[wanabidii] Je, Kufanya biashara ni kipaji?

Wednesday, September 11, 2013
na Albert Sanga, Iringa — Msomaji mmojaaliyejitambulisha kwa jina moja la Jackson, alinitumia pongezi na kisha akaniuliza swali hili; "Sanga kwa nini wataaalamu mnasema biashara ni kipaji? Usemi huu huwa una maana gani? Na mfano hai tazama jamaa zetu Wahindi, kwa watanzania angalia kanda ya kaskazini Wachaga; kwa nyanda za juu angalia Wakinga. Unasemaje hapo?"Katika makala ya leo nitajikita kulijibu swali hili.

Bahati nzuri ni kwamba mimi nimesoma  Shahada ya Biashara nikiwa chuo kikuu na huu mjadala wa ikiwa biashara ni kipaji ama laa ulikuwa ni sehemu ya 'assigments' zetu katika somo la Ujasiriamali (Entrepreneurship). Mjadala huu  huwa unapatikana katika kitu wanachokiita tetesi (myths) kuhusu ujasiriamali. 

Ni katika 'myths' hizi ndipo utakutana na swali lisemalo Je, wajasiriamali huzaliwa ama hutengenezwa? (Are Entrepreneurs Made or born?). Swali hili huambatana na malumbano makali yenye ushahidi kutoka kila upande (ikiwa wanazaliwa ama wanatengenezwa). Bila shaka ni katika mjadala ama maandiko ya namna hii ndipo msomaji wetu Jackson akadadisi ili kujiridhisha ikiwa Biashara ni kipaji ama laa?

Katika swali hili sitakuwa na jibu la moja kwa moja na hatua kwa hatua naweza kupishana na wataalamu
wengine wa masuala ya biashara. Hata hivyo mjadala wangu utaegemea upande wa uzoefu wa kivitendo katika eneo hili la biashara. 

Bahati nzuri ni kuwa mimi ni Mkinga na tena ni mfanyabiashara. Hivyo kwa sehemu fulani ninawasaa wa kueleza hiki kinachoitwa siri ya mafanikio na vipaji vya wakinga (na ndugu zao wachaga) katika biashara. Katika makala haya nitawagusa Wakinga na Wachaga kwanza na ndugu zetu Wahindi nitawapumzisha kidogo leo.

Lakini pia ninapenda niziweke vizuri takwimu tunapoendelea. Kitakwimu ni kwamba watu kutoka makabila mbalimbali nchini Tanzania miaka ya zamani (na zaidi sana miaka ya sasa) wamekuwa wakijishughulisha na biashara. Kwa hiyo sio Wakinga na Wachaga pekee waliobobea kwenye biashara; ingawa kuna ushahidi usio na shaka kwamba wengi wa Wakinga na Wachaga wanaokuwa kwenye biashara, hung'aa na kufanikiwa kwa spidi.

Kuna utafiti nimewahi kufanya ulioniwezesha kupata misukumo ya kimafanikio kwenye biashara baina ya Wachaga na Wakinga.  Katika utafiti wangu nilibaini misukumo ya aina mbili; "push power" na "pull power". "Push power" ni ule msukumo unaomlazimisha mtu kutoka eneo duni kiuchumi kuingia kulitafuta eneo bora kiuchumi. "Pull power"  ni msukumo anaokuwa nao mtu unaotokana na namna anavyoona hatua za wenzie kiuchumi.

Kihistoria Wachaga waliwahi kujanjaruka ukilinganisha na Wakinga. Kuwahi kwa dini maeneo ya uchagani, kuwahi kwa shule, kuingizwa kwa mazao ya kibiashara pamoja na uimara wa tawala za kichifu kulipelekea Wachaga wengi wawahi kujitambua. Wengi wao tangu zamani wakabahatika kusoma, wakabahatika kuwa na imani za kidini pamoja na kutambua umuhimu na thamani ya ardhi. 

Kwa kadiri miaka ilivyokuwa inaenda watoto wa Kichaga wanavyokua walibahatika kuwa na watu wa mfano wa kujifunzia namna ya kuishi kiimani, namna ya kukazana masomoni,  namna ya kutumia ardhi kwa umakini; kitu ambacho kilipelekea wengi kuwa katika mtazamo wa kibiashara. 

Kutokana na hili vijana wengi wa Kichaga wakawa na cha kujisemea moyoni; mathalani; "Nataka na mimi nisome niwe kama fulani aliyepo sehemu fulani" ama "nataka na mimi nianzishe biashara niwe kama fulani aliyepo sehemu fulani" Hiki ndicho ambacho tunakiita "Pull Power"

Kwa upande wa Wakinga wao mambo hayakuwaendea sawa tangu zamani. Maeneo ya Ukingani (kule Makete na Njombe) mwamko wa elimu ulichelewa sana, mila na imani za kishirikina zilikuwa na mizizi mikubwa mno kiasi kwamba dini nyingi hazikujikita tangu zamani. Hili lilipelekea Wakinga wengi kukosa kwenda shule, walichelewa kutambua thamani na nguvu ya ardhi; na mwisho wengi walijikuta kuwa hali za kiuchumi ni ngumu na mbaya.

Historia inatueleza kwamba kutokana na ugumu wa maisha asilimia kubwa ya vijana wa Kikinga walikuwa wakilazimika kuchukuliwa kama manamba na kwenda kufanya kazi kwenye mashamba ya miwa (Kilombero na Mtibwa), kwenye mashamba ya katani (Tanga na Morogoro), kwenye mashamba ya chai (Mufindi na Njombe). 

Hivyo utagundua kuwa kilichokuwa kikiwalazimisha kwenda huko na huko kutafuta maisha ilikuwa ni ugumu wa maisha wa mahali walipokuwepo. Hii hali ya mtu kujikuta huna namna isipokuwa kuondoka na kwenda kutafuta ndicho tunachokiita "Push Power".

Wakinga wengi walipokuwa wakifika maeneo hayo ya mashamba (wakiwa kama manamba) wengi walikuwa wakipaona mahali hapo kama "peponi" wakilinganisha na mazingira ya kifukara waliyoyaacha kule kwao Ukingani. Kutokana na hili wengi wao walikuwa wakiazimu mioyoni mwao, kupambana kufa na kupona ili kutorudia ufukara waliokuwa nao kule makwao. 

Wengi wa Wakinga waliokuwa katika maeneo haya walikuwa wanakataa kurudi makwao ule muda wa msimu unapoisha. Kwa kuwa walikuwa wanabaki katika maeneo yale, na kwa kuwa walikuwa wanataka sana kujikwamua na ufukara, na kwa kuwa wengi hawakuwa na elimu za kuweza kuajiriwa, ilikuwa wanalazimika kuanza biashara. 

Mara zote ili mtu ufanikiwe na kukabiliana na changamoto ni lazima kuwe na msukumo mkubwa ndani yako unaokulazimisha kuendelea kufanya kile unachokifanya. "Push Power" ndani ya Wakinga ilikuwa kubwa sana kiasi kwamba mtu alikuwa anaona ni bora afe yeye kuliko kupoteza mtaji alioa nao kwenye biashara.

Baada ya kutambua 'backgrounds' zilizopelekea makabila haya mawili kuanza kupenda na kujifunza biashara nije sasa katika eneo linalowaunganisha Wakinga na Wachaga hata tunaona mafanikio yao katika biashara. Tabia nyingi (kama sio zote) walizonazo Wakinga na Wachaga zinafanana na ndizo zinazowapelekea kufanikiwa sana katika eneo la biashra.

Wakinga na Wachaga wana tabia ya kupendana na kushirikina sana. Ukiona Mkinga ameanzisha duka sehemu basi muda si mrefu ataenda kule kwao kijijini na kumchukua ndugu ama mdogo wake. Akishamchukua atamuweka dukani awe anauza, atamfundisha biashara na mwisho wa siku atamgawia mtaji. 

Hulka hii pia ipo kwa wingi mno kwa Wachaga. Kutokana na moyo huu wa kupendana, kupeana mitaji na kufundishana biashara ndiko kunakopelekea watu wengi wa makabila haya kupata wasaa wa kuanzisha biashara kwa wingi.  Mkinga na Mchaga huona fahari kubwa sana anapoona mtu wa kabila lake amefanikiwa. 

Sisemi kuwa Wakinga na Wachaga wana ukabila, la hasha! Lakini ninachokithibitisha ni kuwa hawana wivu wa kifitina. Ukiona Mchaga ama Mkinga ana wivu kwa mwenzake basi ujue ni wa kimaendeleo. Hiki ni kitu kizuri ambacho watu wengine wote yafaa wajifunze. 

Kitu kingine ambacho Wakinga na Wachaga wanacho ni katika eneo la kusimamia malengo. Mkinga akishapanga kuwa mwaka huu ni lazima nifungue duka la pili; hayumbi, hatetereki na wala haahilishi lengo lake hilo mpaka aone limetimia. 

Na asilimia kubwa (kama sio wote) ya Wakinga licha ya kwamba wengi hawakubahatika kwenda shule; lakini kuna utamaduni imara sana wa kufanya biashara kwa malengo. Mtafute mfanyabiashara yeyote wa Kikinga popote alipo muulize una malengo gani mwaka  huu; yaani hata kama yupo usingizini atashtuka na kukutajia malengo yake. 

Utamaduni huu wa kupanga na kusimamia malengo upo kwa wingi sana kwa Wachaga pia. Watafute Wachaga uone watakavyokuorodheshea mambo wanayopanga kuyatekeleza kule kwao Uchagani na katika maeneo wanayoishi-Utafurahi mwenyewe! Na hili sote tunalifahamu kuwa, "Ukitaka kufanikiwa katika jambo lolote hakikisha unapanga na kuyasimamia malengo"

Hulka nyingine inayochagiza watu wa makabila haya kufanikiwa sana kibiashara ni kuweka na kuheshimu akiba. Kwa upande wa Wakinga, watoto tangu wanapozaliwa na kuendelea kukua huwa wanafundishwa tabia ya kuweka na kuheshimu akiba iwe ni ya mazao ama fedha. 

Ukienda kule Ukingani utakutana na vijumba vidogo vidogo viitwavyo "vibana" ambavyo vinatumika kuhifadhia mazao mbalimbali. Kanuni kubwa ni kuwa hutakiwi kutumia akiba ya mazao hayo kabla ya kufika kwa msimu mwingine wa kuvuna. 

Unapoitumia akiba iliyomo kwenye "kibana" ni lazima uhakikishe kuwa umeshavuna mazao mengine ya kubadilishia humo. Wakinga wanaamini kuwa mtu unaetegemewa kwenye jamii unatakiwa kuwa na vitu wakati wote. Sifahamu kwa Wachaga wanafanyaje katika suala la akiba ya mazao lakini ninafahamu sifa yao katika akiba ya fedha.

Pia Wakinga katika suala la fedha kuna akiba huwa inaitwa "Ekhefumbato". Hii ni fedha ambayo inakuwemo ndani ama benki ambayo haitakiwi kuguswa kwa namna yeyote ile bila kuwepo ya kubadilishia. Kama akiba hiyo (Ekhefumbato) imewekwa kwa lengo la kujengea nyumba hapo baadae, Mkinga (halisi) hatathubutu kuigusa akiba hiyo hata kama imetokea mtoto amefukuzwa shule kwa kukosa ada.

Mkinga yupo tayari kwenda kukopa kwa jirani alipe ada ya mtoto lakini sio kugusa akiba kinyume na malengo ya msingi. Hata Wachaga huwa hawana mchezo katika suala la kuheshimu akiba zao iwe ni nyumbani ama benki. Hii ni siri nyingine kubwa inayopelekea wafanyabiashara wa makabila haya mawili kufanikiwa sana kibiashara.

Jingine linalowafanikisha hawa jamaa ni nidhamu ya matumizi. Hii nidhamu ya matumizi watu wengi huitafsiri vibaya kwa kusema ni ubahili. Watu wengi wanaamini kuwa Wachaga na Wakinga ni wabahili sana. Huwa nasikia wanauita "Umangi" na "Ukinga". Kimsingi hili neno Ubahili mimi huwa nalitafsiri kwa namna hii, "Ni kutumia fedha kwa kadiri ya ilivyokusudiwa na kupuuza mahitaji yanayoibuka nje ya makusudi na yasiyo na umuhimu mkubwa hata kama yakipuuzwa". 

Unapotumia fedha kwa kadiri ya ulivyokusudia wewe na unapokuwa na utamaduni wa kutomridhisha kila anaekuomba fedha 'automatically'utaitwa bahili! Lakini nidhamu ya matumizi iliyopo miongoni mwa Wakinga na Wachaga ni pana sana na inawasaidia kwa namna nzuri sana. 

Mkinga na Mchaga huwezi kumkuta akiendekeza starehe ama matumizi yanayozidi faida yake katika biashara. Mkinga ni bingwa wa kubana matumizi, kiasi kwamba hata awe na duka chakula cha kula dukani kinatoka nyumbani, akisafiri kibiaashara halali hoteli za gharama kubwa. Katika haya yote kwa nini wasifanikiwe?

Natambua kuwa kuna 'myths' mbalimbali kuhusu  mafanikio ya makabila haya kibiashara. Wakinga wanasemwa kwamba wanatumia ushirikina katika biashara zao na Wachaga wanatuhumiwa kwa ujambazi. Licha ya kwamba makala zijazo nitachambua 'myths' hizi lakini niharakishe kusema kuwa hayo ni mambo ya kupuuzwa badala yake tujifunze kutoka haya mazuri niliyoyachambua.

Watanzania wote tunastahili ushindi kiuchumi!

stepwiseexpert@gmail.com, +255 719 127 901.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Related Posts

0 Comments