1.0 Utangulizi:
MAONI haya yanalenga katika maeneo matatu makubwa. Kwanza yanalenga katika kuainisha haja na namna ya kutanua demokrasia (kwa kuiwajibisha zaidi serikali). Kama ilivyo sasa katika Katiba, serikali, na hasa Rais, wana madaraka na majukumu mengi na makubwa. Pamoja na mambo mengine, Rais ni Mkuu wa Dola, Mkuu wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.
Kulingana na madaraka na majukumu hayo, Rais na serikali hawawajibiki ipasavyo. Rais ni Sehemu ya Bunge, lakini si Mbunge na hawajibiki Bungeni. Aidha, Rais ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri, lakini si Mjumbe wa Baraza hilo. Hata ikabidi Baraza la Mawaziri kujiuzulu, Rais anabaki madarakani. Pia Rais huteuwa Mawaziri ambao wanawajibika kwake na siyo kwa Bunge. Mfumo wa serikali mchanganyiko kati ya mfumo wa Urais (Presidential System) na ule wa Kibunge (Parliamentary System) na umejenga Urais wa Kifalme (Imperial Presidency) ambao hauisihi baada ya uhuru.
Pili, maoni haya yanalenga katika kuainisha haja na namna ya kuimarisha muundo wa serikali na, hasa, Muungano. Katiba ya Muungano ilijengwa juu ya nguzo kuu tatu, yaani: Chama Dola (State Party), Urais wa Utendaji (Executive Presidency) na Serikali mbili za Muungano. Baadhi ya nguzo hizi sasa hazipo. Mfumo wa chama Dola umeondoka. Aidha, Rais wa Zanzibar siyo tena Makamu wa Rais na kiungo muhimu cha Muungano. Kwa hiyo, ni dhahiri kwamba, tangu kuondoka kwa nguzo hizi na kuja kwa mfumo wa vyama vingi. Msingi wa muungano katika Katiba na msingi wa Katiba ya Muungano umedhoofika. Nguzo iliyobaki ya Serikali mbili pekee haiwezi kuisimamisha katiba ya sasa. Hali ambayo imeleta haja ya kubadili muundo wa serikali na katiba.
Tatu, maoni haya yanalenga katika kuainisha haja na njia za kuinua wanyonge. Katiba ya sasa inachukulia kuwa watu wote ni sawa; au ina dhana kuwa usawa utakuja kutokana na nia nzuri (good will) ya watu wa juu. Ukweli ni kwamba watu ni tofauti. Kuna watu (wa baadhi ya mikoa, makabila, maumbile, jinsia na itikadi) ambao kwa sababu za kihistoria na nyinginezo wamekuwa na hali duni. Kuwachukulia watu hawa kuwa wako sawa na wale wenye hali bora ni kutowajali na kutotambua hali halisi ya jamii yetu.
Isitoshe, Katiba ya sasa inadaiwa kuwa haina dini (Secular). Kama ni hivyo, inalinda vipi haki za jamii ambayo ina dini? Masuala haya ni muhimu kwa vile, kama dini, Secularism ni itikadi na ina wafuasi wake. Inawezekana kwamba Secularism ni itikadi dhidi ya dini. Si makosa pia kusema kuwa katiba isiyo na dini ni katiba ya watu wasio na dini (Secularists); au katiba ya watu ambao dini zao hazina mifumo ya kikatiba. Katiba hiyo inaweza isijali haki za watu ambao dini zao zina mifumo kamili ya maisha. Kuwatendea haki waumini wa itikadi zote, Katiba isiyo na DINI haitoshi. Inayotakiwa ni Katiba isiyo na ITIKADI yoyote (hata ya ujamaa); au katiba yenye mchanganyiko muafaka wa itikadi zote. Kwa maneno mingine, katiba inayotakiwa ni ile isiyopendelea itikadi yeyote, lakini inayolinda itikadi zote.
2.0 Mapendekezo:
2.1 Muundo wa Dola:
2.1.1 Serikali:
(a) Urais:
Rais aendelee kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi kwa zaidi ya asilimia 50 ya wapiga kura wote. Na iwapo hatapatikana yeyote mwenye kupata zaidi ya asilimia 50, itabidi mshindi wa kwanza na pili wapigiwe tena kura ili kuweza kumpata mshindi wa zaidi ya asilimia 50 za wapiga kura wote.
Rais ni lazima athibitishwe na Mahakama katika kipindi cha mwezi mmoja baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.
Kuwepo na uwezekano wa kuhoji matokeo ya uchaguzi wa Rais kupitia Mahakama, ikiwa kuna sababu za msingi za kufanya hivyo (kama vile vitendo vya rushwa au ubadhilifu wa kura), kabla matokeo hayo kuthibitishwa na Mahakama.
Wagombea binafsi wa Urais waruhusiwe.
Rais asiwe sehemu ya Bunge. Sheria zipitishwe na Bunge bila ya kuwa na haja ya Rais kuidhinisha.
(b) Baraza la Mawaziri:
Rais aendelee kuteua Mawaziri, ikiwa ni pamoja na Waziri Mkuu, lakini kutoka nje ya Bunge. Iwapo atamteua Mbunge kuwa Waziri, Mbunge huyo atawajibika kujiuzulu Ubunge.
Baraza la Mawaziri baada ya kuteuliwa na Rais lithibitishwe na Bunge.
Mawaziri wahudhurie vikao vya Bunge kama "ex-officios". Wachangie katika mijadala na kujibu maswali Bungeni, lakini siyo kama "Front Benchers" na wasiwe na haki ya kupiga kura.
(c) Uwajibikaji:
Ikiwa Bunge litakataa mara mbili mfululizo, mswada wa fedha au mswada wowote wa sheria ambao unahitaji kupitishwa kwa kupigiwa kura kwa theluthi mbili ya Wabunge, serikali itabidi ijiuzulu ikiwa ni pamoja na Rais.
(d) Vyombo vya Dola:
Jeshi:
Kuwe na Armed Forces Service Commission itakayoteuwa maafisa waandamizi wa majeshi. Wakuu jeshi, polisi, ,magereza na usalama wa Taifa, watapendekezwa na Commission na kuthibitishwa na Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama baada ya "Public hearing".
Utumishi serikalini:
Uteuzi wa watumishi serikalini utafanywa na Tume ya Utumishi Serikalini, mpaka ngazi ya Katibu Mkuu.
Mwanasheria Mkuu wa serikali, "Controller & Auditor General" watapendekezwa na Rais na kuthibitishwa na Bunge. Mwanasheria Mkuu wa Serikali atakuwa "ex-officio" kwenye Baraza la Mawaziri pamoja na Bunge na hatatoka kwenye chama chochote.
(e) Serikali za mitaa:
Serikali za mitaa zisiwe sehemu ya serikali kuu.
Ianzie vijijini hadi wilayani.
Viongozi wa kisiasa wilayani wawe Ma-Meya na/au wenyeviti wa Halmashauri za wilaya.
Watendaji wakuu wa serikali kuu wilayani wasiwe wanasiasa na wateuliwe na Tume ya Utumishi Serikalini.
2.1.2 Bunge na Wabunge:
(a) Spika:
Spika wa Bunge asiwe Mbunge. Hii itampa uwezo zaidi Spika wa kuwa "Impartial".
Anaweza kujipendekeza au kupendekezwa na Chama chochote cha siasa, NGO, n.k.
Asiwe na haki ya kupiga kura.
(b) Wabunge:
Ili kupanua zaidi demokrasia, wagombea binafsi (Private candidates) waruhusiwe. Kuna sehemu kubwa ya jamii ambayo fikra na mwelekeo wao haufungamani na chama chochote cha siasa, na wangependa kuwakilishwa bungeni kupitia wagombea binafsi.
Wabunge wote wachaguliwe moja kwa moja na wananchi.
Kusiwe na "Proportional representation" na viti maalum kwa sababu umuhimu wake unaondoka kwa kuwepo wagombea binafsi.
Wabunge wasiteuliwe kushika nyadhifa za madaraka katika mashirika ya umma na serikalini, kama vile: Ukuu wa Mikoa, Ubalozi n.k.
2.1.3 Mahakama:
Kuwe na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa. Utumishi wa Mahakama uwe chini ya Tume ya Utumishi wa Mahakama.
(a) Mahakama Kuu:
Iongozwe na Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu apendekezwe na Tume ya Utumishi wa Mahakama na athibitishwe na Kamati ya Sheria ya Bunge baada ya "Public hearing".
Jaji Mkuu asiwe Jaji wa Mahakama ya Rufaa.
(b) Mahakama ya Rufaa:
Kuwe na Majaji wa Rufaa watakaoteuliwa kwa mtindo ule ule wa Jaji Mkuu.
Majaji wa Rufaa wasiwe Majaji wa Mahakama Kuu.
2.2 Muungano:
Mapendekezo ya muundo wa serikali moja ni mapendekezo ambayo yanaweza kupelekea kumezwa kwa Zanzibar na yakipitishwa yanaweza kuvunja muungano. Kwa hiyo, suala la serikali moja lisitajwe kabisa.
Muundo wa serikali mbili ulijengeka juu ya msingi wa chama kimoja. Katika mfumo wa vyama vingi muundo huu umepoteza msingi wake na hauna budi kuondoka. Aidha, katika mfumo wa serikali mbili huenda Zanzibar isimezwe lakini ikabaki mdomoni mwa Tanganyika ikitafunwa.
Kuwepo muundo wa serikali tatu.
2.3 Kuinua wanyonge (Affirmative Action)
Katika haki za binadamu Katiba ya sasa inategemea usawa wa watu binafsi (equality of individuals). Lakini watu binafsi ni sehemu ya vikundi katika jamii ambavyo kwa sababu za kihistoria na nyinginezo haviko sawa. Kwahivyo haitoshi kutoa kipaumbele kwa dhana ya usawa bila ya serikali na taasisi zake kuwa na wajibu wa kutoa upendeleo wa makusudi kwa vikundi vya wanyonge (Underprivileged).
Katiba ilinde na itetee haki za wanyonge kwa kuipa serikali jukumu maalum la kuwainua watu (wa mikoa, makabila, jinsia, maumbile na dini) ambao kutokana na sababu mbalimbali wameachwa nyuma kimaendeleo. Katika "Bill of Rights" kuwe na kifungu kinachoamuru serikali, mashirika ya umma, makampuni binafsi, NGOs, n.k., kuwa na upendeleo wa makusudi kwa vikundi hivi.
3.0 Mwisho:
Hadi hapa kumependekezwa mengi; yakiwemo: Mfumo wa dola iliyo na Bunge huru lenye uwezo wa kuiwajibisha serikali; muungano wenye ridhaa ya wapiga kura wa bara na visiwani; serikali za mitaa zenye demokrasia ya kutoka chini; na hatua madhubuti za kuinua vikundi mbalimbali vya wanyonge.
Mapendekezo haya ni makubwa, ni ya msingi na, bila shaka, yatahitaji Katiba mpya. Yamezingatia hali halisi ili kukidhi mahitaji yote muhimu ya kisiasa na kijamii. Mapendekezo haya yanategemeana. Kwa hiyo, yataleta maana zaidi iwapo yatazingatiwa kwa pamoja. Ni wazi kwamba baadhi ya mabadiliko yaliyopendekezwa yanahitaji ridhaa ya wananchi kupitia kura ya maoni. Mengine, hasa yale yanayohusu muungano, itabidi yapate ridhaa ya theluthi mbili ya wapiga kura wa pande zote mbili. Hata hivyo, lisilobudi hutendwa.
Mapendekezo haya yametayarishwa na kutolewa na Kamati ya Madhehebu ya Halmashauri Kuu ya Kiislamu ya Tanzania ambayo inawakilisha jumuiya za madhehebu ya Kiislamu, yaani:
1. Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).
2. Jumuiya ya Bohra.
3. Jumuiya ya Ibadhi.
4. Jumuiya ya Shia Ithnaasheri.
5. Jumuiya ya Shia Imami Ismaili.
6. Jumuiya ya Sunni.
--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
0 Comments