[wanabidii] Rais na CCM watalipeleka taifa kubaya

Saturday, March 22, 2014
Tuko katika mchakato wa kuandaa katiba mpya. Katika hili hatuhitaji kuheshimiana na kusema funika kombe -- - --.
Tunahitaji kuambizana ukweli.
Kuna hoja za msingi katika mjadala wa katiba na muundo wa Muungano imekuwa hoja kubwa japo kuna mambo mengi ya kujadili.
1    Tume iliyoundwa kuratibu mawazo yetu imetoa maoni yake.
2    Jana Rais amekuja naye akatoa maoni yake alipokuwa akizindia bunge la katiba.
3    Leo kwenye taarifa ya habari tumeona Rais wa Zanzibar akizindua matembezi ya vijana wa CCM kuhimiza watanzania kuunga mkono mfumo wa serikali moja. Ijulikane inafanyika hivyo wakati bunge linaendelea kutafuta muafaka. na huu ni ujumbe kwa wajumbe wa CCM walioko bungeni.

Tume kati ya mambo yaliyoifanya ipendekeze mfumo wa serikali mbili ni kuwa Muungano ulivyo sasa ni wa Serikali mbili katika nchi Mbili wakati waasisi wetu waliacha nchi ikiwa moja na serikali mbili.
Jingine ni kuwa katiba ya zanzibar inavunja katiba ya jamhuri ya Muungano kiasi  kwamba Rais wa jamhuri ya Muungano anaonekana kuwa Rais wa tanzania bara.

Katika maelezo marefu ya rais hakujaribu hata kidogo kujibu hoja hizo ili angalau kulisaidia bunge kufikiria namna ya kuunda katiba yenye mfumo wa serikali mbili bila mitafaruku tunayoiona.

Rais wa zanzibar katika uzinduzi w matembezi ya mshikamano hakujibu hoja muhimu ambazo zunaweza kusaidia bunge kujadili katiba yenye mfumo wa serikali mbili. Badala yake naweza kusema anawachochea vijana kupuuza wote wenye hoja za msingi bila shaka akiwemo Warioba.

Tume inasema haiwezekani kuibadili katiba ya Zanzibar ili kurahisisha uwezekano wa mfumo wa serikali mbili bila mitafaruku ya kikatiba na utendaji.
Rais wa jamhuri na Rais wa zanzibar wala hawaliongelei angalau tukaona mwanga.
Nini maana yake?
Wananchi tunaanza kukata tamaa. Maoni ya wananchi katika kipimajoto cha leo wameonyesha hivyo (taarifa ya habari ITV saa mbili 22 March 201).
Kama kweli Marais wetu hawalioni hilo basi hawafai kuwa viongozi. Wanapaswa kuliona. kama wanaliona wanalipuuza maana yake wanalitakia taifa kuwa na katiba ambayo haitatui matatizo tuliyo nayo ambayo ni sababu ya kutaka kuandika katiba mpya.

Kama kuna mtu anadharau mambo haya basi ajue analipeleka taifa kubaya.
1    Watanganyika wameishaona sasa kuwa ndani ya muungano wamebeba mzigo mkubwa. Rais na CCM hawawezi tena kuficha ukweli huo.
2    Anayesema serikali tatu ni mzigo anasahau kuwa kila kukicha nchi inagawanywa katika wilaya na mikoa na huo ndio mzigo kuliko serikali ya tatu ambayo ipo imejificha ndani ya Serikali ya muungano. lakini pia mfumo unaopendekezwa unafanya jumla ya viongozi kuwa wachache kuliko ilivyo sasa ambapo tuna serikali kubwa sana.
3     Vyanzo vya mapato kusikia kiongozi wa ngazi kubwa hivyo anaona kuwa tutavitoa kwenye nyanya na wala sio meno ya tembo zinazouawa kwa manufaa yao, si dhahabu zinazotajilisha wageni kupitia misamaha ya kodi, si maziwa mbuga za wanyama pori na raslimali nyingine ila ameona nyanya kama njia ya kupata mapato ya serikali. na hii ni aibu ya taifa.

Jumla ya haya yote lazima tutarajie kweli taifa kuvurugika. Anayefikiri kuwa waTanganyika wataendelea kuona muungano wa serikali mbili nchi mbili, Anayetarajia kuwa kwa ukubwa wake atachezewa na bwana mdogo kwa kisingizio cha serikali mbili- Anajidanganya. Heri mimi nikijidanganya. Ni mdogo sana. mkubwa akijidanganya tutarajie magumu. Vijana wa Tanganyika watakaposimama hawatakuja kuomba kurekebisha muungano. Watataka taifa lao. hatujui kama watakuwa na sifa zini za taifa lao. wanaweza kupitiliza na kutaka Tanganyika isiyo na Mpemba au muunguja. Likitokea najua wanasiasa watasimama na kulaumu. kama nitakuwepo nitawambia kuwa 'ni ninyi mnaosababisha hili kwa kuwa mliukataa mfumo sahihi wa Muungano'.
Wakati wa kuepusha hayo ni sasa. Tutumie busara kupata mfumo sahihi wa Muungano wetu. kama ni serikali mbili basi tukubali iwe nchi moja. na hii inawezekana kama Wazanzigari watakubali kuiondoa katiba yao na kuondoa maguvu waliyombambikiza rais wao. Kama hiyo ni haramu basi serikali mbili ni haramu pia. kama tukizilazimisha hapo ndipo utakaokuwa ulikuwa mwisho wa Muungano.
Kwa watanzania nawatazamisha katika matukio haya:
Sheria ya mwanzo ilikuwa inaelekeza Tume ya mabadiliko ya katiba ingeendelea kuwepo hadi baada ya kura ya wananchi. Kwa sheria hiyo sasa hivi wajumbe wa tume wangekuwa bungeni wakijibu maswali magumu kama aliyoulisa Rais. baadaye sheria ilibadilishwa _Kwanini?
Mwanzoni ilipangwa Bunge la katiba lizinduliwe ndipo lipokee rasimu y katiba. Ikabadilishwa ikabidi Tume iwakilishe maoni yake kabla ya bunge hilo kuzinduliwa _Jiulize Kwa nini?
Wakati wa kuwashirisha rasimu Mwenyekiti alipangiwa dakika 60 (120), Kama sio wajumbe wenye akili basi hotuba ya Warioba isingetolewa yote- Kwa nini?
Nakubaliana na G. Washington Rais wa Kwanza wa marekani kuwa: Huwezi kudanganya watu wote wakati wote. Unaweza kudanganya watu wote kwa wakati fulani. au kuwadanyagya watu fulani wakati wote. Ipo siku waTanganyika hawatadanyanyika. Tukilijua leo hayatatukuta magumu.
Elisa Muhingo

Share this :

Related Posts

0 Comments