[wanabidii] Hatua iliyofikiwa katika kuanzisha Umoja wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki

Wednesday, August 07, 2013

TAARIFA YA HATUA ILIYOFIKIWA NA NCHI WANACHAMA WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI KATIKA MAJADILIANO YA KUANZISHA UMOJA WA FEDHA


1.0       UTANGULIZI

Ibara ya 5(2) ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inabainisha kuwa Umoja wa Fedha ni hatua ya tatu ya Mtangamano wa Afrika Mashariki. Madhumuni ya Umoja wa Fedha ni kujenga ukanda tulivu wa kifedha (monetary and financial stability zone) utakaoharakisha kusaidia ukuaji wa biashara na shughuli za kiuchumi ndani ya Jumuiya. Katika kufikia malengo haya ya Umoja wa Fedha Nchi Wanachama, ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki, hukubaliana yafuatayo:-

i. Kuongeza kiwango na kasi ya mtangamano wa masoko ya fedha na mitaji (deepen financial market integration);
ii. Kuhuisha sera za kibajeti za nchi Wanachama (harmonisation of national fiscal policies);
iii. Kuwa na utaratibu wa kuendesha shughuli za uchumi bila kukinzana na malengo ya Umoja wa Fedha;
iv. Kuunda Benki Kuu moja ya Jumuiya (EACB) itakayosimamia Sera moja ya fedha(single monetary policy) na sera moja ya viwango vya ubadilishanaji fedha (exchange rate policy); na
v. Kuanzisha sarafu moja ya Jumuiya;

2.0    HATUA ILIYOFIKIWA

Mchakato wa uundaji Umoja wa Fedha wa Afrika Mashariki ulianzishwa na Kikao cha 15 cha Baraza la 
Mawaziri la Afrika Mashariki kilichofanyika mwezi Machi, 2008 baadaye kuidhinishwa na Kikao cha Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (Summit). Utafiti wa Umoja wa Fedha ulifanyika, kukamilishwa na taarifa ya utafiti kujadiliwa na Nchi Wanachama kupitia Baraza la Mawaziri la Jumuiya ambalo liliunda Kikosi Kazi cha Majadiliano ya Umoja wa Fedha mwezi Machi, 2010 na Baraza la Mawaziri la Kisekta la Umoja wa Fedha liliundwa mwezi Novemba, 2010 na kupewa jukumu la kusimamia majadiliano ili kukamilisha zoezi hilo.  Hata hivyo, majadiliano hayo hayakuweza kukamilika mwezi Desemba, 2012 kutokana na Nchi Wanachama kuhitaji muda zaidi wa kujadiliana na kufikia makubaliano katika maeneo kadhaa nyeti ikiwemo vigezo vya kuhuisha uchumi mpana (Macroeconomic Convergence Criteria).

Hivyo, Viongozi Wakuu wa Jumuiya walipokutana tarehe 31 Novemba, 2012 waliongeza muda wa majadiliano. Napenda kuwafahamisha kuwa majadiliano hayo sasa yamekamilikaambapo Rasimu ya Itifaki ya Umoja wa Fedha iliidhinishwa katika Mkutano wa Dharura wa 27 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya uliofanyika kuanzia tarehe 17 – 18 Julai, 2013. Hatua inayoendelea ni  Itifaki  hiyo kupitiwa na Baraza la Mawaziri la Kisekta la Sheria ili kujiridhisha kama Rasimu inakidhi matakwa ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kisheria. Aidha Rasimu  inategemewa kuwasilishwa kwa Viongozi Wakuu wa Jumuiya mwezi Novemba, 2013.

3.0    MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIWA

Msingi Mkuu wa Umoja wa Fedha ni Nchi Wanachama kufikia Vigezo vya Kuhuisha Uchumi Mpana (Macroeconomic Convergence Criteria). Vigezo ni:-
a)      Kiwango cha Juu cha Mfumuko wa Bei kisichozidi asilimia 8 (Ceiling on Headline Inflation of 8%);
b)      Kiwango cha Juu cha Nakisi ya Bajeti ikijumuisha misaada kisichozidi asilimia 3 ya Pato la Taifa (Fiscal Deficit ceiling including grants of 3% of GDP);
c)      Kiwango cha Juu cha Deni la Taifa kisichozidi asilimia 50% ya Pato la Taifa (Ceiling on Public Debt of 50% of GDP); na
d)      Akiba ya Fedha za Kigeni ya kutosheleza mahitaji ya miezi minne na nusu (Reserve cover of 4.5 months of imports).

Tofauti na Itifaki nyingine za Jumuiya   Rasimu ya Itifaki ya Umoja wa Fedha inaainisha kuwa endapo Nchi Tatu zitafikia vigezo hivyo, Jumuiya ya Afrika Mashariki itaanza kutekeleza Umoja wa Fedha kwa kuingia kwenye ukanda wa Sarafu Moja, na nchi nyingine wanachama zitajiunga baadaye, kadiri zitakavyoweza kutimiza vigezo husika.

Pamoja na Rasimu ya Itifaki ya Umoja wa Fedha, Jumuiya ya Afrika Mashariki imeandaa Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Umoja wa Fedha.  Mpango Kazi huo umezingatia hatua zinazohitajika katika utekelezaji wa hatua za awali za Mtangamano, uainishaji wa vigezo vya uchumi mpana (Macroeconomic Convergence Criteria), na uanzishaji wa Taasisi na Sheria stahiki. Kulingana na Mpango kazi huu Jumuiya inatarajia kukamilisha yaliyaonishwa katika Mpango kazi na kuwa na sarafu Moja ya Jumuiya ifikapo mwaka 2024.

Imetolewa na:
WIZARA YA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI


Source: http://www.wavuti.com/4/post/2013/08/hatua-iliyofikiwa-katika-kuanzisha-umoja-wa-fedha-wa-jumuiya-ya-afrika-mashariki.html#ixzz2bHDcFyx4

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

Share this :

Related Posts

0 Comments