[wanabidii] RAISI KIKWETE NA WAZIRI MEMBE, NAWATUNUKU TUZO YA DEMOKRASIA NA UTAWALA BORA

Friday, February 14, 2014
" Maneno Diplomasia na Sera ya Mambo ya Nje yamekuwa yakitumika wakati
mwingine kumaanisha kitu kimoja, pamoja na kuwa yana maana tofauti.
Diplomasia ni uhusiano wa kimataifa kati ya nchi na nchi na kati ya nchi na
mashirika ya kimataifa. Uhusiano huu hutengenezewa mbinu na mikakati ya
utekelezaji wake kwa kila nchi kupitia sera zao za mambo ya nje. 

Sera ya Mambo ya Nje ni tamko la nchi lenye kutoa mwongozo na mwelekeo
kuhusu madhumuni, malengo na misingi ya nchi katika kuhusiana na nchi,
mashirika ya kimataifa na wadau wengine nje ya nchi. Tamko hili pia ni
mwendelezo wa sera ya ndani ya nchi. Sera ya Mambo ya Nje ya nchi ni chombo
kinachobeba zana na mbinu za utekelezaji wa diplomasia. 

Sera huainisha pia misimamo ambayo nchi inaipigania na ile inayoipinga. Tamko
hili ni muhimu kwa kuwa ni utambulisho wa nchi kimataifa, na tamko hili huakisi
sera na misingi ya ndani ya nchi. Mratibu mkuu wa utekelezaji wa sera hii ni
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, na sera hii hutekelezwa na
serikali nzima na wadau wengine ndani ya nchi, ambao shughuli zao zinahusiana
na masuala ya kimataifa. Ifahamike pia, Mkuu wa Nchi ndiye Mwanadiplomasia namba moja, na Waziri wa Mambo ya Nje ni Mwanadiplomasia namba mbili
katika nchi yoyote. 

Sera ya nje, tulipotoka na tulipo.

Sera ya Mambo ya Nje ya 2001 ndiyo inayotoa mwongozo katika kufikia malengo
ya nchi nje. Sera hiyo inatambua na kulinda misingi ya Tanzania ya
kutofungamana na upande wowote, kutetea wanyonge, kudumisha ushirikiano
wa kimataifa, kuunga mkono juhudi za kimataifa, ujirani mwema na kudumisha
uhuru wetu. Sera, imetambua pia mafanikio yaliyopatikana katika diplomasia ya
siasa na mchango wake kwenye ukombozi wa nchi za Afrika. 

Sera hii imeelekeza misingi yote idumishwe, na juhudi zote sasa zilenge kupanua
maslahi yetu ya kiuchumi kwa kupanua wigo wa marafiki, ushiriki wetu
kimataifa na ushirikishaji mpana wa wadau, ikiwamo sekta binafsi. Diplomasia
yetu sasa tofauti na awali, inatakiwa ilete manufaa ya kiuchumi ikiwa ni pamoja
na kufungua masoko kwa biashara za Watanzania, bidhaa, kuvutia wawekezaji
na kuongeza watalii. Mkakati huu wa kutekeleza sera, umepewa jina la Diplomasia ya Uchumi.

Diplomasia, kama ilivyo mikakati mingine inayo vigezo na vipimo vyake.
Diplomasia hufanyiwa tathmini mara kwa mara ili kuendana na mabadiliko ya
kidunia. Diplomasia ya nchi, hupimwa kwa kulinganisha na diplomasia ya nchi
nyingine. Hivyo, kusema kuwa Diplomasia yetu imefanikiwa au kufeli, tunapaswa
kuipima dhidi ya malengo yaliyoainishwa kwenye sera, kisha kuilinganisha
Diplomasia ya nchi nyingine zinazoshabihiana.

Uimara wa diplomasia yetu. 

Uimara wa diplomasia ya nchi ni ushawishi wake kimataifa. Ushawishi wa nchi,
kihistoria umekuwa ukiambatana na nguvu ya kiuchumi au kijeshi (Diplomasia
ya Nguvu). Nguvu hizi mbili ni matokeo ya sera za ndani ya nchi. Hata hivyo, si
lazima kuwa kila nchi yenye moja au vigezo hivyo viwili kufanikiwa katika
diplomasia. Ziko nchi, ikiwamo Tanzania ambazo zimefanikiwa sana kuwa na
ushawishi mkubwa, pamoja na kutokuwa na nguvu hizo duniani, kutokana na uimara wa sera yake ya mambo ya nje, na wanadiplomasia wake (Nguvu ya
Diplomasia). 

Ni dhahiri kuwa hatuwezi kulinganisha diplomasia ya Tanzania na diplomasia ya
nchi zilizoendelea kama Marekani, China, Ufaransa, Uingereza na Urusi. Nchi hizi
ni nchi kubwa katika anga la kimataifa, ni wajumbe wa kudumu wa Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa wenye kura ya turufu, ni nchi zenye nguvu za
kijeshi na kiuchumi na nchi zenye maslahi mapana duniani. Kukua au kudorora
kwa uchumi wa dunia kunategemea sana maendeleo ya chumi za nchi hizo. 

Diplomasia ya Tanzania inaweza kupimwa kwa kulinganishwa na nchi za Kusini
mwa Jangwa la Sahara, maana kimataifa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara
huwekwa katika kapu moja. Nchi zinazoaminiwa kuwa na nguvu kubwa za
kijeshi na kiuchumi kusini mwa Jangwa la Sahara ni Nigeria na Afrika Kusini.
Jambo linaloshangaza wengi duniani ni kuwa, Tanzania imeonekana kung'ara na
kuwa na ushawishi mkubwa kimataifa sawa au pengine kuzidi nchi hizo mbili, pamoja na kutokuwa na nguvu kubwa ya uchumi au jeshi. Hakuna nchi
nyingine, ukiondoa hizo mbili, yenye ushawishi na sauti kimataifa zaidi ya
Tanzania. 

Nataka kuepuka kufanya kile ambacho Komredi Jenerali Ulimwengu (katika makala yake, gazeti la Raia Mwema ambapo amebeza mafanikio ya diplomasia ya Tanzania) amefanya cha kuzungumza bila ushahidi. Maana wako Watanzania wanaoamini kuwa sifa njema au jambo jema haliwezi kufanywa na serikali, tena Serikali ya Awamu ya Nne. Hawa watataka kubeza hoja yangu kuwa kiushawishi barani Afrika, Tanzania iko katika ligi moja, na pengine inazidi nchi za Afrika Kusini na Nigeria, nchi ambazo zina nguvu kubwa za kiuchumi na kijeshi.

Kujenga taswira nzuri ya nchi na ushawishi kimataifa ni moja ya kielelezo cha
nguvu ya diplomasia ya nchi. Jukumu hili, ni moja ya jukumu gumu sana katika
diplomasia. Hii ni kwa sababu, taswira ya nchi inaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa
mipango au sera za nchi nyingine za kiuchumi dhidi yako. Mfano, ikiwa nchi yako
ikionekana ni kitovu cha ugaidi, nchi inaweza kuwekewa vikwazo vya kiuchumi
na hivyo kugharimu uchumi wa nchi husika. 

Taswira ya nchi hulindwa kwa kila hali na baadhi ya nchi hutumia gharama
kubwa kwenye propaganda kulinda taswira ya nchi zao. Katika ripoti ya
2009-2010 ya kampuni za Marekani zenye kutoa huduma za uwakala kwa nchi
nyingine inaonyesha kuwa nchi za Afrika zinatumia fedha nyingi kuosha taswira
zao kwenye Bunge na Seneti ya Marekani. Katika nchi hizi, Kenya inashikilia
nafasi ya nane kati ya kumi za juu ikiwa imetumia kiasi cha dola za Marekani milioni moja na laki saba ($1.7 milioni), huku Afrika Kusini ikitumia ($18
milioni), Angola ($7 milioni), Nigeria ($1.8 milioni). 

Taarifa hiyo inaeleza, mwaka 2008 Kenya ilitumia kiasi cha dola za Marekani
milioni mbili na laki nne ($2.4 milioni) kuilipa Kampuni ya Chlopak, Leonard
Schechler and Associate kwa lengo la kurekebisha taswira yake nchini Marekani
baada ya machafuko ya 2007. Itakumbukwa kuwa, wakati huo, Tanzania
ilitembelewa na Rais George Bush wa Marekani katika ziara ambayo haijawahi
kufanywa na Rais wa Marekani kuitembelea nchi kwa siku nne, kusini mwa Jangwa la Sahara. Tanzania imeyapata hayo bila kutumia mawakala na wapiga
debe ndani ya Marekani. 

Njia nyingine ya kupima uwezo na ushawishi wa Diplomasia ya Tanzania ni
kuangalia uwekezaji ambao Tanzania inaufanya katika Diplomasia na
kulinganisha na nchi zingine za Afrika. Ni muhimu kabla ya kuhukumu kuangalia
ukubwa wa bajeti, watumishi na mtandao wa Balozi katika kuhukumu ikiwa
Diplomasia yetu imefeli ama kufaulu. Maana, hatuwezi kusema mtu amefeli
kama hatukumpa nyenzo za kufanyia kazi, maana atakuwa amefeli kabla hajaanza. Katika hili, nitalinganisha nchi za Nigeria, Afrika Kusini, Kenya na
Tanzania ili tuweze kupata picha kamili. 

Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria ina maofisa wapatao 2,000, Balozi 87 nje ya
nchi na Balozi zipatazo 70, na Balozi ndogo 37 zinazowakilisha nchi zao nchini
Nigeria. Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria ilitengewa kiasi cha dola za Marekani
milioni mia tatu ishirini na tatu ($ 323 milioni) kwa mwaka 2012 kwa ajili ya
kazi zake. Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini kwa upande wake inao
wafanyakazi wapatao 4,535, Balozi 104 nje ya nchi, Balozi 126 za nje ya nchi zilizoko Pretoria na mwaka 2012 ilitengewa Bajeti ya Randi Bilioni 5.1 sawa na
Dola za Marekani milioni 483. Jirani zetu Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya
inazo Balozi 53 nje, Balozi 75 za nje ya nchi zilizoko Nairobi na Wizara ilitengewa
kiasi cha dola za Marekani milioni 172 kwa mwaka wa fedha 2012. 

Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania inazo Balozi 33 tu nje ya nchi na ni
mwenyeji wa Balozi 55 na Mashirika ya Kimataifa 22 nchini. Aidha, Wizara ina
wafanyakazi wasiozidi 350 tu ikijumuisha kada zote, ndani na nje ya nchi, na
mwaka 2012 Wizara ilitengewa Bajeti ya shilingi bilioni 97 tu ambayo ni sawa na
dola za Marekani milioni 60.8. Ikumbukwe kuwa, fedha hiyo ni asilimia 44 tu ya
mahitaji halisi ya bilioni 222 yakihusisha ufunguzi wa Balozi mpya, kuongeza rasilimali watu balozini, kukarabati majengo ya Ubalozi na kutekeleza mkakati wa
Diplomasia ya Uchumi. 

Kwa hesabu nyepesi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
inapata theluthi moja ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya. Kwa lugha
nyingine, Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria ni mara nne ya Bajeti
yetu, na Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini ni mara nane ya
Bajeti ya Wizara yetu. Haihitaji miujiza kukubali kuwa Wizara ya Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa ya Tanzania inafanya kazi kubwa sana ikilinganishwa na kiasi cha fedha, rasilimali watu na mtandao wa Balozi ilizonazo.

Takwimu hapo juu zinatupa sababu ya kujivunia kuwa Tanzania ina 'Nguvu ya
Diplomasia' kuliko 'Diplomasia ya Nguvu'. Kirasilimali na kimtandao, Tanzania
haifui dafu kwa wenzetu wa Nigeria, Afrika Kusini na hata Kenya. Pamoja na
hayo, nguvu ya ushawishi wa Tanzania duniani ni sawa au zaidi ya nchi hizo.
Haihitaji akili nyingi za kiuchambuzi kukubali kuwa, Tanzania inavuna zaidi ya
inachopanda katika Diplomasia. Inashangaza kuwa, watu wa nje wanaona hivyo na wanajifunza kutoka kwetu, lakini wenzetu wa ndani wanabeza. Ni vyema,
kuzingatia takwimu hizo hapo juu ili kuoanisha na mafanikio ya Diplomasia
nitakayoainisha hapa. 

Mafanikio ya Diplomasia yetu 

Mafanikio ya diplomasia yanaweza kupimika kwa kutumia viashiria. Viashiria hivi
hutumika kama vielelezo vya nguvu ya diplomasia ya nchi yoyote. Kwa
madhumuni ya makala hii, viashiria vitano vimetumika. Viashiria hivi si timilifu,
viashiria vingine lukuki hutumika kutokana na mahitaji mahsusi. Viashiria vitano
ninavyotumia hapa, vinatosheleza kwa madhumuni ya makala hii kama
ifuatavyo;- 

Nafasi za Kimataifa 

Moja ya kipimo cha nchi cha nguvu yake ya diplomasia ni nafasi yake kimataifa.
Nafasi ya nchi kimataifa inajumuisha nafasi za uteuzi na uchaguzi ambayo nchi
hupata kimataifa. Kuteuliwa na kuchaguliwa huko, ni kielelezo cha kukubaliwa
na kuaminiwa kwa nchi katika Jumuiya ya Kimataifa.

Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, Tanzania imepata nafasi nyingi kimataifa
ikiwemo Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (2004/2006),
Uenyekiti wa Umoja wa Afrika (2008/2009), Uenyekiti wa Asasi ya Ulinzi na
Usalama ya SADC (2008/2009 na 2012/2013) na ujumbe wa Baraza la Usalama
la Umoja wa Afrika (2012/2013 na 2014/2015). 

Tanzania iliweka historia katika Uenyekiti wa AU chini ya Rais Jakaya Kikwete
kwa kukumbana na mapinduzi katika nchi nne za Mauritania, Guinea, Guinea
Bissau na Madagascar. Ni katika wakati huo kwa mara ya kwanza, tena kwa
kupendekezwa na Tanzania ilikubaliwa AU haitautambua uongozi wowote
utakaopindua serikali na kisha kugombea uchaguzi mkuu kwa lengo la
kutakatisha mapinduzi. 

Azimio hilo liliweka mwanzo mpya katika Afrika, na hadi leo, hakuna kiongozi
aliyepindua ambaye amegombea uchaguzi mkuu baada ya mapinduzi. Ushahidi
wa hivi karibuni ni huu wa Rais Andy Rajoelina kutogombea uchaguzi
Madagascar kwa kubanwa na kipengele hicho. Isisahaulike pia, ni katika kipindi
hicho Tanzania iliongoza AU kwenda kung'oa uasi wa Kanali Bakar wa Kisiwa cha
Anjuani huko Comoro. Ilipomaliza muda wake, nchi za Afrika zilishawishi Tanzania kuendelea na Uenyekiti wa AU jambo lisilo la kawaida, lakini Rais
Kikwete akasimamia msingi wa Tanzania wa kuheshimu vipindi vya madaraka. 

Tanzania imefanya mambo makubwa pia katika kipindi chake SADC ikiwemo
kuongoza jitihada za amani nchini DRC kulikozaa Azimio la Umoja wa Mataifa la
kupeleka kikosi maalumu cha kulinda amani dhidi ya waasi wa M23. Kazi
iliyofanyika huko si ya kusimulia, maana kila mwenye masikio amesikia. Ushiriki
wa Tanzania katika kutokomeza waasi wa M23 kuna faida tatu kubwa; kwanza:
kuleta amani kwa wananchi wa DRC Mashariki, pili: kuepusha nchi yetu na tatizo la wakimbizi na utapakaaji wa silaha ndogondogo na nyepesi, jambo linalotishia
amani na usalama wetu, na tatu: kufungua fursa za kiuchumi na kibiashara
baina ya watu wetu na wale wa DRC kutokana na kurejea kwa amani mashariki
ya DRC. Hii ni Dipomasia ya Uchumi. 

Mafanikio haya ni mengi, nilichogusia ni vitu vichache sana kuonyesha nafasi ya
taifa letu duniani, Afrika na kusini mwa Afrika. Tunao pia Watanzania
waliochaguliwa na wengine kuteuliwa kushika nyadhifa kubwa kimataifa ikiwemo
nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa iliyoshikiliwa na Dk. Asha-
Rose Migiro; Balozi Wilfredy Ngirwa, kuchaguliwa kwa kishindo kuwa Mwenyekiti
Huru wa Baraza la Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO); Rais Kikwete ameteuliwa kushika nyadhifa nyingi kimataifa ikiwemo uenyekiti wa Kamati ya
Marais Kumi wa Afrika kuandaa msimamo wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabia
Nchi, Jopo la Wasuluhishi wa Mgogoro wa Ivory Coast, na hata majuzi, alipewa
nafasi ya kipekee kuzungumza kwenye mazishi ya Rais Mstaafu, Nelson Mandela.
Mtu yeyote anayeitazama Tanzania kwenye medani za kikanda na kimataifa
hatachelea hata kidogo kupaza sauti na kusema kuwa diplomasia ya Tanzania iko katika daraja la juu sana kwa kipindi hiki kuliko kipindi kingine chochote kile. 

Ushawishi na misimamo katika uamuzi 

Tanzania imeendeleza desturi yake ya kuwa na misimamo isiyotetereka katika
masuala mbalimbali duniani. Desturi hii ni mwendelezo wa Diplomasia ya Siasa
na Ukombozi chini ya Mwalimu Julius Nyerere. Leo hii, Tanzania ni moja ya nchi
chache zenye uthubutu wa kutofautiana na nchi kubwa duniani na hata
kutamka misimamo inayopishana nayo, na bado ikaheshimika. 

Yoyote mwenye kuhofu juu ya jeuri hii ya Tanzania anapaswa kuwa huru
kufuatilia upigaji kura wa Tanzania katika maazimio ya Umoja wa Mataifa
yanayohusu kukemea vikwazo vya Marekani dhidi ya Cuba, Haki ya Wapalestina
kujitawala na Haki ya Wapalestina kujiunga na Shirika la Umoja wa Mataifa la
Sayansi na Elimu (UNESCO). Aidha, Tanzania haijasita kukemea kilichofanywa
na nchi za NATO dhidi ya Libya na imepiga kura ya kuzuia matumizi ya nguvu ya NATO nchini Syria kwa kuzuia kile cha Libya kujirudia. 

Pamoja na Tanzania kuwa na misimamo mikali kwenye mambo ya msingi,
imeendelea kuaminiwa na kuheshimiwa na mataifa makubwa na nchi zote
duniani. Tunaheshimiwa kwa kuwa, sisi si wanafiki na tunamaamisha
tunachosema. Rekodi yetu inazungumza yenyewe na hivyo ni taifa
linaloaminika, na mfano barani Afrika. Ndio maana, katika masuala makubwa ya
dunia, na Afrika, Tanzania hualikwa, kwa kuwa sauti yake ni muhimu kimataifa. 

Ushawishi huu katika uamuzi wa kimataifa na kikanda unatokana pia na uzito
wa Mwanadiplomasia namba moja na namba mbili wa Tanzania, yaani Rais
Kikwete na Waziri Bernard Membe. Rais Kikwete ni mwanadiplomasia mkongwe,
amekuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa miaka 10 kabla ya kuwa Rais. Waziri
Membe amekuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa miaka 7 sasa, jambo
linalomfanya kuwa Waziri mkongwe katika AU, ambapo mawaziri wakongwe wamebaki wanne yaani Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Lesotho,
Uganda na Zimbabwe. Uzoefu huu unawafanya waaminike na wakabidhiwe
majukumu mengi, na hivyo kualikwa mara kwa mara kwenye mikutano ya
kimataifa. 

Ziara za viongozi 

Ziara za viongozi wa nje nchini na mialiko ya kiongozi wa nchi nje ni kiashiria cha
nafasi ya nchi duniani, hususan katika ulimwengu wa diplomasia. Tanzania
tumetembelewa na viongozi wa nchi kubwa duniani achilia mbali nchi za kati.
Nyingi ya ziara hizi ni za kirafiki na kikazi. Tanzania imetembelewa na Rais
George Bush wa Marekani na Rais Hu Jintao wa China mwaka 2008. Kama
haitoshi, mwaka 2013, Tanzania ikatembelewa tena na Rais Xi Jinping ikiwa ni ziara yake ya kwanza barani Afrika baada ya kuingia madarakani, na akatumia
fursa hiyo kutangaza Sera ya China barani Afrika. Mwaka huo huo, Rais Barack
Obama naye akatembelea Tanzania na akachagua Tanzania kuwa sehemu ya
kutangazia Sera ya Marekani katika ushirikiano wa Nishati na Bara la Afrika,
Power Africa Initiative (PAI). Wakati Rais Obama anafanya ziara ya kikazi, rais
wengine wawili wastaafu wa Marekani (George Bush na Clinton) nao walitembelea Tanzania. Kwa mara ya kwanza katika historia ya dunia, marais
watatu wa Marekani wanatembelea nchi kwa wakati mmoja. 

Tanzania ilitembelewa pia na Waziri Mkuu wa India na Rais wa Brazil, mataifa
haya ni sehemu ya nchi zinazounda kundi la nchi zenye uchumi mkubwa duniani
yaani Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini (BRICS). Hapa sijaweka orodha
ya utitiri wa mawaziri wakuu na mawaziri wa ushirikiano waliofika nchini.
Tukumbuke kuwa, viongozi hawa wakubwa hawatembelei nchi yoyote tu.
Kutembelea kwao Tanzania ni kipimo cha imani yao kwa nchi na Rais Kikwete na sera yake ya nje. Nchi zingine Afrika zingependa sana kupata ugeni mzito wa
aina hii lakini hawana ushawishi wa kutosha kidiplomasia kutafutwa na viongozi
wa nchi kubwa duniani. 

Fursa za kiuchumi 

Diplomasia yetu leo, tofauti na Diplomasia ya Siasa na Ukombozi tuliyokuwa
nayo huko nyuma, imejikita katika kulinda na kupanua maslahi ya kiuchumi.
Diplomasia ya Siasa na Ukombozi ilitufanya tuchague maadui na marafiki, ziko
nchi hatukushirikiana nazo ikiwemo Afrika Kusini, Korea na Israel. Sasa,
tunashirikiana na kila nchi katika kupanua fursa za kiuchumi zikiwemo nchi hizo
tatu. Sasa, tofauti na zamani, Diplomasia inautumikia uchumi na si uchumi kutumikia siasa kama ilivyokuwa huko nyuma. 

Diplomasia ya Uchumi ya Tanzania inalenga kama ilivyoelekezwa na Sera ya
Mambo ya Nje kujishughulisha na kujenga uchumi wa nchi. Viongozi na Balozi
zetu zimekuwa zikifanya kazi hiyo, tena katika mazingira magumu ya uhaba wa
bajeti kama nilivyochanganua hapo awali. Mabalozi wetu sasa si tu wanakutana
na mabalozi wenzao, bali pia wafanyabiashara na wawekezaji. 
Fursa za kiuchumi na kijamii ambazo zimefunuliwa na Diplomasia ya Uchumi ni
lukuki. Ziara ya Rais George Bush akiwa nchini alisaini makubaliano ya kuipatia
Tanzania dola za Marekani milioni 698 kwa ajili ya miundombinu, nishati na afya.
Fedha zile ndizo zimejenga barabara ya Masasi-Songea-Mbaba Bay, Tanga-
Horohoro na kujenga miundombinu ya kusambaza umeme. Mshindo wa miradi
hii katika uchumi wetu hauwezi kupuuzwa, miundombinu hii imeifungua nchi, sasa maeneo kama Mbamba Bay yaliyokuwa pembezoni, sasa yanafikika. 

Ziara ya hivi karibuni ya Rais wa China, imetufungulia fursa ya kujengwa
itakayokuwa bandari kubwa kuliko zote Afrika Mashariki huko Bagamoyo,
itakayogharimu takribani dola za Marekani bilioni 10. Bandari hiyo itawezesha
meli kubwa za kimataifa zenye uwezo wa kupakia makontena 6,000 kuweka
nanga Bandari ya Bagamoyo. Bandari hiyo itageuza Bagamoyo kuwa Jiji la
Bandari litakalounganishwa kwa barabara na reli na Jiji la Dar es Salaam na hadi Msata. Tayari taarifa za ujenzi wa bandari hii zimekwisha leta kiwewe juu ya uhai
wa bandari za majirani zetu. Yote haya ni matunda ya Diplomasia ya Uchumi ya
Tanzania.

Hali kadhalika Tanzania imepatiwa fursa ya kuuza bidhaa China ambalo ndilo
soko kubwa kwa sasa. Sasa Tanzania inaweza kuuza tumbaku China, nchi
ambayo inanunua tumbaku kwa wingi kuliko nchi yoyote duniani. Juhudi hizi
zimetokana na hasara waliyopata wakulima wa tumbaku wa Tanzania katika
msimu wa 2011/2012 ambako, tani 30,000 zilikosa soko baada ya nchi za Ulaya
kupunguza matumizi ya tumbaku. Ikumbukwe kuwa, nchi haiwezi kuuza tumbaku nchini China bila ya kuwa na mkataba maalumu, ambao ni zao la
juhudi za Waziri Membe baada ya mkutano wa China na Afrika uliofanyika
Beijing, mwaka 2012. 

Mikataba ya aina hii imesainiwa pia Oman, Kuwait na nchi nyingine mashariki ya
kati. Baadhi ya sekta binafsi tayari zimekwisha changamkia fursa hizi ikiwamo
Benki ya CRDB iliyofungua tawi huko Bujumbura na Benki ya Exim iliyofungua
tawi huko Moroni, Visiwa vya Comoro. Ziko kampuni nyingine nyingi za Tanzania
ambazo zinachangamkia fursa hizi, hali iliyopelekea Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa kutunukiwa tuzo ya mwaka 2013 na Taasisi ya CEO Round Table, kutokana na mchango wake wa kuisaidia sekta binafsi kufanya kazi
vizuri na serikali. Ni vizuri walio na wasiwasi kuhusu uwezo wa Wizara ya Mambo
ya Nje wa kusimamia utekelezaji wa Sera ya Diplomasia ya Uchumi wakauliza
taasisi mbalimbali za sekta binafsi kama CEO Round Table. 

Uwakilishi Nje ya Nchi 

Tanzania imepanua uwakilishi wake nje na kuongeza Balozi sita mpya kati ya
2005 hadi 2013. Balozi mpya zimefunguliwa katika maeneo ambayo yanakuwa
kwa kasi kiuchumi, na yenye maslahi ya kiuchumi kwa Tanzania. Leo Tanzania
tunazo Balozi zetu Oman, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Malaysia, Brazil, na
hivi karibuni visiwa vya Comoro na Uholanzi. Katika kipindi hicho hicho, Balozi za
Brazil, Oman, Korea Kusini na Qatar zimefunguliwa nchini, pamoja na mashirika ya kimataifa. 

Idadi ya Balozi ambazo zimefunguliwa nje katika kipindi cha miaka minane ni
ndogo. Tanzania bado haijaweza kufikia nchi nyingi katika mtandao wake wa
Balozi. Jitihada zimefanywa kufungua Balozi za Heshima 18 kwa ajili ya kutoa
huduma za kikonseli kwa watalii na wawekezaji. Uchache huo hautokani na
upungufu wa dhamira bali fedha. Hata pale ambapo inazo Balozi, bado ina uhaba
wa waambata biashara, waambata uchumi na waambata utalii kwa ajili ya kutekeleza jukumu la kukuza utalii, biashara na uwekezaji. 

Tunapaswa kupongeza juhudi za wanadiplomasia wetu kwani hata mafanikio
tunayoyapata ni zaidi ya kiasi tulichowekeza. Idadi ya Balozi zetu nje ni theluthi
tu ya Balozi za Nigeria na Afrika Kusini na nusu ya Balozi za Kenya. Upande wa
rasilimali watu, idadi ya wanadiplomasia wetu wizarani na balozini ni chini ya
asilimia 10 ya idadi ya wanadiplomasia wa Afrika Kusini, na robo ya idadi ya
wanadiplomasia wa Nigeria. Tofauti za kibajeti ndio tusiguse maana ni kubwa kupindukia. Bado, Tanzania inapishana viwiko na Afrika Kusini na Nigeria katika
nyanja ya Diplomasia. Tunapaswa kujipongeza si kubeza"
( Hii ni nukuu Kutoka katika makala ya Balozi Mstaafu baada ya kutumikia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa miaka 28).

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Related Posts

0 Comments