[wanabidii] Rais ataja hatua saba kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi

Wednesday, November 20, 2013
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais ataja hatua saba kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amependekeza hatua saba za msingi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kupunguza uzalishaji wa gesijoto na kuongeza fedha za kukabiliana na hali hiyo duniani.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa ni siri ya wazi kuwa Afrika inateseka zaidi kwa kukabiliwa na changamoto nyingi na za kila aina kutokana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na ukweli kuwa inachangia kidogo sana katika kuzalisha gesijoto na kuharibu mazingira.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabia Nchi wa COP19/CMP9 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa wa Michezo wa Poland, mjini Warsaw, jioni ya leo, Jumanne, Novemba 19, 2013, Rais Kikwete amewaambia mamia ya washiriki wa Mkutano huo kuwa dunia inahitaji kuchukua hatua saba za msingi kukabiliana na hali hiyo.

Hatua hizo ni zifuatazo:
(a) Kukubaliana kuhusu njia za msingi za kitaasisi za jinsi ya kuzifidia nchi kutokana na upotevu unaotokana na mabadiliko ya tabia nchi.
(b) Kukubaliana kuhusu ni taasisi ipi itasimamia shughuli zinazohusiana na misitu. Taasisi itakayohakikisha na kusimamia namna ipi nchi masikini zinavyoweza kufidiwa kifedha kutokana na upunguzaji wa gesijoto.
(c) Kukubaliana kuhusu misingi, masharti na maelekezo ambayo yatasimamia hatua za kupunguza gesijoto katika nchi zilizoendelea.
(d) Hatua na njia ambazo zitaongoza nchi zilizoendelea kupunguza gesijoto zinatakiwa kukubaliwa na kuelezwa waziwazi.
(e) Kuna umuhimu wa haraka wa kuupatia Mfuko wa Mazingira wa Kijani fedha za kuanzisha na kuimarisha Mfuko huo. Kwa sasa ni Mfuko mtupu. Lazima tuhakikishe kuwa unajazwa ipasavyo. Aidha, lazima tukubaliane namna gani kiasi cha dola za Marekani Bilioni 100 zilizokubaliwa kuchangwa kila mwaka zitakavyopatikana na kugawanywa.
(f) Kituo cha Teknolojia ya Mazingira na Mtandao kitafute jinsi ya kuondoa vikwazo katika masuala yanayohusiana na uhamishaji wa teknolojia kutoka nchi tajiri kwenda nchi zinazoendelea na kumaliza changamoto zinahusiana na Haki Miliki.
(g) Kwenye COP hii tunahitaji kukubaliana kuhusu baadhi ya mambo yanayohusiana na upunguzaji wa gesijoto.

Rais Kikwete alikuwa anazungumza kwa niaba ya viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) katika nafasi yake akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Viongozi wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi (CAHOSCC).

Rais Kikwete amekuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo tokea Januari, mwaka huu, 2013, wakati alipochaguliwa na viongozi wenzake kushika nafasi hiyo kufuatia kifo cha aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mheshimiwa Meles Zenawi, Septemba, mwaka jana.

Viongozi wengine ambao wamezungumza katika Mkutano huo wa ufunguzi ambao Mwenyekiti wake alikuwa ni Rais wa COP 19 Mheshimiwa Marcin Korolec, Waziri wa Mazingira wa Poland ni Waziri Mkuu wa Poland, Mheshimiwa Donard Tusk na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Ban Ki Moon.

Wengine ni Rais wa Mkutano wa 68 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Balozi John Williams Ashe ambaye ni Balozi wa Antigua na Barbuda katika Umoja wa Mataifa na Katibu Mtendaji wa Mkataba wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi wa Umoja wa Mataifa (UNFCC), Mheshimiwa Christiana Figueres.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments