo sasa wengi wao tunawaona kama ‘maadui kuliko walinzi’. Natabiri kuwa Serikaliinayotengenezwa na Rasimu hii itakuwa ni ya kujihudumia zaidi (self serving) kuliko kuhudumia wananchi. Ibara ya 10 (c)ya kwenye Rasimu inayozungumzia uwezeshwaji wa kiuchumi ni kama matakwa (wishes) tu ambayo Serikali hiyo haitayatekeleza kwani siyo mambo ya Muungano. Matokeo yake basi Serikali hii itakosa uhalali wa kuendelea kuwepo, kwani haitagusa vipaumbele vya wananchi kama vile afya, elimu, ujenzi wa miundombinu n.k. Nachelea kufikiri kuwa tutakuwa na Rais ambaye atanadi sera ya kutujengea mahusiano mazuri ya kimuungano na kimataifa, amani na usalama (tu) wakati sisi watoto wa wakulima tunataabika na umaskini! Kwa mtazamo wangu Rasimu hii inaikuza tu iliyokuwa Wizara ya Muungano na kuiongezea mamlaka ya kidola.


Pili, Rasimu hii inaunda Serikali ambayo, ingawa itakuwa na nguvu za kijeshi, lakini itakosa nguvu za kiuchumi. Ibara ya 231 ya Rasimu inaonyesha vyanzo vya mapato ya Serikali. Yawezekana ukusanywaji wa mapato utaboreshwa zaidi, kama vile faini za Trafiki barabarani, na ushuru wa bidhaa, lakini Tume ya Katiba ilitambua wazi kuwa mapato hayo hayatatosha kuendesha Serikali, ndipo wakapendekezakuwepo kwa michango kutoka kwa Serikali washirika. Ukiangalia Mashirikisho yaliyopo duniani, kama vile Marekani, Urusi, Canada na Australia, mpango wa Tanzania ni wa kipekee. Mbaya zaidi ni kuwa upekee huu hausaidii kujenga muungano. Rasimu hii inatungenezea Seriakali ya Muungano itakayoendeshwa kwa kutegemea maelewano mazuri kati ya Rais wa Muungano na wale wa Serikali washirika. Huu ni msingi dhaifu wa kuendesha Serikali. Na serikali isiyo na mapato ya uhakika ni kama ‘kasha tupu’.Ripoti ya Tume inaonyesha walitathmini muundo wa Shirikisho la Urusi. Cha kushangaza, hawakutilia maanani shirikisho hilo ambalo kwa makusudi kabisa limeweka biashara za kimataifa, rasilimali za shirikisho na kodi za shirikisho kuwa mambo ya Muungano wao. Inashangaza pale Rasimu  (Ibara ya 228) inapoipa Serikali hii mamlaka ya kukopa wakati haitakuwa na vyanzo vya mapato ya uhakika ya kulipa deni hili!

 

Tatu, natabiri hatari ya kuwepo kwa misuguano kati ya Serikali ya Muungano na Serikali Washirika ambayo itazua maswali kuhusu uhalali wa muungano. Katika suala la kuchangia uendeshwaji wa Serikali ya Muungano, Rasimu haituambii itakuwa katika uwiano gani! Ripoti zinaonyesha katika kipindi cha nyuma Zanzibar walikuwa wanapata mgao na sio kuchangia uendeshwaji wa Serikali ya Mungano. Katika uwiano wowote wa kuchangia utakaopangwa, ni rahisi kwa Tanganyika na Zanzibar kuona kuwa Serikali ya Muungano ni ya ‘kinyonyaji’ kwa kuwa itanyang’anyana mapato na Serikali washirika ili ikajihudumie wakati wao wana jukumu kubwa la kuwahudumia wananchi na ambao ni walipa kodi. Nachelea kufikiri nini kitatokea kama watakao ongoza Serikali hizi, watatoka katika vyama tofauti vya siasa!


Nne, napenda kusisitiza kuwa wanaozungumza kuendesha Serikali ya Muungano kutaongeza gharama wasibezwe hata kidogo. Uendeshaji wa Ofisi ya Rais na Makamo wake, Bunge, Mahakama, Wizara 15, Barozi zote za Tanzania na Taasisi zingine za kimuungano sio jambo dogo. Gharama hii kwa sasa, imejificha ndani ya muundo wa Serikali mbili. Nafahamu kuwa kuna mambo ambayo katiba ya Muungano ya sasa inayatambua kamaMambo ya Muungano lakini hayaendeshwi kimuungano.Muundo wa serikali mbili uliifanya Tanganyika kubeba mzigo huu bila kujua uzito wake. Profesa Samuel Mushi alishawahi kuandika kuwa muundo wa serikali tatu utawafanya Tanganyika na Zanzibar kutambua na kuzitetea rasilimali zao zidi ya Serikalimshirika (economic nationalism). Mimi nasisitiza kuwa muundo huu utawafanya wananchi waanze kuuliza maswali hata kuhusu kugharamia Muungano. Kwa kuwa hawatapata majibu yakuridhisha, watakosa imani na muungano.


Rasimu hii inatuandaakisaikolojia kuuvunja muungano. Ibara ya 269 ya Rasimu inatuambia kuwa (c) kutakuwa na mgawanyo wa rasilimali (e) mgawanyo wa watumishi na (f) mgawanyo wa madeni. Hupaswi kuwa ‘nguli’kujua kuwa huu ni mwanzo wa kutengana rasmi. Wanatuambia ‘tunapaswa kujiandaa kusaikolojia kukubaliana na muundo wa muungano wa serikali tatu’. Tatizo sio serikali tatu, tatizo Serikali hiyo itasimamia mambo gani, na ipo kwa ajili ya nani? Katika kitabu chake cha Uongozi wetu na Hatima ya Taifa, Mwalimu Nyerere anasema, walipounda Muungano wa Serikali tatu, waliangalia uhalisia wa nchi hizi mbili kigiografia (ukubwa wa nchi), idadi ya watu, na uchumi wao. Hawakutaka kurudufisha tu miundo ya kanda zingine bila kuangalia uhalisia wa mazingira yao. Mambo haya bado yana umuhimu leo kama ilivyokuwa 1964. Napenda Watanzania watambue kuwa, pamoja na kuwa kulikuwa na kero za Muungano, lakini ni muundo wa serikali mbili ulioufanya Muungano wetu udumu hadi leo hii.


Kama tunataka muundo wa Seriakali tatu, eti ili kudumisha utambulisho wa Tanganyika kwa kuwa tunawatukuza sana wakoloni waliotuita Tanganyika, na kwa maslahi ya kisiasa (tuongeze nafasi za kiuongozi ili kila mtu apate kula, au baadhi yetu tunaodhani kutarahisisha namna ya kushika mamlaka ya nchi), si budi basi Seriaki ya Muungano tukaiongezea meno ya kiuchumi na kuipa jukumu la kutuletea maendeleo. Tunaitaka Serikali ya Muungano:  mosi, ikusanye kodi zote (baadhi ya kodi zinaweza achwa kwa Serikali washirika ili waendeshe mambo yao yasiyo ya muungano). Pawepo na ushirikiano na serikali washirika juu ya kukusanya kodi hizo. Pili, Serikali ya Muungano ikope kwa niaba ya shirikisho kwa kuzingatia uwiano sahii na mahitaji ya nchi washirika. Tatu, Serikali ya Muungano idhibiti biashara za nje. Nasisitiza, ili Serikali hii ya Muungano ipate uhalali wa kuendelea kuwepo, ni vyema pia ikawa na wizara za kimuungano zitakazotoa hudumu moja kwa moja kwa raia. Napendekeza hapa wizara ya Uchumi na Mipangoitakayokuwa na ushirikiano wa moja kwa moja na taasisi za kimaendeleo za nchi washirika. Wizara hii inaweza kutekeleza Ibara ya 10 (c) kwa umakini mkubwa. Napendekeza pia ziwepo wizara zitakazoshughulikia suala la Elimu na Afya, kwani wizara hizi ndio uti wa mgongo katika taifa linalokusudia kupunguza umaskini na kuleta ustawi wa jamii.


Ningependa kutanabaisha kuwa, Serikali ya Muungano na katiba yake haitalindwa kwa mtutu wa bunduki wala Ibara ya (8), (9), (69) na (119) zinazolenga kuweka vikwazo ili muungano usivunjwe, bali kukubalika kwake na wananchi. Hata nchi zilizojitenga zilikuwa na katiba na mtutu wa bunduki ambavyo havikusaidia. Tunahitaji kuitazama Rasimu hii kwa jicho la uhalisia na sio ushabiki wa aina yeyote, au tu kwa fikra kuwa mawazo ya Nyerere yamepitwa na wakati na sisi tunataka mabadiliko. Kuonja ni kuzuri sana lakini angalia usije ukaonja sumu. Pale ambapo Mwenyekiti au Wajumbe wa Tume wanainadi Rasimu hii, ningependa watueleze na matizo ya mambo wanayoyapendekeza, ambayo yapo wazi katika ripoti zao.


Hitimisho: Katika moja ya makala zake katika gazeti la Citizen, Dkt. Kitila Mkumbo alitabiri kuwa Muundo wa Serikali tatu utasambaratishwa katika Bunge la Katiba kwa kuwa CCM, ambao hawaungi mkono serikali tatu, wanauwakilishi mkubwa katika Bunge hilo. Kwa maoni yangu, kama utabiri wa Mkumbo utatimia, CCM watakuwa wamejali maslahi ya Taifa kwa kiwango kikubwa sana kama wataamua kuukataa muundo huu. Kujali maslahi ya taifa, na kukataa vitu visivyotufaa sio suala la sera ya chama, bali ni utashi.Ingawa naamini wapo watu ndani ya CCM tangu zamani wanaotaka serikali tatu. Mwisho, tuna zaidi ya miaka 20 sasa tangu Demokrasia ya vyama vingi ianzishwe a miaka 50 ya muungano. Naamini wananchi wana upeo mkubwa sasa kuweza kuamua mambo yao wenyewe. Hatuna sababu ya kutumia njia ndefu kuuvunja muungano. Ni vyema wananchi wakaamuakidemokrasia kuendelea na muungano au la!


Richard Mbunda


Mhadhiri Msaidizi, Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. rmbunda@gmail.com


--

Yona Fares Maro

Institut d'études de sécurité - SA


--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments