"HATUKUBALI hata kidogo kuwaruhusu Wazungu na Wahindi kuingia Chama cha Wafanyakazi Relini, na niko tayari kwenda jela kulikosemwa mtu akipingapinga atapelekwa".
Hayo aliyasema Bw. Samuel Katungutu mwandishi Mkuu wa TRAU katika mkutano wa hadhara mjini Dar es Salaam jana jioni. Bw. Katungutu alieleza kwamba majadiliano yao na viongozi wenzake kutoka Kenya na Uganda, mbele ya mwamuzi Chifu Lugusha hayakuafikiana.
"Wiki mbili zilizopita, majadiliano hayo yalikuwa yakiendeshwa mjini Nairobi, lakini yalipokwama ilishauriwa wajumbe waje Dar es Salaam kwenye nchi huru huenda wakafanikiwa; kumbe yakakwama kabisa".
"Kwa hiyo", alisema Bwana Katungutu, jambo lililobakia ni kuanzisha mastaplani yetu ya pili, ambayo hatutaitangaza magazetini wala redioni ili kuwapa "maadui" wetu faida; bali tutawaarifu wanachama wetu tu".
Akamalizia kutamka kwamba iwapo Wahindi na Wazungu wanapenda kujiunga na vyama vyetu, basi waende TFL kunakoruhusiwa mseto.
Katika mkutano huo, Bw. Walter Otenyo, Mwandishi Mkuu wa chama cha wareli nchini Kenya alitamka kwa nguvu; "Adui ni adui wa Waafrika wenzake, kwa sababu, wakati yeye anapata zaidi ya shilingi 6,000 kwa mwezi, anapendekeza mikutanoni kwamba Waafrika wanapaswa kupata mishahara ya chini ya shilingi 101 tu kwa mwezi.
Akaongeza: "Adu amechafua hali ya mishahara katika Tanganyika, na sasa anaendelea kuchafua katika kazi za umoja za serikali ya Tanganyika, Kenya na Uganda.
Akasema: "Hii si ajabu kwamba mtu anayeshiba kuwasahau wenzake wenye njaa kwa sababu hata akina Mzee Kenyatta na Bw. Sagini (Waziri wa Elimu nchini Kenya) wamewapeleka watoto zao kwenye shule za Wahindi na Wazungu baada ya waalimu Waafrika kugoma kutaka haki zao. Je, huo ndio umoja? aliuliza.
Bw. Otenyo aliwashauri kwa nguvu viongozi wenzake wa Tanganyika wasikubali Wahindi na Wazungu kuingia katika TRAU au jamaa hao watabakia watu wa juu siku zote.
Bwana Abdallah Mwamba, Mwenyekiti wa Tawi la Dar es Salaam la TRAU alisema kwa huzuni: "Tumwachie Mungu taabu zetu na shida zetu".
MTANGAZAJI wa Tanganyika Broadcasting Corporation Bibi Khadija Said yupo London katika sauti ya BBC kwa mafunzo juu ya kazi yake ya utangazaji redioni.
Watangazaji wengine kutoka nchi mbalimbali wanahudhuria mafunzo hayo. Ofisa wa BBC ambaye kazi yake ni kuwafunza watangazaji hao ni Bw. G. Seymour ambaye alisema kwamba Bibi Khadija na wenziwe wakimaliza mafunzo yao wataweza kuendelea vizuri na kazi wakirejea makwao.
Mafunzo haya yameanzishwa tangu 1954 kwa ajili ya kusaidia utangazaji wa habari kwa redio na watangazaji kiasi cha 200 kutoka nchi 29 wamepata faida kutokana na mafunzo kama haya. Mafunzo haya huchukua muda wa wiki kumi na yanahusiana na kazi za utangazaji wa redio.
Wakimaliza mafunzo yao watarejea katika nchi zao na kuendelea na kazi kama kawaida.
MZUNGU mwingine ambae ni Meneja wa kampuni ya kuuza dawa, Arusha Bw. R. Bawley ameamriwa aihame Tanganyika, Mzungu huyo amepewa saa 48 tu kufanya hivyo.
Ripoti iliyopokelewa jana na gazeti hili ni kwamba Bwana Bawley alionekana akiondoka na matokaa kuelekea Kenya.
Sababu za kufukuzwa Mzungu huyo ni ufedhuli na kuwadharau Waafrika.
Mwandishi wetu akizungumza na na Regional Commissiner wa Jimbo la Kaskazini, Bwana P. Walwa jana alijulishwa kwamba jambo hilo alilihakikisha yeye mwenyewe alipofukuzwa na Meneja huyo.
Bwana Walwa alipata malalamiko kutoka kwa watu wengi kuhusu ufedhuli wa meneja huyo. Watu wengine walisema kwamba huwafukuza watu dukani kwake au kuwatupia fedha wakinunua vitu.
Bwana Walwa alikwenda katika duka hilo ili ahakikishe mwenyewe kabla ya kuchukua hatua na kwenda kufika Bawley akamwambia 'nenda zako'.
Hapo Bwana Walwa alitoka na kutoa habari hizi kwa polisi.
Radhi yakataliwa:
Asubuhi yake Meneja huyo alikwenda kuomba radhi akisema hakujua kuwa yule aliyemfukuza alikuwa Regional Commssioner.
Bwana Walwa alikataa kumsamehe kwa sababu, alisema 'dharau ile ilifanyiwa Waafrika wote'.
Bwana Walwa alimwambia mwandishi wetu hiyo jana kwamba yeye alitembelea jimbo lote akiwaonya watu waheshimiane. Aliona si haki wengine waachiwe kufanya dharau.
...Bawley sasa ni Mzungu wa sita kuondolewa kwa visa kama hivyo tangu nchi hii ipate uhuru wake.
MNAMO siku ya Ijumaa mambo yalikwenda kombo huko kwenye kambi ya wafanyakazi wa Kawe, wakati kisura alipoamua kunywa sumu afupishe maisha yake kwa sababu mumewe hataki kumpa talaka yake ambayo amekuwa anamdai kwa muda mrefu sasa.
Ilikuwa siku hiyo mchana Bwana, jina ndani ya faili, alirejea zake kazini na kumkuta mkewe katulia vilee akiwa na fikara zake. Bwana alimwita mkewe na kumwomba amtayarishie maji ya kuoga, lakini kisura akaja juu kwamba kazi hiyo hanayo tena angojealo ni talaka yake tu na si mengine!
Kamtandika:
Bwana kusikia hayo, naye bado anampenda kisura, akaona afadhali kuyaharibu mambo, akaanza kumtandika kisura alivyoweza, na alimtandika kweli! Kisura kuona yamechacha akakimbilia kwenye ulinzi huko polisi na kueleza yaliyompata. Baada ya muda wakampa ruhusa kurejea huko makaoni kwake.
Kajinywea sumu:
Kisura akaona mambo sasa yanakwenda kombo na takala hapati, nakujiondokea bila talaka atakosa sheria akatulia na kuamua kujiondokea duniani. Akafanya kila njia akaipata sumu na kuinywa. Saa chache tu, majira yakisema saa 12.00 jioni hali ya kisura ikaanza kubadilika, njiani kurudisha kadi. Mume kuona yanamharibikia akaitaarifu polisi, majirani na akina yakhe tukajikusanya kuona vioja.
999 Magereti
Mnamo majira ya saa moja usiku walinzi wakaja ndani ya 999 na bila kuchelewa mpira kuchemka kukimbilia. Baada ya matibabu kisura kapata hujambo na sasa anaendelea vema. Sijui atachukua hatua gani tena akisha pona na talaka inagoma.
MNAMO siku ya Ijumaa mambo yalikwenda kombo huko kwenye kambi ya wafanyakazi wa Kawe, wakati kisura alipoamua kunywa sumu afupishe maisha yake kwa sababu mumewe hataki kumpa talaka yake ambayo amekuwa anamdai kwa muda mrefu sasa.
Ilikuwa siku hiyo mchana Bwana, jina ndani ya faili, alirejea zake kazini na kumkuta mkewe katulia vilee akiwa na fikara zake. Bwana alimwita mkewe na kumwomba amtayarishie maji ya kuoga, lakini kisura akaja juu kwamba kazi hiyo hanayo tena angojealo ni talaka yake tu na si mengine!
Kamtandika:
Bwana kusikia hayo, naye bado anampenda kisura, akaona afadhali kuyaharibu mambo, akaanza kumtandika kisura alivyoweza, na alimtandika kweli! Kisura kuona yamechacha akakimbilia kwenye ulinzi huko polisi na kueleza yaliyompata. Baada ya muda wakampa ruhusa kurejea huko makaoni kwake.
Kajinywea sumu:
Kisura akaona mambo sasa yanakwenda kombo na takala hapati, nakujiondokea bila talaka atakosa sheria akatulia na kuamua kujiondokea duniani. Akafanya kila njia akaipata sumu na kuinywa. Saa chache tu, majira yakisema saa 12.00 jioni hali ya kisura ikaanza kubadilika, njiani kurudisha kadi. Mume kuona yanamharibikia akaitaarifu polisi, majirani na akina yakhe tukajikusanya kuona vioja.
999 Magereti
Mnamo majira ya saa moja usiku walinzi wakaja ndani ya 999 na bila kuchelewa mpira kuchemka kukimbilia. Baada ya matibabu kisura kapata hujambo na sasa anaendelea vema. Sijui atachukua hatua gani tena akisha pona na talaka inagoma.
WAZIRI wa Elimu nchini Tanganyika Bw. Oscar Kambona aliwaambia watu huko Morogoro kuwa "Serikali inanuia kabisa kuzikabidhi serikali za mitaa madaraka kamili ya kuendesha shule zote za elimu ya mwanzo, Primary Education.
Bw. Kambona alikuwa akiongea haya huko Morogoro hivi karibuni katika ziara yake fupi kuwakagua watu wake waliomchagua.
Misaada:
Waziri huyo alizidi kuhakikisha kuwa, serikali itakuwa tayari kutoa fedha kama misada ili kuwezesha shule hizo ziendelezwe katika kila wilaya. Hata hivyo, Maofisa wa shule katika kila sehemu hizo watasaidia kutoa maoni yao kama washauri.
Kulikuwa na migogoro kama mitatu inayozuia kupanuliwa kwa elimu humu nchini. Alinena Bw. Kambona akiwahutubia wajumbe waliokuwa wakiwakilisha chama cha TAPA. Shida kubwa ni kwamba, nusu ya watoto wawezao kuhudhuria masomo huwa hawaamriwi kufanya hivyo.
Kosa kubwa:
Na hata wale wapatao bahati ya kusoma, mara kwa mara huacha masomo yao baada tu ya kufika darasa la nne, hilo lilikuwa kosa sana kwa wazazi. Alitamka.
Ingawa kulikuwa na lawama kwamba watoto hao huacha shule kwa ajili ya kukosa malipizi ya ada, lakini ni lazima wazazi wafanye kila njia kuondoa shida hiyo. Jambo hili ambalo ni moja kati ya migogoro mingi, linatokea kwa ajili ya upungufu wa fedha katika Tanganyika nzima, hata pesa za kuwalipa walimu nazo zina wasiwasi.
Picha kamili:
Waziri huyo alimaliza usemi wake kwamba katika mpango wake wa elimu ya miaka mitatu ambao unatazamiwa kuanzishwa baada ya miezi miezi michache ijayo, bila shaka utatoa picha kamili na mipango ya elimu ya nchi ya Tanganyika hapo baadaye.
--
MZALENDO, Jumapili, Novemba 3, 1985.
RAIS Nyerere amewaomba wazee nchini kumsaidia Rais mteule, Ndugu Ali Hassan Mwinyi kama ambavyo walivyomsaidia yeye wakati wa kudai uhuru na baada ya uhuru.
Mwalimu akizungumza na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam katika sherehe za kuagana nao zilizofanyika jana kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, mjini Dar es Salaam alisema mambo makubwa ya nchi ya kimaendeleo yanayoanzishwa hayawezi kufanikiwa kama hayana baraka za wazee.
"Kama mlivyonisaidia mimi, msaidieni na mwenzangu. Anaihtaji sana msaada wenu", alisema Mwalimu ambaye anastaafu Urais kesho kutwa wakati Ndugu Mwinyi atakapoapishwa kuwa Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano.
Mwalimu ambaye katika hotuba yake alizungumzia kwa kirefu misaada mbalimbali aliyopewa na wazee nchini wakati wa kudai uhuru, alieleza kuwa pamoja na kuwa misingi mizuri imejengwa nchini, matazamio ya wananchi ni makubwa jambo ambalo alisema linamfanya Ndugu Mwinyi awe na kazi kubwa mbele yake.
Aliwashukuru kwa msaada, imani na kuelewa kwao mambo na ushirikiano mzuri waliompa katika miaka 24 ya uhuru wa taifa na pia katika harakati za kuutafuta. "Kila nilipotembea nchini wakati wa kudai uhuru watu wa kwanza walionielewa walikuwa wazee", alisema.
Mwalimu aliwataka vijana nchini kuiga mfano wa wazee hao na pia kufanya kazi za kujitolea ili kuliwezesha taifa kufikia hatua kubwa zaidi ya kimaendeleo.
Akigusia mchango uliotolewa na vijana enzi za kudai uhuru ambao wengi wao hivi sasa ni wazee, Mwalimu alisema Tanzania haiwezi kufanya maendeleo makubwa bila vijana kufanya kazi za kujitolea.
Alisema vijana ndio wengi nchini ni wasomi na wana nguvu na kwamba bila wao kutumiwa kwa kufanya kazi za kujitolea, maendeleo makubwa hayawezi kufikiwa.
Mwalimu aliwakumbusha baadhi ya michango ya vijana wa zamani ya kujitolewa iliyosaidia kupatikana kwa uhuru. "Kazi za vijana wa zamani ilikuwa kufanya kazi za hiari kwa ajili ya TANU na kuimba, alisema.
Aliwataka vijana kuchagua kazi ambazo wanaweza kuzifanya kwa kujitolea ili kusaidia taifa kufikia maendeleo makubwa zaidi.
Katika risala yao kwa Mwalimu, wazee hao walimpongeza Mwalimu kwa uamuzi wake wa kustaafu na kumtaka wakati akiwa Mwenyekiti wa Chama kufanya kila analoweza kukiimarisha Chama. "Chama ndicho kilichotukomboa ... Chama ndicho kilichotukomboa... Chama ni baba na mama", walisema wazee hao.
Miongoni mwa zawadi walizompa Mwalimu katika sherehe hizo ni baiskeli, jembe, panga, kiti na mkongojo.
Leo Mwalimu atapokea maandamano makubwa ya walimu wa mkoa wa Dar es Salaam yatakayoanzia Arnautoglu hadi Ikulu ambako ataagana nao.
Mapema jana Rais Nyerere alikabidhiwa rasmi "nishani ya Mkuu wa nchi" kutoka Chama cha Kimataifa cha Klabu ya Misaada za Lions kutokana na chama hicho kutambua mchango wa Mwalimu katika kuwasaidia binadamu.
Katika sherehe iliyofanyika nyumbani kwake Msasani, mjini Dar es Salaam asubuhi, Mwalimu pia alikabidhiwa shilingi laki moja atakazozitumia kwa ajili ya mradi wowote wa maendeleo jinsi atakavyoona yeye katika eneo lolote nchini.
Mwafrika, Alhamisi Juni 22, 1961
BWANA Lifa Chipaka alisema jana kwamba bado anaendelea na cheo chake cha Mwenyekiti wa African National Congress. Ripoti iliyotolewa na chama hicho juzi kusema Chipaka hatakiwi kwahiyo ajiuzulu aliita kuwa ni ya uongo mtupu, wala haitambui.
Bwana Chipaka alidai kuwa hiyo Districk Committee iliyosemwa kuwa imemfukuza kazi yeye haifahamu, wala hata kama iko yeye anafikiri kuwa haiwezi kumtoa kazi Mwenyekiti wa chama cha Tanganyika nzima.
Akafyatuka, "Mtemvu lazima atoke yeye katika Congress maana ameharibu jina la chama, alipokuwa akisafiri huko na huko ulimwenguni. Alipokuwa China Mtemvu alijiita Waziri Mkuu wa Tanganyika", alisema Bwana Chipaka. Hapo hapo akatoa bahasha ya barua kutoka China aliyoletewa Mtemvu kwa cheo cha Waziri Mkuu wa Tanganyika.
Aliendelea, "Mimi nilikubaliana na Bwana Mtemvu kuwa niende Unguja, mwenyewe akanipa barua nikampelekea Bwana Ali Muhsin. Nilifanikiwa sana, ndiyo maana sasa Mtemvu ananionea gele.
"Nilipokuwa Unguja nilikuwa kama Mfalme, na sasa Mtemvu hapandezwi na kufanikiwa kwangu huko na Mtemvu anashirikiana na Marijani ili kuniangusha. Wala sipendelei Marijani awe Katibu wa Mtemvu.
Chipaka aliongeza, " Mtemvu alipokwenda nchi za Mashariki, hakufanikiwa kama vile nilivyofanikiwa mimi Unguja. Alipewa vitu vingi lakini aliporudi huku alijifanya kwamba vilikuwa zawadi alizopewa yeye mwenyewe wala hazikutolewa kwa Congress.
Halmshauri Kuu ya chama ilikuwa ikikutana tangu Jumamosi ikimfikiria Bwana Mtemvu, alisema Bwana Chipaka.
Akazidi kueleza, "Nilipokwenda Unguja nilimweleza Bwana Muhsin kuwa sikuwa na kitu, akanipa senti fulani, lakini sasa wakina Mtemvu na Omido wanavitaka hata visenti nilivyopewa Unguja nivitoe kwenye chama. Lakini Mtemvu mwenyewe hakurudi na hata senti moja kutoka nchi za Mashariki.
"Hawawezi kunitoa katika Congress kwa sababu wanachama wote wako upande wangu nami nina kila ushahidi wa haya ninayosema. Hafai
Aliendelea, "Mtemvu hafai kwa uongozi, ndio maana Sanga aliacha chama cha Congress. Katika barua yake ya kuacha kazi Sanga mwenyewe alisema wazi kwamba yeye hawezi kuwa Katibu na Mtemvu kuwa Rais wa Congress, aliona kwamba hawawezi kufanya kazi pamoja".
Naye Bwana Omido Katibu Mwenezi wa Congress alisema kwamba mashitaka ya Bwana Chipaka hayana msingi wowote. Alisema kwamba jana usiku habari ya Bwana Chipaka ilikuwa ikifikiriwa na Halmashauri Kuu ya Congress.
Makaburu wadhibiti habari
JOHANNESBURG, Afrika Kusini
UTAWALA wa makaburu wa Afrika Kusini jana ulipiga marufuku vyombo vya habari kupiga picha na kutangaza habari za ghasia za Wazalendo ambazo zimeikumba Afrika Kusini kwa muda wa mwaka mmoja na miezi minane na kutangazwa katika magazeti ya dunia nzima pamoja na kwenye televisheni.
Waziri wa sheria wa makaburu Louis Le Grange alisema kuwa wapiga picha hawaruhusiwi kupiga picha za mapambano na migomo katika maeneo ambayo yamewekwa chini ya amri ya hali ya hatari isipokuwa tu kwa kibali maalum kutoka kwa polisi na kwamba waandishi wa habari hawaruhusiwi kuandika habari katika maeneo hayo. Hayo yalitangazwa katika gazeti la serikali lililotolewa jana.
Rais Peter Botha, ambaye serikali yake inavilaumu vyombo vya habari kwa kuandika habari zinazohusu ghasia nchini Afrika Kusini ambazo zimeifanya Afrika Kusini ishutumiwe na dunia nzima, Alhamisi iliyopita alivionya vyombo vya habari vya nchi za nje visiandike mabaya tu kuhusu Afrika Kusini.
Hatua hiyo ya Afrika Kusini ambayo itainyima dunia kufahamu unyama unaofanywa na polisi kwa wazalendo imechukuliwa wakati askari wa makaburu wamesambaa kwenye mitaa ya Johannesburg baada ya kuwepo na ghasia katika siku za hivi karibuni.
Waandishi wa habari kutoka nje ambao wamekuwa wakiandika habari kuhusu ghasia ambapo zaidi ya watu 800 wamekufa, wameshutumiwa na serikali ya Afrika Kusini kwa kile inachokiita upendeleo wakati wanapoandika habari zao.
Zaidi ya waandishi wa habari 170 kutoka nje wako Afrika Kusini wakati ambapo wengine zaidi wanazidi kuja kwa madhumuni ya kuandika habari za wimbi la mapambano nchini Afrika Kusini.
Mzalendo Jumapili, Novemba 3, 1985
CHIFU Adam Sapi Mkwawa alichaguliwa tena jana kwa mara ya tano kuwa Spika wa Bunge, baada ya kuchaguliwa kwa kura zote 189.
Upigaji wa kura kumchagua Spika wa Bunge ulianza saa 10 alasiri wakati Bunge lilipoketi likiwa Kamati ya Chama ambapo Chifu Sapi alikuwa ndiye mgombea pekee wa nafasi hiyo.
Uchaguzi wa Spika ulifanywa kwa kura ya siri. Katibu wa Bunge ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ndugu Elias Kazimoto ndiye aliyesimamia uchaguzi huo.
Baada ya wabunge kupiga kura zao, Ndugu Kazimoto aliwateua Ndugu Amran Mayagila, Mbunge wa Iringa Mjini na Ndugu Masoud Omar Masoud (Mkuu wa mkoa, Kaskazini Pemba) kusimamia kuhesabu kura.
Baada ya kura kuhesabiwa, Ndugu Kazimoto alisema: "kwa mujibu wa sehemu ya 22 ya Kanuni za Bunge, Chifu Adam Sapi amechaguliwa kwa kauli moja kuwa Spika wa Bunge".
Huku akishangiliwa, Ndugu Kazimoto aliwaomba Ndugu Austine Shaba, Mbunge wa Mtwara Mjini na Ndugu Masoud Omar Masoud kumtafuta Spika "popote alipo" ili achukue nafasi yake.
Ndugu Sapi alipelekwa kwenye ukumbi wa Bunge akiongozwa na Wabunge hao wawili huku wakizungukwa na wapiga kura hadi kwenye nafasi yake ambapo alimpa.
Ndugu Sapi ambaye ni mzee anayeheshimiwa kwa jinsi anavyoliongoza Bunge, aliwashukuru wote kwa kumchagua na kuwapongeza kwa kuchaguliwa kwao kuwa Wabunge.
"Mimi nikiwa raia wa Tanzania naona fahari sana kuchaguliwa na naahidi kwamba nitalitumikia taifa kwa uwezo wangu wote", alisema Ndugu Sapi.
Mara baada ya kuapa, Spika wa Bunge alitangaza kuwa Waziri Mkuu, Ndugu Salim Ahmed Salim, ambaye pia ni kiongozi wa shughuli za serikali bungeni ndiye atakayekuwa wa kwanza kuapa akifuatiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ndugu Anna Abdallah. Baadaye walifuatia wabunge wengine.
Mafisadi wa Marekani wafukuzwa Guinea
Uhuru, Alhamisi, Novemba 10, 1966
RAIS Ahmed Sekou Toure wa Guinea ametoa amri ya kuwafukuza Wamarekani wote waliokwenda nchini huko kwa kazi za kujitolea (Peace Corps) na kuamuru waondoke nchini Guinea katika muda wa siku nane.
Amri hiyo aliitoa juzi alasiri kwenye mkutano wa hadhara baada ya kugunduliwa kuwa Wamarekani hao walihusika na vitendo vya kifisadi vilivyosababisha kukamatwa na kuzuiliwa kwa wajumbe 19 wa Guinea nchini Ghana, wakiwa safarini kuelekea Addis Ababa kwenye mkutano wa mawaziri wa nchi za kigeni.
Kufuatana na habari zilizotangazwa mjini Washington, Amerika inasemekana kuwa Rais Toure alisema alipokuwa akitoa amri hiyo kwamba Wamarekani 64 wa kujitolea waliopo mjini Conakry (mji mkuu wa Guinea) pamoja na wengine wengi ambao wametawanyika katika vijiji na miji mbalimbali ya Guinea, pamoja na jamii nane za Kimarekani ni lazima waondoke nchini humo katika muda wa siku nane.
Katika siku chache zilizopita, baada ya tu ya kukamatwa na kuzuiliwa kwa wajumbe wa Guinea nchini Ghana, serikali ya Guinea iliweka amri ya kuwazuia Wamarekani hao wa kujitolea wasitembee ovyo kama wanavyotaka nchini humo, lakini baadaye amri hiyo iliondolewa, imeelezwa kutoka Washington.
Msemaji mmoja wa Marekani wa kujitolea alisema baada ya kutolewa kwa amri hiyo kwamba inaelekea kuwa serikali ya Guinea itaizingatia amri hiyo ya Rais Toure, jambo ambalo Marekani hao hawatakuwa na la kusema.
Akaongeza "ikiwa kama ni hivyo basi sisi hatutakuwa na kipingamizi chochote na tutaweza kuondoka katika muda wa wiki moja".
Msemaji mmoja wa serikali ya Amerika mjini Washington alidai kwamba kufukuzwa kwa Wamarekani hao wa kujitolea kumefanyika kutokana na kukamatwa kwa wajumbe wa Guinea nchini Ghana baada ya kuteremshwa kwa nguvu kutoka katika ndege ya Kimarekani ambapo serikali ya Kimarekani haikuchukua hatua yoyote kuwatetea wajumbe hao.
China na Urusi zalaumiana
Uhuru, Alhamisi, Agosti 14, 1969
HONG KONG, Jumatano
CHINA imedai kwamba majeshi ya Urusi yakiwa na vifaru, magari yenye silaha na helikopta yalishambulia sehemu ya China, yakaua na kujeruhu wanajeshi kadhaa wa Kichina.
Serikali ya China, katika taarifa kali ya malalamiko iliyotangazwa na Redio Peking imesema kwamba mapigano hayo ya mpakani yalitokea katika jimbo la Sikiang ambako China imefanya majaribio ya mabomu ya atomik.
Taarifa hiyo imetaka kuondoka haraka kwa majeshi yote ya Kirusi na ikasema kuwa ndiyo yenye dhamana ya matokeo ya kile ilichokieleza kuwa ni "uchokozi wa dhahiri".
Taarifa hiyo iliyotolewa na Balozi wa Urusi mjini Peking pia ilisema kwamba majeshi ya China yalipigana ili kujihami.
Pia iliilaumu Urusi kwa kupeleka vifaru vingi na majeshi "katika juhudi ya kutaka kusababisha vita zaidi".
Wakati huo huo, huko Moscow serikali ya Urusi ilitangaza leo kwamba mejshi mengi ya Kichina yenye silaha yalivuka mpaka wa Mashariki kutoka jimbo la Sikiang wakaingia katika sehemu ya Urusi lakini wakarudishwa nyuma na majeshi ya Urusi.
Shirika la Habari la Tass limesema kwamba serikali ya Urusi imetoa malalamiko kwa China kuhusu "uchokozi huu mpya" na imerudia maonyo ya kwanza kwamba "uingiliaji wowote katika ardhi ya Urusi utajibiwa vikali".
Tass limesema kwamba mapigano yalikuwa katika sehemu ya Kazakhstan, sehemu iliyokuwa na mapigano wakati wa mkutano wa vyama vya Kikomunisti mwezi Juni.
Shirika la Habari la Tass limesema kwamba maafisa wa Kichina wametiwa nguvuni katika ardhi ya Urusi. Lilisema kwamba kumetokea vifo na majeruhi katika mapigano hayo lakini halikutoa maelezo kamili.
Na Yassin Sadik
VIONGOZI wa Makao Makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania BAKWATA juzi walianza kufanyia kazi zao 'uhamishoni' katika eneo la Upanga Magharibi nyumbani kwa mkubwa mmoja wa baraza hilo ili kupanga mashambulizi ya kukomboa ofisi zao zilizowekwa chini ya ulinzi siku ya Jumamosi na Waislamu wanaopendelea mageuzi ndani ya BAKWATA.
Uchunguzi uliofanywa na waandishi wa habari jana utokana na tukio hili la aina yake hapa nchini, umeonyesha kuwa zaidi ya Masheikh 20 na viongozi wa BAKWATA wa mikoa yote ya Tanzania bara ambao walikuwa mjini Dar es Salaam kusubiri jawabu la kuonana na Rais Ali Hassan Mwinyi baada ya mkutano wa Morogoro juu ya kusakamwa BAKWATA, walionekana kufadhaika na wengine wakijadili majaliwa ya uongozi wa Waislamu.
Huko Kinondoni yaliko makao makuu, waandishi wa habari walikuta kundi kubwa la Waislamu wanaendelea kuchunga milango yote ya ofisi na majengo mengine, ikiwemo nyumba ya Sheikh Mkuu huku magari yakiwaletea vyakula na huduma zinazostahiki.
Ulinzi wa aina hiyo umewekwa pia katika ofisi ya BAKWATA mkoa wa Dar es Salaam iliyoko kona ya mtaa wa Agrey na Lumumba, na pia Alharamain ambako huko palikuwa panalindwa kwa doria kali.
Baadhi ya waliokuwa wanadhibiti ulinzi wa shule hiyo ni kati ya walimu 14 waliofukuzwa shuleni hapo mwezi Oktoba mwaka jana kwa kile kilichoelezwa kuwa hawakuelewana na Mkuu wa Chuo kuhusu maslahi na mikataba ya kazi.
Mmoja wa maofisa walioonekana kusimamia mipango ya kuchukua uendeshaji wa ofisi za BAKWATA aliwaeleza waandishi wa habari jana hiyo kuwa watakuwa tayari kulegeza msimamo wao ikiwa viongozi wawili wa makao makuu watatangaza kujiuzulu wenyewe. Viongozi hao aliwataja kuwa ni Alhaj Suleiman Hegga ambaye ni Kaimu Makamu Mwenyekiti na Alhaj Mahami Rajabu Kundya ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu.
Kwa mujibu wa ofisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini viongozi hao inadaiwa wanaendesha chombo cha Waislamu kama kampuni ya mtu binafsi au kambi ya jeshi.
Alipoulizwa kuhusu hatua waliyochukua baada ya kukamata maofisi ya BAKWATA, msemaji huyo alieleza kuwa "vinginevyo tumeshaiomba serikali iwaondoshe watu hao wawili kwa ajili ya usalama na amani ya Taifa hili, isimamishe katiba ya BAKWATA ya 1984 na hapo hapo Sheikh Mkuu awajibike kwa kufumbia macho maovu, dhulma, dharau na madhambi yanayofanywa na watendaji wake dhidi ya Waislamu wa nchi hii kwa zaidi ya miaka 15 sasa.
Juhudi za kumpata Sheikh Mkuu Hemed bin Jumaa bin Hemed zilishindikana jana ili kupata maelezo yake juu ya mgogoro huu maana inasemekana kuwa siku moja kabla ya tukio hilo alihamisha familia yake iliyokuwa inaishi karibu na Makao Makuu ya BAKWATA na hivyo kila akitafutwa huambiwa "yuko Tanga".
Mwenyekiti wa jumuiya hizo za Kiislamu ambazo inadaiwa zimeungana kuchukua nafasi ya BAKWATA Sheikh Salum Khamis alieleza kuwa katiba ya kuendesha baraza hilo jipya imepitishwa Jumamosi walipokutana Waislamu wa nchi nzima, na tayari imeshawasilishwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ili kuchukuliwa hatua zinazostahili.
Alipoulizwa juu ya kuvamia ofisi za watu, ofisa mwingine ambaye naye aliomba asitajwe jina alidai kuwa "hata hao wakubwa wawili (Hegga na Kundya) wanaong'ang'ania uongozi hawakukabidhiwa baraza hilo bali walifanya hila na ujanja kwa siri na kutangaza ghafla kuwa wametwaa madaraka, na makabidhiano (kama yapo) yalifanyika baada ya kuwatimua wenzao maofisini.
Mpaka sasa ni miezi 18 Waislamu hatujaitwa kuelezwa walikabidhiwa nini, kitu gani kimepungua au kuongezeka, makosa gani yaliyowapelekea kuwaondosha wenzao na maendeleo gani yamepatikana, hivyo tumechoka kutapeliwa na watu ambao hata serikali iliwatimua kwa kujifanya maarufu kumbe wabadhilifu", alieleza huku akionyesha uchungu.
Mpaka sasa kila upande unadai kuwa umepeleka taarifa zake Ikulu na kuomba maamuzi ya Rais Mwinyi juu ya purukushani za uongozi imara wa Waislamu.
Wakati gazeti hili linakwenda mitamboni polisi waliendelea kufanya doria kwenye maeneo hayo ili kuhakikisha usalama wa wananchi. Hata hivyo wafanyakazi wa makao makuu na mkoa wa Dar es Salaam walionekana nje ya ofisi zao wakisubiri hatima ya patashika za ukubwa.
WAZIRI wa Mambo ya Nchi za Nje Ndugu Benjamin Mkapa aliwasili mjini Khartoum jana akiwa na salamu kutOka kwa Rais Nyerere kwenda kwa Rais Jaafar Nimeiri wa Sudan, Shirika la Habari la Sudan (SUNA) limeeleza.
Shirika hilo limesema kwamba, salamu hizo zitaimarisha uhusiano wa nchi hizi mbili, pia zitafafanua hali ya hivi sasa katika Afrika Mashariki, lakini halikutoa maelezo zaidi.
Congress itawafukuza wageni Lejiko - Mtemvu
Mwafrika Jumanne Septemba 25, 1962
"AMRI kali kali zinakuja katika serikali ya TANU ya Jamhuri, kwa hiyo ukipigia kura TANU, unajipalia Makaa ya moto yakuunguze kichwani; pia unakaribisha taabu".
Haya yalisemwa na Bw. Mtemvu, Rais wa Congress katika mkutano wa hadhara juzi mjini Dar es Salaam huko Magomeni.
Akasema: Wapiga kura wakiichagua Congress (wala si Mtemvu labda mnayechukiana), bali hutamwona tena Mzungu au Mhindi ndani ya Baraza la Taifa.
Pia watemi watarudishwa katika utemi wao; sheria za wafanya kazi za kugoma iwapo hawafanywi haki zitarejeshwa; na hata marejinoli kamishna na maarea kamishna ambao hivi sasa ni watumishi wa serikali bali ni macheameni wa TANU wataachishwa kazi hizo.
Ukoloni wa ndani
Kuhusu habari za ukoloni wa kisirisiri uliomo serikali na kuitwa Afrikanaizesheni, Bw. Mtemvu alisema katika kila ofisi ya Waziri, yupo Mzungu anayeitwa 'Staff Officer". Je, kazi ya Mzungu huyo ni nini? Kama si kupeleka habari za siri zenu kwao London? (bomoa!!!!!)
Akasema kwamba TANU haiwezi kuondoa mseto kwa sababu uhuru huu usingepatikana ila kwa sababu TANU imeahidiana na Uingereza mseto uwepo.
Vile vile TANU inaona ugumu kuvunja ahadi zake na ndiyo sababu Wazungu chungu nzima pamoja na Wahindi wamejiandikisha kuwa raia wa Tanganyika. Je, watawezaje kuwabagua ndani ya Baraza la Taifa? aliuliza Bwana Mtemvu.
Kamishna aeleza mafanikio ya mkoa
Mwafrika Alhamisi Machi 12, 1964
REGIONAL Commissioner wa Mkoa wa Pwani Bwana Suleiman Kitundu alipokuwa akihutubia mkutano wa Halmashauri ya maendeleo ya mkoa wa Pwani uliofanyika mjini Dar es Salaam majuzi, Kamishna huyo aliieleza komiti hiyo mipango mbalimbali ambayo ilipangwa mwaka jana na imefanikiwa.
Akianza kueleza kwa sehemu mbalimbali alisema kwamba sehemu ya Kisarawe barabara tatu, shule tano za Lower, Primary, nyumba nne, dispensary moja, barabara nane zenye urefu wa maili sabini na tatu na soko moja.
Makadirio ya majengo haya yanakadiriwa kuwa shilingi 47,410 msaAda wa kupata vitu vilivyojengea ni shilingi 9,400.50 na akiba imekuwa shilingi 38,009.
Katika sehemu ya Mzizima shule mbili za Upper Primary, kisima kimoja, madaraja matatu, nyumba mbili za kukaa watu, stoo moja ya ofisi na mabarabara manne yenye urefu wa maili kumi na nne. Fedha za akiba zilifikia shilingi 43,577.88.
Sehemu ya Mafia ni dispensari moja tu ndio ambayo imemalizika na gharama yake ni shilingi 5,110.32 msaada ulitolewa ni shilingi 1,720.92 na akiba imefikia shilingi 3,390.
Bwana Kitundu aliuambia mkutano kwamba sehemu ya Bagamoyo na Rufiji ni lazima ziongeze juhudi zao na kama hazikufanya hivyo ni wazi ziTarudisha maendeleo yao ya uchumi wa mkoa huu.
Regional Commissioner aliwashukuru vijana wa National Service kwa kusaidia kujenga daraja la Mbwamaji na pia alitoa shukrani zake kwa chama cha Dar es Salaam Football Association kukubali kuchezesha michezo ya mpira ambayo imewezekana shilingi 700 kupatikana.
Mpaka sasa mfuko huo wa maendeleo umefikia shilingi 6,000 ambazo zitatumika kwa mipango mbalimbali.
MafunGu mawili ya misaada yametolewa kwa sehemu ya makao mapya ya Mafia na Mbwamaji. Mafia imepokea shilingi 500 na Mbwamaji shilingi 722 kutoka mfuko huo.
Aliyempiga mfumaniwa kaachiwa
Mwafrika Jumanne Agosti 28, 1962
OMARI bin Musa, kabila Mpogoro aliyekuwa ameshitakiwa kortini huko Magomeni mjini Dar es Salaam kwa sababu ya kumjeruhi vibaya sana Bwana mmoja wa Kihaya aitwaye Dotratios Karema, aliAchiliwa huru jana na Hakimu Bw. Balozi Rehani, kwamba mshitakiwa huyo alikuwa na sababu ya kutosha ya kumwumiza bwana huyo baada ya kumfumania na mkewe.
Hakimu alitamka kuwa mtu yeyote angekasirika na kuchukua hatua aliyofanya mshitakiwa ya kupigana, kama angemkuta mtu mwingine akizini na mkewe.
Alimwonya mshitaki ajihadhari na tabia ya kutembea na wake za wenzake; alimwonya asiwe na makuu ya kujifanya hajui Kiswahili, kumbe wakati wote alipokuwa akizungumza na bibi huyo alitumia Kiswahili.
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
0 Comments