*TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI*
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi
ameelezea hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa Ilani yake siku 100
tangu alipoingia madarakani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo (Februari 7 mwaka huu) katika
mkutano uliofanyika katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam,
Rais Malinzi aliainisha maeneo kadhaa yaliyopewa kipaumbele na tayari
yameanza kufanyiwa kazi pamoja na changamoto zilizopo.
Alisema muundo wa Idara ya Ufundi umebadilishwa kwa kuundwa vitengo vya
ufundi, elimu na maendeleo ya mpira wa miguu huku maeneo ambayo tayari
yameanza kufanyiwa kazi kuwa ni;
Ujenzi wa kituo cha mpira wa miguu (football centre of excellency), timu
kupanda daraja, kuanzisha mashindano mapya na kufufua ya zamani, mpira wa
miguu wa wanawake, maandalizi ya vijana (grassroot football), tiba, walimu
na makocha, utawala, uhusiano na Zanzibar, klabu za mpira wa miguu,
wachezaji, masoko na uwekezaji, kitengo cha habari, viwanja na timu ya
Taifa (Taifa Stars).
Rais Malinzi amesema changamoto zilizopo kwa sasa ni matumizi ya tiketi za
elektroniki, ufinyu wa bajeti, madeni, nidhamu, maadili na uchezeshaji wa
waamuzi.
Ametoa mwito kwa wadau wote nchini wakiongozwa na Serikali, Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Afrika (CAF), Afrika Mashariki na Kati
(CECAFA), vyombo vya habari, mashirika ya umma na kampuni binafsi
kushikamana na kuwa kitu kimoja kwa nia ya kuinua kiwango cha mpira wa
miguu Tanzania. (TAARIFA NZIMA YA RAIS IMEAMBATANISHWA)
*KILA LA KHERI YANGA, AZAM*
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linazitakia kila la kheri klabu
za Yanga na Azam ambazo timu zake zinatuwakilisha kwenye mashindano ya Ligi
ya Mabingwa Afrika (CL) na Kombe la Shirikisho (CC).
Yanga inacheza na Komorozine ya Comoro katika mechi ya kwanza ya raundi ya
awali ya CL itakayochezwa kesho (Februari 8 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Nayo Azam inaikaribisha Ferroviario de Beira ya Msumbiji katika mchezo wa
kwanza wa raundi ya awali ya CC utakaochezwa Jumapili (Februari 9 mwaka
huu) saa 10 kamili kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es
Salaam.
Ni matumaini yetu kuwa timu hizo mbili zitatuwakilisha vizuri kwenye
michuano hiyo, na kuwataka Watanzania wajitokeze kwa wingi viwanjani
kuziunga mkono hasa kwa vile zinacheza nyumbani.
*TWIGA STARS YAHAMISHIA KAMBI DAR*
Timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake (Twiga Stars) imehamishia kambi
yake jijini Dar es Salaam kutoka Mlandizi mkoani Pwani ikiwa ni sehemu ya
maandalizi ya mechi ya michuano ya Afrika (AWC) dhidi ya Zambia.
Kikosi hicho chini ya Kocha Rogasian Kaijage kimepiga kambi katika hosteli
ya Msimbazi Center kikiwa na wachezaji 25 kutoka 30 ambao kilianza nao
katika kambi ya Mlandizi mkoani Pwani.
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza dhidi ya Zambia itachezwa Februari
14 kwenye Uwanja wa Nkoloma jijini Lusaka. Timu zitarudiana wiki mbili
baadaye jijini Dar es Salaam.
Wachezaji waliopo katika kikosi hicho ni Amina Ally, Amisa Athuman,
Anastasia Anthony, Asha Rashid, Esther Chabruma, Eto Mlenzi, Evelyn
Sekikubo, Fatuma Bashiri, Fatuma Hassan, Fatuma Issa, Fatuma Mustafa na
Fatuma Omari.
Wengine ni Flora Kayanda, Happiness Hezron, Maimuna Said, Mwajuma Abdallah,
Mwapewa Mtumwa, Najiat Abbas, Pulkeria Charaji, Shelder Boniface, Sophia
Mwasikili, Therese Yona, Vumilia Maarifa, Winfrida Daniel na Zena Khamis.
*PRISONS, RUVU SHOOTING KUUMANA SOKOINE*
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara
inaendelea kesho (Februari 8 mwaka huu) kwa mechi moja kati ya Tanzania
Prisons na Ruvu Shooting itakayofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine
jijini Mbeya.
Mechi nyingine nne za ligi hiyo zitachezwa keshokutwa (Februari 9 mwaka
huu) kwenye viwanja mbalimbali. Mgambo Shooting vs Simba (Mkwakwani,
Tanga), Oljoro JKT vs Kagera Sugar (Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha),
Rhino Rangers vs Coastal Union (Ali Hassan Mwinyi, Tabora) na Mbeya City vs
Mtibwa Sugar (Sokoine, Mbeya).
*FDL YAANZA VUMBI LA MZUNGUKO WA PILI*
Mzunguko wa pili wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) unaanza kesho (Februari 8
mwaka huu) kwa mechi za kundi A na B wakati kundi C lenyewe litaanza mechi
zake Februari 22 mwaka huu.
Mechi za kundi A ni Green Warriors vs Tessema (Uwanja wa Mabatini,
Mlandizi), Polisi Dar es Salaam vs Transit Camp (Uwanja wa Karume, Dar es
Salaam). Februari 9 mwaka huu ni African Lyon vs Villa Squad (Uwanja wa
Mabatini, Mlandizi) na Friends Rangers vs Ndanda (Uwanja wa Karume, Dar es
Salaam).
Kundi B kwa kesho (Februari 8 mwaka huu) ni Polisi Morogoro vs Burkina Faso
(Jamhuri, Morogoro), Lipuli vs Mkamba Rangers (Samora, Iringa), Kurugenzi
vs Kimondo (Wambi, Mufindi) na Mlale JKT vs Majimaji (Majimaji, Songea).
*Boniface Wambura Mgoyo*
*Ofisa Habari na Mawasiliano*
*Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)*
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
0 Comments