[Mabadiliko] Papara za Kugawa Vitalu Vipya vya Gesi asilia: Tumerogwa, ujasiriamali binafsi ama Uzalendo uliopitiliza?

Friday, October 04, 2013

Papara za Kugawa Vitalu Vipya vya Utafiti wa Gesi Asilia Bila Sera, Sheria na Kanuni: Tumerogwa, Ujasiriamali Binafsi ama Uzalendo Uliopitiliza? (I)

Na Hamisi Kigwangalla, MB.

Wakati wa kipindi cha bunge la bajeti, Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini, aliliarifu bunge kuwa serikali ilikamilisha kazi ya kuipitia mikataba ya gesi asilia mnamo mwezi Novemba 2012 na akasema kuwa "kukamilika kwa kazi hiyo kumeiwezesha serikali kubaini maeneo yanayohitaji kuboreshwa katika mikataba hiyo. Pia, matokeo ya uchambuzi wa mikataba hiyo yatasaidia katika uundaji wa sera, sheria na kanuni za usimamizi wa sekta ndogo za mafuta na gesi asilia itakayokidhi matakwa ya watanzania." Kanuni hii ilinithibitishia jambo moja, kuwa hatuko sawa katika njia tunayopita kuelekea kufanya uvunaji wa raslimali hii adhimu na urithi wetu wa bure; kwamba hatuna sera, sheria na kanuni, sasa tunaendeleaje kutoa vitalu vipya kila siku?

Ufahamu wangu mdogo kwenye mambo haya umeniwezesha kuamini kuwa sheria ya petroli (The petroleum (exploration and production) act) ya mwaka 1980 haikidhi haja ya kuendesha kazi za utafiti na uzalishaji wa gesi asilia, na hata biashara ya gesi asilia. Hata nilipoisoma ile sera mpya ya gesi (draft) nilibaini wazi kabisa nayo inakiri kuwa hatuna mfumo madhubuti wa kisheria na kitaasisi, yaani 'legal and regulatory framework', wa kuendesha vizuri sekta hii nyeti.

Prof. Sospeter Muhongo aliwahi akinukuliwa akisema kuwa tusipokimbia kuanza kuvuna gesi, majirani zetu watatuwahi. Kwani gesi inaoza? Sasa tunavyokimbia namna hii bila kujua tunafaidikaje si tutajikuta tumefika kwenye gesi sawa na wenzetu ama tumewawahi lakini hatuifaidi, kipi bora sasa? Leo hatuna sera, tunajuaje wajibu wa kila mtu kwenye shughuli za uvunaji? Ambapo gesi inachimbwa, watu wenyeji wana haki na wajibu upi? Masuala ya fidia kwa wananchi watakaoathirika kwa namna moja ama nyingine yamekaaje? Wenzetu wa Kenya wamezuia mafuta yao yasichimbwe mpaka kwanza wawe na sera, sisi tunakimbilia wapi?

Wakati tukikiri kuwa hatuna sera, sheria na kanuni mpya na za kisasa zinazoweza kukidhi mahitaji ya Taifa ya uvunaji na uwekezaji kwenye sekta hii nyeti, hivi majuzi Wizara ya Nishati na Madini imetoa tangazo la kualika wawekezaji kwenye 'mkutano na maonesho ya pili ya Tanzania ya mafuta na gesi 2013' utakaofanyika Dar es salaam ukumbi wa Mwalimu Nyerere International Convention Center kuanzia tarehe 23 hadi 25 mwezi huu (oktoba), ambapo mzunguko wa nne wa kugawa leseni za vitalu vya gesi kwenye bahari kuu na kaskazini mwa ziwa Tanganyika (The 4th Tanzania offshore and North Lake Tanganyika licensing round) utazinduliwa.

Katika tangazo hilo lililotolewa na Wizara ya Nishati na Madini kupitia shirika letu la uendelezaji petroli nchini (Tanzania Petroleum Development Corporation, TPDC) vitalu saba vyenye ukubwa wa wastani wa kilomita za mraba 3000 kila kimoja vitagawiwa kwenye bahari kuu kwa mtindo wa kuwapa wawekezaji leseni za utafiti kwa asilimia 100 na vitalu viwili vitabaki kuwa mali ya serikali chini ya shirika lake la TPDC ambapo atatafutwa muwekezaji mshirika wa kufanya naye utafiti wa pamoja. Vitalu vikigawanywa kwa mtindo wa kuwaachia wawekezaji jukumu la utafiti (exploration) maana yake ni kwamba kuanzia siku ya kwanza ya utafiti wanaanza kurekodi gharama zao na wakimaliza na kufanikiwa kugundua gesi, wanapoanza zoezi la kuivuna na kuiuza sasa hiyo gesi wanaanza kukata asilimia si chini ya 70 ya mauzo yote kama gharama zao. Asilimia 30 tu inayobaki ndiyo itagawanywa kwa Tanzania kupata asilimia 60 na wawekezaji kupata asilimia 40. Hii kwa lugha ya kitaalamu wanaita ni 'production sharing agreement (PSA).' Hapa kuna maswali mengi sana ya kujiuliza, nani anafanya kazi ya kuzihakiki gharama wanazoingia hawa wawekezaji ili watakapokuja kuanza kuzikata tuwe na uhakika kuwa ndizo gharama halisi walizotumia?

Na katika vile vitalu viwili ambavyo anapewa TPDC mkataba utakuwa tofauti kwa kuwa kuanzia mwanzoni shirika letu wenyewe litaingia kwenye utafiti hadi uzalishaji na hatimaye mauzo. Na hapa kwa hakika tutarajie kuwa na mgao mkubwa zaidi wa faida kwa kuwa tutakuwa tumeshiriki toka mwanzoni. Na hata kama mbia wetu akisema ameweka gharama fulani tutaweza kuzihakiki maana na sisi tumo. Pia hata uhamishaji wa utaalamu na teknolojia (technology transfer), kujenga uwezo wetu wa kiuendeshaji wa zoezi hili la uvunaji wa raslimali za gesi asilia na mafuta na hata wa kifedha ni jambo litakalofanyika kirahisi katika mtindo huu, na siyo ule wa kuligeuza taifa letu shamba la bibi kwa kuwaachia mabeberu waje wavune tu. Huu ndiyo mfumo wa kufuatwa na nchi yoyote ile yenye watu wazalendo, wanaojitambua na wanaojua biashara. Na ambao wako 'serious' dhidi ya vita ya kupambana na umaskini. Wanaoguswa na shida za wananchi za siku hadi siku, wanaoongozwa na utaifa na si na njaa za matumbo yao.

Leo kampuni ya Statoil ya Norway aliyegundua visima vya gesi huko kwenye bahari kuu ya Tanzania ni kampuni inayomilikiwa na serikali yao kwa zaidi ya asilimia 67, na imeitajirisha nchi yao. Pia kampuni kama Petronas ya Malaysia, National Gas Company ya Trinidad and Tobago zinafanya kazi kwa kufuata 'model' ya Norway.

Kwa nini sasa TPDC isiwe 'Statoil' ya Tanzania? Hili ni swali lenye thamani ya zaidi ya dola za kimarekani milioni moja. Namtaka Prof. Sospeter Muhongo, ambaye amekuwa akijinasibu kwa usomi wake awajibu watanzania. Aoneshe uwezo wake. Awaambie watanzania elimu yake imetusaidia nini kuleta majibu ya swali hili.

Swali lingine lenye kunitatiza na naamini pia watanzania wengi linawatatiza ni kwamba, ni kwa nini tunaharakisha namna hii kuingia kwenye ugawaji wa vitalu vya gesi ilhali hatuna sera, sheria na kanuni mpya? Waziri huyu msomi na mtafiti haoni hatari ya hizi papara zetu kweli? Haoni hatari ya kumaliza kugawa vitalu vyote kisha kurudi kinyume nyume sasa kuanza kuomba mikataba na wawekezaji irekebishwe kufuata sera, sheria na kanuni mpya? Na hapo wanasheria watakuwa wameishaweka vipengele vya kutuzuia kufanya hivyo (stability clauses) kwenye mikataba na hatimaye kuishia kuwapigia magoti kuwabembeleza tu?

Kila siku tunazungumzia uwazi kwenye sekta hizi za raslimali ya gesi, mafuta na madini na Tanzania imesaini mkataba wa kimataifa wa uwazi kwenye sekta hizi (Extractive Industries Transparency Initiative), hivi kuna uwazi kweli hata kidogo tu kwenye haya maamuzi ya Prof. Muhongo na maluteni wake pale Wizara ya Nishati na Madini? Kwanza wanapata wapi uhalali (legitimacy) wa kusaini mikataba kwa kutumia sheria ambayo wao wenyewe wanakiri imepitwa na wakati na ndiyo maana wameanzisha mchakato wa kutunga sera, sheria na kanuni mpya?

Hakuna atakayebisha kuwa ili tuwe salama ni lazima twende kwa hesabu sana, kwanza tuwe na mfumo thabiti wa kisheria na kitaasisi (strong legal and institutional framework); sasa leo hii ndiyo tunahangaika kuandika sera, na kusomesha raslimali watu kwenye sekta hizi, ni lini wataiva na kuanza kutumika - miaka zaidi ya mitatu ni lazima ipite!

Prof. Muhongo hivi anazo kweli takwimu za kodi tulizopata kutokana na migodi mikubwa ya uchimbaji wa dhahabu? Hana taarifa kuwa tulianza kupata kodi pale Rais Kikwete alipoamua kuingilia kati na kuanzisha mazungumzo na wawekezaji hawa kufuatia tume ya Jaji Bomani ndipo tuliposhuhudia wakianza kulipa kodi ya kampuni (corporate tax) ya asilimia 30? Kabla ya hapo kila siku walikuwa wakisema hawafanyi faida na hivyo hawapaswi kulipa kodi. Leo kuna kampuni ngapi za uchimbaji wa dhahabu zimefunga migodi yao bila kulipa hata shilingi moja na nyingine kulipa miaka miwili hadi minne ya kurashia rashia tu kwa 'soni' ili kujijengea mazingira rafiki ya kupewa kitalu kipya wavune tena dhahabu? Wakati wimbi la kuingia kwa wawekezaji hawa wakubwa kwenye migodi ya dhahabu linashika kasi, kisingizio cha kuwaondoa kwa nguvu wachimbaji wadogo na wananchi wenyeji wa maeneo hayo kwenye maeneo yao (kama wageni kwenye nchi yao) kilikuwa tuwakaribishe wawekezaji watalipa kodi, watajenga shule na hospitali, wataongeza ajira nchini n.k. Hivi ni shule ngapi zimejengwa kwa mfano na Resolute pale kwetu Nzega? Wananchi wenyewe wameweza kujenga shule ngapi kwa pesa ya kilimo cha jembe lao la mkono tu? Sheria mpya ya madini ilipokuja imetusaidiaje sisi kama Taifa? Tumekuwa na sheria nzuri lakini haina meno kwenye mikataba ya zamani.

Wawekezaji hawakuleta maendeleo yoyote ya kupigia mfano, ambayo hata leo unaweza kuonesha. Hakuna tofauti kati ya Nzega iliyokuwa na mgodi mkubwa wa dhahabu na Igunga ambayo haikuwa na mgodi mkubwa kama ule katika kipindi hicho hicho – inakuwa bora hata Mwadui ya Williamson Diamonds kule Shinyanga ina utofauti na vijiji jirani na hata mjini Shinyanga kwa wakati ule! Wawekezaji kwenye sekta ya dhahabu hawakuleta maendeleo kwa wenyeji wanaowazunguka wakidai kuwa hawawajibiki kimkataba kufanya hivyo. Je, tumejipangaje kwenye sekta ya gesi? Kwa nini tusitulie kwanza, tukatengeneza sera ya kuwahudumia wenyeji ( a policy on local content initiatives) ili 'tuwawajibishe' wawekezaji, tujue wenyeji watafaidikaje na nchi itafaidikaje, na wao washirikishwe kwenye mchakato huo ili twende pamoja?

Kama ilivyo kwa mambo yote yanayoendelea kwenye gesi, na kama ilivyokuwa kwenye ile sekta ya madini, usiri wa maksudi ama wa kutojua umegubika namna ya wenyeji kufaidika. Tunaambiwa watanzania wataajiriwa, watauza bidhaa zao kwenye makampuni ya madini na uchumi wa maeneo hayo utakuwa kwa kasi, mchanganuo wa kina wa namna haya yatakavyotekelezeka umeandikwa kwenye sera, sheria ama kanuni ipi? Mkakati wa kuwawezesha wazawa wafanikishe haya kwa viwango vinavyotakiwa uko wapi? Maana haya makampuni huja na 'viwango' vyao vya nyanya na vitunguu na vinginevyo, sasa je sisi tumejiandaa vipi kuwawezesha wenyeji wafaidike na soko hili jipya na la uhakika?

Je, tuna sera gani ya kutunza na kutumia mapato yanayotokana na gesi? Kwa sasa, kwa ufahamu wangu, hatuna. Kwa nini tusijipange tukatunga sera, sheria na kanuni safi za kutuongoza, tukajenga mtaji wa raslimali watu ya kutosha, tukawekeza mtaji kwenye TPDC yetu ndipo tukaingia sasa kutafuta 'wabia' wa kusaidiana nao kutafiti na hatimaye kuwekeza, siyo wa kuwapa vitalu 'wawekeze!'. Watanzania tunatamani tuwe na TPDC inayofanana na Statoil. Je, Prof. Muhongo yuko tayari kutupa hiyo?

Tukikamilisha mchakato wa kujenga mfumo thabiti wa kisheria na kitaasisi kwa njia ya kidemokrasia ya uwazi na shirikishi tutakuwa tumewapa uhalali akina Prof. Muhongo na wenzake sasa kufanya maamuzi ya utekelezaji yanayofuata sera, sheria, kanuni na mikakati iliyowekwa.

Kwa nini tusijipange kuifanya TPDC yetu kuwa 'Statoil' (mwekezaji) kwenye nchi nyingine huko tunakoelekea? Kama tungeliamua vema huko tutokako, STAMICO leo ingekuwa tajiri na ingekuwa inachimba dhahabu kama Ashanti Goldfields Corporation ya Ghana. Tusikosee tena kwenye gesi.

Tuna haraka gani, na ya nini? Ya kwenda wapi? Kuhakikisha tu gesi imechimbwa – na kwamba sisi kufaidika ama kutofaidika siyo ishu? Kwani kuna umaarufu gani tunaupata kwa kugawa vitalu vya gesi vyote leo? Na mwani ni lazima wavigawe vyote hao waliopo wizarani leo? Tunatunga sera, sheria na kanuni mpya ili zije zitumike kwenye nini wakati vitalu vyote tunagawa leo kwa kutumia sheria ya kizamani? Haya ni maswali yanayohitaji majibu kuntu. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo akipenda anaweza kuja kutukata kiu yetu ya kujua. Atuelezee kwa kina. Na kama anataka nchi hii imkumbuke kwa kushiriki kuijenga afanye uamuzi sahihi - asimamishe ugawaji wa vitalu vipya vya gesi, akamilishe mchakato wa kujenga mfumo wa kisheria na kitaasisi ndipo aendelee. Ila kama anataka alaumiwe na vitukuu na vining'ina vyake mwenyewe aendelee na hii papara yake.

Dkt. Hamisi Kigwangalla (MB) ni Mbunge wa Jimbo la Nzega na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).


--
"Vision is the ability to see the invisible!"
Hamisi A. Kigwangalla, MD, MPH, MBA
P.O.Box 22499,
Dar es salaam.
Tanzania.
Phone No: +255 754 636963
                +255 782 636963
website: www.peercorpstrust.org or www.hamisikigwangalla.com
Email: hamisi.kigwangalla@peercorpstrust.org or info@hamisikigwangalla.com
Skype ID: hkigwangalla
Blog: blog.hamisikigwangalla.com 

--
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la 'Mabadiliko'.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda; mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com
Utapokea Email ya kudhibitisha kujiondoa kwako.
 
TEMBELEA Facebook yetu:
http://www.facebook.com/MabadilikoForums?ref=hl
 
For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forum" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
To post to this group, send email to mabadilikotanzania@googlegroups.com.
Visit this group at http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Related Posts

0 Comments